Sunday, March 17, 2019

Mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC ujao kufanyika Tanzania



Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Council of Ministers), lililokuwa likiendelea na mkutano huko Windhoek, Namibia, limehitimisha mkutano huo  kwa Tanzania kuwakaribisha viongozi hao kushiriki katika mkutano unaofuata wa baraza hilo ambao utafanyika Dar es salaam, Tanzania, Agosti 2019.


Akizungumza wakati wa kuhitimisha mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano waAfrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi(Mb.), ameelezea furaha yake kwa Tanzania ambayo ni miongoni mwa mataifa yaliyoshiriki katika ukombozi dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi katika nchi mbalimbali Kusini mwa Afrika kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kuahidi kufanya maandalizi ya kutosha. 


Naye Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni  Naibu Waziri Mkuu wa Namibia na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Netumbo Nandi-Ndaitwah, amehitimisha mkutano huo kwa kuziomba nchi wanachama wa SADC zilizoshiriki katika mkutano huo  kuhakikisha masuala yaliyoafikiwa katika mkutano huo yanatekelezwa kwa wakati.


Baadhi ya musuala yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na Taarifa ya Utekelezaji wa mipango na mikakati ya SADC; Taarifa ya Kamati ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na Kamati ya Usimamizi wa Rasilimali watu; Hatua zilizofikiwa katika mchakato wa Visiwa vya Komoro kujiunga na SADC na Mpango wa Kuanzisha chuo cha Uhawilishwaji cha SADC (SADC  University of Transformation).Masuala Uendelezaji wa viwanda katika kanda; Utekelezaji wa Mkakati wa Kanda wa Mawasiliano na Mabadiliko ya Kitaasisi katika Umoja wa Afrika(AU).

Waziri Ofisi ya Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Issa Haji Ussi Gavu (mwenye tai ya bluu)Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, wakati wa mkutano huo.

Baadhi ya wajumbe wakiimba wimbo wa SADC wakati wa kuhitimisha mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC.

Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena Tax, akiteta jambo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.