TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Balozi wa Canada atembelea Wizara ya Mambo ya Nje
Bw. Jestas A. Nyamanga,
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika-Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa
Canada hapa nchini Mhe. Pamela O’Donnell tarehe 11 Machi 2019.
Mazungumzo hayo
yaliyofanyika jijini Dar es Salam yamelenga kuimarisha uhusiano baina ya
Tanzania na Canada. Mataifa haya mawili, kwa kipindi kirefu yamekuwa
yakishirikiana kwenye masuala ya afya, elimu, ukuzaji wa uchumi, Utawala Bora
pamoja na biashara na uwekezaji.
Katika mazungumzo hayo,
Balozi wa Canada amemhakikishia Kaimu Mkurugenzi kuwa, Serikali ya Canada
inaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano katika kuleta
Maendeleo na kuondoa umaskini na kwamba Canada itatekeleza kwa ufanisi miradi
iliyopo inayotekelezwa kupitia Serikali , Mashirika ya Umoja wa Mataifa na
Asasi zisizo za Kiserikali(NGOs).
Wakati huo huo, Kaimu
Mkurugenzi alimkaribisha Balozi huyo mpya nchini na kuishukuru Serikali ya
Canada kwa ushirikiano mzuri na wakihistoria uliodumu baina ya Tanzania na
Canada .
Aidha, aliishukuru
Serikali ya Canada kwa kuisaidia Tanzania katika miradi muhimu na ya kipaumbele
hususan miradi ya afya, elimu na ukuzaji wa uchumi. Alimhakikishia ushirikiano
thabiti wa Wizara na Serikali kwa jumla katika kuhakikisha miradi iliyopo
inatekelezwa kwa ufanisi na mingine mipya inaibuliwa.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.