TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Prof. Kabudi apokea Salamu za Pongezi kutoka kwa Waziri wa Mambo
ya Nje wa China
Mheshimiwa Prof. Palamagamba J. Kabudi (Mb),
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, leo tarehe 13 Machi,
2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa WANG Ke, Balozi wa Jamhuri
ya Watu wa China.
Mheshimiwa WANG Ke pamoja na masuala mengine
amewasilisha kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
barua ya pongezi kutoka kwa Mheshimiwa Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa
Jamhuri ya Watu wa China kufuatia Prof. Kabudi kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki.
Aidha Prof. Kabudi kupitia kwa Mheshimwa Balozi ameshukuru
kwa salamu hizo za pongezi alizopokea.
Katika mazungumzo yao, Prof. Kabudi na Balozi WANG
Ke, wameahidi kufanya kazi kwa pamoja ili kuimarisha ushirikiano wa kihistoria
baina ya nchi hizo mbili. Na kwa pamoja wamesisitiza umuhimu wa kuendelea na
jitihada za kuimarisha mahusiano ya kisiasa, kijamii, kiuchumi hususan kwenye maeneo
la uwekezaji, biashara, utalii na miundombinu.
Prof. Kabudi ametumia fursa hiyo kuishukuru
Jamhuri ya Watu wa China kwa misaada ya kimaendeleo wanayoendelea kuitoa na
kwamba Serikali inafurahishwa na Jinsi China inavyounga mkono jitihada zake za
kuwaletea wananchi maendeleo na kujenga uchumi.
Tanzania na China zimekuwa na mahusiano ya
kidiplomasia tangu mwaka 1964 na mwaka huu zinatarajia kuadhimisha miaka 55 ya
ushirikiano huo.
Mheshimiwa Wang amekuwa Balozi wa kwanza kuonana
na Mhe. Kabudi tangu kuteuliwa kwake na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kuiongoza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki,
Dodoma.
13 Machi
2019
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.