Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Rais wa Bunge la Cuba, Mhe. Esteban Lazo Harnandez, mjini Havana, Cuba.
|
Mhe. Harnandez kulia akipokea zawadi ya mlango
wa mji Mkongwe kutoka kwa Balozi Seif kama ishara ya kufunguliwa milango ya
kuitembelea Zanzibar.
|
Mhe. Harnandez akimtembeza Mhe. Balozi Iddi katika sehemu mbalimbali za jengo la Bunge ya Cuba lenye historia ya muda mrefu ambazo zimewekwa kama kumbukumbu ya taifa hilo. |
Mhe. Balozi Iddi wa pili
kutoka kulia na ujumbe wake akifanya mazungumzo na uongozi wa Wizara ya Afya mjini Havana, Cuba.
|
=====================================
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amelitembelea Bunge la Cuba na
kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa bunge la nchi hiyo, Mhe. Esteban
Lazo Harnandez.
Katika
mazungumzo baina ya viongozi hao wawili, Mhe. Harnandez ameahidi kuwa, Cuba
itaendelea kudumisha ushirikiano wake wa kidiplomasia na Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, katika kuendeleza wananchi wake licha ya taifa hilo la Caribean
kupita katika mabadiliko ya kisiasa, uchumi na utamaduni.
Mhe.
Harnandez alieleza kuwa, kutokana na mabadiliko yaliyopo sasa katika mfumo wa
dunia katika masuala ya uchumi, siasa na utamaduni Jamhuri ya Cuba
imelazimika kufanya mabadiliko ya katiba yake ili yalingane na mfumo huo wa
dunia inayoizunguka.
Alifafanua
kuwa, tayari Bunge la Cuba limeshafanya marekebisho katika katiba yake kutoa
nafasi kwa wananchi wake kuwa na uwezo na uhuru wa kumiliki nyumba, ardhi
pamoja na uwepo wa waziri mkuu atakayekuwa na mamlaka ya kusimamia utendaji wa
serikali.
Mhe.
Harnandez alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, kwamba katika vikao
vya bunge hilo vinavyotarajiwa kuanza wiki ijayo baada ya kukamilika kwa
uchaguzi wa wabunge, serikali ya nchi hiyo itakuwa imepiga hatua kubwa zaidi ya
maendeleo kutokana na mabadiliko hayo.
Rais huyo
wa Bunge la Cuba alisisitiza kwamba taasisi za kifedha zitalazimika kuzingatia
ukusanyaji bora zaidi wa mapato katika maeneo yote ya uchumi ili kuimarisha
ushiriki wa wananchi waliowengi katika mfumo huo.
Mhe.
Harnandez alihitimisha kwa kumuhakikishia Balozi Seif kwamba, uhusiano wa
muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili utaendelea kuimarishwa na kukuzwa
katika muda wote.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Iddi alimpongeza Mhe. Harnandez kwa
kuchaguliwa tena kuliongoza bunge hilo na kueleza kuwa, hatua hiyo inaonesha wazi ishara halisi ya kukubalika
vyema na wananchi wa nchi hiyo kupitia viongozi wake.
Halikadhalika,
Mhe. Balozi Iddi alieleza kuwa, kwa ujumla Zanzibar itaendelea kufuatilia
mabadiliko ya Cuba na kuangalia endapo inaweza kuiga mabadiliko hayo ili
kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi walio wengi.
Mhe.
Balozi Iddi na ujumbe wake ulihitimisha ziara yake nchini humo kwa
kufanya mazungumzo na uongozi wa Wizara ya Afya ya Cuba uliokuwa ukiongozwa na
Naibu Waziri, Mhe. Bibi Marcia Cobas, katika makao makuu ya wizara hiyo
yaliyopo Havana, Cuba.
Katika
mazungumzo hayo ya ushirikiano wa kindugu, Balozi Iddi alisema matunda ya
darasa la madaktari wazalendo waliosimamiwa na wataalamu pamoja na wahadhiri wa
nchi ya Cuba yameanza kutoa matumaini.Alifafanua kuwa, kitendo cha
Serikali ya Cuba kukubali kupunguza gharama kubwa ya kuwaendeleza madaktari hao
wazalendo wapatao 15 katika shahada ya juu ya udaktari wa uzamili nchini humo
kinaendelea kuleta faraja kubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja
na watu wake.
Alisema
wakati Zanzibar ikiendelea kutekeleza sera ya afya ya kuwa na miuondombinu ya
huduma za afya katika umbali usiozidi kilomita tano kundi hilo na madaktari
linaloendelea kuongezeka kila mwaka litakuwa mkombozi wa utekelezaji wa sera
hiyo muhimu.
Naye
Kaibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Bibi Asha Ali Abdullah, aliueleza uongozi
huo wa Wizara ya Afya Cuba kwamba, hivi sasa Zanzibar inapita katika
kipindi cha kujiimarisha kwenye mapambano yake dhidi ya maradhi yasiyoambukiza.
Bibi
Abdullah alisema maradhi yasiyoambukiza kama Kisukari pamoja na Shindikizo la
Damu hivi sasa yamekuwa yakiathiri wananchi walio wengi na kuleta vifo vingi.
Hata hivyo, jitihada zinachukuliwa ili kupunguza kasi ya athari za
maradhi hayo na kuimaliza kabisa kadhia hiyo kabisa.
Alibainisha
kuwa, maradhi ya Malaria hivi sasa yamepungua kutokana na kampeni kubwa
iliyofanywa na serikali kwa kushirikiana na taasisi na mataifa wahisani katika
kuangamiza vilui lui vya maradhi hayo.
Katibu
Mkuu huyo wa Wizara ya Afya Zanzibar alimuhakikishia Naibu Waziri wa Afya wa
Cuba kwamba ushauri wote walioupata katika ziara yao kwenye taasisi za Afya
nchini Cuba likiwemo suala la upatikanaji wa dawa litazingatiwa na iwapo
linaweza kuleta afueni ya gharama kwa Zanzibar litachukuliwa hatua mara moja.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.