Sunday, March 24, 2019

Prof. Kabudi afungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi amelitaka Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo kubuni mikakati na mbinu mpya za utekelezaji na namna ya kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza na kuhimiza Wafanyakazi kujituma na kuondokana na uzembe katika utumishi wa Umma.

Profesa Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo Dodoma wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na Rais Dkt John Pombe Magufuli kuiongoza Wizara hiyo na kuongeza kuwa, ni wajibu wa Baraza hilo kubuni mbinu na mikakati mipya ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza  pamoja na kuhimiza ushirikishwaji wa watumishi badala ya kusubiri mtu mwingine kuzitatua changamoto hizo.

“Sote tunatambua kuwa ushirikishwaji wa watumishi kwenye mipango ya Taasisi na Wizara ni jukumu la kisheria na kwa miaka yote Serikali imekuwa ikisisitiza taasisi kujenga na kutekeleza utaratibu wa kuwashirikisha watumishi kwa kuwa kunaongeza umiliki wa mipango iliyowekwa” 

Aidha, Waziri Profesa Palamagamba John Kabudi amelisisitiza Baraza hilo kupitia upya vipaumbele vilivyowekwa na jinsi gani ya kuvitekeleza, akitolea mfano namna ya kutekeleza kipaumbele cha diplomasia ya uchumi kwa kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nje, watalii na kutafuta fursa mbalimbali ikiwemo masoko ya bidhaa za kilimo kutoka Tanzania.

Pia kwa mwaka huu wa 2019 amelitaka Baraza hilo la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kujiandaa mapema na kuwashirikisha wote wanaohusika katika na mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika  (SADC) kwa kuwa mwezi Agosti  2019 Tanzania itachukua nafasi ya uenyekiti wa Jumuiya hiyo.

“ Hili ni tukio kubwa ambalo ni lazima tujipange vizuri, mara baada ya kazi ya kuandaa bajeti ya wizara ya 2019/2020 lazima tuanze kazi ya kujiandaa kwa mkutano wa SADC mara moja”

Profesa Palamagamba John Kabudi amelitaka pia Baraza la wafanyakazi la wizara hiyo kutathmini kwa kina shughuli zitakazotekelezwa katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha na kuyapitia kwa umakini maeneo yote yaliyopewa kipaumbele na serikali na kubaini mipango na mikakati mizuri katika kutekeleza vipaumbele hivyo.

Imetolewa na: 
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma, Tarehe 24 Machi 2019

=======================================================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi rasmi wa  Mkutano wa Baraza hilo uliofanyika jijini Dodoma, tarehe 24 Machi 2019. Prof. Kabudi aliwataka wajumbe wa Baraza hilo ambao ni wawakilishi wa watumishi wote wa Wizara kuhakikisha wanatekeleza majukumu kwa kuzingatia vipaumbele vya Wizara ikiwemo Diplomasia ya Uchumi ili kukuza uwekezaji na biashara pamoja na kuvutia utalii  kwa maslahi mapana ya Taifa
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakimsikiliza Mhe. Prof. Kabudi (hayupo pichani)


Sehemu nyingine ya wajumbe wa Baraza wakati wa mkutano wao wa mwaka

Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ambao ni wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wakifuatilia mkutano

Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi ukiendelea na wajumbe wakifuatilia


Wajumbe wa Baraza
Mhe. Prof. Kabudi akiwa katika picha ya pamoja  na wajumbe wa meza kuu mara baada ya kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Baraza, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi, kushoto kwake ni Katibu wa  Baraza, Bw. Magabilo Murobi. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bibi Savera Kazaura na kushoto ni Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara , Bw. Hassan Mnondwa

Mhe. Prof. Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa TUGHE wa Wizara

Picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.