TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Hakuna Mtanzania aliyepoteza maisha
kwenye ajali ya ndege iliyotokea Ethiopia
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea kwa masikitiko makubwa, taarifa kuhusu
ajali ya ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Ethiopia, iliyotokea tarehe 10
Machi 2019 nchini Ethiopia na kusababisha vifo vya watu wote 157 waliokuwemo
kwenye ndege hiyo.
Ndege
hiyo ya abiria, aina ya Boeing 737 yenye
namba za usajili ET 302 iliyokuwa inafanya safari zake za kawaida kutokea
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole, mjini Addis Ababa, Ethiopia kuelekea
mjini Nairobi, Kenya, ilikuwa imebeba abiria 149 kutoka mataifa mbalimbali na
wafanyakazi wa kwenye ndege wapatao 8.
Kwa
mujibu wa taarifa kuhusu ajali hiyo, iliyotolewa kwa waandishi wa habari na
Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la Ethiopia, ikiwemo orodha ya abiria
na mataifa wanayotoka, hakuna Mtanzania aliyekuwemo kwenye ndege hiyo.
Orodha
ya nchi na idadi ya raia (kwenye mabano) waliokuwa kwenye ndege hiyo ni kama ifuatavyo: Kenya (32), Canada (18),
Ethiopia (9), China (8), Italia (8), Marekani (8), Ufaransa (7), Uingereza (7),
Misri (6), Ujerumani (5), India (4), Slovakia (4), Austria (3), Urusi (3),
Sweden (3), Hispania (2), Israel (2), Morocco (2) na Poland (2).
Nchi
zingine ni Ubelgiji (1), Djibouti (1), Indonesia (1), Ireland (1), Msumbiji
(1), Norway (1), Rwanda (1), Saudi Arabia (1), Sudan (1), Somalia (1), Serbia
(1), Togo (1), Uganda (1), Yemen (1), Nepal (1), Nigeria (1) na raia aliyekuwa
na hati ya kusafiria ya Umoja wa Mataifa (1).
Mamlaka
husika zimeanza uchunguzi ili kujua chanzo cha ajali hiyo.
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaungana na wote walioguswa na msiba huu
mzito kutoa pole kwa mataifa yote yaliyopoteza raia wake kwenye ajali hiyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma.
10 Machi 2019
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.