Thursday, August 29, 2019

WAZIRI WA MAMBO YA NJE, MHE. PROF. PALAMAGAMBA JOHN KABUDI AFANYA MAZUNGUMZO NA MEYA WA JIJI LA NAGAI NCHINI JAPAN


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa kwenye mazungumzo na Meya wa Jiji la Nagai nchini Japan, Mhe. Shigeharu Uchiya. Mazungumzo yao yalihusu Jiji hilo kuwa kambi ya maandalizi ya wanamichezo watakaoshiriki Michezo ya Olyimpic itakayofanyika jijini Tokyo mwaka 2020 wakiwemo kutoka Tanzania. Mazungumzo kati ya Mhe. Prof. Kabudi na Mhe. Uchiya yalifanyika tarehe 29 Agosti 2019 jijini Yokohama pembezoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika unaoendelea jijini hapo.
Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki mazungumzo kati ya Mhe. Prof. Kabudi na Meya wa Jiji la Nagai, Mhe. Shigeharu Uchiya (hawapo pichani). Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bibi Amina Shaaban, akifuatiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Zanzibar, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Japan, Bw. John Kambona na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Bertha Makilagi
Meya wa Jiji la Nagai, Bw. Shigeharu Uchiya akimweleza jambo Mhe. Prof. Kabudi wakati wa mazungumzo kati yao
Ujumbe uliongozana na Meya wa jiji la Nagai, Mhe. Shigeharu Uchiya ukifuatilia mazungumzo.
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mazungumzo
Mhe. Prof. Kabudi akimwonesha Mhe. Uchiya jarida linaloonesha vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini
Mhe. Prof. Kabudi akiagana na Mhe. Shigeharu Uchiya mara baada ya kumaliza mazungumzo kati yao
Mhe. Prof. Kabudi akisalimiana na mmoja wa raia wa Japan aliyewahi kufanya kazi za kujitoleak kwenye sekta ya afya nchini Tanzania miaka ya 1960.

=============================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Prof. Kabudi afanya mazungumzo na Meya wa Jiji la Nagai nchini Japan

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ameishukuru Serikali ya Japan kwa kuishirikisha Tanzania kikamilifu kwenye maandalizi ya Michezo ya Olympic inayotarajiwa kufanyika jijini Tokyo mwaka 2020 ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wanamichezo wanawake kutoka Tanzania.

Mhe.Prof. Kabudi ametoa shukrani hizo wakati wa mkutano wake na Meya wa Jiji la Nagai, Mhe. Shigeharu Uchiya uliofanyika leo tarehe 29 Agosti 2019 jijini Yokohama pembezoni mwa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Ushirikiano na Afrika (TICAD 7).

Mhe. Prof. Kabudi alisema kuwa, anaishukuru Japan kwa kuwa imeonesha nia ya dhati ya kuifanya Tanzania ishiriki kwenye Michezo hiyo muhimu ya Olympic ambayo itafanyika nchini humo mwaka 2020 na kuzishirikisha nchi zote duniani. Mhe. Waziri alifafanua kuwa tayari Serikali hiyo imesaini Hati ya Makubaliano na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo mwezi Julai 2019 kuhusu ushiriki wa Tanzania kwenye michezo hiyo pamoja na kufanikisha ziara ya Timu ya wanariadha kutoka nchini wakiongozwa na mkimbiaji wa mbio za marathon mstaafu, Bw. Juma Ikangaa iliyofanyika mwezi Oktoba 2018. Pia Japan imeahidi kutoa mafunzo kwa wanamichezo wanawake yatakayotolewa jijini Nagai.

 “Ushikiano wa kirafiki kati ya Japan na Tanzania ni wa miaka mingi  hususan kwenye medani za siasa, uchumi na diplomasia. Umefika wakati sasa nchi hizi mbili zishirikiane katika masuala ya kijamii na utamaduni ili kuwaunganisha mtu mmoja mmoja na kwamba ushirikiano huo ndio muhimu kwa ukuaji wa Taifa lolote” alisema Prof. Kabudi.

Aidha, alieleza kufurahishwa na ahadi kuwa Japan itatoa mafunzo kwa wanamichezo wanawake ili kuwajengea uwezo kwenye michezo mbalimbali ikiwemo ile ya Olympic itakayofanyika Tokyo mwaka 2020. “Tumepokea kwa furaha taarifa kwamba Nagai itatoa mafunzo kwa wanamichezo wetu wanawake. Hii itawajengea uwezo mkubwa wanamichezo hao wakati wakijiandaa na mashindano ya Olympic” alisisitiza Prof. Kabudi.

Kadhalika, Mhe. Prof. Kabudi alitumia fursa hiyo kumweleza Mhe. Uchiya kuwa Serikali ya Tanzania imehamishia shughuli zake jijini Dodoma ambako ni Makao Makuu ya nchi na kwamba ipo tayari kuanzisha ushirikiano wa kidada kati ya Jiji la Dodoma na Jiji la Nagai.

Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Nagai, Mhe. Shigeharu Uchiya alisema kwamba jiji hilo litaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania na tayari limeanzisha program ya kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya michezo ambapo Mtanzania, Bw. Bahati Rogers ni miongoni mwa vijana wanaoshiriki program hiyo jijini humo. Pia alisema kuwa aliongoza ujumbe wa watu ishirini kutembelea Tanzania mwaka 2017 kwa ajili ya kubadilisha uzoefu kuhusu michezo.

Serikali ya Japan ambayo imeanza maandalizi ya Michezo ya Kimataifa ya Olympic itakayofanyika jijini Tokyo mwaka 2020, imetenga Jiji la Nagai kuwa kituo cha Wanamichezo wote wa Tanzania kitakachotumika kuwaadaa kabla ya kuanza kushiriki michezo hiyo rasmi. Maandalizi hayo ni pamoja na kuwawezesha wanamichezo kuzoea hali ya hewa, tamaduni, chakula na masuala mengine muhimu kuhusu Japan kabla ya ushiriki wao rasmi wa michezo hiyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasil
iano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Yokohama, Japan
29 Agosti 2019

Wednesday, August 28, 2019

JAPAN YATOA DOLA BILIONI 20 KUSAIDIA MAENDELEO KWA NCHI ZA AFRIKA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

JAPAN YATOA DOLA BILIONI 20 KUSAIDIA MAENDELEO KWA NCHI ZA AFRIKA

Japan imetangaza kutenga kiasi cha dola za kimarekani bilioni 20 kwa kipindi cha miaka mitatu kwa Nchi za Bara la Afrika ili kuziwezesha Nchi hizo kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo itakayoleta mageuzi ya kiuchumi katika Bara la Afrika huku Tanzania ikikazia mkakati wake wa uchumi wa viwanda.

Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe ameyasema hayo wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo Internatinaol Conference on African Development TICAD7) uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Pacifico jijini Yokohama na kuongeza kuwa Serikali ya Japan itaendelea kuchangia maendeleo ya Bara la Afrika kupitia program mbalimbali za ushirikiano kwa kuimarisha rasilimali watu, elimu ya awali kwa watoto na kuboresha huduma ya afya kwa wote.

Mhe. Abe amesema kuwa, kupitia Mpango wa TICAD, ushirikiano kati ya Japan na Afrika umeimarika na kwamba nchi hiyo itaendelea kuhakikisha inahamasisha Kampuni za Japan kuwekeza Afrika ambapo hadi sasa sekta binafsi ya Japan imewekeza dola za marekani bilioni 20 katika nchi mbalimbali za Afrika.

Akizungumzia program mbalimbali zinazotekelezwa na Japan katika kuchangia maendeleo ya Afrika ikiwemo ile ya ABE-African Businness Education Initiative, Waziri Mkuu huyo amesema kuwa tayari vijana zaidi ya 350 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanafanya mafunzo kwa vitendo kwenye Kampuni mbalimbali kupitia mpango huo na wengine 3000 ambao walishapitia mpango huo kama wawezeshaji.

Mhe. Abe amesema kuwa, Japan itaendelea kuchangia kwenye sekta ya afya hususan kwenye masuala ya dawa, lishe na kutoa mafunzo ya ujuzi kuhusu masuala hayo kwa nchi mbalimbali za Afrika. Pia Waziri Mkuu huyo amesisitiza kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Afrika kwenye ujenzi wa miundombinu kama barabara na bandari pamoja kutoa wataalam kwani nchi yake haijawahi kupungukiwa wataalam.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambaye anahudhuria mkutano huo akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema Tanzania ni miongoni mwa Nchi za Afrika zinazozalisha malighafi zinazosafirishwa nje kwa ajili ya kuongezewa thamani jambo linalofanya Bara la Afrika Tanzania ikiwemo kujikuta ikisafirisha ajira na kutengeneza soko la bidhaa kutoka katika mataifa mengine na kwamba sasa Tanzania imedhamiria kupitia viwanda kutumia malighafi zake kuzalisha bidhaa mbalimbali na hivyo kutengeneza ajira kwa watu wake lakini pia kuuza nje ya nchi na kuzalisha fedha za kigeni.
Ameongeza kuwa kupitia mkakati wa Japan kwa nchi za Afrika Tanzania ni mojawapo ya nchi zitakazonufaika na mkakati huo na kuongeza kuwa mojawapo ya maeneo ya kuboresha ili kufikia azma ya Tanzania ya viwanda ni kujenga miundo mbinu imara itakayoweka msingi wa kufikia malengo hayo kwa kuwezesha usafirishaji wa bidhaa pamoja na malighafi zitakazotumika katika viwanda.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amesema tofauti na mikutano iliyotangulia Mkutano huu wa TICAD saba kwa mara ya kwanza umeweka fursa ya kuwa na mpango kazi wa Yokohama ambapo badala ya kuwa na maazimio pekee sasa kutakuwa na fursa ya kuweka malengo vilevile kupima utekelezaji wake na upatikanaji wa fedha.

Rais wa Misri, Mhe. Abdel Fattah el-Sisi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Mwenyekiti mwenza wa Mkutano wa TICAD 7, Mhe. El-Sisi amesema kuwa Afrika kwa sasa inahitaji mapinduzi katika teknolojia na uvumbuzi ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinalolikabili Bara hilo ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana na mabadiliko ya tabia. Aidha, ametoa rai kwa nchi zinalizoendelea kutekeleza ahadi zao pamoja na Mkataba wa Paris kuhusu kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Mhe. Rais El-Sisi alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha wawekezaji kutoka Japan kuwekeza Afrika pamoja na kuzitaka taasisi za kifedha za kimataifa kutoa masharti nafuu ya mikopo ili kukuza na kuimarisha uwekezaji na biashara barani Afrika.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Antonio Guteres ameipongeza Japan kwa ushirikiano wake na nchi za Afrika hususan katika kuunga mkono jitihada mbalimbali za kudumisha amani na usalama baranii humo. Pia amezipongeza nchi za Afrika kwa kuanzisha Mpango wa Eneo Huru la Biashara barani humo ambao kwa kiasi kikubwa utaimarisha sekta ya biashara na uwekezaji na kuchangia maendeleo ya nchi hizo. Mhe. Guteres amesisistiza kuwa nchi za Afrika kwa kushirikiana na Japan ziwekeze kwenye elimu bora kwa vijana hususan kwenye maeneo ya sayansi, hesabu na teknolojia kwani yana mchango mkubwa katika maendeleo. 

Akizungumzia mabadiliko ya tabianchi, Mhe. Guteres amesema kuwa jitihada za pamoja zinahitajika ili kukabiliana na changamoto zitokanazo na mabadiliko hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanaziathiri nchi za Afrika. Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa ameitisha Mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika jijini New York, Marekani mwezi Septemba 2019 ili kwa pamoja nchi zijadili namna ya kuendelea kutatua changamoto hizo.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mhe. Moussa Faki Mahamat ambao hushirikiana na Japan kuandaa mikutano ya TICAD, amesema kuwa, Mkutano wa Saba umekuja na suluhisho kwa vijana kuhusu masuala ya teknolojia na uvumbuzi na kusisistiza kwamba suala hilo ni la kipaumbele kwa nchi za Afrika.

Mkutano wa Saba wa TICAD ambao umebeba kaulimbiu ya Kuiendeleza Afrika kupitia Watu, Teknolojia na Uvumbuzi, umehudhuriwa na zaidi ya washiriki 4,000 pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi 44 za Afrika.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Yokohama, Japan.
28 Agosti 2019

WAZIRI MKUU ASHIRIKI TICAD7- YOKOHOMA,JAPAN

Waziri Mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim M. Majaliwa (Mb) akiwa kaaika Mkutano wa Kimataifa Tokyo kuhusu Maendeleo kwa Bara la Afrika. Nyuma yake ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb). Mkutano huo unafanyika Yokohama,Japan.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) akisaliqmiana na Waziri Mkuu wa Mauritius Mhe Pravind Jugnauth walipokutana na kufanya mazungumzo katika Mji wa Yokohoma Japan.


Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) akisikiliza jambo kutoka kwa Waziri Mkuu wa Mauritius Mhe Pravind Jugnauth. Viongozi wote wawili walikutana na kufanya mazungumzo ya namna ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kidiplomasia baina ya Nchi hizo. wote wapo katika Mji wa Yokohoma,Japan kushiriki mkutano wa TICAD7.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) akiwa na Waziri Mkuu wa Mauritius Mhe Pravind Jugnauth walipokutana na kufanya mazungumzo katika mji wa Yokohoma Japan. Kushoto kwa Mhe. Majaliwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof Palamagamba John Kabudi (Mb).

MHE. WAZIRI MKUU ATEMBELEA BANDA LA TANZANIA LA MAONESHO YA TICAD 7

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana akiangalia mojawapo ya bidhaa nchini Japan alipotembelea banda la maonesho ya vivutio vya utalii wa Tanzania jijini Yokohama, Japan tarehe 28 Agosti 2019.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana na Bi. Edda Magembe, Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini Japan alipotembelea banda la maonesho ya vivutio vya utalii wa Tanzania jijini Yokohama, Japan tarehe 28 Agosti 2019. Mhe. Waziri Mkuu yupo nchini Japan akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) utakaofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019. Maonesho hayo yanaenda sambamba na mkutano huo ambao umetoa fursa kwa nchi za Afrika kujitangaza kwenye masuala ya vivutio vya utalii, uwekezaji na biashara.
Mhe. Waziri Mkuu akisalimiana na mmoja wa washiriki kwenye banda la maonesho la Tanzania. Maonesho hayo yanafanyika sambamba na Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7)

Mhe. Waziri Mkuu akiangalia moja ya kipeperushi kuhusu maeneo ya vivutio vya utalii vilivyopo nchini alipotembelea banda la Tanzania kwenye Mkutano wa TICAD 7 unaofanyika jijini Yokohama, Japan
Mhe. Waziri Mkuu kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi wakiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa maonesho kwenye banda la Tanzania yanayoendelea sambamba na Mkutano wa Saba wa TICAD

Tuesday, August 27, 2019

WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JAPAN AWAANDALIA HAFLA MAALUM MAWAZIRI WANAOSHIRIKI MKUTANO WA SABA WA TICAD

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe.  Kono Taro akimkaribisha  Waziri wa Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi alipowasili kwenye Hoteli ya Royal Palace iliyopo jijini Yokohama kwa ajili ya kushiriki hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Mhe. Taro kwa heshima ya Mawaziri wanaoshiriki Mkutano wa  Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) unaofanyika nchini humo kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019.
Mhe. Taro akizungumza wakati wa hafla hiyo ambapo ameendelea kuwahakikishia  ushirikiano Mawaziri kutoka Afrika 
Mhe. Taro akizungumza huku Mawaziri wakimsikiliza
Mhe. Prof. Kabudi akiwa katika meza moja na Mhe. Taro na Mawaziri wengine kutoka nchi za Afrika wanaoshiriki Mkutano wa Saba wa TICAD
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na Waziri mwenzake wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa  na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan kwa heshima ya Mawaziri kutoka nchi za Afrika wanaoshiriki Mkutano wa Saba wa TICAD
Picha ya pamoja ya Mhe. Taro na Mawaziri kutoka nchi za Afrika wanaoshiriki Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) utakaofanyika Yokohama, Japan kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisalimiana na Mawaziri wenzake akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor (kulia) mara baada ya kumalizika kwa hafla maalum iliyoandaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Taro.

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, PROF. PALAMAGAMBA JOHN KABUDI ASHIRIKI MKUTANO WA MAWAZIRI WA TICAD JIJINI YOKOHAMA, JAPAN


Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe.Kono Taro (mwenye tai ya rangi ya chungwa) akifungua rasmi Mkutano wa Mawaziri wa maandalizi ya Mkutano wa Saba wa Kimataifa kuhusu Mandeleo ya Afrika (TICAD 7) . Ufunguzi huo umefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Pacifico jijini Yokohama, Japan  tarehe 27 Agosti 2019.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (wa tatu kushoto kwenye meza nyeupe) akifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa TICAD wa Mawaziri uliofanyika Yokohama, Japan tarehe 27 Agosti 2019

Mkutano ukiendelea

===========================================================


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MKUTANO WA MAWAZIRI WA MAANDALIZI YA MKUTANO WA SABA WA TOKYO KUHUSU MAENDELEO YA AFRIKA (TICAD 7) WAFANYIKA JIJINI YOKOHAMA, JAPAN

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi leo tarehe 27 Agosti 2019 ameshiriki Mkutano wa Mawaziri wa Maandalizi ya Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Pacifico jijini Yokohama, Japan.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine unatarajiwa kupitia na kupitisha rasimu ya Azimio la Yokohama na Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Azimio hilo litakalowasilishwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaoanza tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019 kwa ajili ya kuridhiwa.

Akifungungua mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Kono Taro amezipongeza nchi za Afrika kwa kupiga hatua katika maendeleo kupitia ushirikiano na Japan na kwamba nchi yake itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na nchi hizo ili kuziwezesha kufikia malengo ikiwemo mapinduzi ya viwanda.

Mhe. Taro alisema kuwa, ushirikiano kati ya Afrika na Japan kupitia mpango wa TICAD umeendelea kuimarika tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka 1993 na kwamba ni matarajio yake Mkutano wa Saba utakuwa wa tija zaidi kwa pande hizo mbili.

“Nawakaribisha Mawaziri wenzangu Yokohama ambapo maandalizi ya mkutano wa saba wa kimataifa wa Tokyo kuhusu maendeleo ya Afrika yanaendelea. Jukumu letu ni kupitia na kupitisha rasimu ya Azimio la Yokohama na Mpango kazi wake ili hatimaye litunufaishe sote pale litakapopitishwa na Wakuu wa nchi” alisema Mhe. Taro.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano huo, Mhe. Sameh Shoukry ameipongeza Japan kwa kuendelea kuandaa mikutano hiyo ambayo ina nia ya kuifikisha Afrika katika mapinduzi ya viwanda na kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana na umaskini.

Kwa upande wake, Naibu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ambao ni miongoni mwa waandaaji wa Mkutano wa Saba wa TICAD, Bw. Kwesi Quartey amesema kuwa, mkutano huo unafanyika wakati Umoja wa Afrika unaendelea kutekeleza agenda 2063. Agenda hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuziwezesha nchi za Afrika kufikia maendeleo ya hali ya juu kwenye sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, teknolojia na miundombinu.

Kadhalika Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za Kanda ya Afrika kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika, Bw. Lamin Manneh alisema kuwa ushirikiano kati ya Afrika na Japan kupitia TICAD umekuwa na mchango mkubwa kwenye maendeleo ya Bara la Afrika. Aliongeza kuwsema kuwa, Shirika lake ambalo linasimamia maendeleo linaridhishwa na ushirikiano uliopo kati ya Japan na Afrika ambao kwa kiasi kikubwa umefanikiwa.

Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Ushirikiano na Afrika pamoja na mambo mengine unatoa fursa ya kupanga mikakati ya ushirikiano na agenda za kimaendeleo zitakazotelezwa kati ya Japan na Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.

Agenda za mkutano wa mwaka huu zinalenga kujadili mageuzi ya kiuchumi na kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kukuza sekta na uvumbuzi. Pia kuimarisha usalama na ustahimilivu endelevu kwenye jamii pamoja na kuendeleza jitihada za kuimarisha amani na usalama barani Afrika. Agenda za Mkutano wa Saba zinaenda sambamba na agenda 2063 ya Umoja wa Afrika, Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa na maazimio mengine ya kimataifa kama Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa.

Mkutano huu ambao umewashirikisha Mawaziri kutoka nchi za Afrika, na wadau mbalimbali wa maendeleo unafanyika ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Yokohama, Japan.
27 Agosti 2019


Monday, August 26, 2019

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI PROF. PALAMAGAMBA JOHN KABUDI (MB) ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA ULIOPO TOKYO NCHINI JAPAN.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwasili katika Ubalozi wa Tanzania uliopo Tokyo,Japan. Katikati ni Kaimu Balozi wa Tanzania Nchini Japan Bw. John Kambona akifuatiwa na Bi. Edda Magembe Afisa Ubalozi. August 26,2019. 

Kaimu Balozi wa Tanzania Nchini Japan Bw. John Kambona (katikati) akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) mara baada ya kuwasili katika Ubalozi wa Tanzania uliopo Tokyo,Japna anayefuatia ni  Bi. Edda Magembe Afisa Ubalozi. August 26,2019.  
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akitoa maelekezo kwa Kaimu Balozi wa Tanzania Tokyo,Japan Bw. John Kambona akiwa na Afisa Ubalozi Bi. Edda Magembe. August 26,2019.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa anaingia katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania uliopo Tokyo,Japan. August 26,2019.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika moja ya Maktaba ya vitabu iliyopo katika Ubalozi wa Tanzania - Tokyo,Japan. August 26,2019.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akikagua aina  ya vitabu vilivyopo katika Maktaba ya Ubalozi wa Tanzania Nchini Japan. August,26,2019.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika ofisi ya Balozi wa Tanzania Nchini Japan. August 26,2019.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongoza kikao kazi cha ujumbe wa Tanzania uliopo Yakohama Nchini Japan kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika 2019 (TICAD7 YOKOHAMA 2019). August 26,2019.

Kaimu Balozi wa Tokyo - Japan Bw. John Kambona akiwa anatoa maelezo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) na baadhi ya ujumbe uliopo Yakohama, Japan kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika 2019 (TICAD7 YOKOHAMA 2019). August 26,2019.

Baadhi ya wajumbe waliopo Yakohama-Japan kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika 2019 (TICAD7 YOKOHAMA 2019) wakiwa katika kikao kazi cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi(hayupo Pichani). August 26,2019.

================================================================


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MKUTANO WA SABA WA TOKYO KUHUSU MAENDELEO YA AFRIKA (TICAD 7)

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amewasili jijini Yokohama, Japan tarehe 26 Agosti kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 7 wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD 7) utakaofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019.

Mkutano huu wa Saba utatanguliwa na kikao cha Maafisa Waandamizi wakiwemo Makatibu Wakuu na Mabalozi tarehe 25 na 26 Agosti 2019 ukifuatiwa na kikao cha Mawaziri tarehe 27 Agosti, 2019 na utahitimiswa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019. Kauli mbiu ya Mkutano huu ni “Kuendeleza Maendeleo ya Afrika kupitia Watu, Teknolojia na Uvumbuzi”.

Mkutano wa Saba pamoja na mambo mengine unatoa fursa ya kupanga mikakati ya ushirikiano na agenda za kimaendeleo zitakazotelezwa kati ya Japan na Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.

Agenda za mkutano wa mwaka huu zinalenga kujadili mageuzi ya kiuchumi na kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kukuza sekta na uvumbuzi. Pia kuimarisha usalama na ustahimilivu endelevu kwenye jamii pamoja na kuendeleza jitihada za kuimarisha amani na usalama barani Afrika. Agenda za Mkutano wa Saba zinaenda sambamba na agenda 2063 ya Umoja wa Afrika, Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa na maazimio mengine ya kimataifa kama Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa.

Kutokana na mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya kiuchumi barani Afrika, Mkutano wa TICAD 7 umeandaa ratiba maalum itakayozishirikisha taasisi binafsi na za umma kwenye majadiliano ya kibiashara yatakayofanyika tarehe 29 Agosti 2019. Lengo la majadiliano hayo ni kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Serikali wamiliki wa Kampuni, wafanyabiashara na wawekezaji ili kujadili kwa pamoja masuala mbalimbali ya kukuza baishara, uwekezaji na utalii kati ya Japan na Afrika.

Kadhalika  wakati wa mkutano wa saba nchi zote za Afrika zimepatiwa nafasi ya kushiriki katika shughuli mbalimbali kwa lengo la kutangaza fursa za biashara, uwekezaji na vivutio vya utalii za nchi husika. Tanzania kupitia Bodi ya Utalii (TTB) imejipanga kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini wakati wa mkutano huo.

Mkutano wa Saba wa TICAD utahitimishwa kwa Wakuu wa Nchi kupitisha Azimio la Yokohama na Mpango Kazi wa utekelezaji wa Azimio hilo. Serikali ya Japan ilianzisha jukwaa la majadiliano kati yake na nchi za Afrika mwaka 1993 kwa ajili ya kujadili maendeleo na nchi hizo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ataongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Yokohama, Japan.
26 Agosti 2019

Friday, August 23, 2019

Naibu Waziri Mhe.Dkt Damas Ndumbaro afanya mazungumzo na Mabalozi


Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (kulia) akiwa katika mazungumzo na Mhe.Yonas Yosef Sanbe Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania yaliyofanyika katika ofisi ndogo ya Wizara, jijini Dar es Salaam Agosti 23, 2019

Baloz Sanbe katika mazungumzo hayo ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuna kuganishwa Mkunao wa SADC HAPA
Mhe. Dkt Ndumbaro Naibu Waziri akiwa katika mazungumzo na Mhe. Balozi Sanbe walipokutana kwa mazungumzo.
Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (kulia) akimsikiliza Mhe. Mousa Farhang Balozi wa Iran nchini, walipokutana kwa mazungumzo ofisi ndogo za Wizara jiji Dar es Salaam.

 Katika mazungumzo yao, waliwili hao walijikita kujadili masuala mbalimbali ya kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili. 
Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (kulia) akisalimiana na  Mhe. Mousa Farhang Balozi wa Iran nchini Tanzania
Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (kulia) akimsikiliza Mhe. Abdelilah Benryane Balozi wa Morocco nchini Tanzania
Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati akifanya mazungumzo  na Balozi wa Morocco Mhe. Abdelilah Benryane
Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (kulia) akisalimia na Mhe. Abdelilah BenryaneBalozi wa Morocco

Wakati huohuo Mhe. Pro. Palamagamba Kabudi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania  Mhe. Wang Ke
Sehemu ya Wafanyakazi wa Ubalozi wa China wakifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea

Mhe. Pro. Palamagamba Kabudi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki akiwa katika mzungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania  Mhe. Wang Ke yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Agosti 23, 2019