17 Oktoba, 2019
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA 18 WA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA NCHI ZA AFRIKA NA NORDIC KUANZIA TAREHE 7-8 NOVEMBA 2019
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic (Norway, Denmark, Finland, Sweden na Iceland) unaotarajiwa kufanyika tarehe 08 Novemba 2019 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.Hii ni mara ya kwanza kwa mkutano huu kufanyika hapa nchini tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000.
Mkutano huu unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki takribani 250 ambao kati yao thelathini na nne (34) ni Mawaziri wa Mambo ya Nje akiwemo Mhe. Prof. Palamagamba J.A.M. Kabudi (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kadhalika, Mabalozi wa nchi shiriki za Afrika katika nchi za Nordic, Mabalozi wa nchi za Nordic hapa nchini, watendaji kutoka Wizara za Mambo ya Nje za nchi shiriki, wawakilishi wa taasisi za biashara na uwekezaji na Wafanyabiashara za hapa nchini wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huu.
Lengo la kuanzishwa kwa mkutano huu, ambao kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka 2000, ilikuwa ni kutoa nafasi kwa nchi za Nordic na nchi chache za Afrika marafiki zao wa karibu, kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili, kuainisha vipaumbele katika ushirikiano huo na kuweka mikakati ya pamoja ya kutekeleza vipaumbele hivyo. Nchi za Afrika na Nordic zimekuwa zikipokezana uenyeji wa mikutano hii kila mwaka. Mwaka 2017, mkutano huu ulifanyika Abuja, Nigeria na mwaka 2018 ulifanyika Copenhagen, Denmark na mwaka huu, utafanyika Tanzania.
Kwa mwaka huu, mkutano huu utajadili namna ya kuimarisha mahusiano yenye tija kwa maendeleo ya nchi washiriki hususan namna ya kukuza ushirikiano kwenye sekta ya biashara na uwekezaji kwa maendeleo endelevu. Aidha, ushirikiano kwenye masuala ya ulinzi na usalama unatarajiwa kupewa kipaumbele kwenye mkutano huu ikizingatiwa kuwa utekelezaji wa shughuli za maendeleo unategemea uwepo wa amani na usalama.
Tanzania ni nchi ya kipaumbele kwa nchi za Nordic. Ushirikiano kati ya Tanzania na nchi za Nordic ulianza hata kabla ya uhuru wa Tanganyika ambapo wamisionari kutoka nchi hizo walikuja kufanya kazi hapa nchini kwenye sekta za afya na elimu. Katika sekta ya elimu, nchi hizo zilianzisha Kituo cha Kilimo cha Uyole na Kituo cha Elimu cha Kibaha kupitia Mradi wa Nordic-Tanganyika Project. Ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na nchi za Nordic ulichangiwa kwa kiwango kikubwa na falsafa zilizokuwa zinafanana kuhusu maendeleo ya watu, ukombozi wa Afrika, urafiki miongoni mwa viongozi wetu na nafasi ya kimkakati ya Tanzania katika Bara la Afrika.
Hadi sasa, Tanzania ni nchi pekee iliyopokea msaada mkubwa kifedha kutoka katika nchi za Nordic. Kuanzia mwaka 2013 hadi 2019, Tanzania imepokea takribani shilingi za kitanzania bilioni 900 kutoka kwa nchi za Nordic. Nchi hizo zimekuwa zikisaidia sekta mbalimbali hapa nchini ikiwemo: elimu; afya; miundombinu; nishati; TEHAMA; utafiti; ukusanyaji wa kodi; bajeti; misitu; usawa wa jinsia; hali ya hewa; na ukuzaji wa sekta ya biashara. Kufuatia ushirikiano huu wa kihistoria kati ya Tanzania na nchi za Nordic, nchi hizo ziliiomba Serikali ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu na Serikali kuridhia kwa minajili ya kuendelea kuboresha ushirikiano kati ya pande hizi mbili kwa manufaa ya pande zote.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam.