Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na Balozi Mteule wa Rwanda nchini, Meja Jenerali Karamba Charles jijini Dar es Salaam.
|
Prof. Kabudi akutana, kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Balozi Manfredo Fanti.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam ambapo Waziri Kabudi amemueleza Balozi Fanti kuwa Uhusiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya ni wa Muda mrefu tangu mwaka 1975 ambao hadi sasa Tanzania imekuwa na mahusiano imara na umoja huo.
"Ushirikiano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya umelenga kupunguza umasikini, kukuza maendeleo endelevu, na kusaidia ujumuishaji wa Tanzania katika uchumi wa dunia, mpango kazi wa ushirikiano huu unaundwa na nguzo kuu tatu ambazo ni maendeleo ya uchumi, biashara na uwekezaji pamoja na mazungumzo ya kisiasa. Msaada wa Umoja wa Ulaya umeweza kushughulikia changamoto mbalimbali katika ajenda za maendeleo ya kitaifa" Alisema Prof. Kabudi
Waziri Kabudi ameongeza kuwa, kulingana na takwimu za mwaka 2017, Umoja wa Ulaya unaonekana ndiye mshirika mkubwa zaidi wa biashara ya bidhaa kwa Tanzania baada ya India, kwa asilimia 13.1. Bidhaa zinazoingizwa kutoka Umoja wa Ulaya ni pamoja na mashine, vifaa, bidhaa za kemikali na vifaa vya usafirishaji.
Prof. Kabudi amegusia pia mazungumzo ya kisiasa na kueleza kuwa ni nguzo muhimu ya uhusiano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya. Mazungumzo ya kisiasa yanalenga kuongeza uwazi na umoja ili kukuza uelewa wa pamoja katika vyama vya siasa.
Balozi mteule wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Balozi Manfredo Fanti amesema kuwa Umoja huo upo tayari kusaidia Tanzania na kuhakikisha kuwa sera za nchi zinasonga mbele ili kuiwezesha Tanzania kuwa na maendeleo endelevu na kusaidia malengo ya nchi.
"Pia tupo tayari kuhakikisha kuwa uwekezaji na biashara unaofanywa kati ya Umoja wa Ulaya pamoja na Tanzania unakuwa wa manufaa kwa pande zote lengo likiwa ni kukuza sekta ya biashara hapa Tanzania" Balozi Fanti
Katika tukio jingine Waziri wa Mamno ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mteule wa Rwanda hapa nchini, Meja Jenerali Karamba Charles ambaye ameelezea uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Rwanda ni wa kiwango cha juu na kuongeza kuwa jukumu lake kubwa kwa sasa ni kuongeza kiwango cha biashara na uswekezaji kati ya Nchi hizo mbili.
Meja Jenerali Karamba Charles ameyasema hayo wakati akikabidhi nakala za hati ya utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) kuchukua nafasi ya aliyekuwa Balozi wa Rwanda Nchini Tanzania Balozi Eugene Kayihura ambaye amemaliza muda wake.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar Es Salaam,Tanzania
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.