11 Oktoba 2019,
Dodoma
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Madereva wa taxi kutoka Uingereza wapanda Mlima Kilimanjaro
Timu ya madereva taxi watano kutoka Uingereza
ilifanya ziara nchini kuanzia tarehe 28 Septemba hadi 10 Oktoba 2019. Ziara
hiyo iliratibiwa na Wizara kupitia Ubalozi wetu London kwa kushirikiana na TTB.
Timu hiyo ilikuja nchini kwa ajili ya kupanda mlima Kilimanjaro ikiwa ni zoezi
la hisani ili kuchangisha fedha kwa ajili ya maveterani wa kijeshi (military
veterans) huko Uingereza.
Katika kutambua uamuzi mzuri wa timu hiyo kuuchagua
mlima Kilimanjaro kwa zoezi hilo la hisani na kwa malengo ya kunufaika na ujio
wao katika kutangaza vivutio vyetu vya utalii nchini Uingereza, Wizara ya Mambo
ya Nje kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iliwaandalia timu hiyo
ziara ya kutembelea vivutio vya utalii mbalimbali hapa nchini zikiwemo mbuga za
wanyama za Serengeti, Ngorongoro na Tarangire.
Vilevile, Timu hiyo ya madereva taxi baada ya
kumaliza kutembelea vivutio vilivyotajwa hapo juu walitangazwa kuwa mabalozi wa
hiari wa utalii (tourism goodwill
ambassadors) wa Tanzania kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vya hapa
nchini wawapo katika shughuli zao huko Uingereza. Hafla ya kuwatangaza
ilifanyika Hotel ya Mount Meru Arusha. Baada ya kutangazwa kuwa mabalozi wa hiari,
walisaini Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya timu hiyo na TTB tayari kwa
kutekeleza majukumu yao.
Tukio hilo lilihudhuliwa na Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki, akimuwakilisha Mhe. Dkt.
Hamisi Kigwangallah (Mb), Waziri wa Maliasili na Utalii na Mkuu wa mkoa wa
Arusha Mhe. Mrisho Gambo. Aidha, Mgeni Rasmi katika shughuli hiyo alikuwa Balozi
wa Uingereza hapa nchini, Mhe. Sarah Cooke.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki,
|
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mrisho Gambo akitoa neno katika hafla ya uwekaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Timu ya Madereva wa taxi watano kutoka Uingereza. Makubaliano hayo yalihusu timu ya madereva wa Uingereza kuwa Mabalozi wa hiari wa kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania nchini Uingereza. |
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.