12 Oktoba 2019, Arusha.
Mkutano wa 30 wa Baraza la
kisekta la Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango
umemalizika tarehe 12 Oktoba 2019 kwenye Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki, Jijini Arusha - Tanzania. Mkutano huu wa siku sita (06) umefanyika
katika Ngazi zifuatazo:
- Mkutano
katika Ngazi ya Maafisa Waandamizi tarehe 7 na 8 Oktoba, 2019;
- Mkutano
katika Ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 9 na 10 Oktoba 2019 na
- Mkutano
katika Ngazi ya Mawaziri tarehe 11 na 12 Oktoba 2019.
Ujumbe wa Tanzania katika
mkutano huu umeongozwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas D. Ndumbaro (Mb) akisaidiana na Waziri wa
Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent L. Bashungwa (Mb); Waziri
wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Augustine P. Mahiga (Mb); Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaju (Mb); Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mary Mwanjelwa
pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Mkutano huu umetoa maamuzi na
maelekezo mbalimbali ya kisera na kimkakati kwa Nchi Wanachama pamoja na
Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Utekelezaji wa
maamuzi na maelekezo ya mikutano ya Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki iliyopita pamoja na mkutano wa 10 hadi 28
wa Baraza la kisekta la Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya
Afrika Mashariki na Mipango; Utekelezaji wa Soko la pamoja la Afrika Mashariki; Utekeleaji
wa maagizo katika taarifa ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (2000 –
2017); Vipaumbele vya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwaka 2020/21; Maelekezo
kuhusiana na mikutano ya Wakuu wa taasisi za masuala ya Uhamiaji na Kazi za
Jumuiya, na maagizo ya hadidu za rejea za maandalizi ya mkakati wa mpango wa
sita wa maendeleo ya Afrika Mashariki (2021/22).
Aidha, mkutano huu ulitoa mapendekezo katika taarifa
ya hali ya ulipaji wa michango ya Nchi Wanachama katika Jumuiya; Taarifa ya uhamasishaji
katika masuala ya rasilimali za jumuiya ya Afrika Mashariki na mikakati ya
ushirikiano; Taarifa ya Tume ya Ukaguzi ya Jumuiya kwa mwaka 2017/18; Taarifa
ya maendeleo ya makubaliano ya maeneo huru ya biashara katika utatu wa
COMESA-EAC-SADC;Taarifa ya maendeleo ya makubaliano kuhusu eneo huru la
kibiashara barani Afrika (AFCFTA); Taarifa ya maendeleo ya masuala ya kisiasa,
na Kalenda ya majukumu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha mwezi
Julai hadi Desemba 2019.
Vilevile, wajumbe wa mkutano wamejadili
kuhusiana na maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa jumuiya
ya Afrika Mashariki mwaka 2000, baada ya kuvunjika kwa jumuiya ya awali
iliyoundwa mwaka 1967 na kuvunjika mwaka 1977.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.