Thursday, October 10, 2019

                                         TAARIFA KWA UMMA

UJIO WA WATALII ZAIDI YA 1000 KUTOKA ISRAEL

Tanzania inatarajia kupokea watalii zaidi ya 1000 kutoka nchini Israel ambao wanakuja nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii mwezi huu wa Oktoba.

Kundi la kwanza lililokuwa na zaidi ya watalii 200 liliwasili nchini kuanzia tarehe 05 Oktoba na kundi la pili lenye zaidi ya watalii 520 linatarajiwa kuwasili nchini tarehe 12 na kundi la tatu lenye watalii zaidi ya 200 litawasili nchini tarehe 13 Oktoba kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Watalii wengine zaidi wanatarajiwa kuwasili nchini mwezi huu baada ya Makampuni ya Uwakala wa Utalii kukamilisha taratibu za safari zao.

Watalii hao wanatarajiwa kutembelea Visiwa vya Zanzibar, Hifadhi za Taifa za Serengeti, Tarangire na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Ujio wa watalii hao unatokana na jitihada za kuitangaza nchi zinazofanywa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Israel kwa kushirikiana na wadau wa utalii  wa ndani na nje ya nchi.

Tanzania imejipanga kuwapokea na kuwatembeza watalii hao katika vivutio vya utalii vilivyoko nchini. Serikali inawakaribisha watalii hao kutembelea vivutio hivyo vya utalii ambavyo nchi imebarikiwa kuwa navyo ili wakawe mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania nchini kwao na kwingine watakakokwenda.

Imetolewa na:

Dkt. Faraji K. Mnyepe
Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
DODOMA

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.