Baadhi
ya ujumbe wa Diaspora ukiwa umesimama wakati wa kuimba wimbo wa taifa wa
Tanzania katika kongamano la sita la Diaspora lililofanyika Zanzibar
Na
Nelson Kessy, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, amewahakikishia wanadiaspora
kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itasimamia na kuhakikisha kuwa sheria ya
Diaspora inakamilika kabla ya mwezi Mei, 2020.
Rais Dkt. Shein ametoa
kauli hiyo leo mjini Zanzibar wakati alipokuwa akifungua rasmi kongamano la
sita la Diaspora ambalo limeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi-Zanzibar. Dhamira ya kongamano hili kuendeleza
ushirikiano uliopangwa na Diaspora na wawekezaji kama wadau wa maendeleo nchini
chini ya kauli mbiu ya "mtu kwao ndio ngao".
Ndugu wanadiaspora mwaka
jana nilieleza jitihada za kuanziasha ofisi za Diaspora hapa Zanzibar kwa
kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati ule kwa
kuanziasha Diaspora.
"Kutokana na kutambua
umuhimu wa watanzania waishio nje ya nchi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania iliunda idara maalumu ya kushughulikia masuala ya Diaspora katika
wizara ya Mambo ya nje mwaka 2010 ili kuvitekeleza kwa vitendo azma yetu ya
kuwashirikisha wanadiaspora Tanzania katika kuendeleza nchi yetu," Amesema Dkt. Shein
Ameongeza kuwa kwa umuhimu
huohuo, na kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya ccm ya mwaka 2010 na kuyapa
nguvu masuala ya Diaspora tulianzisha kitengo cha Diapora na baadae idara ya
Diaspora ilinzishwa hapa Zanzibar. Tulitengeneza
sera maalumu ya wanadiaspora, na sasa tupo mbioni kuanzisha sheria ya Diaspora,
nimefurahi kuwa rasimu ya sheria hiyo imefikia katika hatua nzuri.
"Kwa matiki hiyo
basi, namuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Issa Haji Ussi Gavu kuhakikisha
anasimamia kwa karibu sana utayarishaji na kukamilika kwa rasimu ya sheria hiyo
na iwasilishwe kwenye Baraza la wawakilishi kabla ya mwezi mei 2020,"
Amesema Dkt. Shein na kuongeza kuwa atahakikisha kuwa kabla ya kumaliza muda
wangu wa Urais hapa Zanzibar sheria hiyo
itakuwa imekaa vizuri kimkakati, kisera pamoja na kisheria kwa upande wa
Zanzibar.
Aidha, Rais Shein,
aliwapongeza wanadiaspora kwa michango yao ambayo wamekuwa wakiitoa kwa
kusaidia Serikali, pamoja na mambo mengine michango hiyo imekuwa ikisaidia
kijamiii na kiuchumi.
Awali akitoa salamu za
wanadiaspora, Mwenyekiti wa wanadiaspora, Norman Jasson alisema kuwa mchakato
wa sera ya Diaspora umekuwa ni wa muda mrefu na kumekuwepo na ukimya takribani
miaka mitatu na kumuomba Rais Dkt. Shein kuwasaidia kusimamia zoezi hilo.
"Sera ya Diaspora ina
umuhimu wa kipekee kwani tunaamini kuwa sera hiyo itakapokamilika itatoa majibu
ya maswali mengi ambayo yamekuwa yakitunyima usingizi. Tunaamini sera hii
itasaidia sio tu masuala ya uraia wan chi mbili au hadhi maalum, bali pia
masuala mengine kama umiliki wa ardhi, mirathi, ndoa kwa wenyeji na wageni,
ruhusa ya makazi nchini kupitia vibali au visa na mengine mengi," amesema
Bwn. Jasson
Aliongeza kuwa, pia
wanadiaspora wanaamini kuwa sera hiyo itarahisisha utungaji wa sheria
itakayowatambua watanzania wote walio ughaibuni bila kujali kama tayari
wameshachukua uraia wa nchi nyingine au kama tayari wana vibali vya makazi
katika nchi wanazoishi na pia bila kujaliwaliingiaje ughaibuni katika kusaka
maisha.
Bwana Jasson aliongeza
kuwa, msingi wa wanadiaspora ni utanzania wao na utayari wa kushiriki katika
jitihada za kusuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii kama vile kuhamasisha
wawekezaji kuja kuwekeza nchini ambapo kwa sasa TDC-Global tayari imewaleta Tanzania
watu wenye nia ya kuwekeza.
"Serikali ya Jamhuri
ya Muungano ya Tanzania kwa kushirikiana na Diaspora itafanikisha mambo mengi
kwa kuanzisha mkakati wa wa kuhakikisha kuwa watanzania waishio nje ya nchi
wanatayarishiwa mfumo ambao utasaidia kukusanya michango ya kwa ajili ya miradi
mbalimbali ya maendeleo," amesema Bwn. Jasson.
Kwa upande wake, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, George Simbachawene
akitoa shukrani kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.
Shein amesema kuwa sera ya Diaspora kwa upande wa Tanzania rasimu ya kwanza
tayari imekamilika na hatua inayofuata ni kuwashirikisha wadau mbalimbali
wakiwemo wanadiaspora wenyewe kupitia balozi zetu ili na wao waweze kutoa
mawazo yao.
"Mhe. Rais, kwa sasa
sera ipo katika hatua nzuri, jitihada kubwa zinaendelea na jambo hili
linahitaji kushughulikiwa kwa uangalifu mkubwa kwa sababu ya historia ya nchi
yetu," Amesema Simbachawene.
Aidha, Waziri Simbachawene
aliongeza kuwa ni muhimu kutumia wanadiaspora kama fursa, sekta muhimu katika ujenzi
wa uchumi wa taifa letu na mataifa mengi dunini yanafanya hivyo.
Pamoja na mambo mengine,
kongamano hili la sita la Diaspora limejadili mada saba ambazo ni urejeshaji wa
taka za plastiki, Tanzania na uwekezaji, Diaspora na uwekezaji, Mradi wa nyumba
za bei nafuu, kilimo cha kisasa, kubadili mfumo wa utalii wa Zanzibar pamoja na
Mradi wa daraja la Zanzibar - Tanzania bara.
Mwezi Augusti, 2018 watanzania
waishio ughaibuni (Diaspora) walikutana Chake Chake, kisiwani Pemba katika
kongamano la tano la Diaspora kufuatia
utaratibu uliowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kuwakutanisha kila mwaka
Watanzania waishio ughaibuni.
|