Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi,
Mhe. Irene Kasyanju amemnadi mgombea wa Tanzania anayewania nafasi ya ujumbe
kwenye Kamati ya Ushauri ya Mfuko wa Pamoja wa Mazao Duniani (Common Fund for
Commodities – CFC) alipotembelea Ofisi za Mfuko huo zilizoko mjini Amsterdam,
Uholanzi tarehe 02 Septemba, 2020.
Balozi Kasyanju alikwenda CFC kufanya
mazungumzo na pia kumpongeza rasmi Mkurugenzi Mwendeshaji wa CFC, Mhe.
Balozi Sheikh Mohammed Belal kwa kushika nafasi ya kuiongoza CFC kwa
kipindi cha miaka minne, kazi aliyoianza rasmi mwezi Aprili 2020 baada ya
kuchaguliwa kwa kauli moja kushika wadhifa huo wakati wa Mkutano Mkuu wa 31 wa
Baraza la Uongozi la CFC uliofanyika tarehe 04 Desemba 2019. Katika mazungumzo
yao Balozi Kasyanju alimhakikishia Mwenyeji wake huyo ushirikiano wa Tanzania kwa
Taasisi yake na kutoa shukrani za dhati kufuatia mikopo yenye riba nafuu
iliyotolewa kwa ajili ya kuboresha miradi mitatu inayoendelea hivi sasa nchini
Tanzania.
Balozi Kasyanju aliitumia fursa hiyo
sawia kumnadi mgombea wa Tanzania, Dkt. Jacqueline David Mkindi, ambaye
ni Mkurugenzi Mtendaji wa “Tanzania Horticultural Association (TAHA)” iliyoko
mjini Arusha. Balozi Kasyanju alimuelezea Dkt. Mkindi kuwa ni kiongozi mahiri
na mchapa kazi na akadhihirisha kwamba endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo
ataiwakilisha vema Tanzania kwa kuwa mshauri bora na makini kwa CFC na Nchi
zote Wanachama wa CFC na hivyo kuleta mwamko mpya kwenye Taasisi hiyo muhimu.
CFC iliundwa mwaka
1989 kwa mujibu wa taratibu za Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuboresha na
kuleta maendeleo kwa jamii ya wakulima na wazalishaji wa bidhaa katika Nchi
Zinazoendelea. Hivyo basi, CFC imejikita katika kutoa ufadhili wa mikopo kwa
ajili ya miradi ya maendeleo kwa kutumia rasilimali zake zinazotokana na
michango ya hiari ya Nchi Wanachama na Wafadhili.
Tanzania ni Mwanachama hai wa CFC na katika
Taasisi hii inawakilishwa kwenye Baraza lake la Uongozi na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Viwanda na Biashara, kama Gavana; na Balozi wa Tanzania Nchini
Uholanzi ambaye ni Gavana Msaidizi. Aidha, Tanzania imewahi kushika nafasi ya
Mkurugenzi Mwendeshaji wa CFC na vile vile mjumbe wa Kamati ya Ushauri ya CFC
zaidi ya miaka 10 iliyopita. Hivyo, ni wakati mwingine muafaka kwa Tanzania
kushika nafasi kwenye CFC hasa baada ya kutambua kwamba Mkurugenzi Mwendeshaji
huyu mpya ameingia na nguvu mpya za kuleta mageuzi kwenye Taasisi yake na
kuifanya iwe yenye tija zaidi kwa Wanachama wake.
Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju akipokea
Taarifa ya Mwaka 2019 ya Mfuko wa Pamoja wa Mazao Duniani (Common Fund for Commodities – CFC) kutoka kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa CFC, Mhe.
Balozi Sheikh Mohammed Belal, baada ya mazungumzo yao.
Balozi Irene Kasyanju akimkabidhi
Mhe. Balozi Belal vipeperushi na majarida 20 yanayotangaza Utalii wa Tanzania
yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza na Kidachi kwa ajili ya kusambazwa kwa
wadau.
Balozi Irene Kasyanju na Mhe. Balozi
Belal wakiwa pamoja na wasaidizi wao Bi. Linda Mkony (kushoto), Mtumishi wa
Ubalozi; na kulia ni Bw.Hector Besong, CFC Portfolio and Risk Manager.