Thursday, June 24, 2021

MAKATIBU WAKUU WA SEKTA YA KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA WA EAC WAKUTANA JIJINI ARUSHA

Mkutano wa 14 Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Ngazi ya Makatibu Wakuu umefanyika leo tarehe 24 Juni 2021  jijini Arusha ikiwa ni maandalizi ya mwisho kuelekea Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika jijini hapa tarehe 25 Juni 2021.

 

Lengo la Mkutano wa 14 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Kilimo  na Usalama wa Chakula pamoja na mambo mengine ni kupitia na kujadili utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Baraza la Mawaziri wa Jumuiya pamoja na kupitia na kujadili masuala mbalimbali  muhimu ya kisera, kimkakati, miradi na program zinazotekelezwa katika sekta ya kilimo.

 

Katika Mkutano wao, Makatibu Wakuu, pamoja na mambo mengine wamepokea na kupjadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwao na Wataalam ikiwemo, Taarifa ya Usalama wa Chakula ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu Mradi wa Afrika wa Kilimo cha Ushindani cha Mpunga kwa Kanda ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu Maendeleo ya Mifugo; Taarifa kuhusu Mradi wa Kuzuia na Kudhibiti Sumukuvu; Taarifa kuhusu Maendeleo ya Uvuvi; na Taarifa kuhusu Uhamasishaji wa Uchangiaji Rasilimali.

 

Awali akifungua Mkutano huo, Mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ushirika wa Kenya, Prof. Hamadi Iddi Boga ametoa rai kwa wajumbe wa mkutano huo kuendelea kushirikiana katika kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo kwenye jumuiya  ili kujihakikishia usalama wa chakula.   

 

Amesema kuwa changamoto nyingi za kilimo zinazozikabili nchi wanachama  zinafanana hivyo ni vizuri nchi zote zikajikita kufanyia kazi changamoto hizo pamoja na kutekeleza program na maazimio yanayofikiwa kwenye mikutano mbalimbali ili hatimaye kuboresha sekta ya kilimo na usalama wa chakula ambayo ni muhimu kwa ustawi wa wananchi.

“Nawashukuru sana kwa kuja na kushiriki kwenye mkutano huu muhimu. Naelewa kwamba usalama wa chakula ni jukumu letu sote kama nchi wanachama na kwa vile tunapitia changamoto zinazofanana ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na corona ni vizuri tukaja na mbinu za pamoja kuzikabili changamoto hizo na kuendeleza sekta hii muhimu ya kilimo” alisema Prof. Boga.

 

Katika hotuba yake ililiyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Sekta za Uzalishaji katika Sekretarieti, Bw. Jean Havugimana,  Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughilikia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo amewashauri wafanyabiashara wa mazao ya kilimo katika Nchi Wanachama kushirikiana na mamlaka zinazosimamia usalama wa chakula na viwango ili kupata ushauri wa kitaalam kwa ajili ya kuzalisha bidhaa salama na zenye ushindani katika soko. Kadhalika ameshauri elimu kuhusu kilimo itiliwe mkazo kwa nchi wanachama ili kuzalisha wataalam wengi kwenye sekta hii na pia kukuza ajira kwa vijana ambao ni kundi kubwa zaidi katika nchi wanachama.

 

Kwa upande wake, mwenyeji wa Mkutano huo ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo wa Tanzania, Dkt. Andrew Massawe amewakaribisha na kuwashukuru wajumbe waliosafiri kutoka kwenye nchi zao hadi jijini Arusha licha ya changamoto ya ugonjwa wa Corona  na kuwatakia mkutano mwema na wenye manufaa kwa wananchi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Ngazi ya Makatibu Wakuu umeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Andrew Massawe na kuhudhuriwa pia na Katibu Mkuu  wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatama pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Sekta mbalimbali zinazojishughulisha na masuala ya kilimo na usalama wa chakula hapa nchini. 


Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Andrew Massawe (kushoto) akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Arusha tarehe 24 Juni 2021 kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa 14 wa Baraza la Kiseikta la Mawaziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika jijini hapa tarehe 25 Juni 2021.  Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatama.

Mwenyekiti wa Mkutano wa Makatibu Wakuu ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ushirika wa Kenya, Prof. Hamadi Iddi Boga akifungua Mkutano huo uliofanyika jijini Arusha tarehe 24 Juni 2021 kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya Mkutano wa 14 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 25 Juni 2021.

Mkurugenzi wa Sekta ya Uzalishaji katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Jean Havugimana akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo wakati wa Mkutano wa Makatibu Wakuu

Sehemu ya ujumbe wa Kenya ukishiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Andrew Massawe akiwa kwenye Mkutano wa Makatibu Wakuu. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatama na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu Tanzania, Bw. Partick Ngwediadi

Kiongozi wa ujumbe wa Burundi kama anavyoonekana puchani

Sehemu ya ujumbe wa sekretarieti katika mkutano

Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Benjamin Mwesiga akishiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu pamoja na Bibi Jackline Mpuya kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa.

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania wakishiriki mkutano wa Makatibu Wakuu wanaoshughulikia sekt aya kilimo na usalama wa chakula

Ujumbe wa Tanzania wakiwa kwenye mkutano

Mkutano ukiendelea

Wajumbe wakifuatilia matukio mbalimbli kwenye Mkutano

Wajumbe kutoka Sekta za kilimo na usalama wa chakula wakishiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu 

Mkutano ukiendelea

Wadau wa kilimo wakiwa kwenye mkutano 

Mkutano ukiendelea

 

Wednesday, June 23, 2021

BALOZI MBAROUK AKUTANA NA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA POLAND

 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (katikati) akisalimiana na Naibu Waziri Mambo ya Nje wa Poland anayeshughulikia na masuala ya Siasa, Uchumi na Maendeleo kwa nchi za Afrika Mhe.Pawel Jablonski alipowasili ofisini kwake jijini Dodoma

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (katikati)  akiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje wa Poland anayeshughulikia na masuala ya Siasa, Uchumi na Maendeleo kwa nchi za Afrika Mhe.Pawel Jablonski (kushoto) wakizungumza kulia ni  Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Mhe. Dkt. Abdallah Possi .

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na Naibu Waziri Mambo ya Nje wa Poland anayeshughulikia na masuala ya Siasa, Uchumi na Maendeleo kwa nchi za Afrika Mhe.Pawel Jablonski walipokutana kwa  mazungumzo ofisini kwake jijini Dodoma

Naibu Waziri Mambo ya Nje wa Poland anayeshughulikia na masuala ya Siasa, Uchumi na Maendeleo kwa nchi za Afrika Mhe.Pawel Jablonski akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk walipokutana kwa mazungumzo ofisini kwake jijini Dodoma

Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Mhe. Dkt. Abdallah Possi (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ulaya na Amerika Bw. Hassan Mwamwetta waifuatilia mazungumzo kati ya Mawaziri hao.

Naibu Waziri Mambo ya Nje wa Poland anayeshughulikia na masuala ya Siasa, Uchumi na Maendeleo kwa nchi za Afrika Mhe.Pawel Jablonski akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk walipokutana kwa mazungumzo ofisini kwake jijini Dodoma. Kulia kwa Mhe. Waziri Mbarouk wakishuhudia massikilizo hayo ni Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Mhe. Dkt. Abdallah Possi na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ulaya na Amerika Bw. Hassan Mwamwetta.




Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mambo ya Nje wa Poland anayeshughulikia na masuala ya Siasa, Uchumi na Maendeleo kwa nchi za Afrika Mhe.Pawel Jablonski ofisini kwake jijini Dodoma.

Akiongelea kikao hicho Balozi Mbarouk amesema kuwa wamejadiliana juu ya kuimarisha mahusiano yaaliyopo kati ya Tanzania na Poland ikiwa ni pamoja na kuanzisha uwekezaji mpya nchini, kuwezesha wanafunzi na wataalamu wetuu kujifunza na kupata utaalmu hasa katika matibabu ya moyo, masikio, pua na Koo.

“Tumekutana hapa na Mhe Naibu Waziri kutoka nchini Poland, tumezungumza na kujadliana juu ya namna bora za kuendelea kuimarisha mahusiano baina ya nchi zetu , tuna maeneo mengi ambayo tunashirikiana baina ya nchi zetu, lakini pia nimewaomba kuanzisha uwekezaji mpya nchini, ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi za masomo kwa ameneo ya matibabu ya moyo, masikio,pua na koo”, amesema Balozi Mbarouk.

Amesema kuwa wamejadiliana juu ya kuhakikisha ujenzi wa Kiwanda cha matrekta cha Kibaha na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia nafaka na kuongeza kuwa ujio wa Naibu Waziri huyo utawezesha kukwamua miradi hiyo na hivyo kuikamilisha kama ilivyopangwa

Akizungumza katika kikao hicho Naibu Waziri huyo ameelezea utayari wa Poland katika kuhakikisha mahusiano kati ya Poland na Tanzania yanaimarika na kuendelea kuisaidia Tanzania katika sekta za elimu, kilimo hasa ikizingatiwa kuwa Poland imeendelea kwa kiasi kikubwa kupitia kilimo.

Amesema Poland iko tayari kuisaidia Tanzania kaatika maeneo ya elimu kwa kutoa nafasi za masomo nchin Poland ikiwa ni pamoja na ufadhili kwa wanafunzii wa Kitanzania, uwepo wa mifumo ya kisasa ya kutolea maji taka, kilimo na maendeleo ya usalama wa chakula.

Naibu Waziri huyo. Mhe. Powel yuko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku nne ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Dkt. Abdallah Possi pamoja na Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka nchni Poland waliobobea katika maeneo ya teknolojia ya kisasa katika sekta za kibenki (smart teknologies) teknolojia ya kisasa katika sekta ya umeme (smart technologies for electricity sector -smart meter connection and lighting systems) na ulipaji kwa kutumia teknolojia za kisasa (smart payment apps).

Naibu Waziri huyo na timu wanatarajia kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Shirika la Umeme nchii (TANESCO) Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Benki za CRDB na NMB na Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF).



Ziara ya naaibu Waziri huyo imefuatia mwaliko uliotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Idara ya Ulaya na Marekani




NAIBU WAZIRI MAMBO YA NJE WA POLAND MHE.PAWEL JABLONSKI AWASILI JIJINI DODOMA




Naibu Waziri Mambo ya Nje wa Poland anayehusika na masuala ya Siasa, Uchumi na Maendeleo kwa nchi za Afrika Mhe.Pawel Jablonski awasili jijini Dodoma kwa ziara ya kikazi.



Naibu Waziri Mambo ya Nje wa Poland anayehusika na masuala ya Siasa, Uchumi na Maendeleo kwa nchi za Afrika Mhe.Pawel Jablonski akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumaani Mhe. Dkt. Abdallaah Possi katika uwanja wa ndege jijini Dodoma.

Naibu Waziri Mambo ya Nje wa Poland anayehusika na masuala ya Siasa, Uchumi na Maendeleo kwa nchi za Afrika Mhe.Pawel Jablonski akiwa na Balozi wa Poland nchini Mhe. Krzysztof Buzalski

Ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchii Poland ulioambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia Naibu Waziri Mambo ya Nje wa Poland anayehusika na masuala ya Siasa, Uchumi na Maendeleo kwa nchi za Afrika ambaye yuko nchni kwa ziara ya kikazi kufuatiaa mwaliko wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  



Naibu Waziri Mambo ya Nje wa Poland anayehusika na masuala ya Siasa, Uchumi na Maendeleo kwa nchi za Afrika Mhe.Pawel Jablonski awasili jijini Dodoma kwa ziara ya kikazi.

Mhe. Powel  ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Dkt. Abdallah Possi pamoja na Balozi wa Poland hapa nchini Mhe. Krzysztof Buzalski. 

Naibu Waziri huyo atakutana na kufanya mazungumzo ya pamoja na watendaji wa Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maji, Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Uwekezaji, Kilimo na Fedha na Mipango hapa jijini Dodoma. 

Naibu Waziri huyo ameambatana na timu ya wawekezaji na wafanyabiashara  waliobobea katika maeneo ya teknolojia ya kisasa katika sekta za kibenki (smart teknologies) teknolojia ya kisasa katika sekta ya umeme (smart technologies for electricity sector -smart meter connection and lighting systems) na ulipaji kwa kutumia teknolojia za kisasa ( smart payment apps). 

Wataalamu hao wakiwa jijini Dar es Salaam watakutana na Ofisi ya Mkuu wa  Mkoa wa Dar es Salaam, TANESCO, TPSF, Benki za CRDB, NMB na NSSF



Tuesday, June 22, 2021

MKUTANO WA SADC WA BARAZA LA MAWAZIRI SADC WAENDELEA MAPUTO - MSUMBIJI


Katibu Mkuu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Edward Sokoine(katikati) muda mfupi kabla ya kuanza kikao cha Baraza la Mawaziri wa SADC Mjini Maputo,Msumbiji. Kushoto kwa Balozi Sokoine ni Balozi Grace Martni na kulia ni Balozi Mteule Agnes Kayola 

Katibu Mkuu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Stergomena Tax akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Edward Sokoine muda mfupi kabla ya kuanza kikao cha Baraza la Mawaziri wa SADC Mjini Maputo,Msumbiji. . Kulia kwa Dkt. Tax ni Balozi Grace Martini na kushoto kwa Balozi Sokine ni Balozi Mteule Agnes Kayola
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Edward Sokoine akifuatilia mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC unaoendelea Maputo,Msumbiji . Nyuma ya Balozi Sokoine kulia ni Balozi Grace Martini na kushoto ni Balozi Mteule Agnes Kayola

 Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ukiwa unaendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Joachim Chissano Maputo,Nchini Msumbiji

Rais wa Ufaransa amtunikia Nishani Balozi Radhia


Rais wa Ufaransa amtunikia Nishani Balozi Radhia

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amemtunukia Balozi Mstaafu, Mhe. Radhia N. Msuya wa Tanzania, nishani ya “National Order of Merit”. Balozi Msuya amevikwa nishani hiyo jijini Dar Es Salaam na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mhe. Frederick Clavier kwa niaba ya Rais Macron tarehe 17 Juni 2021

 

Balozi Msuya ametunukiwa nishani hiyo kutokana na mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Ufaransa wakati akiwa Mkurugenzi wa Ulaya na Amerika  katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2006-2010). Ametambuliwa kwa mchango mahsusi aliyoutoa wakati Ufaransa ilipokuwa Rais wa Umoja wa Ulaya.

 

Nishani hiyo ilianzishwa mwaka 1963 kwa nia ya kutambua mchango wa watunukiwa wake katika kuendeleza ushirikiano na Ufaransa hasa katika ustawi wa dunia. Baadhi ya watu mashuhuri waliowahi kutunukiwa nishani hiyo ni Rais François Mitterrand wa Ufaransa; Mfalme Juan Carlos I wa Uhispania na Bw. Njoroge Mungai wa Kenya.

 

Balozi Radhia ni mwanadiplomasia aliyefanya kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka 35.  Ambapo alishika nafasi mbalimbali katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania, Umoja wa Mataifa, uliopo New York, Marekani na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza.

 

Mwaka 2010 mpaka 2016 Balozi Radhia aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, akisimamia masuala ya SADC, Botswana, Lesotho na Namibia. Mwaka 2017 Balozi Radhia Msuya alipata uhamisho kutoka Wizara ya Mambo ya Nje kwenda Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kama Msaidizi wa Katibu Tawala. Nafasi hii aliitumikia hadi alipostaafu utumishi wa umma mwaka 2018. Kwa sasa Balozi Radhia Msuya yuko katika kampuni binafsi ya ushauri inayojishughulisha na masuala ya uwekezaji na diplomasia ya uchumi.


 

Monday, June 21, 2021

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA MWAKILISHI MKAZI WA UNDP


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula  akizungumza na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Mhe. Cristine Musisi (kushoto) ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (katikati) akizungumza na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Mhe. Christine Musisi (kushoto) huku Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Mteule Makocha Tembele akishuhudia mazungumzo hayo yaliyofanyika katika mji wa Serikali jijini Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula  akizungumza huku Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Mhe. Cristine Musisi akimsikiliza ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Mhe. Cristine Musisi  baada ya kumaliza mazungumzo yao ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Mhe. Cristine Musisi ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma.

Katika mazungumzo hayo Viongozi hao wamejadiliana na kukubaliana kuendelea kuimarisha mahusiano kati ya UNDP , Wizara ya Mambo ya Nje na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha lengo la kupatikana kwa maendeleo linafikiwa kwa pamoja.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mulamula alimuhakikishia Bibi Musisi utayari wa Tanzania katika kuimarisha mahusiano na UNDP na kumueleza kuwa  Serikali ya Tanzania imejipanga kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa vitendo.

Mhe. Waziri pia amemuhakikishia Bibi Musisi kuwa Wizara yake inatilia mkazo kauli ya Serikali ya kuvutia na kuweka  mazingira mazuri ya uwekezaji na kufanya biashara nchini ili kuvutia wawekezaji na wafanya biashara kuja kuwekeza nchini kwa maendeleo ya Taifa.

Mhe Waziri alisisitiza kuwa Wizara inatilia mkazo pia suala la kuwajengea ujuzi wataalamu wake katika maeneo ya teknolojia ya habari na mawasiliano ili kwenda na wakati na hivyo kuendesha na kushiriki mikutano kwa njia ya mtandao hasa wakati huu wa ugonjwa wa CCOVID 19, ujuzi wa kufanya uchambuzi na namna bora ya kuwasiliana ili kuhakikisha Tanzania inanufaika na utekelezaji wa diplomasia ya uchumi..

Naye Mwakilishi Mkazi wa UNDP Mhe. Musisi alimuhakikishia Mhe. Waziri Mulamula kuwa UNDP ipo tayari na itaendelea kushirikiana na Wizara kwa karibu na kuendelea kutoa wataalam na mafunzo kwa watendaji wa Serikali ili kuendeleza ujuzi wa watendaji serikalini na kuwafanya kutoa huduma bora zaidi kwa Taifa na wananchi wake.

Amesema UNDP itaendelea kusaidia utoaji wa mafunzo,  kuendesha na kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania na Tanzania ujumla.  




MKUTANO WA 17 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA KISEKTA LA UCHUKUZI, MAWASILIANO NA HALI YA HEWA LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI WAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM.

Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa (TCM) umeanza kufanyika leo jijini Dar es Salaam. Mkutano huu utakaofanyika kwa lipindi cha siku tano (5) kuanzia tarehe 21 hadi 25 Juni 2021 unatarajiwa kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa programu na miradi, maamuzi na maagizo ya mikutano ya awali katika sekta za miundombinu ya uchukuzi mawasiliano na hali ya hewa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Mkutano huu ambao unafanyika kwa njia ya ana kwa ana na mtandao, na kuhudhuriwa na Nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unatarajiwa kufanya yafuatayo; 

Moja, Kupitisha Mkakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Usalama Barabarani (EAC Road Safety Strategy). Mkakati huu unaombatana na Mpango Kazi wa Usalama Barabarani wa kipindi cha miaka 10 (2021-2030) unalenga kuchukua hatua madhubuti za kuboresha usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kudhibiti adhari zinazopelekea ulemavu, upotevu wa maisha pamoja na mali kutokana ajari za barabarani. 

Mbili, Kuridhia kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya Uendeshaji na Usimamizi wa Anga la Juu la Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hati hii ya Makubaliano inalenga kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa za anga, kuimarisha usalama na mawasiliano ya usafiri wa anga kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na

Tatu, Kuridhia uanzishwaji wa Taasisi ya Mawasiliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutakoambatana na kupitisha Andiko la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sambamba na hayo, katika ngazi ya Mawaziri wanatarajiwa kukubali kuibadili Taasisi ya Mawasiliano ya Afrika Mashariki (East African Communication Organization –EACO) kuwa Taasisi rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo itakuwa na jukumu la simamia sekta ya Mawasiliano ndani ya Jumuiya. 

Kama ilivyo ada ya Mikutano ya Baraza la Mawaziri ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanyika katika ngazi tatu, Mkutano huu pia utafanyika katika ngazi tatu ambazo ni, Ngazi ya Wataalamu Waandamizi tarehe 21 na 22 Juni, 2021; Makatibu Wakuu, tarehe 23 na 24 Juni, 2021 na Mawaziri, tarehe 25 Juni, 2021.

Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Bw. Eliabi Chodota akichangia jambo kwenye Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Washiriki wa Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa kutoka nchini Burundi wakifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam. 
Washiriki kutoka nchini Kenya wakifuatilia Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa uliokuwa ukiendelea.
Sehemu ya Washiriki kutoka nchini Sudani Kusini wakifuatilia Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.

Mshiriki kutoka nchini Uganda akiwasilisha mchango wake kwenye Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.
Mkutano ukiendelea

MAANDALIZI YA MKUTANO WA 14 WA MAWAZIRI WA EAC WA SEKTA YA KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA YAANZA JIJINI ARUSHA

Mkutano wa 14 Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Ngazi ya Wataalam umeanza leo tarehe 21 Juni 2021 jijini Arusha ukiwashirikisha Wataalam wa Kilimo kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo.


Mkutano wa Wataalam utafuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 24 Juni 2021 na kuhitimishwa na Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika tarehe 25 Juni 2021.


Lengo la Mkutano wa 14 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Kilimo  na Usalama wa Chakula pamoja na mambo mengine ni kupitia na kujadili utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Baraza la Mawaziri wa Jumuiya pamoja na kupitia na kujadili masuala mbalimbali  muhimu ya kisera, kikmkakati, miradi na program zinazotekelezwa katika sekta ya kilimo.


Kadhalika agenda muhimu zitajadiliwa wakati wa mkutano huo ambazo ni pamoja na Taarifa ya Usalama wa Chakula ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu Mradi wa Afrika wa Kilimo cha Ushindani cha Mpunga kwa Kanda ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu Maendeleo ya Mifugo; Taarifa kuhusu Mradi wa Kuzuia na Kudhibiti Sumukuvu; Taarifa kuhusu Maendeleo ya Uvuvi; na Taarifa kuhusu Uhamasishaji wa Uchangiaji Rasilimali.


Awali akifungua Mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Muthuki, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo anayeshughilikia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo amezitaka Nchi Wanachama kujikita kwenye kilimo cha ushindani na kuboresha viwango vya mazao yanayozalishwa na nchi zote wanachama ili kupata soko la ndani na nje ya jumuiya la mazao hayo kwa manufaa ya wananchi wa jumuiya.


Pia amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuendelea kuwajengea uwezo wakulima katika maeneo yao kwa kutoa elimu ya kilimo bora na chenye manufaa ili kupata mazao bora yenye viwango vinavyokubalika ndani na nje ya mipaka ya nchi wanachama.


“Napenda kuzihimiza nchi wanachama kutoa elimu ya kilimo bora kwa wakulima wao pamoja na kuwajengea uwezo ili kuwawezesha kuzalisha mazao bora na yenye viwango vinavyokubalika ndani ya jumuiya na nje ili hatimaye wunufaike na soko la ndani na nje ya jumuiya” alisisitiza Dkt. Muthuki kwenye hotuba yake.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mkutano huo wa Ngazi ya Wataalam, Bw. Julius Mwabu kutoka Jamhuri ya Kenya aliwataka wajumbe wa mkutano huo kujadili na kutoa mapendekezo yenye tija kuhusu Sekta ya Kilimo na Usalama wa Chakula kwani ni miongoni mwa sekta muhimu zinazotegemewa na wananchi wote wa nchi wanachama wa Jumuiaya ya Afrika Mashariki.


Aliongeza kuwa, mbali na changamoto ya ugonjwa wa corona uliozikumba nchi mbalimbali duniani zikiwemo zile za Jumuiya ya Afrika Mashariki, yapo mafanikio kadhaa yaliyopatikana katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula na kuwaomba wajumbe kujadili na kutoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hiyo ili kuziwezesha nchi wanachama kutotetereka katika kipindi hiki ambacho ugonjwa huo bado haujatokomezwa.


Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Ngazi ya Wataalam umeongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Kilimo, Bw. Gungu Mibavu na kuhudhuriwa pia na Maafisa Waandamizi kutoka Sekta mbalimbali zinazojishughulisha na masuala ya kilimo na usalama wa chakula hapa nchini. 

Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Kilimo, Bw. Gungu Mibavu akizungumza kama kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Wataalam uliofanyika jijini Arusha tarehe 21 Juni 2021 ikiwa ni maandalizi ya awali ya Mkutano wa 14 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika jijini hapa tarehe 25 Juni 2021. Mkutano wa ngazi ya wataalam utafuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu tarehe 24 Juni 2021.
Mwenyekiti wa Mkutano wa Ngazi ya Wataalam, Bw. Julius Mwabu kutoka Kenya akiwa na Mkurugenzi wa Sekta ya Uzalishaji katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw.Jean Havugimana (kulia) pamoja na Katibu wa Mkutano huo kutoka Burundi

Mwenyekiti wa Mkutano wa Ngazi ya Wataalam, Bw. Mwabu akizungumza wakati wa mkutano huo
Mkurugenzi wa Sekta ya Uzalishaji kutoka Sekrtarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Havugimana naye akizungumza wakati wa mkutano wa wataalam

Ujumbe wa Kenya ulioshiriki mkutano wa wataalam
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Kenya ukifuatilia mkutano
Mjumbe wa Burundi naye akishiriki mkutano wa wataalam
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Benjamin Mwesiga akishiriki mkutano wa wataalam
Ujumbe wa Tanzania ukiwa kwenye mkutano wa wataalam
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania kutoka sekta mbalimbali zinazojishughulisha na kilimo wakifuatilia mkutano wa wataalam
Mkutano ukiendelea
Wajumbe kutoka Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakishiriki mkutano wa wataalam
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania katika mkutano
Mkutano ukiendelea
Mshiriki mwingine wa mkutano kutoka Tanzania