Thursday, October 13, 2022

WAZIRI WA MAMBO YA NJE AKUTANA NA WATUMISHI WA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI ZAMBIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amekutana na kufanya kikao na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia tarehe 13 Oktoba 2022 katika ofisi za ubalozi huo Jijini Lusaka, Zambia.

Mhe. Tax amekutana na watumishi wa Ubalozi huo baada ya kuwasili nchini Zambia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 14 Oktoba 2022.

Akiongea katika kikao na watumishi hao Mhe. Waziri Tax ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia ni wa kihistoria na kidugu uliojengwa kupitia ujirani mwema na misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Mataifa hayo mawili Hayati Baba wa Taifa la Tanzania Mw. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Keneth Kaunda wa Zambia. Kupitia kikao hicho, Mheshimiwa Waziri Tax ameelekeza Ubalozi kuendelea kuwa kiungo katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa kufuata misingi iliyowekwa na Waasisi wa Mataifa hayo.

“Fanyeni kazi kwa bidii hususan wakati huu tunapotekeleza diplomasia ya uchumi ili ushirikiano wetu uweze kuleta ukombozi wa kiuchumi kwa maslahi mapana ya nchi yetu”alisema Mhe. Waziri Tax.

Naye Balozi wa Tanzania nchi Zambia anayemaliza muda wake Mhe. Hassan Yahya Simba akisoma taarifa ya utekelezaji, ameeleza kuwa ubalozi unaendelea kusimamia ushirikiano wa mataifa hayo mawili kwa kuhakikisha unafatilia kwa karibu maslahi ya Taifa na maslahi ya Watanzania wanaoishi na kuingia nchini Zambia kwa shughuli mbalimbali.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Dkt. Tax ametumia nafasi hiyo kutembelea majengo yanayomilikiwa na ubalozi wa Zambia pamoja na ofisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) zilizopo jijini Lusaka, Zambia.

Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia umekuwa ofisi ya kwanza ya uwakilishi kutembelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax tangu aapishwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na watumishi (hawapo pichani) wa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania jijini Lusaka, Zambia katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Ubalozi huo tarehe 13 Oktoba 2022.

Mhe. Dkt, Tax (kulia) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine wakifuatilia kikao hicho kilichofanyika tarehe 13 Oktoba 2022 jijini Lusaka Zambia.

Mheshimiwa Waziri Tax akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia tarehe 13 Oktoba 2022 jijini Lusaka Zambia, kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Zambia anayemaliza muda wake, Mhe. Hassan Simba Yahya.

Maafisa wa Ubalozi wakifuatilia kikao hicho.

Kutoka Kulia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakipokea taarifa ya maendeleo ya ukarabati wa jengo la ofisi na nyumba za Serikali ya Jamhuri ya Tanzania zilizopo nchini Zambia kutoka kwa Mhe. Balozi Hassan Yahya Simba alipotembelea nyumba za watumishi wa Ubalozi huo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Utawala na Fedha wa Ubalozi huo Bw. Humphrey Shangarai (kushoto) alipotembelea nyumba za watumishi wa ubalozi huo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika ofisi za Bandari ya Dar es Salaam (TPA) zilizopo jijini Lusaka, Zambia tarehe 13 Oktoba 2022. Aliyesimama ni Mwakilishi wa TPA nchini Zambia, Bw. Hamis Chambali.

Picha ya pamoja.





Wednesday, October 12, 2022

TANZANIA NA ZAMBIA ZAAZIMIA KUMALIZA CHANGAMOTO ZA KIBIASHARA NA USAFIRISHAJI

Tanzania na Zambia zimedhamiria kumaliza changamoto za kibiashara na usafirishaji zinazowakabili wafanyabiashara ili kuruhusu biashara na usafirishaji wa bidhaa ufanyike bila vikwazo baina ya nchi hizo.

Hayo yamebainishwa katika hotuba ya ufunguzi iliyosomwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine wakati wa Mkutano 10 wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zambia ngazi ya Wataalam unaofanyika leo tarehe 12 Oktoba 2022 jijini Lusaka Zambia.

Balozi Sokoine aliwasisitiza watendaji kutumia mkutano huo kuandaa mikakati ya pamoja itakayosaidia kuondoa vikwazo vya kibiashara na kutengeneza mazingira wezeshi kwa sekta ya umma na binafsi ili ziweze kufanya uwekezaji utakaoleta maendeleo endelevu kwa ajili ya maslahi mapana ya kiuchumi kwa pande zote mbili.

“Tanzania ina dhamira ya dhati ya kuimarisha ushirikiano wake wa kindugu na kihistoria na Zambia ili kuendeleza jitihada zilizoasisiwa na waasisi wa mataifa yetu kwa kuweka na mfumo rasmi wa ushirikiano unaowezesha ufuatiliaji wa utekelezaji katika masuala ya ushirikiano” alisema Balozi Sokoine.

Aidha, alieleza kuwa ushirikiano imara na wenye mafanikio ni ule unaojengwa kwa mfumo rasmi ambao unaruhusu kukutana na kufanya majadiliano ya mara kwa mara hivyo, alieleza kuwa ana amini kupitia mkutano huu maeneo yote ya ushirikiano yenye changamoto yatajadiliwa kwa kina kwa maslahi ya nchi zote mbili na wananchi wake.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Bw. Chembo Mbula alieleza kuwa ni muhimu majadiliano yakaangalia kwa kina maeneo muhimu yatakayowezesha pande zote mbili kuwa na mchango katika maendeleo ya mtangamano wa kikanda.

“Nchi zetu zimepiga hatua kiuchumi na katika maendeleo ya jamii tangu kumalizika kwa mkutano wa tisa wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya ushirikiano baina yetu, hivyo ni vyema majadiliano yakaendana na uhalisia wa mabadilika hayo” alisema, Bw. Mbula.

Pamoja na mambo mengine mkutano huu utapitia na kujadili utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Tisa wa Tume ya Kudumu ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia uliofanyika tarehe 25 na 26 Februari 2016 jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ulioanza tarehe 11 Oktoba 2022 kwa ngazi ya Wataalam, utafuatiwa mkutano wa Makatibu Wakuu na utahitimishwa kwa mkutano wa ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 14 Oktoba 2022 jijini humo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zambia ngazi ya Wataalam unaofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Bw. Chembo Mbula akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zambia ngazi ya Wataalam unaofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia.

Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz wakifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.

Kutoka kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Bw. Ally Gugu na Balozi wa Tanzania nchini Zambia anayemaliza muda wake, Mhe. Hassan Simba Yahya wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa mkutano huo.

Ujumbe kutoka Zambia

Ujumbe kutoka Tanzania.

Sehemu nyingine ya ujumbe kutoka Tanzania.

Maafisa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa mkutano, kutoka kushoto ni  Bi. Lilian Mukasa na Bw. Makama D. Makamba.

Ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kutoka kulia ni Bi. Clementine Msafiri na Bi. Happiness Lyandala wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo.

Ujumbe kutoka Tanzania ukifuatilia ufunguzi wa mkutano, kulia ni Afisa Mambo ya Nje kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Laila Kagombora.

Ujumbe kutoka Tanzania.

Picha ya Pamoja Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine (wa nne kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Bw. Chembo Mbula (wa tatu kutoka kulia) pamoja na viongozi na maafisa waandamizi kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zambia baada ya hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zambia unaofanyika kuanzia tarhe 11 hadi 14 Oktoba jijini Lusaka Zambia.



TUENDELEE KUMUENZI MWALIMU NYERERE- MHE MAKINDA



Kamishna wa Sensa ya mwaka 2022 Mhe. Anne Makinda amewasihi Watanzania kuendelea kuenzi fikra na mitazamo ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Mhe. Makinda ametoa rai hiyo katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam alipofungua Kongamano la kumbukizi ya miaka 23 ya kifo cha Mwalimu Nyerere kilichotokea 1999 jijini London.

Amesema Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa muasisi wa vitu vingi ambavyo nchi yetu inajivunia hadi sasa, ni muasisi wa siasa za kutokufungamana na upande wowote, Ukombozi wa nchi za Bara la Afrika hasa zile za Kusini pamoja na kutokukubaliana na fikra za ukoloni na ubaguzi wa aina yoyote na kusisitiza kuwa ni lazima tuendelee kumuenzi kwa mambo makubwa aliyotufanyia

“Mwalimu alikuwa muasisi wa vitu vingi ambavyo nchi yetu inajivunia hadi sasa, alikuwa muasisi wa siasa za kutofungamana na upande wowote, kusimamia ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na kupinga ukoloni na ubaguzi wa aina yoyote ile, haya mambo ni makubwa sana lazima tuendelee kuyaenzi kwa nguvu zote,” alisema.

Amefafanua kuwa Hayati Mwalimu alitamani kuchelewesha uhuru wa Tanganyika kutokana na imani yake ya ukombozi wa nchi zote za Afrika kwakuwa aliona ukombozi wa mmoja hauna maana kama nchi nyingine hazitakuwa huru.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga amewashukuru watoa mada na washiriki wa kongamano hilo kwa michango yao ambayo imefanya kongamano hilo kufanikiwa na kutoa elimu kwa wengi.

“Watoa mada wetu wamesema mengi ya muhimu sana na tumejifunza kwa kina. Nawashukuru wote kwa mawasilisho yenu muhimu katika kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambalo limetukumbusha mambo mengi yaliyofanywa na Hayati Mwalimu Nyerere,” alisema Balozi Mindi.

Balozi Mindi pia amekipongeza Chuo cha Diplomasia kwa kuandaa Kongamano hilo kwa ajili ya kukumbuka miaka 23 tangu kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na hivyo kuwakutanisha wadau mbalimbali na kuwakumbusha, kujadili na kujifunza mchango wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere katika Kujenga Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia ya Tanzania.

Kongamano hilo lilijadili mchango wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere katika Kuendeleza Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia nchini liliwakutanisha mabalozi wastaafu na wakufunzi wa Chuo cha Diplomasia na wanafunzi wa shule ya Sekondari Jitegemee ya Dar es Salaam.







Tuesday, October 11, 2022

TANZANIA - ZAMBIA WAJADILI MASUALA YA USHIRIKIANO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zambia zinakutana jijini Lusaka, Zambia kujadili masuala ya ushirikiano yaliyokubaliwa baina ya nchi hizo mbili.

Majadiliano hayo yanafanyika katika ngazi ya Wataalam ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Kumi wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia unaofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Oktoba 2022.

Mkutano wa Wataalam utafuatiwa na mkutano ngazi ya Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 12 Oktoba 2022 na kumalizika na mkutano ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 14 Oktoba 2022 jijini Lusaka Zambia.

Mkutano huu unajadili na kutathimini utekelezaji wa maazimio katika sekta mbalimbali za ushirikiano zilizokubaliwa katika mkutano wa tisa uliofanyika tarehe 25 hadi 26 Februari 2016 jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Maeneo ya ushirikiano ni pamoja na; Siasa, Ulinzi na Usalama, Mambo ya Nje, Uhamiaji, Fedha na Uchumi, Sheria, Nishati, Habari na Mawasiliano, Kilimo, Miundombinu, Uchukuzi na Usafirishaji, Elimu, Sayansi na Teknolojia, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo, Uvuvi, Mazingira na Maliaasili, Afya, Elimu, Vijana na Michezo na jinsia.

Mkutano huu unafanyika kufuatia maagizo ya Marais wa pande zote mbili wakati wa ziara ya kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Zambia nchini Tanzania, Mhe. Hakainde Hichilema mapema mwezi Agosti 2022.

Mwenyekiti wa mkutano ngazi ya Wataalamu Mhe. Balozi Hassan Simba Yahya akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia - ngazi ya Wataalam unaofanyika leo tarehe 11 Oktoba 2022 jijini Lusaka Zambia.

Mwenyekiti mwenza wa mkutano ngazi ya wataalamu Bw. Lubasi Mugandi akiongoza ujumbe wa Zambia katika Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia - ngazi ya Wataalam unaofanyika leo tarehe 11 Oktoba 2022 jijini Lusaka Zambia.

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia majadiliano, kulia Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,  Brig. Jen. Michael M. Mumanga na kushoto ni Afisa Mambo ya Nje Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Makamba D. Makamba. 

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia majadiliano

Kutoka kushoto ni Kamishna Msaidizi Idara ya Uchambuzi wa Sera katika Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. William Mhoja na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mtangamano wa Biashara katika Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara wakifuatilia majadiliano katika mkutano wa wataalam.

Kutoka kushoto ni Mkuu wa Utawala na Fedha katika Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia, Bw. Humphrey Shangarai na Afisa Ubalozi Bw. Sunday Iddi wakifuatilia majadiliano.

Ujumbe wa Tanzania.

Mchumi  katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Clementine Msafiri akifuatilia majadiliano.

Afisa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki - Ofisi ya Zanzibar, Bi. Asya  Ali Hamdani akifuatilia mkutano huo.





BALOZI FATMA AFANYA MAZUNGUMZO NA UJUMBE WA WATAALAM WA UMOJA WA AFRIKA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab leo terehe 11 Oktoba 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Wataalam wa Umoja wa Afrika wa Kutathimini utekelezaji wa Agenda 2063, jijini Dodoma.

Ujumbe huo (Technical Working Group on the Evaluation of Agenda 2063) unaoongozwa na Bi. Josephine Etima upo ziarani nchini kuanzia tarehe 10 hadi 14 Oktoba 2022, ambapo utakutana na wadau mbalimbali wa Serikali katika ngazi ya wakurugenzi kwa lengo la kupata maoni yao kuhusu mpango wa utekelezaji wa Agenda 2063 katika kipindi cha muongo mmoja wa kwanza. 

Bi. Josephine na ujumbe wake ambao ulikutana na Balozi Fatma kwa lengo la kuelezea kuhusu ziara yao nchini, amebainisha kuwa maoni yatakayo tolewa na wataalam kuhusu mpango wa utekelezaji wa kipindi cha miaka 10 ya kwanza yatawasaidia kubaini musuala muhimu zaidi ya kuzingatia wakati wa kuandaa mpango wa pili wa miaka 10 ya utekelezaji wa Agenda 2063. 

Kwa upande wake Balozi Fatma akizungumza na ujumbe wa wataalam hao ameelezea hatua mbalimbali za maendeleo zilizofikiwa nchini ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Agenda 2063. Ametaja baadhi ya maendeleo hayo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), mpango utoaji elimu bila malipo, uboreshwaji wa upatikanaji na usambazaji wa madawa na vifaa tiba na uboreshwaji wa huduma za afya vijijini. 

Mbali na hayo Balozi Fatma aliongeza kuwa jitihada zingine zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza Agenda 2063 ni pamoja na kuendesha programu mbalimbali zinazolenga kuwahamasisha Diaspora kushiriki katika shughuli za maendeleo nchini. Vilevile ameeleza kuwa Wizara na Serikali kwa ujumla inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya biashara miongoni wa Waafrika wenyewe kupitia fursa zinazotokana na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA). 

Agenda 2063 ambayo imebeba kauli mbiu isemayo “Afrika Tuitakayo” ("The Africa We Want") inalenga pamoja na mambo mengine kuliunganisha Bara la Afrika katika masuala ya kukuza uchumi; kuhamasisha utawala bora na utawala wa sheria; kuhakikisha maendeleo kwa mtu mmoja mmoja; kuhakikisha amani na usalama unaimarika na kuiweka Afrika kwenye nafasi ya mchangiaji mkuu wa uchumi duniani
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab (kulia) akiwa katika mazungumzo na na Bi. Josephine Etima kiongozi wa ujumbe wa Wataalam wa Umoja wa Afrika wa Kutathimini utekelezaji wa Agenda 2063, yaliyofanyika jijini Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab (kulia) akisalimiana na Bi. Josephine Etima kiongozi wa ujumbe wa Wataalam wa Umoja wa Afrika wa Kutathimini utekelezaji wa Agenda 2063 walipowasili Wizarani jijini Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab (mwenye kilemba) akiwa katika mazungumzo na ujumbe wa Wataalam wa Umoja wa Afrika wa Kutathimini utekelezaji wa Agenda 2063
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab (mwenye kilemba) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Wataalam wa Umoja wa Afrika wa Kutathimini utekelezaji wa Agenda 2063 (kulia kwa Balozi Fatma) na Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje (kushoto kwa Balozi Fatma)
Mazungumzo yakiendelea
Mazungumzo yakiendelea

Monday, October 10, 2022

TAMKO LA PAMOJA KATI YA TANZANIA NA KENYA


 

                                       





 

TANZANIA KENYA ZAKUBALIANA KUENDELEA KUIMARISHA UHUSIANO

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati yake na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto Ikulu jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati yake na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto Ikulu jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto akimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipozungumza katika Mkutano na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati yao Ikulu jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto akizungumza katika  Mkutano na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati yake na Mhe. Rais Samia Ikulu jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto akizungumza katika  Mkutano na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati yake na Mhe. Rais Samia Ikulu jijini Dar es Salaam.



Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax kabla ya kuanza kwa Mkutano wa waandishi wa habari na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya Mhe. Dkt William Ruto baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.



Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Camilius Wambura akifuatilia Mkutano wa waandishi wa habari na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya Mhe. Dkt William Ruto baada ya kumalizika kwa  mazungumzo kati yao Ikulu jijini Dar es Salaam.


 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman (kulia) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine wakifuatilia Mkutano wa waandishi wa habari na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya Mhe. Dkt William Ruto Ikulu jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga akifuatilia Mkutano wa waandishi wa habari na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya Mhe. Dkt William Ruto Ikulu jijini Dar es Salaam.


 

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kenya zimekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi zao kwa manufaa ya pande zote mbili.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema hayo Ikulu jijini Dar wa Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea walichojadili katika mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto aliyekuwa na ziara ya kikazi ya siku mbili  nchini .

 

Ziara hii ya Mhe. Ruto nchini, imetuwezesha kujadili na kuhuisha mahusiano yetu na kutupa nafasi ya kujitathmini mashirikiano baina ya Tanzania na Kenya, na tumekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano baina yan chi zetu, alisema Mhe. Rais

 

Amesema katika mazungumzo yao wamejadili masuala ya kimkakati kuhusiana na ushirikiano baina ya nchi hizo, kikanda na kimataifa na kuongeza kuwa wamekubaliana kukuza na kuimarisha uhusiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Kenya.

 

Mhe. Rais Samia amesema Tanzania inajivunia kuondolewa kwa vikwazo visivyo vya kodi ambavyo vilikuwa vinazuia ufanyaji wa Biashara kati ya Tanzania na Kenya.

 

“Wakati naingia madarakani kulikuwa na vikwazo visivyo vya kodi 68, lakini sasa vimefanyiwa kazi na kubaki 14, ni matarajio yetu kuwa vikwazo vilivyobaki navyo vitamalizwa na hivyo kurahisisha ufanyaji biashara baina ya nchi zetu”, alisema Mhe. Rais.

 

Amesema wamekubaliana kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa Kenya kupitia Nairobi.

Amesema kuwa wamejadili jinsi ya kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa lengo la kuzifanya nchi zao kuwa sehemu salama  na kuongeza kuwa wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika masuala ya kikanda na kimataifa na kukuza Jumuiya ya Afrika Mashariki Kama viongozi waanzilishi wa Jumuiya hiyo pamoja na nchi ya Uganda

 

Akizungumza katika mkutano huo Rais wa Kenya Mhe. William Ruto amesema amedhamiria kuyafikisha mahusiano kati ya Tanzania na Kenya katika levo nyingine na dhamira hiyo itafanikiwa kutokana na utayari uliopo baina ya nchi hizo.

 

Amesema biashara kati ya Tanzania imekuwa ikiongezeka na viongozi hao wanadhamira ya kuongeza ufanyaji wa biashara baina ya Kenya na Tanzania na kufafanua kuwa biashara kati ya nchi hizo  imeongezeka na kuifanya Tanzania kuwa mnufaika mkubwa kuliko ilivyokuwa awali.

 

“Mauzo ya Tanzania nchini Kenya yamekuwa yakiongezeka kwa kasi , kabla ya kuondolewa vikwazo visivyo vya kodi, sasa Kenya wananunua zaidi Tanzania kuliko ilivyo kuwa,” alisema

 

Amesema mauzo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 31 hadi shilingi bilioni 41 na biashara imekuwa kutoka shilingi bilioni 27 hadi shilingi bilioni 51 na hivyo kuleta picha kuwa Tanzania sasa inanufaika sana na ufanyaji wa biashara na Kenya.

 

Amesema wamekubaliana kuwa Mawaziri na wadau wengine wote wanaohusika na biashara wananakutana na kuzifanyia kazi changamoto zinazokabili sekta ya biashara baina ya nchi hizo ili wananchi waweze kufanya biashara .

 

Amesema uongozi wake utatilia mkazo na kuhakikisha ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es salaam hadi Mombasa unaharakishwa na kukamilika kwa wakati.

 

“Tutahakikisha tunatumia fursa ya ujenzi wa bomba la gesi kwenda Mombasa ili kuhakikisha tunatumia maliasili zetu na kuongeza ufanisi wa biashara na kuboresha maisha ya watu wetu, kuongeza na kuimarisha ushindani wa viwanda na wawekezaji wetu ,nchi zetu na ukanda wetu kwa ujumla

 

Amesema kukamilika kwa bomba hilo kutasaidia kukuza mpango wa viwanda katika nchi hizo na kuongeza kuwa utekelezaji wa mpango wa kuwa na mtandao mmoja kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki kwani walishakubaliana na baadhi ya nchi kuwa na mtandao mmoja

 

“Tutahakikisha tunatekeleza mpango huo ili kuwafanya wananchi wetu waweze kufanya biashara na kuwasiliana kwa urahisi na kwa gharama nafuu na hivyo kuendelea kuimarisha mahusiano yetu,” alsiema

 

Amesema wamewaelekeza watendaji katika nchi zao kukutana na kuandaa mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya kabla mwaka huu haujaisha ili kujadili namna ya kuendelea kutatua changamoto zilizopo na hivyo kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo baina ya nchi hizo

 

Amewaambia Watanzania wajue kuwa wana marafiki na ndugu kutoka Kenya na kuahidi kuwa watafanya kazi pamoja na kuongeza kuwa Tanzania na Kenya hawawezi gawana njaa bali watagawana utajiri na fursa ili kujenga umoja kwa manufaa ya nchi zote mbili na watu wake

 

Rais Ruto aliwasili nchini tarehe 09/10/2022  kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili na aliondoka nchini kurejea Kenya tarehe 10/10/2022