Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Jamhuri ya Zambia zimesaini Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa na Mkataba wa Utatu kati ya Chemba za
Biashara za nchi hizo wakati wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya
Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia katika Ngazi ya Mawaziri uliomalizika
tarehe 15 Oktoba 2022 jijini Lusaka.
Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa ulisainiwa kati ya Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Stanley Kabubo.
Wakati huo huo, Mkataba wa Utatu kati ya Chemba ya
Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) na Chemba ya Taifa ya Biashara
ya Zanzibar (ZNCC) za Tanzania na Chemba ya Wafanyabiashara na Viwanda (ZACCI)
ya Zambia ulisainiwa na Rais wa TCCIA, Bw. Paul Koyi na Mtendaji Mkuu wa TCCIA
na Bw. Nerbat Mwapwele kwa niaba ya Mwenyekiti wa ZNCC. Pia kwa upande wa
Zambia mkataba huo ulisainiwa na Mtendaji Mkuu wa ZACCI, Bw. Phil Daka.
Aidha, Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia katika Ngazi ya Mawaziri, ulitanguliwa na mkutano katika ngazi ya wataalam uliofanyika tarehe 11 na 12 Oktoba 2022 na kufuatiwa na Mkutano katika ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 13 Oktoba 2022.
Pamoja na mambo mengine mkutano huo pia ulitathimini utekelezaji wa
makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya
Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema aliyofanya nchini Tanzania mapema mwezi Agosti
2022.
Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Kabubo wakionesha Hati zilizosainiwa kwa wajumbe wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia. |
Kutoka Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Zambia anayemaliza muda wake, Mhe. Hassan Yahya Simba na Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz wakifuatilia hafla ya kufunga Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.
|