Saturday, November 18, 2023

RAIS DKT. MWINYI AWAKARIBISHA WAROMANIA KUWEKEZA ZANZIBAR


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kwa heshima ya Rais wa Romania, Mhe. Klaus Iohannis Ikulu Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezikaribisha kampuni za Romania kuja kuwekeza Zanzibar katika sekta za Uchumi wa Buluu na Utalii ambazo ni sekta za kipaumbele kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dkt. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Novemba 18, 2023 Ikulu Zanzibar wakati wa hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kwa heshima ya Rais wa Romania, Mhe. Klaus Iohannis ambaye yupo nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku nne.

Dkt. Mwinyi amesema kuwa ziara ya Rais Iohannis ni heshima kubwa kwa Zanzibar na imedhihirisha kuwa licha ya nchi hizo mbili kuwa mbali kijiografia lakini zinaweza kufanya kazi pamoja kwa maslahi mapana ya pande zote mbili. 

Aidha, Rais Mwinyi alitoa wito kwa watu wa Romania kuja Zanzibar, kisiwa kilichojaliwa vivutio vingi vya utalii na vinavyovutia.

Alimuhakikishia Rais Iohannis ambaye amepanga kutembelea Mji Mkongwe kuwa hatajutia uamuzi wake kwani atafurahia historia na mandhari nzuri ya Mji huo.

Kwa upande wake, Rais wa Romania alifurahishwa na dira ya Maendeleo ya Zanzibar na kuahidi kuwa Serikali yake itashirikiana na Zanzibar ili kufanikisha utekelezaji wa Dira hiyo. Amesema ziara yake ni moja ya jitihada za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Romania na Tanzania ambao mwezi Mei 2024 utafikisha miaka 60 tangu ulipoanzishwa mwaka 1964.

Rais Iohannis atamaliza ziara yake nchini Novemba 19, 2023 ambapo pamoja na mambo mengine, wakati wa ziara hiyo imeshuhudiwa uwekaji saini wa Hati za Makubaliano kuhusu kushirikiana katika masuala ya utafiti wa kisayansi katika kilimo na usalama wa chakula pamoja na kukabiliana na majanga

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kwa heshima ya Rais wa Romania, Mhe. Klaus Iohannis Ikulu Zanzibar

Meza Kuu wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Taifa ukipigwa kwenye hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kwa heshima ya Rais wa Romania, Mhe. Klaus Iohannis Ikulu Zanzibar
Rais wa Romania, Mhe. Klaus Iohannis akizungumza kwenye hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kwa heshima yake Ikulu Zanzibar

Friday, November 17, 2023

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


 


TANZANIA, ROMANIA KUIMARISHA USHIRIKIANO MAENEO YA KIMKAKATI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameitaja ziara ya Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis ni ya kihistoria na ya kwanza kwa kiongozi wa juu wa Taifa hilo kutembelea nchini na imesaidia kuimarisha ushirikiano katika maeneno ya kimkakati.

Rais samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 17 Novemba 2023 Ikulu jijini Dar es salaam wakati wa mkutano na waandishi wa Habari kuhusu waliyokubaliana na mgeni wake.

Rais Samia ameeleza kuwa katika mazungumzo na mgeni wake wamekubaliana kuwa mataifa yao yataimarisha ushirikiano katika sekta za afya, hususan utengenezaji wa dawa, usindikaji wa mazao ya kilimo, madini pamoja na mbinu za kukabiliana na majanga.

Maeneo mengine ya ushirikiano ambayo viongozi hao wamedhamiria kuyapa kipaumbele ni ufadhili wa masomo ambapo Romania itatoa nafasi 10 kwa ajili ya watanzania kusoma masomo ya udaktari na ufamasia katika mwaka huu wa masomo. Aidha, Tanzania imetoa nafasi tano za masomo kwa wanafunzi wa Romania kuja kusoma nchini katika vyuo watakavyochagua wenyewe.

Rais samia aliongeza kuwa nchi hizo zimedhamiria kukuza kiwango cha biashara na uwekezaji ambacho kwa sasa hakiridhishi licha ya nchi zao kuwa na fursa lukuki za uwekezaji. 

Viongozi hao pia waliokubaliana kushirikiana katika masuala ya kimataifa na hasa mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo itajadiliwa kwa kina katika mkutano wa COP28 uliopangwa kufanyika Umoja wa Falme za Kiarabu mwishoni mwa mwezi Novemba 2023.

Rais Samia alihitimisha maelezo yake kwa kueleza kuwa Mheshimiwa Iohannis na ujumbe wake watatembelea Zanzibar kuzungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi tarehe 18 Novemba, 2023. Viongozi hao wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano hususan uchumi wa buluu na utalii ambazo ni sekta za kipaumbele kwa Zanzibar. 

Naye Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis amesema Romania imekuwa na ushirikiano mzuri na imara wakati wote, na lengo la ziara yake nchini Tanzania ni kuimarisha zaidi uhusiano baina ya mataifa hayo.

Tumekuwa na uhusiano mzuri na imara wakati wote, na katika kuendelea kuimarisha uhusianoi wetu tumekubaliana kuimarisha uhusianio wetu kwenye maeneo ya kimkakati na Tanzania katika sekta za kilimo, ulinzi wa raia, ulinzi wa kimtandao, teknolojia na uchumi,” alisema Rais Iohannis

“kusainiwa na hati hizi mbili za makubaliano ya ushirikiano ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa ushirikiano wetu,” aliongeza Rais Iohannis 

Pamoja na mambo mengine, Rais Iohannis amesema kuwa Romania itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza mambo waliyokubaliana kwa maslahi ya mapana ya pande zote mbili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassana akizungumza waandishi wa habari wakati wa ziara ya Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis, wakifurahia jambo muda mfupi kabla ya kuzungumza na wanahaba Ikulu jijini Dar es Salaam
Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam
Waziri wa Masuala ya Dunia na Mikakati ya Kidiplomasia wa Romania Mhe. Traian-Laurentiu Hristea na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Prof. Raphael T. Chibunda wakionesha Hati za Makubaliano walizosaini katika Hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Wazir Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Masuala ya Dunia na Mikakati ya Kidiplomasia wa Romania Mhe. Traian-Laurentiu Hristea wakisaini Hati za Makubaliano katika Hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Wazir Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Masuala ya Dunia na Mikakati ya Kidiplomasia wa Romania Mhe. Traian-Laurentiu Hristea wakibadirishana Hati za Makubaliano walizosaini katika Hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Masuala ya Dunia na Mikakati ya Kidiplomasia wa Romania Mhe. Traian-Laurentiu Hristea na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Prof. Raphael T. Chibunda wakisaini Hati za Makubaliano katika Hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam

Thursday, November 16, 2023

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA MAWAZIRI KUHUSU USALAMA WA BAHARI YA HINDI

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Tatu wa Mawaziri kuhusu Usalama na Ulinzi wa Bahari  Magharibi mwa Bahari ya Hindi uliofanyika Balaclava nchini Mauritius tarehe 16 Novemba 2023.

 

Mkutano huo ambao umeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda na Biashara za Kimataifa ya Mauritius kwa kushirikiana na Kamisheni ya Bahari ya Hindi, pamoja na mambo mengine ulipokea taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya mikutano ya aina hiyo iliyofanyika mwaka 2018 na 2019 pamoja na kujadili hatua za kuchukua ili kuimarisha ulinzi na usalama wa bahari. 

 

Kadhalika, wakati wa Mkutano huo, Nchi mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa na kikanda na wadau wa maendeleo zilipitisha  Azimio la Pamoja  kuhusu umuhimu wa  ushirikiano  na nguvu ya pamoja katika kulinda watumiaji wa Bahari ya Hindi dhidi ya changamoto mbalimbali zinazotokana na matumizi ya bahari ikiwemo ongezeko la makosa yanayovuka mipaka, uharamia na uvuvi haramu.

 

Ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Rosemary Jairo, Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Mauritius, Bw. Marday Venkatasamy na Maafisa Waandamizi kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania na Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe ambao unawakilisha pia nchini Mauritius.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame (wa pili kulia) akishiriki Mkutano wa Tatu wa Mawaziri kuhusu Usalama na Ulinzi wa Bahari Magharibi mwa Bahari ya Hindi uliofanyika Balaclava nchini Mauritius tarehe 16 Novemba 2023. Mhe. Makame aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo.
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Mauritius, Bw. Marday Venkatasamy.  Mhe. Makame aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Tatu wa Mawaziri kuhusu Usalama na Ulinzi wa Bahari  Magharibi mwa Bahari ya Hindi uliofanyika Balaclava nchini Mauritius tarehe 16 Novemba 2023.

Waziri wa Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Mauritius, Bw. Marday Venkatasamy, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki, Bi. Rosemary Jairo (wa pili kulia) na Afisa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe ambao unawakilisha pia Mauritius, Bi. Gwantwa  Mwaisaka wakati wa  Mkutano wa Tatu wa Mawaziri kuhusu Usalama na Ulinzi wa Bahari  Magharibi mwa Bahari ya Hindi uliofanyika Balaclava nchini Mauritius tarehe 16 Novemba 2023.

Mhe. Makame (wa nne kulia waliosimama) katika picha ya pamoja na Viongozi wengine walioshiriki Mkutano wa Tatu wa Mawaziri kuhusu Usalama na Ulinzi wa Bahari  Magharibi mwa Bahari ya Hindi uliofanyika Balaclava nchini Mauritius tarehe 16 Novemba 2023.



 

RAIS WA ROMANIA AWASILI NCHINI


Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis, amewasili nchini kwa ziara ya Kitaifa kuanzia leo tarehe 16 hadi 19 Novemba 2023 kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere amepokelewa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb.)

Lengo la ziara hiyo ni pamoja na kushawishi uwekezaji zaidi na kuvutia watalii wengi kutoka nchini Romania.

Aidha katika mazungumzo rasmi yatakayofanyika tarehe 17 Novemba 2023 Rais huyo na mwenyeji wake watajadili namna bora ya kukuza na kuimarisha ushirikiano kati sekta za elimu, afya, kilimo nishati na madini.

Kabla ya kuondoka nchini tarehe 19 Novemba 2023 Rais wa Romania atapata fursa ya kwenda Zanzibar ambapo atazungumza na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kutembelea Mji Mkongwe ambao ni moja kati ya vivutio vikubwa vya utalii duniani
Rais wa Romania Mheshimiwa Klaus Iohannis akiwapungia wananchi waliojitokeza kumlaki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis akiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb.) alipompokea wakati akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)

Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis kizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb.)  alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam

Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis kizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb.)  alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam
Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis akisalimiana na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samuel Shelukindo alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam

Wednesday, November 15, 2023

RAIS WA ROMANIA KUFANYA ZIARA YA KITAIFA NCHINI



 

“TANZANIA NI SEHEMU SALAMA KWA BIASHARA NA UWEKEZAJI” WAZIRI MAKAMBA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), amezihakikishia sekta binafsi na za umma nchini Uholanzi kuwa Tanzania ni sehemu salama ya biashara na kuwekeza.

Hayo yameelezwa wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uholanzi lililofanyika jijini The Hague, Uholanzi tarehe 14 Novemba 2023.

Kongamano hilo lililotanguliwa na mkutano wa ndani kati ya sekta za umma na binafsi za nchi hizo, ambapo zilitumia fursa hiyo kujadili kwa kina fursa zilizopo Tanzania pamoja na taratibu nyingine zinazotakiwa kufuatwa na wawekezaji na wafanyabiashara kutoka mataifa mengine.

Kongamano hilo lililokuwa na kauli mbiu isemayo “Ushirikiano sawa kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu” liliandaliwa na kuratibiwa na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini The Hague, Uholanzi kwa kushirikiana na Baraza la Biashara kati ya Uholanzi na Afrika (NABC).

Akifungua kongamano hilo Waziri Makamba pia alieleza kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka azma ya kutekeleza kwa vitendo dira ya Serikali ya kufanikisha ushindani na uanzishaji wa viwanda kwa maendeleo ya Taifa.

Kongamano likiendelea

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akihutubia katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uholanzi lililofanyika jijini The Hague, Uholanzi. Kongamano hilo limeratibiwa na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Baraza la Biashara kati ya Uholanzi na Afrika (NABC)

Picha ya pamoja meza kuu na wawakilishi kutoka sekta za umma za Tanzania na Uholanzi walioshiriki katika kongamano hilo.

Mjumbe wa kongamano kutoka Uholanzi akiwasilisha hoja zake kwa Waziri Makamba ili ziweze kufafanuliwa wakati wa kongamano hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akisalimiana na Mabalozi wa Afrika wanaowakilisha nchini Uholanzi waliposhiriki katika kongamano.

Mheshimiwa Waziri Makamba akishuhudia zoezi la kubadilishana Hati za Makubaliano ya Ushirikiano (MoUs) kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzani (TIC), Bw. Gilead Teri na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Biashara kati ya Uholanzi na Afrika, Bi. Rosmarijn Fens wakati wa kongamano hilo jijini The Hague, Uholanzi.


Tuesday, November 14, 2023

MCHAKATO HADHI MAALUM KWA DIASPORA KUKAMILIKA MWAKA 2024



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na Watanzania wanaoishi nchini Uholanzi katika kikao kilichofanyika jijini The Hague, Uholanzi ambapo amewasisitiza Watanzania hao kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Taifa lao.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kukamilisha utaratibu wa kuwapatia Hadhi Maalum Watanzania waishio nje ya nchi, yaani diaspora ifikapo mwaka 2024.

Hayo yamesemwa katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na diaspora wa Tanzania nchini Uholanzi kwa heshima ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) aliyepo nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 13 - 15 Novemba 2023.

Akifafanua masuala mbalimbali yaliyowasilishwa kupitia risala ya Watanzania iliyosomwa na Mwakilishi wa Umoja wa Watanzania waishio nchini Uholanzi, Bi. Sylvana Lubuva, Mhe. Makamba alisema utekelezaji wa Hadhi Maalumu unategemea kufanyika kwa mapitio ya baadhi ya sheria za nchi kama ile ya ardhi na uhamiaji ili kurahisisha utekelezaji wenye tija kwa walengwa, yaani diaspora na kwamba mchakato huo unatajiwa kukamilika kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

“Miongoni mwa masuala yatakayopewa kipaumbele kwenye Hadhi Maalum ni haki ya kurithi au kurithishwa mali kwa diaspora wa Kitanzania aishiye nje ya nchi. Ili kutekeleza hili kuna maeneo ya sheria yetu lazima yabadilishwe ili watoto wenu wanaoishi huku nje waweze kurithi au kumiliki ardhi” alisema Waziri Makamba.

Sambamba na hilo, ni utaratibu wa kulipa visa pindi diaspora wa Tanzania wanaporudi nyumbani. “Kwenye Hadhi Maalum, mtaruhusiwa kuja nyumbani na kukaa kwa muda mnaotaka bila malipo ya visa. Lakini kwanza ni lazima sheria yetu ya uhamiaji ipitiwe na kurekebishwa, ili kuruhusu kurudi nyumbani bila kulipishwa visa” alisisitiza Waziri Makamba.

Baadhi ya masuala mengine yatakayowanufaisha watumiaji wa Hadhi Maalum ni fursa na motisha mbalimbali za kuwekeza nchini Tanzania kupitia Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC). 

Kadhalika, Mheshimiwa Makamba alisisitiza umuhimu wa kujisajili kwenye mfumo wa Diaspora Digital Hub ambapo alisema licha ya kusaidia kuwatambua Watanzania waishio nje ya nchi, pia inarahisisha kwa kiasi kikubwa kuwarejesha nchini pindi majanga makubwa yanapotokea maeneo mbalimbali duniani. 

“Serikali ya Awamu ya sita chini ya uongozi imara wa Mama Samia Suluhu Hassan, imeelekeza kuokoa Mtanzania au Watanzania popote pale walipo pindi majanga yanapowakuta. Imefanya hivyo kuwaokoa Watanzania waliokua masomoni Ukraine, imewarejesha nyumbani Watanzania waliokuwa Sudan na hivi karibuni Israeli” Mhe. Makamba aliongeza.

Mazoezi haya ya kuwarejesha Watanzania nyumbani hufanyika chini ya uratibu wa Ofisi za Ubalozi zilizopo nchi husika au nchi jirani na hivyo huratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mhe. Makamba yupo nchini Uholanzi kwa ziara ya kikazi ambapo siku ya pili ya ziara hiyo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uholanzi.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka katika ofisi za Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uholanzi, jumla ya watanzania wapatao elfu tatu (3,000) wanaishi nchini Uholanzi na maeneo ya karibu.
Mambo ya Nje na Ushirikinao wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akisalimiana na baadhi ya watanzania wanaoishi nchini Uholanzi 
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Carilone Chipeta akifafanua jambo wakati wa mkutano wa Mheshimiwa Waziri na Diaspora uliofanyika jijini The Hague, Uholanzi.
Sehemu ya Watendaji wa  Wizara wakifuatilia mkutano wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Diaspora wa Tanzania nchini Uholanzi
Sehemu ya Watumishi wa  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano wa Waziri Makamba na Diaspora wa Tanzania nchini Uholanzi
Afisa Mwandamizi kutoka Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Ramadhan Mzuzuri akifafanua masuala mbalimbali yanayohusu Diaspora katika mkutano wa Mheshiwa Waziri na Diaspora uliofanyika jijini The Hague, Uholanzi.
Mambo ya Nje na Ushirikinao wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe aliofuatana nao katika ziara hiyo, watumishi wa ubalozi na watanzania wanaoishi nchini Uholanzi baada ya kumalizika kwa 
Sehemu ya Watumishi wa  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano wa Waziri Makamba na Diaspora wa Tanzania nchini Uholanzi