Wednesday, January 24, 2024

MAKAMU WA RAIS WA CUBA ATEMBELEA KIWANDA CHA VIUADUDU CHA KIBAHA

Makamu  Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Valdes Mesa amesema Serikali ya Cuba itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha  kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha  mkoani Pwani ili kiendelee kuhudumia Watanzania na nchi nyingine za Afrika.


Mhe. Mesa ametoa kauli hiyo leo tarehe 24 Januari 2024 alipotembelea Kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024.


Amesema nchi yake itaendelea kutoa msaada wa kitaalam kwa mamlaka za Tanzania ili kukiwezesha kiwanda hicho kuzalisha bidhaa tofautitouti mbali na viuadudu vya malaria,  zikiwemo mbolea, viuatilifu na bidhaa nyingine za kilimo


Pia amesema kiwanda hicho kitaendelea kuwa mfano wa ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Cuba katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.


“Nimepata bahati ya kukitembelea kiwanda hiki kwa mara ya pili sasa, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2016 wakati kinakamilishwa. Napongeza hatua iliyofikiwa kwenye uzalishaji” amesema Mhe. Mesa.



Amesema kiwanda hicho kinatakiwa kutunzwa kwani ni chanzo cha ajira kwa watanzania lakini pia kinakuza uchumi wa Tanzania pamoja na kuimarisha afya za watanzania.


Awali akizungumza kumkaribisha Mhe. Mesa katika kiwanda hicho, Mkuu wa Mkoa wa Pwani , Mhe. Abubakar Kunenge amesema kuwa anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda kwenye mkoa huo na kuwakaribisha wawekezaji zaidi kutoka Cuba kuja kuwekeza.


Miongoni mwa Viongozi wengine walioshiriki ziara ya Mhe. Mesa kwenye kiwanda hicho ni Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki, Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne Vera. 

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akimpokea Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa mara baada ya kuwasili katika kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani. Mhe. Mesa yupo nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024
Mhe. Mesa akiwa amepokelewa na Mhe. Dkt. Kijaji mara baada ya kuwasili kwenye kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Mhe. Dkt. Kijaji akitoa taarifa fupi kwa Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Mesa baada ya kuwasili kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Mhe. Meda akizungumza alipokitembelea kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani. Kiwanda hicho kimejengwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge akizungumza wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Mesa alipotembelea kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani.
Meza kuu
Waziri wa maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki akifuatilia hotuba ya Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Mesa alipotembelea kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani.


Viongozi na wageni waalikwa kutoka Mkoa wa Pwani walioshiriki ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba alipotembelea kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Mkutano ukiendelea

 

WAZIRI MAKAMBA ATETA NA WATUMISHI UBALOZI WA JAKARTA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akikaribishwa na Mtumishi wa Ubalozi Bw. Suleiman ......alipowasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi .

Balozi wa Tanzania nchini Indonesia Mhe. Makocha Tembele akimuwekea Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba kitabu cha wageni alipotembelea  Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi

 

Balozi wa Tanzania nchini Indonesia Mhe. Makocha Tembele akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba alipotembelea  Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumish
Mwakilishi wa watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Indonesia Bw. Suleiman .........akizungumza neno mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba  alipotembelea  Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi


 

Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Indonesia wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba  alipotembelea  Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi hao

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba ametembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi Ubalozini.

Akizungumza Ubalozini hapo Mhe. Makamba amewapongeza watumishi hao kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kuiwakilisha vyema Tanzania.

Aidha, amewasihi watumishi hao kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kuchapa kazi na kutimiza azma ya kuanzishwa Ubalozi huo na kufikia matarajio ya serikali kutoka kwao.

“Nyinyi ni wawakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Indonesia mna wajibu wa kuchapa kazi , kushirikiana na kuwa wamoja katika kushirikiana na  Indonesia na kufanya mambo yaende”, na kuongeza “mnatakiwa msiende kinyume na matarajio ambayo nchi inayo, nyinyi ni wawakilishi wa nchi kwa hiyo hulka, maneno, muonekano na vitendo vyenu lazima viakisi nchi yenu, na mhakikishe mnalilinda hilo,” alisisitiza Mhe. Waziri Makamba.

Alisema Tanzania inawategemea watumishi hao kuleta manufaa nyumbani kwa kuvutia biashara na wawekezaji na wadau wengine ambao watasaidia juhudi za kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

Amesema ziara ya Mhe. Rais nchini Indonesia ni bahati kubwa  kwa ubalozi huo kwakuwa mwaka jana ulimleta Rais wa Indonesia Tanzania na safari hiii umemleta Mhe. Rais Indonesia, “wenzenu wanamaliza muda wao bila kupata nafasi kama hii, hili ni jambo la kujivunia na mjipongeze kwa kazi nzuri.

Akiwa Ubalozini hapo Waziri Makamba amempongeza Balozi wa Tanzania nchini Indonesia Mhe. Makocha Tembele kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ubalozini hapo.

“Tunajivunia sana uwezo wako Jakarta, uendelee kuchapa kazi na hatutachoka kukusaidia itakapobidi kufanya hivyo,” alisema

Amesema ziara hizo za wakuu wa nchi ni jitihada za kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Indonesia ambao mwaka huu unatimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.

Ameongeza kuwa ziara hiyo pia inalenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika maeneo ya kımkakati ya biashara, uwekezaji, afya, elimu, uchumi wa buluu na kilimo na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kwa faida ya pande zote mbili.

Mhe. Makamba yuko nchini Indonesia kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itakayofanyika nchini humo tarehe 24-26 Januari, 2024.



 

MAKAMU WA RAIS WA CUBA ATEMBELEA TAASISI YA MWALIMU NYERERE NA KUMJULIA HALI MAMA MARIA NYERERE

Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa ametembelea Makao Makuu ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere yaliyopo jijini Dar es Salaam na kuzungumza na Wafanyakazi wa Taasisi hiyo pamoja na Wajumbe wa Umoja wa Urafiki wa Tanzania na Cuba.


Mara baada ya kuwasili, Mhe. Mesa alipokelewa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Bw. Joseph Butiku pamoja na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi hiyo, Mhe. Stephen Wasira.


Pamoja na mambo mengine Mhe. Mesa alipokea taarifa kuhusu utendaji wa Taasisi hiyo isiyo ya Serikali ambayo ilianzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kuhamasisha  amani, umoja na maendeleo ya watu pamoja na kuenzi mchango wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika utu na maendeleo ya watu pamoja na kutunza kumbukumbu mbalimbali za kazi zake ikiwemo vitabu, majarida, machapisho na picha.



Wakati huohuo, Mhe. Mesa amemtembelea, Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumsalimia na kumjulia hali.



Katika mazungumzo yao, Mhe. Mesa amemweleza Mama Maria kuwa amewiwa kumtembelea kama ishara ya kuenzi urafiki wa Tanzania na Cuba ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Fidel Castro na mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere katika kujenga amani, umoja na mshikamano na kuwa mstari wa mbele kwenye harakati za ukombozi kusini mwa Afrika. Kadhalika amemtakia afya njema na maisha marefu Mama Maria.


Kwa upande wake Mama Maria amemshukuru Mhe. Mesa kwa kutenga muda na kumtembelea.


Mazungumzo kati yao yalihudhuriwa pia na Watoto wa Hayati Baba wa Taifa akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku akimpokea Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa alipotembelea Taasisi hiyo tarehe 24 Januari 2024. Mhe. Mesa alifanya ziara ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024

Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akizungumza alipotembelea Taasisi ya Mwalimu Nyerere wakati wa ziara yake nchini
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku akimzawadia Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa vitabu na machapisho mbalimbali ya Hayati Mwalimu Nyerere alipotembelea Taasisi hiyo tarehe 24 Januari 2024.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku akizungumza wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa (kushoto) alipotembelea Taasisi hiyo tarehe 24 Januari 2024. Wengine katika picha ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (wa pili kushoto) na Balozi wa Tanzania nchini Cuba. Mhe. Humphrey Polepole.
Mhe. Mesa akiwa katika meza kuu na Mhe. Kairuki na Mhe. Polepole
Mkutano ukiendelea
Mkutano ukiendelea. Kulia ni Mhe. Stephen Wasira, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kushoto ni Prof. Shivji
Sehemu ya wanafunzi
Wageni waalikwa wakimsikiliza Mhe. Mesa
Mkutano ukiendelea


...............ZIARA YA MHE. MESA KWA MAMA MARIA NYERERE

Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akisalimiana na Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere alipomtembelea kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumsalimia na kumjulia hali. Mhe. Mesa yupo nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024
Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere ambaye pia ni mtoto wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere alipowatembelea kwenye makazi yao jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumsalimia na kumjulia hali Mama Maria Nyerere. Mhe. Mesa yupo nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024
Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akizungumza na Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere alipomtembelea kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumsalimia na kumjulia hali. Mhe. Mesa yupo nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole pamoja na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Vera
Mhe. Mesa akiwa katika picha ya pamja na Mama Maria Nyerer alipomtembelea nyumbani kwake jijini Dar es Salaam
Mhe. Makongoro akiwa na Wanafamilia wengine wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Mesa alipowatembelea
Mhe. Makongoro akizungumza 
Picha ya pamoja kati Mhe. Mesa, Mama Maria Nyerere na wanafamilia wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere






 

BALOZI FATMA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA JUMUIYA MBALIMBALI NCHINI OMAN

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Mohammed amekutana kwa nyakati tofauti na Viongozi wa Jumuiya ya Maimamu wa Kitanzania waliopo Oman pamoja na Uongozi wa Jumuiya ya Al-Wadood Charitable Group ya Oman waliomtembelea ofisini kwake jijini Muscat hivi karibuni.

Pamoja na mambo mengine, Jumuiya hizo zilimtembelea Balozi Fatma kwa lengo la kujitambulisha kwake rasmi  baada ya kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini humo pamoja na kuwasilisha maoni ya Jumuiya hiyo kuhusu ajira zao nchini Oman na changamoto wanazokabiliana nazo

Katika taarifa yao, maimamu wa kitanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Sheikh Zubeir Nkwavi waliwasilisha maoni kuhusu ajira zao nchini humo na changamoto wanazokabiliana nazo. Walieleza kuwa, Jumuiya hiyo ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 2020 imefanikiwa kusajili wanachama 88 wakiwemo maimamu na walimu katika misikiti mbalimbali nchini Oman. 

Pia Jumuiya hiyo imefanikiwa kuendesha shughuli  mbalimbali ikiwemo kusaidiana wakati wa misiba, kutoa michango wakati wa maafa, kuendesha mafunzo ya dini na kuanzisha mfuko wa akiba nchini humo.

Alisema kuwa pamoja na mafanikio hayo, Umoja huo unakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa Bima za Afya kwa wanachama wake, kukosa mlezi wa Jumuiya na kukosa udhamini wa masomo na kumuomba Mhe. Balozi Fatma kuwasaidia kutafuta suluhu ya changamoto hizo kwa kushirikiana na Serikali ya Oman.

Kwa upande wake, Mhe.  Balozi Fatma aliwashukuru Viongozi hao na kuwapongeza kwa kufanikiwa kupata ajira nchini Oman na hivyo kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini Tanzania. 

Kuhusu mikataba ya ajira alisema ipo haja ya kuwepo makubaliano baina ya Taasisi za Kidini za nchi mbili hizi ili  kuwa kuweka mustakbali mzuri wa ajira zao.

Kadhalika Balozi Fatma aliwaahidi viongozi hao kuwa,  atazungumza na Mamlaka husika za nchini Oman katika kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazowakabili pamoja na kusisitiza umuhimu wa kuwa na mikataba rasmi ya ajira ili kupata haki zinazostahili ikiwemo bima ya Afya, likizo na stahiki nyingine. 

Kwa upande wao, Jumuiya ya Al-Wadood Charitable Group ambayo inajihusisha na utoaji wa misaada kwa watu wenye mahitaji, wajane, wasiojiweza na yatima hapa nchini ikiongozwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Abdulqadir Al-Jahdhamy waliwasilisha  taarifa na mipango yao ya mwaka kuhusu utoaji wa misaada hiyo. 

Naye Mhe. Balozi Fatma ameishukuru Jumuiya hiyo kwa misaada yao nchini na kuwaomba kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kusaidia miradi mbalimbali ya kupunguza umasikini na ukali wa maisha kwa Watanzania. Pia amewaomba kusaidia kujenga mabweni katika mikoa yenye uhitaji hususan kwa wanafunzi wa kike. 

Jumuiya ya Al-Wadood Charitable Group pia imekuwa ikishiriki katika ujenzi wa misikiti, kutoa vifaa tiba, kuchimba visima na kugharamia masomo kwa Watanzania katika mikoa mbalimbali nchini

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab akimkabidhi nyaraka kiongozi wa Jumuiya ya Maimamu wa Kitanzania ukiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Zubeir Nkwavi  

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Mohammed akimkabidhi nyaraka Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Abdulqadir Al-Jahdhamy 

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab katika picha ya Pamoja na Uongozi wa Jumuiya ya Maimamu wa Kitanzania ulioongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Zubeir Nkwavi 

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Mohammed katika picha ya pamoja na Uongozi wa Jumuiya ya Al-Wadood Charitable Group Sheikh Abdulqadir Al-Jahdhamy (wa kwanza kulia) katika Ofisi za Ubalozi Oman


  









TANZANIA, CUBA KUIMARISHA SEKTA ZA KIPAUMBELE

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Cuba zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa maendeleo katika sekta za kipaumbele ambazo ni elimu, afya, kilimo na utalii.

Makubaliano hayo yameafikiwa wakati Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango alipokutana kwa mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya makubaliano hayo ilielezwa na viongozi hao wawili wakati wa mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Januari 2024.

Awali, viongozi hao walishuhudia utiaji saini wa Hati mbili za Makubaliano ya Ushirikiano (MoUs) ambazo ni makubaliano kati ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Chuo Kikuu cha Artimesa Diaz Gonzalez cha Cuba. 

Hati ya pili ya Makubaliano ni kati ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania(TMDA) na Kituo cha Afya cha Taifa cha Udhibiti na Vifaa Tiba (CECMED) cha Serikali ya Cuba kwa lengo la kupanua wigo na kuongeza matumizi ya teknolojia katika masuala ya dawa na vifaa tiba.

Kadhalika, Dkt. Mpango aliongeza kuwa, Serikali ya Cuba imekubali kuendelea kuimarisha kiwanda cha Viuatilifu cha Biotech, Kibaha, Pwani ambapo kwa sasa kitaanza kutengeneza dawa za binadamu na kilimo na kuwa kiwanda cha kipekee barani Afrika. 

“katika mazungumzo yetu tumekubaliana Cuba waje kuimarisha kiwanda cha Viatilifu cha Biotech cha Kibaha na kwa sasa kiwanda hicho kitaanza kutengeneza dawa za binadamu za aina zaidi ya 10 sambamba na kuongeza wigo wa masoko ukanda wa Afrika Mashariki,”alisema Dkt. Mpango.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria baina ya mataifa hayo uliodumu kwa muda mrefu. 

Kwa upande wa Makamu wa Rais wa Cuba, Salvador Mesa ameisifu Tanzania kwa kuitetea Cuba kimataifa na kusimama kupinga vikwazo wanavyowekewa vya kiuchumi na kusema imekuwa Nchi hizo ni ndugu na rafiki wa kweli.

“Tunaishukuru Tanzania kwa kutuunga mkono dhidi ya vikwazo tulivyowekewa vya kiuchumi, mmetutetea kupinga na kutaka vikwazo hivyo viondolewe ili kutuwezesha kutumia rasilimali zetu na kukuza uchumi,” alisema Mhe. Mesa.

Mhe. Mesa aliongeza kuwa lengo la ziara yake nchini ni kuimarisha na kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta ya elimu, afya, kilimo, siasa na utalii na kuwa Cuba itaendelea kukitangaza Kiswahili nchini humo na Ukanda wa Amerika ya Kusini.

Wakati huohuo, Mhe. Mesa amekutana kwa mazungumzo na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili masuala ya ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba. 

Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa wakishuhudia utiaji saini wa Hati za Makubaliano ya Ushikiano kati ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania(TMDA) na Kituo cha Afya cha Taifa cha Udhibiti na Vifaa Tiba (CECMED) cha Serikali ya Cuba, Ikulu Jijini Dar es Salaam. Hati hizo zimesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) Bw. Adam Fimbo na Naibu Waziri wa Afya wa Cuba, Mhe. Reinol Garcia Mareno

Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa wakiongea na waandishi wa habari Ikulu Jijini Dar es Salaam. 

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Cuba, Prof. Adianez Fernandez wakionesha (MoUs) walizosaini Jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akizungumza na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson katika Ofisi Ndogo za Bunge Jijini Dar es Salaam

Kikao cha Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akizungumza na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson kikiendelea katika Ofisi Ndogo za Bunge Jijini Dar es Salaam




NAIBU WAZIRI MKUU WA CHINA AHITIMISHA ZIARA YAKE NCHINI

Naibu Waziri Mkuu wa China, Mhe. Liu Guozhong amehitimisha ziara yake ya kikazi nchini aliyoianza tarehe 22 Januari 2024. 

Baada ya kuhitimisha ziara hiyo Mhe. Guozhong ameagwa na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (Mb.) ambaye aliambatana na viongozi wengine waandamizi wa Serikali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) tarehe 24 Januari 2024 jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (Mb.) (wa pili kushoto), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (katikati), Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini China, Khamis Omar wakimuaga Mhe. Gouzhong.

Wakiteta jambo wakati wa kumuaga Mhe. Gouzhong.

 

Tuesday, January 23, 2024

MAKAMU WA RAIS WA CUBA AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA KIKAZI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mhe. Salvador Valdés Mesa amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 23 - 25 Januari, 2024. 

Mara baada ya kuwasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Mesa alipokelewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb.)

Akiwa nchini, Mhe. Mesa atakutana kwa mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete na pia atatembelea Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Mhe. Mesa pia atamtembelea Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere pamoja na kutembelea kiwanda kinachozalisha dawa za viuadudu ya Biolarvicide cha Kibaha, Pwani.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mhe. Salvador Valdés Mesa akisalimiana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mhe. Salvador Valdés Mesa akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mhe. Salvador Valdés Mesa akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mhe. Salvador Valdés Mesa akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam