Friday, August 9, 2024
TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA MAWAZIRI WA OACPS
WAZIRI KOMBO AJITAMBULISHA KWA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akiwa katika picha na Viongozi na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki |
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) |
Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Yusuf Mndolwa akijitambulisha kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman |
Naibu Katinu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa akijitambulisha kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman |
WAZIRI KOMBO AJITAMBULISHA KWA RAIS WA ZANZIBAR
Picha ya pamoja |
Thursday, August 8, 2024
MAKATIBU WAKUU WA SADC WAKUTANA JIJINI HARARE
Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana Harare, Zimbabwe kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa 44 wa
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya husika utakaofanyika tarehe 17-18 Agosti,
2024.
Mkutano huo unatarajia kujadili masuala mbalimbali ikiwemo, hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC, usalama wa chakula na lishe kwenye kanda na Utekelezaji wa Mpango wa Manunuzi ya Pamoja ya Huduma za Afya ya SADC unaoratibiwa na Bohari ya Dawa (MSD) ya Tanzania.
Aidha, hafla ya
ufunguzi wa mkutano huo imewezesha makabidhiano ya nafasi ya unyekekiti katika
ngazi ya Mkutano wa Makatibu Wakuu ambapo Mwenyekiti aliyemaliza muda wake,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Balozi Nazaré José Salvador amekabidhi nafasi hiyo
kwa mwenyekiti mpya, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya
Kimataifa wa Jamhuri ya Zimbambwe, Balozi Albert Ranganai Chimbindi
akisisitiza kumpa ushirikiano katika nafasi hiyo.
Naye Balozi Chimbindi amemshukuru Mwenyekiti aliyemaliza muda
wake kwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Pia ameahidi kuzingatia ushauri
aliokuwa akiutoa kwa Sekretariet ya SADC na kufanya kazi pamoja ili kuyafikia
malengo ya jumuiya hiyo kwa maslahi jumuishi.
“Tumepiga hatua lakini bado tuna kila sababu ya kuweka bidii
kwenye ujenzi wa miundombinu, usafiri na hatimaye tuweze kuifikia SADC
tunayoitaka. Niwahakikishie kuwa Zimbabwe ipo tayari kufanya kazi pamoja nanyi
kwa kufuata malengo, kanuni na mikataba ya SADC'', Balozi Chimbindi.
Mkutano wa Wakuu wa
Nchi na Serikali SADC utatanguliwa na
mikutano ya awali kwa ajili ya maandalizi ambayo ni: Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi
ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics,
Defence and Security) utakaofanyika tarehe 16 Agosti 2018 ambao
utapitia na kujadili hali ya siasa, ulinzi na usalama katika kanda kwa
kipindi cha Agosti 2023 hadi Agosti 2024. Mkutano huu utahusisha nchi tatu za
SADC Organ TROIKA na wajumbe wake ambao ni Angola (Mwenyekiti wa sasa wa
Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama), Zambia (Makamu
Mwenyekiti wa Organ) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mwenyekiti wa Organ
aliyemaliza muda wa uenyekiti wa Asasi).
Mikutano mingine ni:
Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 14 Agosti 2024 pamoja;
na Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika
utakaofanyika kuanzia tarehe 8 hadi 11 Agosti, 2024.
===================================
Kushoto ni Afisa Sheria Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Felister Lero na Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Joseph Haule wakifatilia mkutano. |
Picha ya pamoja:
Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) baada ya
ufunguzi wa Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika
tarehe 8 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.
|
Monday, August 5, 2024
WAZIRI KOMBO APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO KUTOKA KWA MABALOZI WATEULE WA ZIMBABWE, ITALIA NA RWANDA NCHINI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) amepokea Nakala za Hati za Utambulisho
kutoka kwa Balozi Mteule wa Zimbabwe nchini, Mhe. Helen Bawange Ndingani, Balozi
Mteule wa Italia nchini, Mhe. Giuseppe Sean Coppola na Balozi Mteule wa Rwanda nchini,
Mhe. Jenerali Patrick Nyamvumba katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es
Salaaam tarehe 5 Agosti, 2024.
Akipokea nakala hizo Waziri Kombo amewapongeza mabalozi hao
kwa uteuzi waliuopata na pia amewaahidi ushirikiano katika utekelezaji wa
majukumu yao kwa kipindi watakachokuwa nchini kuziwakilisha nchi zao.
Aidha, ameeleza Mabalozi hao Wateule wanatarajiwa kuwasilisha
Hati za Utambulisho kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania tarehe 12 na 13 Agosti, 2024.
Akiongea na Balozi Mteule wa Zimbambwe nchini, Mhe. Ndingani,
Waziri Kombo ameeleza kuwa Tanzania na Zimbabwe zimekuwa na ushirikiano wa
kihistoria na kindugu ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo mawili Hayati, Mwl.
Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati, Robert Mugabe wa Zimbabwe.
Vilevile, akamkaribisha Mhe. Ndingani kutembelea Maktaba ya Hayati Mwl. Nyerere iliyopo Butiama, mkoani Mara ambayo imesheheni historia yake.
Balozi Kombo pia, akaeleza umuhimu wa kuwekeza na kurithisha
historia ya ukombozi kwa vijana ili waweze kufahamu kwa kina namna waasisi hao
walivyojitoa kupigania uhuru wa Bara la Afrika hususan harakati za ukombozi wa nchi
za Kusini mwa Afrika.
Viongozi hao pia wamejadili juu ya umuhimu wa kufanyika kwa Mkutano
wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zimbabwe ambapo
ameeleza kuwa Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano huo. Tanzania na
Zimbabwe zinashirikiana katika masuala ya biashara, uwekezaji, usafirishaji,
usalama wa chakula, mabadiliko ya tabia nchi, elimu, Sanaa na utamaduni, na
sekta nyingine za kisiasa.
Akizungumza na Balozi Mteule wa Italia nchini, Mhe. Coppola, Mhe. Waziri Kombo amesisitiza kuwa Tanzania ina nia ya dhati ya kuendeleza ushirikiano na nchi hiyo ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kupitia mpango wa ushirikiano wa Italia na Afrika unaofahamika kama “Mattei Plan”. Tanzania na Italia zinashirikiana katika sekta za utalii, elimu, Maji, biashara na uwekezaji, kilimo, mifugo na uvuvi, na kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na ngozi ili kukuza biashara yake kimataifa.
Tanzania na Italia zinatarajia kuwa na Kongamano la biashara
litakalofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Desemba, 2024 kwa lengo la kukuza
sekta ya biashara na za kiuchumi kwa maslahi mapana ya pande zote mbili amabapo,
pembezoni mwa kongamano hilo kutafanyika mashauriano ya kisiasa.
Vilevile, katika mazungumzo yake na Balozi wa Rwanda, Mhe. Jenerali,
Patrick Nyamvumba, Mhe. Waziri Kombo ameeleza kuwa Tanzania itaendelea
kushirikiana na Rwanda kupitia ujirani wa nchi hizo mbili sambamba na kusimamia
makubaliano mbalimbali yaliyokubaliwa katika nyakati tofauti na majukwaa mbalimbali
ambayo nchi hizo mbili zimekubaliana kuyatekeleza.
Tanzania na Rwanda zinashirikiana katika sekta za mawasiliano, biashara na uwekezaji, usafirishaji, elimu, utamaduni na michezo, miundombinu, kilimo na mifugo.
Jukumu hili la kupokea Nakala za Hati za Utambulisho
limefanywa na Mhe. Waziri Kombo kwa mara ya kwanza tangu aapishwe na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika nafasi
ya Waziri wa Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
=======================================
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka
kwa Balozi Mteule wa Zimbabwe nchini, Mhe. Helen Bawange Ndingani (Kushoto).
Mapokezi hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es
Salaaam tarehe 6 Agosti, 2024.
=======================================
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka
kwa Balozi Mteule wa Italia nchini, Mhe. Giuseppe Sean Coppola (Kushoto).
Mapokezi hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es
Salaaam tarehe 6 Agosti, 2024.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka
kwa Balozi Mteule wa Rwanda nchini, Mhe. Jenerali Patrick Nyamvumba
(kushoto). Mapokezi hayo yamefanyka katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es
Salaaam tarehe 5 Agosti, 2024.
Friday, August 2, 2024
WAZIRI KOMBO AMWAKILISHA RAIS SAMIA KWENYE UAPISHO WA RAIS WA IRAN
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akiagana na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mhe. Masoud Pezeshkian mara baada ya hafla ya chakula cha usiku kilichoandaliwa na Rais wa Iran kwa ajili ya wageni wake. |
Thursday, August 1, 2024
NAIBU KATIBU MKUU MAMBO YA NJE AFUNGUA MKUTANO KUJADILI ITIFAKI YA UMOJA WA AFRIKA KUHUSU UHURU WA WATU KUSAFIRI BILA VIKWAZO
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa ametoa wito kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika kuridhia Itifaki ya Uhuru wa Watu Kusafiri bila Vikwazo ili kurahisisha ufanyaji biashara baina ya nchi hizo kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).
Balozi Mussa ametoa wito huo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo na uzoefu kutoka Jumuiya za Kikanda na Umoja wa Ulaya uliofanyika leo Agosti 01, 2024 mjini Unguja, Zanzibar.
Amesema kuwa faida za Itifaki hiyo ni nyingi kwa watu wa Afrika ambapo mbali na kurahisisha usafiri wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine, lakini pia ni muhimu katika ukuzaji rasilimali watu na kutengeneza fursa kwa vijana kama vile biashara, utalii, kuimarisha utamaduni miongoni mwa watu na kwa kiasi kikubwa itakuza uchumi wa nchi za Afrika. Itifaki hiyo pia itawawezesha raia kutoka nchi za Afrika kuishi na kujenga uchumi kwa maendeleo endelevu ya Bara la Afrika.
Amesema mafanikio ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) ambao umeanza kutekelezwa na nchi wanachama tangu mwaka 2021, yatafikiwa kikamilifu pale nchi zote wanachama zitakaporidhia Itifaki hii ili kwenda sambamba na Itifaki nyingine za Uhuru wa Kuingiza Bidhaa na Uhuru wa Kutoa Huduma.
“Ninafurahi kwamba Nchi nyingi na Jumuiya za Kikanda za Kiuchumi kama EAC, ECOWAS, IGAD na SADC zimefanyia kazi Itifaki hii kupitia kanda zao na lengo ni kuongeza zaidi uhuru wa watu wa Afrika kutembea kutoka nchi moja kwenda nyingine”, amesema Balozi Mussa.
Pia amewataka wajumbe wa mkutano huo kujadili changamoto mbalimbali zinazokwamisha kuridhiwa kwa Itifaki hiyo ambayo ilipitishwa na nchi za Afrika mwaka 2018. Hadi sasa ni nchi nne pekee zimeridhia itifaki hiyo inayohitaji nchi 15 kuiridhia ili kuanza utekelezaji wake.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Balozi na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Shiyo amesema kuwa Mkutano huo utajikita katika kuainisha changamoto na nini kifanyike ili kuwezesha kuridhiwa na kuanza kutumika kwa Itifaki hiyo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Bara la Afrika hususan katika sekta ya ukuzaji biashara, utalii na uchumi kwa ujumla. Pia amesema wajumbe watajadili, kujifunza na kubadilishana uzoefu kutoka Jumuiya za Kikanda na nchi ambazo tayari zimeridhia Itifaki hiyo.
Naye Mkuu wa Idara ya masuala ya Kibinadamu na Harakati Huru kutoka AIJC, Mhe. Rita Amijkhobu amesema Itifaki hiyo ikianza kutumika itainganisha Afrika na kuwa kitu kimoja ambapo itawezesha watu kupita kwenye mipaka kwenda nchi nyingine bila vikwazo hatua itakayosaidia mzunguko wa biashara kukua kwa haraka.
Balozi na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Shiyo akizungumza na kuwakaribisha wageni waliokuja nchini kuhudhuria Mkutano wa majadiliano. |
Mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo ukiendelea. |