Tuesday, September 3, 2024

WAZIRI KOMBO AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KWENYE MKUTANO WA MAWAZIRI WA FOCAC.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo wakipitia nyaraka za mkutano wa Mawaziri wa FOCAC muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano huo. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (9th Ministerial Conference of the Forum on China-Africa Cooperation) uliofanyika tarehe 3 Septemba 2024 jijini Beijing, China.

Mkutano huo pamoja na masuala mengine umejadili na kupitisha agenda za Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC) unaotarajiwa kufanyika jijini humo kuanzia Septemba 4-6, 2024. 

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China ambaye pia ni mwenyeki mwenza wa mkutano huo Mhe. Wang Yi ameeleza kuwa ushirikiano wa China na Afrika hautazamwi kuwa ni wakindugu na urafiki pekee bali unalenga kuchagiza kasi ya maendeleo ya pande zote mbili kwa kutatua changamoto zinazokabili jamii.

Ameongeza kuwa FOCAC limekuwa jukwaa muhimu linalotoa fursa hadhimu kwa Viongozi wa China na Afrika kukutana na kujadili kwa pamoja masuala muhimu ya kimkakati kwa mustakabali mwema wa mataifa hayo na watu wake. 

Vilevile Waziri Wang ameeleza kuridhishwa kwake na kupongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa masuala yaliyokubaliwa katika mkutano wa 8 wa FOCAC uliofanyika jijini Dakar, Senegal ikiwemo kwenye sekta ya ujenzi wa miundombinu,viwanda na kilimo, biashara na uwekezaji, ubunifu na teknolojia. 

Kwa upande wake Waziri Mambo ya Nje wa Senegal ambaye pia ni mwenyeketi mwenza wa mkutano huo Mhe. Yacine Fall ameeleza kuwa China ni mshirika wa kimkakati wa maendeleo kwa Mataifa ya Afrika hivyo uhusiano wa kindungu uliopo kati ya pande hizo mbili unapaswa kudumishwa na kulindwa daima kwa manufaa ya pande zote mbili. 

Aidha, mkutano huo kwa kauli moja umepitisha rasimu ya agenda ya Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC, rasimu ya tamko na mpango wa utekelezaji na tathimini ya utekelezaji wa masuala yaliyofikiwa katika mkutano wa 8 wa FOCAC.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umejumuisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Khamis Mussa Omar na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Bi. Felista Lugabwa ukiongozwa na Waziri Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akifuatilia Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika jijini Beijing, China, tarehe 3 Septemba 2024.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Wang Yi akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika jijini Beijing, China, tarehe 3 Septemba 2024.
 Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika ukiendelea jijini Beijing, China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akifurahia jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Musalia Mudavadi muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika

Monday, September 2, 2024

WAZIRI KOMBO AWASILI NCHINI CHINA KUSHIRIKI FOCAC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili Jamhuri ya Watu wa China leo tarehe 2 Septemba 2024 kushiriki katika Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC) utakaofanyika jijini Beijing kuanzia tarehe 4 hadi 6 Septemba 2024.

Mkutano huo unaolenga kukuza ushirikiano na maendeleo ya pamoja kati ya China na Afrika utatanguliwa na mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika leo tarehe 2 Septemba 2024, ambapo Tanzania imekilishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samuel Shelukindo na ngazi ya Mawaziri tarehe 3 Septemba 2024.

Katika mkutano huo wa ngazi ya Mawaziri miongoni mwa masuala mengine, kipaumbele ni kujadili na kupitisha rasimu ya agenda ya Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC.

Agenda zingine ni pamoja na kufanya tathimini ya utekelezaji wa masuala yaliyofikiwa katika mkutano wa 8 wa FOCAC uliofanyika jijini Dakar, Senegal, na kujadili na kupitisha rasimu ya tamko na mpango wa utekelezaji. 

Mbali na kushiriki mkutano wa FOCAC, Waziri Kombo anatarajiwa kufanya mikutano ya pembezoni na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchini Algeria, Egypt na Libya ambapo watajadili masuala mbalimbali yanayolenga kudumisha na kukuza zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia. 

Mkutano huu unaofanyika kwa mara ya 9 tokea kuanzishwa kwake mwaka 2000, unaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kushirikiana ili Kuendeleza Usasa na Kujenga Jamii Bora ya China na Afrika kwa Mustakabali wa Pamoja”. Kauli mbiu hii inalenga kuwahamasisha Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na China kujadili kuhusu masuala muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika na China ili kuchagiza kasi ya maendeleo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing Waziri Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Khamis Mussa Omar na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian muda mfupi baada ya kuwasili jijini Beijing, China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian na Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Khamis Mussa Omar muda mfupi baada ya kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing, China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian muda mfupi baada ya kuwasili jijini Beijing, China.

Sunday, September 1, 2024

RAIS MWINYI AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA INDONESIA KUWEKEZA NCHINI KATIKA SEKTA YA UCHUMI WA BULUU

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha wawekezaji kutoka Indonesia na sehemu nyingine duniani kuja kuwekeza nchini katika Sekta ya Uchumi wa Buluu hususan kwenye maeneo ya Utalii, Bandari, Uvuvi na Kilimo cha Baharini, Uchukuzi na uchimbaji wa Mafuta na Gesi.

 

Mhe. Rais Mwinyi ametoa mwaliko huo wakati akifungua rasmi Jukwaa la Uwekezaji kati ya Zanzibar na Indonesia lililofanyika jijini Bali, Indonesia leo tarehe 1 Septemba, 2024.

 

Mhe. Rais Mwinyi ambaye yupo nchini hapa kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Jukwaa la Pili la Ushirikiano wa Indonesia na Afrika amesema, Indonesia ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa kwenye sekta ya uchumi wa buluu duniani na kwamba Tanzania imejipanga kunufaika kupitia sekta hiyo kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo wawekezaji kutoka Indonesia na kwingine duniani.

 

 “Tunaamini kwamba uzoefu uliowawezesha Indonesia kupiga hatua kubwa kwenye Sekta ya Uchumi wa Buluu utatuwezesha na sisi kujifunza na kufanikiwa. Hivyo tumekuja kuwaonesha na kujifunza  kutoka kwa wenzetu waliopiga hatua kwenye maeneo niliyozungumzia ikiwemo Uvuvi, kilimo cha mwani, uchukuzi, utalii na uchimbaji wa mafuta na gesi” amesema Mhe. Rais Mwinyi.

 

Awali akizungumza kwenye Kongamano hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Mhe. Pahala Mansury amesema Sera ya Mambo ya Nje ya Indonesia na ile ya Tanzania zinafanana kwa kiasi kikubwa ambapo zote zinasisitiza katika kuchochea maendeleo kupitia diplomasia ya uchumi. Hivyo, Kongamano hilo ni njia mojawapo ya kutekeleza sera hizo katika kuhamasisha uwekezaji na biashara ili kuinua uchumi wa nchi hizi mbili.

 

Pia alimshukuru Mhe. Rais Mwinyi na ujumbe wake kwa kushiriki Kongamano hilo ambalo linalenga kuangazia maeneo mapya ya ushirikiano baina ya Tanzania na Indonesia katika sekta ya uchumi wa buluu kwa manufaa ya pande mbili.

 

Wakati wa Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), mada mbalimbali kuhusu uwekezaji ziliwasilishwa na Taasisi za Tanzania ikiwemo ZIPA na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

 

Ujumbe wa Mhe. Rais Mwinyi ulioshiriki Jukwaa hilo unamjumuisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Sharif Ali Sharif, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Mhe. Amina Khamis Shaaban, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Mhe. Macocha Tembele pamoja na wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania na Indonesia.

 

Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika utafanyika jijini Bali, kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2024.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia lililofanyika jijini Bali tarehe 1 Septemba 2024 pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika litakalofanyika nchini hapa kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2024. Mhe. Rais Mwinyi alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Jukwaa hilo
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Mhe. Pahala Mansury akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde (kulia) akishiriki Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia. Kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi naye akishiriki Kongamano hilo. 
Mhe. Rais Dkt. Mwinyi akiwa ameongozana na Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Mhe. Macocha Tembele mara baada ya kuwasili kwa ajilio ya kushiriki Kongamano la  Biashara kati ya Zanzibara na Indonesia lililofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika
Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Silima Haji akishiriki Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Bw. John Kambona akiwa na Afisa Dawati kutoka Idara hiyo, Bw. Suleiman Magoma wakishiriki Kongamano la Biashara
Sehemu ya wafanyabiashara na wawekezaji wa Indonesia wakishiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Zanzibar na Indonesia
Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Indonesia, Bw. Suleiman Saleh akishiriki Kongamano hilo
Picha ya pamoja
 

Saturday, August 31, 2024

RAIS DKT. MWINYI AWASILI INDONESIA


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewasili jijini Bali,Indonesia leo tarehe 31 Agosti 2024 kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Pili la Indonesia na Afrika unaofanyika jijini hapa kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2024.

Mara baada ya kuwasili Mhe. Rais Mwinyi ambaye ameambatana na mwenza wake Mhe. Mama Mariam Mwinyi pamoja na Viongozi Waandamizi wa Serikali alipokelewa na Naibu Waziri  wa Biashara wa Indonesia Mhe, Jerry Sambuaga. 

Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika ambao utafanyika chini ya kaulimbiu isemayo "Bandung Spirit for Africa's Agenda 2063,” unalenga kuangazia kanuni za pamoja ambazo zimeweka msingi imara wa kuwa na uhusiano jumuishi, usawa na endelevu kati ya Indonesia na Afrika. 

Maeneo muhimu ya ushirikiano yanayotarajiwa kujadiliwa katika Jukwaa hilo ni pamoja na biashara, uwekezaji, kilimo na usalama wa chakula, nishati, uchumi wa buluu, madini, afya na ushirikiano wa maendeleo.

Mbali na kushiriki Mkutano huo, Mhe. Rais Mwinyi atafanya ziara ya kikazi nchini Indonesia kuanzia tarehe 04 hadi 06 Septemba 2024. 

 


Sunday, August 25, 2024

Ujumbe wa Tanzania washiriki Mazoezi ya ‘Walk the Talk’


Brazzaville, Congo 

25 Agosti 2024

 

Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, wameungana na mgombea wa Tanzania kwa nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Faustine Ndugulile (MB), katika mazoezi ya ‘Walk the Talk’.

 

Tukio hili la mazoezi ya ‘Walk the Talk’ lililofanyika Jijini Brazzaville, na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali waliowasili; lina lenga kuimarisha afya pamoja na kupiga vita magonjwa yasiyoambukiza. 

 

Wakiwa kwenye mazoezi hayo, Waziri Mhagama na Waziri Kombo walipata fursa ya kusalimiana na mawaziri wenzao  na kuwaomba kuunga mkono mgombea wa Tanzania Dkt. Ndugulile katika juhudi zake za kuwania nafasi hii muhimu, huku wakisisitiza umuhimu wa kuwa na maisha yenye afya na kufuata mifumo bora ya kuzuia magonjwa.

 

Wakati wa tukio hilo, viongozi hawa wa Tanzania walikuwa sehemu ya ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioandamana na Dkt. Ndugulile kwa ajili ya kumnadi na kumpigia kura katika uchaguzi wa Mkutano wa 74 wa WHO Kanda ya Afrika.

 

Ushiriki wa Tanzania kwenye mazoezi haya ni sehemu ya maandalizi na mkakati wa kuhakikisha kuwa Dkt. Ndugulile anapata uungwaji mkono kutoka kwenye nchi wanachama wa WHO, na pia kuonesha dhamira ya Tanzania katika kukuza afya ya jamii. 

 

Pamoja na Mawaziri hawa wawili, ujumbe wa Tanzania kwenye mazoezi hayo umejumuisha pia wabunge mahiri kwenye masuala ya chaguzi za kimataifa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni  Mwenyekiti wa Bunge Mhe. Dkt. Joseph Kizito Mhagama, pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Elibariki Emmanuel Kingu. Wengine ni Mhe. Neema Kichiki Lugangira, Mhe. Shamsia Azizi Mtamba, na Mhe. George Ranwell Mwenisongole.

 

Kauli Mbiu ya Dkt. Ndugulile kwenye kinyang’anyiro hiki ni “Pamoja, Tujenge Afya Bora Barani Afrika” yaani “Building a Healthier Africa Together” 



 


 

WAZIRI CHUMI ASHIRIKI MKUTANO MAALUM WA AFYA WA TICAD 9








Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi tarehe 24 Agosti 2024, ameshiriki mkutano Maalum wa afya pembezoni ya Mkutano wa Tisa wa TICAD ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo. Mkutano huo uliongozwa na mada ya Ushirikiano Mpya kwa Usawa wa Afya Barani Afrika: Kuharakisha Ufikaji wa Huduma za Afya kwa Wote kwa Ubunifu kuelekea 2030.” Mkutano huo uliandaliwa na Muungano wa Chanjo (GAVI) na Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ulilenga kuangazia umuhimu wa ushirikiano na ubunifu katika kufanikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote barani Afrika. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Bunge la Japani Mhe. Fukazawa Yoichi. Kwa kushiriki katika mkutano huo Tanzania ilipata fursa ya kujionea namna bora ya kutoa huduma za afya kwa watu wote ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hizo bila ya kikwazo cha kukosa hela.

WAZIRI CHUMI ASHIRIKI UZINDUZI WA LOGO YA SUMMIT YA TICAD9 2025 JAPAN

 





Tarehe 24 Agosti,2024, Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi ameshiriki katika hafla ya uzinduzi wa logo ya Mkutano wa Tisa wa TICAD wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika 2025 nchini Japan. 

Uzinduzi wa Logo hiyo ya Summit ya #TICAD9 umefanyika jijini Tokyo wakati wa Mkutano wa TICAD ngazi ya Mawaziri, ambao unafanya maandalizi ya Summit hiyo inayotarajiwa kufanyika tarehe 20 - 22 Agosti 2025, jijini Yokohama, Japan. Uzinduzi huo ullihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi za nchini
Japan ambao pia, walionesha huduma mbalimbali wanazozitoa katika nchi za Afrika. 

Katika tukio hilo, Mhe. Naibu Waziri Chumi akiambatana na Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda walipata nafasi ya kusalimiana na wadau wa taasisi na kampuni za Japan zenye ubia na Tanzania.

Saturday, August 24, 2024

TANZANIA YAZISIHI NCHI ZA AFRIKA KUSHIRIKIANA KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOZIKABILI NCHI ZAO

 

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akichangia mada ya Amani na Utulivu: kuhakikisha Heshima ya Binadamu na Usalama wa Binadamu kwenye sehemu ya pili ya Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia tarehe 24-25 Agosti 2024.

 


Waziri Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Yoko Kamikawa akifungua  Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia tarehe 24-25 Agosti 2024.

 

Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda akifatilia ufunguzi wa  Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia tarehe 24-25 Agosti 2024.

 

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 wakifuatilia mkutano huo


 

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 wakifuatilia mkutano huo

  

 

Washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa Mkutano huo

  

 

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa wito kwa nchi za Afrika kushirikiana kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo na changamoto mbalimbali zinazozikabili nchi hizo. Pia imemewahimiza wadau wote wa maendeleo kutoka nchini Japan kuendelea  kufanya biashara na kuwekeza zaidi barani Afrika ili kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya binadamu katika bara hilo ikiwa ni katika juhudi za kuendeleza amani na utulivu kikanda na kimataifa.

 

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi alipochangia mada ya Amani na Utulivu: kuhakikisha Heshima ya Binadamu na Usalama wa Binadamu kwenye sehemu ya pili ya Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika nchini Japan tarehe 24-25 Agosti 2024.

 

Ameipongeza Japan kwa kuwa mstari wa mbele kushiriki katika jitihada za kimataifa na kuwaomba washirika wengine wa kimataifa kuiga mfano huo na kuongeza kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa ushiriki sawa na ujumuishaji wa wanawake na wanaume, wasichana na wavulana katika kuhakikisha amani na usalama vinatamalaki.

 

Amesema kutokana na umuhimu huo Tanzania iko katika hatua za mwisho za kuandaa na kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji (NAP) kuhusu Wanawake, Amani na Usalama ikiwa ni utekelezaji wa Azimio Na. 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la mwaka 2000. 

 

Amesema siku zote Tanzania imekuwa na mchango muhimu katika  harakati za upatanishi, mazungumzo ya amani na njia nyingine za kidiplomasia katika kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa ndani na nje ya mipaka yake na ndio maana imefanikiwa kuondoa mizizi ya vita vya kikabila na migogoro kwa kuunganisha makabila takriban 126 na kutumia lugha moja ya Kiswahili kama lugha ya Taifa.

 

Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo Tanzania imeendelea na utamaduni wa kuwapatia hifadhi mamia ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi kutoka nchi jirani na zaidi na kwa sasa Tanzania inahifadhi wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi wapatao 237,997 huku wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.

 

Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe.Yoko Kamikawa umehudhuriwa na Mawaziri, washirika wa TICAD, wawakilishi na waandaaji wenza -Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Benki ya Dunia, Kamisheni ya Umoja wa Afrika na mashirika ya Kimataifa na kikanda, sekta binafsi na  Kiraia kutoka Japan na Afrika.

 

 

 

 

 

 

 

 






Friday, August 23, 2024

NAIBU WAZIRI CHUMI AKUTANA NA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JAPAN

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Kyoto Tsuji alipofika ofisini kwake jijini Tokyo kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Tisa wa ngazi ya Mawaziri wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika utakaofanyika nchini huko tarehe 24-25 Agosti, 2024


Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Kyoto Tsuji alipomtembelea ofisini kwake jijini Tokyo kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Tisa wa ngazi ya Mawaziri wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika utakaofanyika nchini huko tarehe 24-25 Agosti, 2024


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akizungumza alipomtembelea Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Kyoto Tsuji ofisini kwake jijini Tokyo. Wa kwanza kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda akifuatilia mazungumzo hayo


Mazungumzo yakiendelea






Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb) amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Kyoto Tsuji ofisini kwake jijini Tokyo.

Viongozi hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana ili kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Japan kwa manufaa ya pande mbili.

 
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Chumi aliishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kuchangia maendeleo ya Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, uwekezaji, elimu, na afya.

Amesema Tanzania imejipanga kuhakikisha inaongeza kiwango cha biashara na uwekezaji kati yake na Japan na hivyo kuchochea ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya pande zote mbili.

Naye, Mhe. Tsuji ameelezea utayari wa Japan kuendelea kushirikiana na Tanzania na kuimarisha uhusiano uliopo kwa manufaa ya nchi hizo.

Amesema Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania na kuongeza biashara na bara la Afrika ili kuhakikisha maendeleo ya kweli yanapatikana.

Mhe. Chumia yuko nchini Japan kuhudhuria Mkutano wa Tisa wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD) ngazi ya Mawaziri utakaofanyika jijini Tokyo tarehe 24-25 Agosti 2024.

 

TANZANIA KUSHIRIKI MKUTANO WA KIMATAIFA WA TOKYO KUHUSU MAENDELEO YA AFRIKA