Friday, September 20, 2024

NJE - SPORTS Netiboli YAANZA VIZURI SHIMIWI, YAIBAMIZA RAS LINDI

 


Timu ya netiboli ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje - Sports) imeanza kwa kishindo Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) baada ya kuitandika bila huruma Timu ya Ras Lindi kwa magoli 39 -16.

 

Kama wahenga wasemavyo Nyota njema huonekana asubui, katika mchezo huo nyota ya Nje - Sports Netiboli ilianza kuangaza tangu kipenga cha mwamuzi wa mchezo kilivyopulizwa, ikionyesha ustadi wao wa hali ya juu.

 

Akizungumza mara baada ya ushindi huo, Kapteni wa Netiboli Nje – Sport Bi. Faraja Kessy, amesema ushindi huo umetokana na maandalizi mazuri ya muda mrefu, hata hivyo mchezo ulikuwa na ushindani Mkubwa sana lakini tumeibuka na Ushindi Mnono. 

 

"Hakika tunafuraha sana kwa kuanza vizuri katika mchezo wetu wa kwanza wa netiboli. Na matarajio yetu ni kuendelea kufanya vyemza zaidi na kuweza kuibuka washindi katika Michezo hii ya SHIMIWI”. 

 

Vilevile, Bi. Faraja Kessy ameushukuru Uongozi na menejimenti ya Wizara kwa ujumla kwa namna ambavyo wamekuwa mstari wa mbele kutoa hamasa kwa wanamichezo na kuahidi kuendelea kufanya vyema katika michezo iliyobakia katika kundi letu.

 

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Michezo Nje – Sports, Bw. Ismail Abdallah ameendelea kuwapongeza na kuwapa hamasa zaidi wana michezo woote. “Kwakweli leo Mambo yako mazuri nifuraha sana kuona tokea asubui tunapata ushindi tuu”.

 

Kesho Tarehe 21 Septemba, 2024 Nje – Sports wanawake wanatarajia kurusha karata yao ya pili ambapo watamenyana na Mahakama, kwa upande wa Mpira wa Miguu Nje – Sports wanashuka dimbani kucheza mchezo wao wa kwanza ambao watachuana na Utumishi.









Nifuraha kweli kweli.







Nje - Sports Wanawake Kamba yaibuka na ushindi dhidi ya Ras Mara


 

Thursday, September 19, 2024

NJE - SPORTS YAJIGAMBA KUFANYA VYEMA KWENYE MASHINDANO YA SHIMIWI - MOROGORO


Ratiba ya makundi katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayoanza kufanyika mkoani Morogoro imetolewa hadharani, huku Timu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Wanaume (Nje-Sports) inatarajia kurusha karata yake ya kwanza tarehe 21 Septemba, 2024 kwa Kuvaana na Timu ya Ras Mara.

Mwenyekiti wa Nje - Sports Bw. Ismail Abdallah amesema kuwa katika mpira wa miguu, timu ya Nje Sports imepangwa kundi G pamoja na timu za Utumishi, Wizara ya Ujenzi, Ras Mara na Ras Lindi.

Ameeleza pia kuwa timu ya Nje – Sports Kamba (Ke) imepangwa katika kundi B na itapepetana na timu za Hazina, Kilimo na Ras Shinyanga, huku mpira wa Pete ikipangwa kundi H na itaumana na Mahakama, Maadili, na Ras Lindi.

Kwa upande wa Kocha wa Nje – Sports, Bw. Shabani Maganga amesema vijana wote wapo salama na wapo tayari kupambana katika mashindano hayo ili kuibuka na ushindi kwenye kila mchezo kutokana na ubora wa timu waliyonayo.

Leo jioni tarehe 19 Septemba, 2024, Nje Sports imeendelea kufanya mazoezi mepesi ya kujiandaa na mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kuanza kesho tarehe 19 Septemba, 2024.

Nje - Sports inayoshiriki katika michezo mbalimbali mwaka huu, ikiwemo Mpira wa Miguu Wanaume, Kamba wanawake, Mpira wa Pete, Bao, Karata, iliwasili mkoani Morogoro jumatatu tarehe 16 Septemba, 2024 na kuzua gumzo kwenye viunga na mitaa mbalimbali ya mjini Morogoro (Mji kasoro Bahari).



Wednesday, September 18, 2024

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA 11 WA TAASISI YA MERCK FOUNDATION AFRIKA ASIA LUMINARY

 





Balozi Shelukindo aongoza Kikao na Sekretarieti ya SADC

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, ameiongoza timu ya Tanzania ambayo ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-ORGAN)  katika siku ya pili ya kikao na Sekretarieti ya SADC.

Kikao hicho kilichoratibiwa na Bw. Terry Rose, Afisa Mkuu Kamati ya Siasa na Diplomasia ya SADC kimejikita katika kujadili masuala mbalimbali yahusuyo muundo wa kamati hiyo na majukumu yake ndani ya kanda ikiwemo uangalizi wa uchaguzi kwa nchi zinazotarajia kufanya uchaguzi. Nchi hizo ni pamoja na Jamhuri ya Msumbiji, Botswana, Namibia na Mauritius chini ya  Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC (SEOMs) na Baraza la masuala ya Uchaguzi la SADC (SEAC).

Aidha, Kikao hicho kimejadili masuala mengine ikiwemo utekelezaji wa maamuzi  yanayohusu siasa na diplomasia katika Kanda, sera na mikakati ya siasa na diplomasia pamoja na mifumo ya usuluhishi na kuzuia migogoro ili kuimarisha demokrasia na ushirikiano kati ya Nchi Wanachama  kupitia Baraza la Usuluhishi (MRG) na Jopo la Wazee (PoE).


 

Monday, September 9, 2024

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amwakalisha Rais Samia kwenye ufunguzi wa Jukwaa la 16 la Ununuzi wa Umma kwa nchi za Afrika Mashariki.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezitaka Mamlaka za Udhibiti na Ununuzi wa Umma Afrika Mashariki kuzingatia weledi, maadili na uwajibikaji ili kuleta ufanisi uliokusudiwa.


Dkt. Biteko ametoa agizo hilo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Jukwaa la 16 la Ununuzi wa Umma kwa nchi za Afrika Mashariki na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) lililofanyika  Septemba 9, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) cha jijini Arusha.


Mhe.Dkt. Biteko amesema Serikali inatambua kuwa fedha nyingi zinazotengwa kwenye bajeti yake kila mwaka zimekuwa zikitumika kwenye ununuzi wa umma na kuongeza kuwa Serikali imekuwa makini kuhakikisha fedha hizo zinapata usimamizi makini.


“Naomba Wizara ya Fedha mlisimamie hili na haya ni maelekezo ya Mhe. Rais. Majukwaa yaliyofanyika yote yametilia mkazo maadili, weledi, uwazi na uwajibikaji kwani bila ya maadili wananchi hawawezi kupata huduma, pia fedha nyingi zinazotengwa kwa ajili ya wananchi kupata huduma zinaamriwa na kundi hili na kama hatuna taasisi imara za ugavi na ununuzi hatutapata matokeo tarajiwa na hivyo  umasikini utaongezeka,” amesema Dkt. Biteko.


Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Dkt. Leonada Mwagike ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia kwa kufanya maboresho makubwa katika sekta ya ununuzi wa umma na hivyo kuleta tija na kuongeza uwajibikaji ili kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika.


Hafla ya ufunguzi wa Jukwaa  hilo la 16 la Ununuzi wa Umma kwa Nchi za Afrika Mashariki na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), umehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia maswala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Shaibu Mussa.


 Jukwaa hilo la  Ununuzi wa Umma kwa nchi za Afrika Mashariki na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) linafanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa AICC, jijini Arusha.

Saturday, September 7, 2024

RAIS SAMIA AWAHIMIZA DIASPORA KUWEKEZA NCHINI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Watanzania wakiwemo wafanyakazi, wanafunzi na wafanyabiashara wanaoishi nchini China (Diaspora) kwenye mkutano uliofanyika jijini Beijing, tarehe 06 Septemba, 2024.

· Atumia saa 7 kuongea na Wawekezaji na Viongozi wa Makampuni
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi nje ya Nchi (Diaspora) kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana katika sekta mbalimbali nchini. 

Rais Samia ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na Diaspora waishio nchini China katika mkutano uliojumuisha watanzania wanaofanya kazi nchini humo, wafanyabiashara na wanafunzi uliofanyika jijini Beijing tarehe 6 Septemba 2024.

Akizungumza na Diaspora hao waliojitokeza kwa wingi, wakionesha furaha na shauku kubwa ya kuzungumza na Rais Samia, aliwaeleza kuwa licha ya fursa lukuki za kiuchumi zilizopo nchini Serikali imefanya maboresho ya sera na sheria mbalimbali ili kutoa fursa na kutanua wigo kwa Diaspora kuwekeza nchini.

Rais Samia amezitaja fursa hizo zinazopatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi, viwanda, kilimo na madini. Aliongeza kufafanua kuwa, katika sekta ya ujenzi hivi sasa Serikali imeandaa utaratibu mahususi kwa Diaspora, unaowapa fursa ya kujengewa na kumiliki nyumba nchini. 

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaeleza Diaspora kuhusu hatua liyopigwa na Serikali katika kuboresha utoaji huduma za kijamii kwa Wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, na usafirishaji akitolea mfano wa treni iendayo kwa haraka (SGR) ambayo katika kipindi kifupi imeleta mageuzi makubwa kwenye sekta hiyo na ujenzi wake ukiwa unaendelea. Sekta zingine ni nishati, kilimo, maji, mawasiliano na ukuaji wa demokrasia.

“Nyumbani tuko vizuri, mfano sasa hivi safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma inachukua saa 3 hadi 4 pekee kwa kutumia treni yetu mpya tuliyoizindua hivi karibuni. Tumefanya maboresho makubwa ya sera na sheria ili kuwapa fursa ya kuendesha shughuli za kiuchumi kwa urahisi. Njoeni muwekeze nymbani”. Alisema Rais Samia.

Mbali na hayo amepongeza juhudi na uzalendo unaoendelea kuonyeshwa na Diaspora katika kuchangia shughuli za maendeleo nchini ikiwemo kuleta watalii, wawekezaji na kusaidia kuratibu shughuli za matibabu. Aliongeza kusema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la fedha zinazotumwa nyumbani (remittance) kutoka ughaibuni,

Vilevile, Rais Samia ametoa wito kwa Diaspora wa nchini humo na kwa nchi zingine, hususan kwa jamii ya wanafunzi kujiandisha katika vyama vyao vya Jumuiya kwenye maeneo waliyopo. Akasisitiza kuwa hatua hiyo hiyo, licha kusadia kutambuana na kukuza umoja wao inarahisisha namna ya kuwafikia wanapohitaji huma mbalimbali hasa wakati zinapotokea changamoto ikiwemo majanga kama vile mlipuko wa magonjwa. 

Katika hatua nyingine Rais Samia akiwa jijini Beijing amekutana na kufanya mazungumzo na Wawekezaji na Viongozi wa Makampuni Sita (6) makubwa ya nchini humo ikiwemo China Academy of Space Corporation (CASC), China Electronics Corporation, Transsion Group, Weihua Group, China Railway Construction Corporation (CRCC), Acme Consultant Engineers PTE Limited na CND jijini Beijing, tarehe 06 Septemba, 2024.

Katika zoezi hilo alilolifanya kwa takribani saa 7 mfulilulizo bila mapunziko, aliambatana na Watendandaji na Mawaziri wanaosimamia sekta mbalimbali wakiwemo; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo (Mb.), Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb.), Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar Mhe. Omar Said Shaaban, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mb.), Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega (Mb.).

Wengine ni Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (Mb.) Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohamed Khamis Abdullah na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Bw. Gilead Teri.

Rais Samia alikuwa nchini China kushiriki Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika tarehe 4-6 Septemba 2024. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo akifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza Diaspora kwenye mkutano uliofanyika jijini Beijing.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo,akifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza na watazania wanaoishi nchini China (Diaspora) kwenye mkutano uliofanyika jijini Beijing.
 Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia katika Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Felista Rugambwa (katika) akifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza na watazania wanaoishi nchini China (Diaspora) kwenye mkutano uliofanyika jijini Beijing.

Matukio mbalimbali katika mkutano kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Watanzania waishio nchini China (Diaspora) uliofanyika Jijini Beijing tarehe 06 Septemba, 2024.






Matukio mbalimbali wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika mazungu na Wawekezaji na Viongozi wa Makampuni mbalimbali ya China Academy of Space Corporation (CASC), China Electronics Corporation, Transsion Group, Weihua Group, China Railway Construction Corporation (CRCC) pamoja na Acme Consultant Engineers PTE Limited na CND ya nchini China jijini Beijing, China tarehe 06 Septemba. 



Thursday, September 5, 2024

CHINA KUTOA USD 50 BILIONI KUSAIDIA MAENDELEO AFRIKA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika jijini Beijing, China.


· Asisitiza kutoingilia masuala ya ndani ya nchi
· Ahaidi hakuna Taifa likakalosalia nyuma katika safari ya maendeleo
· Ataja vipaumbele 10 vya ushirikiano wa kimkakati na Afrika

Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Xi Jinping ametangaza kutoa kiasi cha dola za Marekani bilioni 50 zitakazo elekezwa kusaidia masuala mbalimbali ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa mataifa ya barani Afrika. 

Ahadi hiyo imetolewa leo tarehe 5 Septemba 2024 alipokuwa akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) jijini Beijing. 

Akifungua mkutano huo Rais Xi Jinping ameeleza kuwa kiasi hicho kitaelekezwa katika sekta mbalimbali kwa lengo la kuchagiza maendeleo ya pande zote mbili bila kuathiri misingi na taratibu za Taifa husika. Aidha, aliongeza kusema kwamba kiasi hicho cha fedha kitaelekezwa katika maeneo kumi (10) ya kipaumbele ya ushirikiano wa kimkakati na Afrika. Aliendelea kwa kuhimiza umuhimu wake katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na usasa huku akisisitiza kuwa hakuna Taifa litakalo baki nyumba katika maendeleo hayo. 

Rais Xi Jinping ameyataja maeneo hayo ya ushirikiano wa kimkakati kuwa ni ubia katika ushirikiano wa maendeleo (partnership action for development cooperation), Afya (partnership action for health), kilimo na ustawi (partnership action for agriculture and livelihood), mwingiliano wa watu na watu (partnership action for people to people exchanges), maendeleo ya kijani (partnership action for green development) na masuala ya ulinzi na usalama (partnership action for common security). 

Maeneo mengine yaliyoainishwa ni ushirikiano katika viwanda (partnership action for industrial chain cooperation), mawasiliano (partnership action for connectivity), ubia katika kukuza biashara (partnership action for trade prosperity) na ubia katika mafunzo (Partnership Action for Mutual Learning among Civilizations).

Aidha Rais Xi Jinping amefafanua kuhusu mgawanyo wa dola za Marekani bilioni 50 zitakazotolewa kama ifuatavyo, bilioni 29 zitaelekezwa katika mikopo, bilioni 11 zitaelekezwa kwenye misaada ya aina mbalimbali na bilioni 10 zitaelekezwa katika uwekezaji kupitia makampuni ya China yatakayoenda kuwekeza katika Nchi mbalimbali barani Afrika.

Ni zama mpya za ushirikiano na usasa kati ya China na Afrika, ushirikiano na urafiki wetu uliodumu katika miongo mingi na kuleta aina mpya ya ubia na ushirikiano katika jumuiya ya mataifa sasa tumefanikiwa kufika katika hatua ya juu ya ushikiano wa kimkakati. Nawahakikishia ninyi wote ndugu na marafiki zangu tuliokusanyika hapa kuwa hakuna Taifa lolote litakalo salia nyuma katika safari hii ya usasa (modernization).Ameeleza Rais Xi Jinping. 



Mbali na hayo Rais Xi Jinping ametaja hatua kadhaa zinazotarajiwa kuchukuliwa na Serikali yake katika kipindi cha miaka 3 ijayo (2025-2027) katika kufikia adhima yake ya kusaidia kuleta mageuzi ya maendeleo na usasa barani Afrika ikiwemo utekelezaji wa miradi 30 ya nishati safi, miradi 30 ya mawasiliano, programu 500 za kilimo cha kisasa na kutoa fursa 60,000 za mafunzo hasa kwa vijana na wanawake. 

Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amehutubia mkutano huo ambao ulipata mwitikio mkubwa kutoka kwa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika, viongozi na watendaji kutoka Taasisi na Mashirika mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa, huku ukifuatiliwa na mamilioni ya watu kote duniani. Rais Samia amehutubia mkutano huo akiwakilisha kanda ya Afrika Mashariki.

Katika hotuba yake Rais Samia ameeleza kuhusu umuhimu wa ushikirikiano wa kimkakati katika kuchagiza maendeleo na kutoa wito kwa pande zote mbili kuendelea kuunganisha nguvu ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Marais wengine kutoka Afrika waliohutubia mkutano huo ni pamoja na Mheshimiwa Matamela Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Bassirou Diomaye Faye wa Senegal, Mheshimwa Mohamed Ould Ghazouani wa Mauritania, Mheshimiwa Denis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Congo na Mheshimiwa Bola Ahmed Adekunle Tinubu wa Nigeria. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali wanaoshiriki Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika jijini Beijing, China tarehe 05 Septemba, 2024
Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Xi Jinping akifungua Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika jijini Beijing, China, tarehe 05 Septemba, 2024

Wednesday, September 4, 2024

HATI YA MAKUBALIANO YA KUBORESHA RELI YA TAZARA YASAINIWA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping na Rais wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema kwa pamoja wameshuhudia uwekaji saini wa hati ya makubaliano (MoU) ya kuboresha reli ya TAZARA uliofanyika katika ukumbi wa The Great Hall of the People jijini Beijing, tarehe 4 Septemba, 2024.

Kwa upande wa Tanzania zoezi la uwekaje saini limefanywa na Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping pamoja na Rais wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema wakishuhudia uwekaji saini wa hati ya makubaliano ya kuboresha reli ya TAZARA katika ukumbi wa The Great Hall of the People jijini Beijing, tarehe 4 Septemba, 2024.

RAIS SAMIA AFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS WA CHINA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa ameambatana na ujumbe wake amefanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Xi Jinping katika ukumbi wa The Great Hall of the People jijini Beijing, Septemba 4, 2024.

Katika mazungumzo hayo Rais wa China Mheshimiwa Xi Jinping ameutaja uhusiano wa Tanzania na China kuwa ni wa mfano barani Afrika.

Mheshimiwa Rais Samia yupo nchini China kushiriki Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC)













Tuesday, September 3, 2024

WAZIRI KOMBO AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KWENYE MKUTANO WA MAWAZIRI WA FOCAC.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo wakipitia nyaraka za mkutano wa Mawaziri wa FOCAC muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano huo. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (9th Ministerial Conference of the Forum on China-Africa Cooperation) uliofanyika tarehe 3 Septemba 2024 jijini Beijing, China.

Mkutano huo pamoja na masuala mengine umejadili na kupitisha agenda za Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC) unaotarajiwa kufanyika jijini humo kuanzia Septemba 4-6, 2024. 

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China ambaye pia ni mwenyeki mwenza wa mkutano huo Mhe. Wang Yi ameeleza kuwa ushirikiano wa China na Afrika hautazamwi kuwa ni wakindugu na urafiki pekee bali unalenga kuchagiza kasi ya maendeleo ya pande zote mbili kwa kutatua changamoto zinazokabili jamii.

Ameongeza kuwa FOCAC limekuwa jukwaa muhimu linalotoa fursa hadhimu kwa Viongozi wa China na Afrika kukutana na kujadili kwa pamoja masuala muhimu ya kimkakati kwa mustakabali mwema wa mataifa hayo na watu wake. 

Vilevile Waziri Wang ameeleza kuridhishwa kwake na kupongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa masuala yaliyokubaliwa katika mkutano wa 8 wa FOCAC uliofanyika jijini Dakar, Senegal ikiwemo kwenye sekta ya ujenzi wa miundombinu,viwanda na kilimo, biashara na uwekezaji, ubunifu na teknolojia. 

Kwa upande wake Waziri Mambo ya Nje wa Senegal ambaye pia ni mwenyeketi mwenza wa mkutano huo Mhe. Yacine Fall ameeleza kuwa China ni mshirika wa kimkakati wa maendeleo kwa Mataifa ya Afrika hivyo uhusiano wa kindungu uliopo kati ya pande hizo mbili unapaswa kudumishwa na kulindwa daima kwa manufaa ya pande zote mbili. 

Aidha, mkutano huo kwa kauli moja umepitisha rasimu ya agenda ya Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC, rasimu ya tamko na mpango wa utekelezaji na tathimini ya utekelezaji wa masuala yaliyofikiwa katika mkutano wa 8 wa FOCAC.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umejumuisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Khamis Mussa Omar na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Bi. Felista Lugabwa ukiongozwa na Waziri Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akifuatilia Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika jijini Beijing, China, tarehe 3 Septemba 2024.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Wang Yi akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika jijini Beijing, China, tarehe 3 Septemba 2024.
 Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika ukiendelea jijini Beijing, China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akifurahia jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Musalia Mudavadi muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika

Monday, September 2, 2024

WAZIRI KOMBO AWASILI NCHINI CHINA KUSHIRIKI FOCAC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili Jamhuri ya Watu wa China leo tarehe 2 Septemba 2024 kushiriki katika Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC) utakaofanyika jijini Beijing kuanzia tarehe 4 hadi 6 Septemba 2024.

Mkutano huo unaolenga kukuza ushirikiano na maendeleo ya pamoja kati ya China na Afrika utatanguliwa na mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika leo tarehe 2 Septemba 2024, ambapo Tanzania imekilishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samuel Shelukindo na ngazi ya Mawaziri tarehe 3 Septemba 2024.

Katika mkutano huo wa ngazi ya Mawaziri miongoni mwa masuala mengine, kipaumbele ni kujadili na kupitisha rasimu ya agenda ya Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC.

Agenda zingine ni pamoja na kufanya tathimini ya utekelezaji wa masuala yaliyofikiwa katika mkutano wa 8 wa FOCAC uliofanyika jijini Dakar, Senegal, na kujadili na kupitisha rasimu ya tamko na mpango wa utekelezaji. 

Mbali na kushiriki mkutano wa FOCAC, Waziri Kombo anatarajiwa kufanya mikutano ya pembezoni na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchini Algeria, Egypt na Libya ambapo watajadili masuala mbalimbali yanayolenga kudumisha na kukuza zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia. 

Mkutano huu unaofanyika kwa mara ya 9 tokea kuanzishwa kwake mwaka 2000, unaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kushirikiana ili Kuendeleza Usasa na Kujenga Jamii Bora ya China na Afrika kwa Mustakabali wa Pamoja”. Kauli mbiu hii inalenga kuwahamasisha Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na China kujadili kuhusu masuala muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika na China ili kuchagiza kasi ya maendeleo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing Waziri Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Khamis Mussa Omar na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian muda mfupi baada ya kuwasili jijini Beijing, China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian na Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Khamis Mussa Omar muda mfupi baada ya kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing, China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian muda mfupi baada ya kuwasili jijini Beijing, China.