Tuesday, May 13, 2014

Waziri Membe awasili Malawi kumwakilisha Mhe. Rais Kikwete kwenye mazishi ya aliyekuwa Balozi wa Malawi nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Blantyre nchini Malawi kwa ajili ya kushiriki mazishi ya aliyekuwa Balozi wa Malawi nchini Tanzania, Marehemu Flossie Gomile-Chidyaonga aliyefarikii dunia tarehe 09 mei, 2014 Jijini na Dar es Salaam na anatarajiwa kuzikwa tarehe 14 Mei, 2014. Mhe. Membe anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye mazishi hayo.
Balozi wa Tanzania nchini Malawi,  Mhe. Patrick Tsere akimweleza jambo Mhe. Membe wakati wa mapokezi.
Mhe. Membe akijaribu kumwelezea Rais wa Malawi, Mhe. Joyce Banda namna alivyozipokea taarifa za kifo cha Balozi Flossie. Kushoto kwa Mhe. Rais Banda ni mume wake Jaji Mkuu Mstaafu Banda na kulia kwa Mhe. Membe ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Ephraim Chiume.
Baadhi ya Wananchi wa Blantyre na sehemu nyingine za Malawi wakiwa uwanjani hapo wakati wa mapokezi ya Mwili wa aliyekuwa Balozi wa Malawi nchini Tanzania, Marehemu Flossie Gomile-Chidyaonga.
Mhe. rais Banda akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John Haule.
Mhe. Rais Banda akisalimiana na Balozi Vincent Kibwana, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mhe. Rais Banda akisalimiana na Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania pamoja na Mabalozi wengine waliofutana na Mhe. Membe nchi Malawi kwenye mazishi ya Marehemu Balozi Flossie.
Mhe. Rais Banda akimtambulisha kwa Mhe. Membe Mtoto pekee wa Marehemu Balozi Flossie-Gomile-Chidyaonga.

Mhe. Rais Banda, Mhe. Membe, Mhe. Chiume na Wajumbe wengine wakisubiri jeneza lililobeba mwili wa marehemu Balozi Flossie kuteremshwa kwenye ndege kwa ajili ya taratibu zingine.
Jeneza lililobeba mwili wa Marehemu Balozi Flossie likiwa limeteremshwa kwenye ndege.
Mhe. Rais Banda akihutubia mara baada ya mapokezi ambapo alitoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano.
Mhe. Membe nae akizungumza machache.
Wananchi wakifuatilia hotuba.
Mwakilishi wa Familia ya  Marehemu Balozi Flossie nae akizungumza kwa niaba ya familia hiyo.
Kwaya ikiimba wakati wa shughuli hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) amemtaja aliyekuwa Balozi wa Malawi nchini Tanzania Marehemu Flossie-Gomile Chidyaonga kama Malkia wa Amani kwa vile alikuwa mstari wa mbele katika vikao vya usuluhishi na kutafuta amani kwenye Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Malawi ikiwa ni Mwenyekiti wa jumuiya hiyo.
Mhe. Membe aliyasema hayo wakati wa mapokezi maalum ya Marehemu Balozi Chidyaonga yaliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Blantayre nchini Malawi na kuhudhuriwa na Rais wa Malawi, Mhe. Joyce Banda, Viongozi wa Serikali ya Malawi, Familia ya Marehemu, Taasisi za Dini, Mabalozi na Wananchi kutoka sehemu mbalimbali za mji huo.

Mhe. Membe ambaye anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete kwenye mazishi ya Marehemu Balozi Flossie Gomile-Chidyaonga alisema kwamba Tanzania, Malawi, nchi za SADC na dunia kwa ujumla imempoteza mwanadiplomasia mahiri ambaye aliujua na kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

“Kwa niaba ya Mhe. Rais Kikwete, Watanzania wote na mimi binafsi nakuomba Mhe. Rais Banda na Wananchi wa Malawi mpokee salamu zetu za pole kwa kumpoteza Balozi Flossie ambaye alikuwa mstari wa mbele katika masuala ya amani kwa Kanda ya SADC na ninamwita Malkia wa Amani kwa juhudi hizo alisema Mhe. Membe”.

Mhe. Membe aliongeza kusema kwamba kutokana na kufanya kazi kwa kujituma na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi, Marehemu  Balozi Flossie alikubalika Serikalini, kwa Mabalozi wenzake na hata katika Taasisi za Elimu ya Juu kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alishiriki katika kutoa mihadhara mara kwa mara.

Katika hotuba yake wakati wa mapokezi hayo, Rais wa Malawi Mhe. Joyce Banda alisema kuwa wameupokea msiba huo wa ghafla kwa majonzi makubwa ambapo kwa namna ya pekee aliishukuru Serikali ya Tanzania hususan Rais Kikwete kwa ushirikiano wa hali ya juu aliouonesha tangu msiba utokee na kutuma ujumbe mzito uliioongozwa na Waziri Membe kumsindikiza Marehemu Flossie nchini Malawi.

“Mimi binafsi na wananchi wa Malawi tunatoa shukrani za dhati kwa ndugu zetu Watanzania hususan  Mhe. Rais Kikwete kwa ushirikiano walioonesha katika kipindi hiki kigumu kwetu. Mhe. Rais Kikwete aliwasiliana na mimi akiwa safarini mara tu msiba ulipotokea. Alielezea kushtushwa na msiba huo wa ghafla kama mimi nilivyoshtushwa. Nilimweleza azma ya Serikali yangu kuhusu kutuma ndege kwa ajili ya kuufuata mwili wa ndugu yetu Flossie lakini alisema nimwachie  hilo ni jukumu lake na amelitekeleza kikamilifu kama tunavyoona” alisema kwa masikitiko Mhe. Banda.

Awali akizungumza kwa niaba ya Familia ya Marehemu Balozi Flossie, Msemaji wa Familia hiyo Bw. Andrew  naye aliishukuru Serikali ya Tanzania na kusema kuwa ushirikiano uliooneshwa katika kipindi hiki kigumu kwao unadhihirisha undugu mkubwa uliopo kati ya Tanzania na Malawi.

Baadhi ya Viongozi wa Serikali na Mabalozi waliofuatana na Mhe. Mhe. Membe kwenye msiba huu ni pamoja na Bw. John Haule, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Balozi Vincent Kibwana, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Kaimu Mkuu wa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania ambaye pia ni Balozi wa Zimbabwe, Balozi wa Zambia nchini, Mhe. Judith Kangoma, Balozi wa Norway nchini na Maafisa wa Ubalozi wa Malawi nchini.

Marehemu Balozi Flossie Gomile-Chidyaonga ambaye alifariki dunia katika Hospitali ya Aga Khan Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Mei, 2014 anatarajiwa kuzikwa katika Mji wa Blantyre nchini Malawi tarehe 14 Mei, 2014.



Monday, May 12, 2014

Waziri Membe ashiriki kuuaga mwili wa aliyekuwa Balozi wa Malawi nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akisaini kwa masikitiko makubwa Kitabu cha Maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Balozi wa Malawi hapa nchini, Hayati Flossie Gomile-Chidyaonga kilichotokea kwenye Hospitali ya Aga Khan Jijini Dar es Salaam tarehe 09 mei 2014.
Mhe. Membe akisalimiana na baadhi ya Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini kabla ya kuanza kwa shughuli za kuuaga mwili wa aliyekuwa Balozi wa Malawi hapa nchini Marehemu Flossie Gomile-Chidyaonga. Shughuli hiyo ilifanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Mei, 2014.
Mhe. Membe akizungumza wakati wa kuuaga mwili wa  aliyekuwa Balozi wa Malawi hapa nchini Marehemu Flossie Gomile-Chidyaonga. Mhe. Membe alimwelezea Hayati Balozi Flossie kama mtu aliyependa amani, mcheshi na msikivu. Alisema Hayati Balozi Flossie alikuwa mstari wa mbele katika suala la mgogoro kati ya Tanzania na Malawi kuhusu Mpaka katika Ziwa Nyasa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. John Haule (wa pili kutoka kulia mstari wa kwanza) akiwa  na Balozi Vincent Kibwana  kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Afrika  pamoja na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini na  Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wakifuatilia hotuba ya Mhe. Membe (hayupo pichani) wakati akimwelezea Hayati Balozi Flossie.

Baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakifuatilia hotuba ya Mhe. Membe (hayupo pichani) wakati wa kuuaga mwili wa aliyekuwa Balozi wa Malawi hapa nchini Hayati Flossie Gomile-Chidyaonga.
Mhe. Membe akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Balozi wa Malawi hapa nchini Hayati Flossie Gomile-Chidyaonga. 
Balozi wa Zambia hapa nchini, Mhe. Judith Kangoma Kapijimpanga akishindwa kujizuia wakati wa kuuaga mwili wa aliyekuwa Balozi wa Malawi hapa nchini Hayati Flossie Gomile-Chidyaonga.
Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi kutoka Serikalini, Taasisi Binafsi na watu mbalimbali wakiuaga mwili wa aliyekuwa Balozi wa Malawi hapa nchini Hayati Flossie Gomile-Chidyaonga.
Picha na Reginald Philip

Mhe. Membe amwakilisha Mhe. Rais Kikwete kushuhudia uwekaji saini mkataba wa ujenzi wa Reli kati ya Kenya na China

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) wa tatu kutoka kushoto waliosimama) kwa pamoja na viongozi wengine   akiwemo Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame, Waziri Mkuu wa China, Mhe. Li Keqiang, Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Museveni na Rais wa Sudan Kusini, Mhe. Salva Kiir wakishuhudia kusainiwa kwa Mkataba wa Ujenzi wa Reli ya kisasa  Afrika Mashariki kati ya Serikali ya Kenya na China. Mhe. Membe alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

Mhe. Membe wakati wa mkutano kabla ya mkataba kusainiwa.

Waziri Membe akimsikiliza Waziri Mkuu wa China, Mhe. Li Keqiang wakati wa mazungumzo.

Mkutano wa viongozi ukiendelea.

Rais Museveni akiongea kwa niaba ya viongozi waalikwa waliohudhuria uwekaji saini wa Mkataba wa Ujenzi wa Reli kati ya Serikali ya China na Kenya.

Sunday, May 11, 2014

TANZIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa John M. Haule akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Juu ya Kifo cha aliyekuwa Balozi wa Mwalawi nchini Tanzania Hayati Mhe. Flossie Chidyaonga kilichotokea kwenye Hospitali ya Aga Khan Jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa Tarehe 09 Mei 2014.

Bwa. John M. Haule akiendelea kuzungumza huku Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Vicent Kibwana (kushoto) akiyafuatilia kwa makini mazungumzo hayo na waandishi wa Habari (hawapo pichani)

Mazungumzo yakiendelea kati ya waandishi wa habari na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Picha na Reginald Philip



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali  imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Balozi wa Malawi hapa nchini Hayati Mhe. Flossie Gomile Chidyaonga kilichotokea juzi Ijumaa tarehe 09 Mei, 2014. Balozi Chidyaonga alifariki akiwa njiani kupelekwa hospitali ya Aga Khan ya hapa Dar es Salaam.

 Balozi Flossie Chidyaonga alizaliwa tarehe 16 Juni, 1960 huko Blantyre nchini Malawi. Balozi Chidyaonga aliitumikia Serikali ya Malawi katika nyadhifa mbalimbali.  Kati ya mwaka 2006 hadi 2010 alikuwa Naibu Balozi wa Malawi nchini Uingereza na baadaye Kaimu Balozi hadi alipoteuliwa kuwa Balozi wa Malawi hapa Tanzanaia.

Siku ya Jumatatu, tarehe 05 Mei, 2014, Balozi Flossie Chidyaonga alishinda vizuri na kufanya shughuli zake kama kawaida. Hata hivyo, ilipofika usiku,  alijisikia vibaya na kupelekwa hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam ambapo alipatiwa Matibabu na kuwekwa mapunziko kuanzia saa 6 usiku hadi saa 12 asubuhi aliporuhusiwa na kupewa dawa za kutumia nyumbani. Balozi Chidyaonga aliendelea kutumia dawa hizo na hali kuonekana kuimarika hadi siku hiyo ya ijumaa, tarehe 09 Mei, 2014. Siku hiyo, aliamka vizuri hadi ilipofika majira ya saa 6 mchana, hali yake ilipobadilika na kukimbizwa tena hospitali ya Aga Khan ambapo alipokelewa Daktari alisema amekwishafariki. Sasa hivi, Mwili wa Marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Uchunguzi wa madaktari umeonesha kuwa marehemu amefariki kutokana na Mshipa Mkuu wa AORTA kuvimba na kupasuka kulikosababisha damu kukusanyika kwenye mfuko wa moyo na hivyo kufanya moyo ushindwe kufanya kazi yake.

Kesho tarehe 12 Mei, 2014 mwili wa Marehemu utachukuliwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kupelekwa kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere ambapo kutafanyika misa ya kumuombea Marehemu na kutoa heshima za mwisho kuanzia saa 4 asubuhi. Mwili wa Marehemu unatarajiwa kusafirishwa kwenda Blantyre, Malawi siku ya Jumanne tarehe 13 Mei, 2014 na mazishi yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumatano tarehe 14 Mei 2014 huko Blantyer, Malawi.

Katika kipindi chote alichokuwa mwakilishi wa Malawi hapa nchini, Balozi Chidyaonga alifanya kazi yake ya kukuza na kuendeleza ushirikiano kati ya nchi zetu mbili kwa umahiri wa hali ya juu. Siku zote alikuwa mstari wa mbele kutoa ushirikiano kwa Serikali na Mabalozi wenzake wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania.

Mungu aiweke roho ya marehemu Balozi Flossie Chidyaonga, mahali pema peponi.

AMEN

Imetolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
 Dar Es Salaam, Tarehe 11 Mei, 2014

Saturday, May 10, 2014

Mikutano ya Waziri Membe na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Uturuki na Wafanyabiashara




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) wa kwanza kulia na ujumbe wake akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Uturuki hayupo pichani jijini Istambul siku ya Ijumaa tarehe 09 Mei, 2014. Mhe. Membe aliliomba Shirika hilo liingie ubia na Shirika la Ndege la Tanzania. Ombi ambalo Mkurugenzi Mtendaji aliahidi kulifanyia kazi ambapo wiki ijayo atatuma timu ya wataalamu ili kuongea na timu ya wataalamu ya ATCL kutathmini namna mashiraka hayo yatakavyoweza kushirikiana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Uturuki wa katikati pamoja na timu yake ikimsikiliza kwa makini Waziri Membe hayupo pichani.

Ujumbe wa Tanzania na wa Shirika la Ndege la Uturuki wakiendelea na mazungumzo

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Uturuki akifanya power point presentation kuhusu utendaji wa shirika lake na matarajio ya kibiashara katika Bara la Afrika na ulimwengu wote kwa ujumla. Alitaja Bara la Afrika kuwa ni bora zaidi kibiashara katika siku zijazo kutokana na ukuaji wa uchumi wa kasi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (kulia) akimkabidhi zawadi Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Uturuki
Waziri Membe kushoto naye anapokea zawadi yake kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Uturuki
zawadi kwa Waziri Membe.



 Mkutano wa Waziri Membe na Wafanyabiashara wakubwa wa Uturuki


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (kati) akiwaeleza wafanyabiashara wakubwa wa Uturuki (baadhi yao wanaonekana katika picha ya chini) fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania. Aliwahamasisha waje kuwekeza Tanzania hususan, katika sekta zitakazoongeza ajira kwa wingi kama vile viwanda vya nguo na kilimo. Wafanyabiashara hao walionesha dhamira ya dhati kuja nchini kuangalia fursa walizotangaziwa.

Baadhi ya Wafanyabiashara wa Uturuki na ujumbe wa Tanzania.

Waziri Membe akibadilishana kadi za mawasiliano na Wafanyabiashara wakubwa wa Uturuki.

Uchaguzi Afrika Kusini ulikuwa huru na wa haki:SADC

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb.)-kushoto  akiwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Lesotho na Namibia pamoja na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Stergomena Tax (Kulia) wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Afrika Kusini. SADC ilikuwa ni miongoni mwa Vyombo vya kikanda na kimataifa vilivyosimamia uchaguzi huo. Katika taarifa yake Waangalizi wa SADC walisema kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru wa haki na uwazi pia amani na utulivu vilitawala.

Baadhi ya Wageni waalikwa na Waandishi wa Habari wakati wa mkutano huo.
Mhe. Dkt. Maalim akiwa katika picha ya pamoja na Dkt. Tax.

Friday, May 9, 2014

Naibu Katibu Mkuu akutana na Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Afrika nchini Thailand

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajabu Gamaha akizungumza na Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Asia ya Kusini, Mashariki ya Kati na Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Thailand.Bwa. Manopchai Vongpakdi. Bw. Katibu Mkuu huyo anaongoza Ujumbe wa watu tisa  ambao upo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania.
Bwa. Vongpakdi nae akichangia jambo wakati wa akizungumza na
Balozi Rajabu Gamaha.

Mazungumzo yakiendelea huku wajumbe wengine wakifuatilia.
Bw. Manopchai Vongpakdi akimkabidhi Balozi Gamaha zawadi ya michoro mashuhuri nchini Thailand mara baada ya mazungumzo yao.

Picha na Reginald Philip

Matukio mbalimbali ya ziara ya kikazi ya Mhe. Membe nchini Uturuki


Waziri Mkuu wa Uturuki, Mhe. Recep Tayyip Erdogan (kulia) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Mhe. Bernard K. Membe (Mb). mazungumzo hayo yalifanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu mjini Ankara, Uturuki tarehe 08 Mei, 2014.
Mazungumzo yanaendelea kati ya Waziri Mkuu wa Uturuki (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania. Mwingine katika picha ni Bibi Victoria Mwakasege, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Waziri Membe kulia akishikana mkono na Waziri Mkuu wa Uturuki mara baada ya viongozi hao kumaliza mazungumzo. 

Mazungumzo kati ya Waziri Membe na Waziri na Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki 

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa aliyevaa shati la njano kulia ukiwa katika mazungumzo na ujumbe wa Uturuki unaongozwa na Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Emrullah Isler wa tatu kutoka kushoto. 

Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Bernard K. Membe akipokea zawadi kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki
Waziri Membe naye akimpa zawadi ya kinyago Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki 
Mhe. Membe na Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki wakijadili suala baada ya zoezi la kukabidhiana zawadi kukamilika


Mazungumzo ya Waziri Membe na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe wa tatu kutoka kushoto na ujumbe wakijadili masuala mbalimbali kuhusu ushirikiano na Uutruki na ujumbe wa Uturuki unaonekana katika picha ya chini.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mhe. Almet Dovutoglu wa pili kutoka kulia akiwa na ujumbe wake wakati wa mazungumzo na Mhe. Membe.

Mkutano na Waandishi wa Habari


Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mhe. Bernard K. Membe akihutubia Mkutano wa Waandishi wa Habari huku akimshika mkono Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mhe. Almet Dovutoglu
Waziri Membe akiendelea kuwahutubia waandishi wa habari hawapo pichani


Mapokezi ya Mhe. Membe nchini Uturuki


Waziri Membe akipeana mikono na watu waliofika Uwanja wa Ndege wa Ankara kumpokea
Waziri Membe kushoto akibadilishana mawazo na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania katika Chumba cha Wageni Maalum kwenye Uwanja wa Ndege wa Ankara
Waziri Membe akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia ambaye pia anawakilisha Uturuki aliyekaa kushoto pamoja na Bw. Salvator Mbilinyi, Afisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia aliyechutama wakibadilishana machache katika Chumba cha Wageni Maalum ndani ya Uwanja wa Ndege wa Ankara.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe akisalimiana na Naibu Meya wa jiji la Ankara ambaye naye alikuja Uwanja wa Ndege kumlaki


Naibu Meya wa jiji la Ankara aliyeketi kushoto akibadilishana mawazo na Mhe. Membe kabala ya kuondoka kutoka katika kiwanja hicho

Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania, Bw. Frank Muhina akiwa kazini kunukuu mambo mbalimbali kutoka kwa Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki. 



Na Ally Kondo, Uturuki

 WATURUKI WAHIMIZWA KUWEKEZA TANZANIA

Waturuki wenye mitaji wamehimizwa kuja Tanzania kuchangamkia fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana nchini. Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Uturuki tarehe 08 na 09 Mei, 2014.
Katika ziara hiyo, Waziri Membe aliweza kuonana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Kitaifa wa Serikali ya Uturuki akiwemo Waziri Mkuu, Mhe. Recep Tayyip Erdogan; Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Emrullah Isler; Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Ahmet Dovutoglu na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Lutfi Elgan.
Aidha, Mhe. Waziri na mwenyeji wake, Mhe. Dovutoglu walifanya mkutano wa pamoja na waandishi habari pamoja na kushiriki chakula cha mchana na wafanyabiashara wakubwa wa Uturuki.  
Mhe. Waziri alieleza kuwa Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji ambazo hazijatumiwa ipasavyo, hivyo ni muda muafaka kwa Waturuki kuwekeza mitaji yao nchini Tanzania kwa faida ya pande zote.
Baadhi ya maeneo ambayo yatakuwa na faida kubwa endapo yatapata wawekezaji ni pamoja na sekta ya usafiri wa anga. Hivyo,  Mhe. Waziri alilihamasisha Shirika la Ndege la Uturuki kuangalia uwezekano wa kuingia ubia na Shirika la Ndege la Tanzania. “Endapo Shirika la Ndege la Tanzania litapata mwekezaji, likawa na ndege za kutosha na kwa sababu Tanzania imezunguukwa na nchi nyingi, wasafiri wengi wa nchi hizo, watatumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuunganisha safari zao kwenda nchi za Ulaya”. Mhe. Membe alisikika akiwambia Viongozi wa Uturuki pamoja na wafanyabiashara wakubwa
Waziri Membe pia aliwahahakishia wawekezaji wa Uturuki watakaokuwa na dhamira ya kuwekeza nchini, kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) itatoa eneo maalum ili wawekezaji hao waweze kujenga viwanda vya uzalishaji. Alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika viwanda vya nguo, mbolea, gesi, zana za kilimo, miundombinu ya umwagiliaji, umwagiliaji wa matone  pamoja na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, nyama na maziwa. Alisema endapo sekta hizo zitafanyiwa kazi ipasavyo basi ukuaji wa uchumi utaenda sambamba na ustawi wa maisha ya watu wa kawaida, kwa sababu sekta hizo zitaongeza ajira kwa maelfu ya vijana wa Tanzania.
Aliendelea kueleza kuwa ili ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki uendelee kuimarika, Serikali itatimiza ahadi yake ya kufungua Ubalozi nchini Uturuki katika mwaka wa Fedha 2014/2015.
Kwa upande wao, Viongozi wa Uturuki walimuhakikishia Mhe. Membe kuwa watawahamasisha wafanyabiashara wa Uturuki kuja kuwekeza Tanzania. Walisema kazi hiyo kwao ni nyepesi na wanahakika itapokelewa vizuri na jumuiya ya wafanyabiashara kwa sababu Tanzania mbali na kuwa na fursa nyingi, pia  ina utulivu wa kisiasa ambao ni kigezo muhimu katika uwekezaji. 
Katika hatua nyingine, Mhe. Membe aliishukuru Serikali ya Uturuki kwa kitendo chake cha kukubali wanamichezo 10 wa Tanzania kuweka kambi ya mafunzo kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Scotland mwezi wa Julai, 2014.
Sanjari na shukrani hizo, alimshukuru pia Balozi wa Uturuki nchini Tanzania na Mke wake kwa jitihada zao za kunusuru maisha ya watu wenye ualbino. Alisema uamuzi wao wa kujenga kijiji ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchukuwa watu wenye ualbino 500 kwa ajili ya kuwapa elimu na stadi nyingine za maisha ni mfano wa kuigwa na jamii ya wasamalia wema.  
Vile vile, Mhe. Waziri aliishukuru Uturuki kwa kulisaidia Shirika la Utangazaji la Taifa Tanzania (TBC)  kwa kulipa vifaa na teknolojia ya kisasa. Alisema kabla  ya msaada huo, TBC ilikuwa inafanya kazi katika mazingira magumu.