Thursday, October 16, 2014

Mhe. Rais Kikwete apokea Hati za Utambulisho za Balozi mpya wa Ufaransa nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Balozi mpya wa Ufaransa hapa nchini, Mhe. Malika Berak alipofika IKULU Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwasilisha Hati za Utambulisho.
Balozi Berak akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili Ikulu
Balozi Berak akisalimiana na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Olivia Maboko huku akishuhudiwa  na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Irene Kasyanju (wa kwanza kulia) na Bibi Victoria Mwakasege (katikati), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika.
Mhe. Rais Kikwete akiwa katika mazungumzo na Mhe. Balozi Berak mara baada ya kupokea Hati zake za utambulisho.
Mhe. Rais Kikwete katika Picha ya pamoja na Balozi Berak na Maafisa kutoka Ubalozi wa Ufaransa nchini.
Picha ya pamoja

Monday, October 13, 2014

Naibu Waziri akutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb.) akimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mhe. Celestin Tunda ya Kasende alipofika Wizarani kwa ajili ya mazungumzo kuhusu masuala ya ushirikiano kati ya Tanzania na DRC. Katika mazungumzo hayo Mhe. Tunda ya Kasende aliishukuru Serikali ya Tanzania na Watanzania kwa ujumla kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha amani inarejea DRC. Mhe. Tunda ya Kasende pamoja na ujumbe wake  yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja.


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Rose Kitandula (kushoto) akiwa na Bw. Adam Isara, Msaidizi wa Naibu Waziri na Bi. Eva Ng'itu wakifuatilia mazungumzo ya Naibu Mawaziri wa Tanzania na DRC (hawapo pichani)
Mhe. Dkt. Maalim akimweleza jambo Mhe. Tunda ya Kasende wakati wa mazungumzo yao.
Sehemu ya ujumbe uliofuatana na Mhe. Tunda ya Kasende wakifuatilia mazungumzo. Kulia ni Dkt. Jean Marie Okwo Bele ambaye ni Mkurugenzi wa Chanjo katika Shirika la Afya Duniani (WHO)
Mazungumzo yakiendelea
Dkt. Maalim akiagana na Mhe. Tunda ya Kasende mara baada ya mazungumzo yao.

Picha na Reginald Philip















Sunday, October 12, 2014

Naibu Waziri ahudhuria mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wa Indian Ocean Rim

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (M.) akiwa kwenye chumba cha mkutano alipohudhuria Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wa Indian Ocean Rim (IOR) uliofanyika Mjini Perth nchini Australia hivi karibuni.
Mkutano wa 14 wa Mawaziri wa Baraza la Mawaziri wa Indian Ocean Rim (IOR) ukiendelea
Naibu Waziri akimsikiliza Mhe. Julie Bishop, Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia  na Mwenyekiti wa IOR
Picha ya pamoja ya Mawaziri kutoka nchi wanachama wa IOR

Saturday, October 11, 2014

Serikali Haiungi Mkono Matumizi ya Silaha za Nyuklia Duniani, Dkt. Masalla


Mjumbe anayewakilisha Tanzania katika Kamati ya Kwanza ya Umoja wa Mataifa, Dkt. Kanali Edward Masalla akisoma hotuba yake iliyohusu masuala ya uteketezaji wa silaha za nyuklia na maangamizi.
å

Wajumbe wengine wa Tanzania wakisikiliza houtuba ya Dkt. Masalla
Na. Ally Kondo, New York

Serikali imesema kuwa inaunga mkono msimamo wa kuteketeza kabisa silaha za nyuklia na silaha nyingine za maangamizi duniani kote. Aidha, inapinga umiliki, utengenezaji pamoja na vitendo vyovyote vya kuashiria kuanzisha vita kwa kutumia silaha hizo au nyinginezo.

Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Tanzania, Dkt. Kanali Edward Masalla alipokuwa anawahutubia wajumbe wa Kamati ya Kwanza ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani siku ya Ijumaa tarehe 10 Oktoba 2014.

Alisema, endapo bomu la nyuklia litatumika hakuna shaka madhara ya kibinadamu na kimaendeleo yatakuwa makubwa. Madhara hayo yatasambaa kutoka nchi moja kwenda nyingine pamoja na kuharibu kabisa mazingira na uoto wa asili kwa karne nyingi zijazo.

Hivyo, Dkt. Masalla alisisitiza umuhimu wa kuanzisha kifungu cha sheria cha kukataza matumizi ya silaha za nyuklia ambapo pia kitaupa nguvu Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha hizo duniani.

Aidha, alibainisha kuwa Tanzania imeweka saini Mikataba na Itifaki mbalimbali za Kimataifa na Kikanda zinazolenga pamoja na mambo mengine kudhibiti, kupunguza, kupambana na kuzuia umiliki wa silaha za nyuklia, kibaiolojia na kemikali pamoja na kuenea kwa haramu kwa silaha ndogo ndogo na nyepesi.

Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia; Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Silaha za Nyuklia; Mkataba kuhusu Mabomu yanayosambaa baada ya Kulipuka; na Mkataba wa Biashara ya Silaha.

Tanzania pia imesaini Mkataba kuhusu Ukanda Huru wa Afrika wa Silaha za Nyuklia (African Nuclear Weapon Free Zone). Hivyo, Tanzania inaunga mkono harakati za kuanzisha Ukanda huru wa silaha za nyuklia duniani kote. Aidha, Tanzania inaunga mkono wito wa kuanzisha ukanda huru wa silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati. Kwa kufanya hivyo, Tanzania inaamini  kuwa itasaidia kuleta hali ya utulivu na amani Mashariki ya Kati pamoja na duniani kote kwa ujumla.

Dkt. Masalla alihitimisha hotuba yake kwa kusema kuwa, Tanzania inaunga mkono na kuhimiza matumizi salama ya nishati na teknolojia ya nyuklia duniani kote. Hivyo, Serikali inatoa wito kwa wanachama wote kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki kwa madhumuni ya kuzingatia viwango vya usalama katika uzalishaji na matumizi ya nishati ya nyuklia.




Waziri Membe Aongoza Matembezi ya Hisani Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Kamilius Membe (Mb.) (wa pili kushoto mstari wa mbele) akishiriki matembezi ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mwokovu ya Kanisa Katoliki Sinza, Dar es Salaam mapema leo asubuhi..Wa kwanza kushoto ni  Paroko, Father  Cuthbert Maganga Sasagu, na wa tatu kushoto ni  Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Bw. Arnold Mwasumbi Makamu Mwenyekiti wa Parokia, Prof. Alfonce Kyessi, alieleza kuwa awamu ya kwanza ya jengo hilo la gorofa tatu litagharimu shilingi milioni 500, ambapo milioni 250 zimeshafika. Katika matembezi ya leo waamini wa Parokia wamechanga milioni 32.8 na Mhe. Membe na marafiki zake 49 wamechanga shilingi milioni moja moja. 
Matembezi ya hisani yaliyoanzia Parokia ya Mtakatifu Maximilian Kolbe Mwenge yakielekea Parokia ya Sinza kupitia barabara ya Shekilango. Matembezi hayo ya kilomita mbili yaliongozwa na Mhe. Membe.
Waziri Membe akizungumza na waamini wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mwokovu Sinza (hawapo pichani)
Baadhi ya waamini wa parokia ya Bikira Maria Mama wa Mwokovu Sinza wakimsikiliza Waziri Membe 
Waziri Membe akiendelea kuzungumza na waamini wa parokia hiyo.
Waziri Membe akipokea Zawadi ya picha kutoka kwa Paroko Sasagu
Waziri Membe akiwa katika picha ya pamoja na viongowa wa parokia ya Sinza.
Waziri Membe akiwa katika picha ya pamoja na wapuliza Tarumbeta

Friday, October 10, 2014

Bunge kupigia kura Katiba Mpya ni Ishara ya kuimarika kwa Utawala Bora


Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bibi Lilian Mukasa akisoma hotuba katika kikao cha Kamati ya Sita ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani



Na. Ally Kondo, New York

Serikali imesema kuwa mchakato wa kuandaa Katiba mpya ambayo imepitishwa na Bunge Maalum la Katiba hivi karibuni ni ishara ya wazi kuwa, Serikali imedhamiria kuongoza nchi kwa mujibu ya matakwa ya wananchi wake na kuzingatia Utawala wa Sheria.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bibi Lilian Mukasa alipokuwa anahutubia Kamati ya Sita ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani siku ya Ijumaa tarehe 10 Oktoba 2014.

Bibi Mukasa aliwambia wajumbe wa Kamati hiyo hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha kuwa huduma za kisheria ambazo kwa kawaida zina gharama kubwa, zinawafikia wananchi, hata wale wenye kipato cha chini.

Hatua hizo ni pamoja na kuongeza idadi ya wanasheria wa Serikali, majaji, mahakimu, kujenga mahakama mpya na kuzifanyia ukarabati zile za zamani.

Aidha, Serikali imekuwa ikiboresha huduma za kiamahakama mara kwa mara na hivi sasa inakusudia kuanzisha mpango  utakaowawezesha wananchi kupata huduma za kisheria kupitia simu zao.

Hatua nyingine ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya Mawakili wa kujitegemea pamoja na kuanzisha Shule ya Sheria ambayo inatoa mchango mkubwa katika sekta hiyo. Aidha, Serikali imekuwa na uataratibu wa kuzihamasisha Kampuni za uwakili zilizoimarika ili zisaidie kutoa msaada wa kisheria bure kwa watu masikini na makundi maalum,

Bibi Mukasa aliendelea kueleza kuwa Serikali inatambua nafasi ya mifumo ya sheria katika maendeleo ya nchi, uundaji wa Serikali, ulindaji wa kanuni za demokrasia kupitia Katiba, kulinda haki za binadamu na kutoa miongozo katika mgawanyo wa  rasiliamali. Hivyo, katika nchi yenye mfumo wa sheria unaotambulika na utawala wa sheria ulioimarika, maendeleo na demokrasia pia vinaimarika.

Alibainisha kuwa ili haki ipatikane lazima kila mtu katika jamii husika awe na nafasi sawa katika vyombo vya sheria. Vikwazo vyovyote kama vile kutojua kusoma na kuandika, umasikini, urasimu katika vyombo vya sheria, upungufu wa fedha na wataalamu wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka kwa wanasiasa pamoja na matajiri vyote vinakwamisha maendeleo.

Vikwazo hivi, pamoja na vingine ni changamoto kubwa katika nchi zinazoendelea. Katika jitihada za kukabiliana nazo, Serikali ya Tanzania imeanzisha  Kitengo cha Msaada wa Sheria katika Wizara ya Katiba na Sheria ambacho jukumu lake ni kuhakikisha kuwa kinatoa msaada wa sheria kwa wanaohitaji.

Thursday, October 9, 2014

Serikali itaendelea na juhudi za kuboresha maisha ya wananchi


Afisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Bibi Ellen Maduhu akisoma hotuba katika Kamati ya Tatu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
Na. Ally Kondo, New York

Serikali imetahadharisha kuwa endapo mchakato wa kuandaa Agenda ya Maendeleo baada ya Mwaka 2015 unaoendelea hivi sasa katika Umoja wa Mataifa, hautazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, dhamira ya kufikia maendeleo endelevu itakuwa ni ndoto kwa kuwa katika kila idadi ya watu watano duniani, mmoja wao ana ulemavu.

Kauli hiyo ilitolewa na Bibi Ellen Maduhu, Afisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, alipokuwa anahutubia wajumbe wa Kamati ya Tatu ya Umoja huo jijini New York, Marekani siku ya Jumatano tarehe 08 Oktoba 2014.

Bibi Maduhu alieleza kuwa wakati utekelezaji wa Malengo ya Milenia unafikia kikomo mwaka 2015, ni muhimu watu wenye ulemavu wakashirikishwa kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Aidha, ni vema nchi zikawa na utaratibu mzuri kuhakikisha kuwa kundi la watu wenye ulemavu linafaidika na hatua za maendeleo zinazopigwa, kwa kuwa hiyo ni haki yao na ni wajibu wakapatiwa.

Hotuba hiyo ilifafanua mikakati mbalimbali inayochukuliwa na Serikali katika kuboresha maeneo mbalimbali ya kijamii kwa faida ya wananchi wake. Maeneo hayo ni pamoja na elimu, afya, ugatuzi wa madaraka na kuondoa umasikini.

Kwa upande wa elimu, alieleza kuwa Serikali inalipa kipaumbele eneo hilo, kwa kuwa inaamini endapo litaimarishwa ipasavyo na kuwafikia watu wote wakiwemo wanyonge itakuwa ni ukombozi kwa sababu itatoa dira ya kuondoa umasikini.

Kwa kuliona hilo, Serikali imechukuwa hatua mbalimbali za kuboresha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya shule ya msingi kwa wote. Mchakato uliopo ni kuhakikisha kuwa elimu ya sekondari nayo itolewe kwa wote. Aidha, Serikali inaimarisha elimu ya ufundi ili iweze kutoa ujuzi kulingana na mahitaji ya sasa. Maboresho hayo pia yanagusa elimu ya juu ambayo inapanuka kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania.

Mbali na maboresho hayo yanayofanywa katika sekta ya elimu, Bibi Maduhu alikiri kuwa bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi na kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na Serikali katika kukabiliana nazo. Changamoto hizo ni pamoja na ubora wa elimu inayotolewa; watoto kutomaliza elimu zao; upungufu wa walimu bora; ukosefu wa vifaa vya kujifunzia kwa njia ya mtandao na vitabu.

Katika sekta ya afya, Serikali imekuwa ikiendelea kuiboresha sekta hiyo kwa  kuhakikisha kuwa watu wote wanapata huduma ya afya ya msingi, licha ya changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa rasilimali watu.

Bibi Maduhu alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wote wanawezeshwa ili waondokane na umasikini, hivyo Serikali imekuwa ikiandaa sera zinazotoa fursa kwa wananchi wote kushiriki katika maamuzi yanayohusu mustakabali wao. Sera hizo ni pamoja na ugatuzi wa madaraka kwenda katika Serikali za mitaa ambako ndipo wananchi wengi wanapatikana.   


Mchakato wa kuanzisha Agenda ya Maendeleo unaridhisha, Balozi Mwinyi


Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Ramadhani Mwinyi akitoa hotuba kwa wajumbe wa Kamati ya Pili inayoshughulikia masuala ya uchumi na maendeleo jijini New York, Marekani. Wanaoekana nyuma ni Bw, Songelael Shilla, Afisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa na Bibi Haikael Shishira, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. 
Balozi Mwinyi akiendelea kuwasilisha hotuba yake, huku Bw. Shilla na Bibi Shishira wakisikiliza kwa makini.


wajumbe wakisikiliza hotuba ya Balozi Mwinyi hayupo pichani.

Na. Ally Kondo, New York

Serikali ya Tanzania imebainisha kuwa inaridhishwa na hatua zilizochukuliwa katika mchakato wa kuandaa Agenda ya Maendeleo baada ya Mwaka 2015. Hatua hizo ni pamoja na Jopo Maalum la Umoja wa Mataifa kuchambua na kupendekeza shabaha na Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo kwa kauli moja yamekubalika yatumike kuwa moja ya chanzo muhimu cha kuandaa Agenda ya Maendeleo baada ya Mwaka 2015.

Hayo yalisemwa na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Ramadhani Mwinyi wakati alipokuwa anahutubia Kamati ya Pili ya  Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya Uchumi na Maendeleo jijini New York siku ya Jumatano tarehe 08 Oktoba 2014.

Hata hivyo, Balozi Mwinyi alitahadharisha kuwa wakati mchakato wa kuandaa Agenda ya Maendeleo baada ya Mwaka 2015 ukiendelea, nchi zisijisahau kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Milenia (MDGs) ambayo yanafikia mwisho ifikapo mwaka 2015. Alielezea matumaini yake kuwa Agenda ya Maendeleo itakapoidhinishwa rasmi mwezi Septemba 2015 itazingatia kazi nzuri iliyofanywa katika utekelezaji wa MDGs.
Balozi Mwinyi aliahidi kuwa yeye na timu yake itashiriki kikamilifu katika kazi za Kamati hiyo kwa kuwa inajadili agenda muhimu zinazohusu maendeleo endelevu. Moja ya agenda hizo ni mabadiliko ya tabianchi ambayo ni changamoto kubwa kwa maisha ya ulimwengu wa sasa.

 Alisema wakati nchi zinajiandaa kuelekea katika mkutano utakaojadili namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika Lima, Peru mwezi Desemba 2014 na baadaye Paris, Ufaransa mwezi Desemba 2015 kuna umuhimu wa kuhimiza ili mikutano hiyo imalizike kukiwa kumepatikana makubaliano yenye nguvu ya Kisheria kuhusu namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake.

Aidha, Balozi Mwinyi aliwambia wajumbe wa Kamati ya Pili kuwa nchi yake inalipa kipaumbele suala la kilimo kwa kuwa ni chanzo cha chakula na ndio shughuli ya Watanzania wengi. Kwa minajili hiyo, Serikali yake inaunga mkono wito wa kujumuisha masuala ya maendeleo ya kilimo, usalama wa chakula na lishe katika Sera na Programu za Maendeleo katika ngazi za Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

Kwa upande wa Kitaifa, Mhe. Mwinyi alitaja baadhi ya hatua ambazo Serikali imezichukuwa katika kuendeleza sekta ya kilimo. Hatua hizo ni pamoja na Mpango wa Kilimo Kwanza na kuanzishwa kwa Mpango Maalum wa Kukuza Kililmo katika Ukanda Kusini (SAGCOT).  


Monday, October 6, 2014

Waziri Membe awa mgeni rasmi katika kuadhimisha Miaka 24 ya Jamhuri ya Muungano wa Ujerumani

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Ujerumani nchini Tanzania, Egon Kochanke (katikati) na mkewe Wendy Marshall Kochanke wakimkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (Mb.) ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tafrija hiyo.
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Ujerumani nchini Tanzania, Egon Kochanke akisoma hotuba yake
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akisoma hotuba yake. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Ujerumani nchini Tanzania, Egon Kochanke wakigonganisha glasi kama ishara ya kusherehekea tafrija hiyo. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Ujerumani nchini Tanzania, Egon Kochanke na mke wa Balozi wakikata keki maalum  kama ishara ya kusherehekea tafrija hiyo. 


Saturday, October 4, 2014

Mada mbalimbali za uelimishaji zawasilishwa kwenye Mkutano wa DICOTA

Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Liberata Mulamula akiwasilisha mada kuhusu Nafasi ya Ubalozi wa Tanzania katika kutoa Huduma kwa Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora). Katika mada hiyo Balozi Mulamula alizungumzia umuhimu wa mawasiliano kati ya Ubalozi na Diaspora na matumizi ya Teknolojia katika kurahisisha mawasiliano hayo.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue katika meza kuu na Balozi Mulamula na wajumbe wengine waliohudhuria mkutano wa DICOTA akiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Rosemary Jairo.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bibi Rosemary Jairo akiwasilisha mada wakati wa Mkutano wa DICOTA kuhusu Nafasi ya Wizara katika kuwashirikisha Diaspora kuchangia Maendeleo ya Nchi".
Bi. Susan Mzee kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Diaspora akiwasilisha Mada kuhusu  Serikali katika kuwashirikisha Diaspora na nini kimefanyika hadi sasa.
Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Gesi Asili katika Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Norbert Kahyoza akiwasilisha Mada kuhusu Usimamizi wa Gesi katika kukuza Uchumi wa nchi wakati wa Mkutano wa DICOTA
Bi Jamila Ilomo kutoka Uhamiaji, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akiwasilisha mada kuhusu Uraia ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dkt. Mariam Ongara kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii akiwasilisha mada kuhusu Hali ya sasa nchini kuhusu Afya ya kina Mama Wajawazito na Watoto wakati wa Mkutano wa DICOTA mjini Durham
Bw. Kofi Anani kutoka Benki ya Dunia nae akiwasilisha mada wakati wa Mkutano wa DICOTA.
Bi. Lulu Mengele, Afisa Mwandamizi kutoka Mfuko wa PPF akiwasilisha mada kuhusu Mfuko huo na umuhimu wake kwa Diaspora wakati wa mkutano wa DICOTA
Dkt. Joe Masawe kutoka Benki Kuu ya Tanzania akiwasilisha mada kuhusu Uchumi na umuhimu wa fedha zinazotumwa na Diaspora katika kuchangia uchumi wa nchi.
Bw. Dickson Ernest kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) akiwasilisha mada wakati wa mkutano wa DICOTA
Bw. Charles Singili kutoka Benki ya Azania nae akiwasilisha mada wakati wa mkutano wa DICOTA
Afisa kutoka EPZA, Bi. Grace Lemunge akiwasilisha mada kuhusu Fursa za Uwekezaji ndani ya EPZA wakati wa mkutano wa DICOTA.
Wajumbe wakifurahia jambo wakati wa mkutano wa DICOTA