Saturday, October 11, 2014

Serikali Haiungi Mkono Matumizi ya Silaha za Nyuklia Duniani, Dkt. Masalla


Mjumbe anayewakilisha Tanzania katika Kamati ya Kwanza ya Umoja wa Mataifa, Dkt. Kanali Edward Masalla akisoma hotuba yake iliyohusu masuala ya uteketezaji wa silaha za nyuklia na maangamizi.
å

Wajumbe wengine wa Tanzania wakisikiliza houtuba ya Dkt. Masalla
Na. Ally Kondo, New York

Serikali imesema kuwa inaunga mkono msimamo wa kuteketeza kabisa silaha za nyuklia na silaha nyingine za maangamizi duniani kote. Aidha, inapinga umiliki, utengenezaji pamoja na vitendo vyovyote vya kuashiria kuanzisha vita kwa kutumia silaha hizo au nyinginezo.

Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Tanzania, Dkt. Kanali Edward Masalla alipokuwa anawahutubia wajumbe wa Kamati ya Kwanza ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani siku ya Ijumaa tarehe 10 Oktoba 2014.

Alisema, endapo bomu la nyuklia litatumika hakuna shaka madhara ya kibinadamu na kimaendeleo yatakuwa makubwa. Madhara hayo yatasambaa kutoka nchi moja kwenda nyingine pamoja na kuharibu kabisa mazingira na uoto wa asili kwa karne nyingi zijazo.

Hivyo, Dkt. Masalla alisisitiza umuhimu wa kuanzisha kifungu cha sheria cha kukataza matumizi ya silaha za nyuklia ambapo pia kitaupa nguvu Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha hizo duniani.

Aidha, alibainisha kuwa Tanzania imeweka saini Mikataba na Itifaki mbalimbali za Kimataifa na Kikanda zinazolenga pamoja na mambo mengine kudhibiti, kupunguza, kupambana na kuzuia umiliki wa silaha za nyuklia, kibaiolojia na kemikali pamoja na kuenea kwa haramu kwa silaha ndogo ndogo na nyepesi.

Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia; Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Silaha za Nyuklia; Mkataba kuhusu Mabomu yanayosambaa baada ya Kulipuka; na Mkataba wa Biashara ya Silaha.

Tanzania pia imesaini Mkataba kuhusu Ukanda Huru wa Afrika wa Silaha za Nyuklia (African Nuclear Weapon Free Zone). Hivyo, Tanzania inaunga mkono harakati za kuanzisha Ukanda huru wa silaha za nyuklia duniani kote. Aidha, Tanzania inaunga mkono wito wa kuanzisha ukanda huru wa silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati. Kwa kufanya hivyo, Tanzania inaamini  kuwa itasaidia kuleta hali ya utulivu na amani Mashariki ya Kati pamoja na duniani kote kwa ujumla.

Dkt. Masalla alihitimisha hotuba yake kwa kusema kuwa, Tanzania inaunga mkono na kuhimiza matumizi salama ya nishati na teknolojia ya nyuklia duniani kote. Hivyo, Serikali inatoa wito kwa wanachama wote kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki kwa madhumuni ya kuzingatia viwango vya usalama katika uzalishaji na matumizi ya nishati ya nyuklia.




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.