Tuesday, October 21, 2014

Warsha kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika yafunguliwa rasmi Mjini Arusha

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal akifungua rasmi Warsha ya Ngazi ya Juu kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika. Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano huo unaofanyika  Jijini Arusha kuanzia tarehe 21 hadi 23 Oktoba, 2014 na itawahusisha Wajumbe Maalum, Wasuluhishi, Mabalozi na Wataalam wa masuala ya Amani. Kaulimbiu ya warsha hiyo ni "Silencing the Guns-Owning the Future" na inalenga kujadili changamoto za usalama Barani Afrika na kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akiwa pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Amani iliyotolewa na Makamu wa Rais,  Mhe. Dkt. Bilal (hayupo pichani)
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim (kushoto) kwa pamoja na aliyewahi kuwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa na  Msuluhishi wa Mgogoro wa Syria, Dkt. Lakhdar Brahim wakisikiliza hotuba ya Mhe. Dkt. Bilal (hayupo pichani)

Sehemu ya Wajumbe wakifuatilia hotuba hiyo akiwemo Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini, Mhe. Filberto Ceriani Sebregondi (kushoto)
Balozi Mstaafu Augustine Mahiga (kushoto) na Mhe. Sirpa Maenpaa wakifuatilia hotuba ya ufunguzi. Balozi Mahiga aliwahi kuwa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Zuhura Bundala akiwa na Balozi Mstaafu Walidi Mangachi wakati wa warsha hiyo ya amani na usalama.

Mwenyekiti wa Warsha hiyo ambaye ni Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika, Balozi Smail Chergui nae akizungumza wakati wa Warsha hiyo.
Wajumbe wakati wa ufunguzi wa warsha.
Sehemu nyingine ya wajumbe wakati wa warsha iliyojadili masuala ya amani na usalama Barani Afrika
Wajumbe zaidi
Warsha ikiendelea na wajumbe wakifuatilia kwa makini
Warsha ikiendelea
Waziri Membe akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali wakati wa mahojiano na waandishi wa habari kuhusu Warsha hiyo ya Amani na Usalama Barani Afrika. Picha zote na Rosemary Malale
=================================================

Na Ally Kondo, Arusha.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal amesema kuwa, licha ya machafuko yanayoendelea hivi sasa katika Bara la Afrika, nchi za Afrika hazina budi kuunganisha nguvu ili ziweze kukabiliana na changamoto mpya zinazoibuka ambazo zinatishia amani, usalama na utulivu wa Bara hili.  Changamoto hizo ni pamoja na ugaidi, uharamia, biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi, biashara ya dawa za kulevya, na biashara haramu ya binadamu.

Hayo aliyasema jijini Arusha siku ya Jumanne tarehe 21 Oktoba 2014 alipokuwa akifungua Warsha ya Ngazi ya Juu kuhusu Amani na Usalama iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika ambayo itafanyika kwa siku tatu hadi Alhamisi tarehe 23 Oktoba 2014.

Makamu wa Rais alieleza kuwa ugaidi ni changamoto kubwa katika Afrika kwa sababu hakuna hata nchi moja ambayo imesalimika na uovu huo. Alisema kuwa, licha ya nchi za Afrika kulengwa na mashambulizi ya kigaidi pia zinatumika na magaidi kufanya mashambulizi yanayolenga maslahi ya nchi za kigeni, kujificha, kuandaa na kusajili magaidi wapya pamoja na kuwa chanzo cha mapato kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao hizo haramu.

Aidha, Dkt. Bilal alibainisha kuwa katika kipindi cha miongo miwili iliyopita Bara la Afrika limeshuhudia likikumbwa na zaidi ya migogoro 20 ambayo imelifanya bara hilo kutambulika na sifa ya kuwa eneo la vita. Ukweli huo unadhihirishwa na idadi kubwa ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa ambapo kati ya vikosi 17 duniani, vikosi 9 vipo Barani Afrika. Aidha, asilimia 60 ya agenda za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinajadili namna ya kurejesha na kuimarisha amani Barani Afrika.

Dkt. Bilal alihimiza nchi za Afrika kuunganisha nguvu ili ziweze kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro katika Bara la Afrika kwa kuwa athari zake ni kubwa. Athari hizo ni pamoja na kudumaza uchumi wa nchi na kuharibu miuondombinu ya kijamii ambayo ilijengwa kwa miaka mingi; kukwamisha juhudi za kupunguza umasikini; ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na kuzalisha wakimbizi na wakimbizi wa ndani.

Hata hivyo, Dkt. Bilal alisifu juhudi zinazofanywa na AU na washirika wake ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kupunguza migogoro Barani Afrika. Kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita, Bara la Afrika limeshuhudia kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe, usuluhishi wa migogoro ya muda mrefu na migogoro ya baada ya uchaguzi katika nchi za Angola, Liberia, Sierra Leone, Rwanda, Burundi, Cote d’Ivoire na Madagascar.

“Kutokana na kuimarika kwa amani barani Afrika, uchumi wa bara hilo umeendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo kati ya nchi kumi duniani ambazo uchumi wake unakua kwa haraka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita nchi sita zinatoka barani Afrika.  Aidha, matarajio katika kipindi cha muongo mmoja ujao, nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara uchumi wake utakua kwa kiwango cha asilimia saba” alisema Dkt. Bilal.

Makamu wa Rais aliendelea kueleza kuwa Bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto za kiusalama kama ilivyo katika nchi za Libya; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Sudan; Somalia; Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini.

Kwa upande wa Sudan Kusini, alisema kuwa Serikali imekubali ombi la Rais wa nchi hiyo, Mhe. Salvar Kiir la kusaidia usuluhishi wa mgogoro huo. Hivyo, Chama cha Mapinduzi tokea tarehe 12 – 18 Oktoba 2014 kimekuwa kikifanya majadiliano na vyama hasimu nchini Sudan Kusini kutafuta suluhu ya mgogoro huo. Alisema kuwa majadiliano hayo hayataingilia au kuharibu majadiliano yanayoendelea nchini Ethiopia ambayo nayo yanalenga kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.

Warsha kuhusu amani na uslama Barani Afrika inayoendelea jijini Arusha ni ya tano kufanyika ambapo warsha zilizotangulia zilifanyika katika nchi za Misri na Cote d’Ivoire. Warsha hizo ambazo huwa zinawakutanisha Wajumbe Maalum, Mabalozi, Wataalamu wa masuala ya usalama zinalenga kujadili changamoto za usalama na namna ya kukabiliana nazo barani Afrika. 

-Mwisho-


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.