Friday, October 3, 2014

Balozi Sefue kufungua rasmi Mkutano wa Baraza la DICOTA

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Liberata Mulamula  na Viongozi wa Baraza la Watanzania waishio Marekani (DICOTA) (hawapo pichani) mara baada ya kukutana nao Hotelini kwake kwa ajili ya kupata taarifa za maandalizi ya Mkutano wa Mwaka wa Baraza hilo atakaoufungua leo tarehe 03 Oktoba, 2014 mjini Durham, North Carolina.

Balozi Mulamula, Viongozi wa DICOTA pamoja na Maafisa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani wakimsikiliza Balozi Sefue (hayupo pichani)


Mkutano wa Tano wa Baraza la Watanzania waishio Marekani (DICOTA 2014) kuanza rasmi mjini Durham
============================================

Na Mwandishi Wetu, Durham

Mkutano wa Tano wa Mwaka wa Baraza la Watanzania waishio Marekani (DICOTA 2014) utafunguliwa rasmi na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue tarehe 03 Oktoba, 2014 mjini Durham nchini Marekani.

Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Kuwawezesha Watanzania waishio ughaibuni (Diasporas) kufikia Mabadiliko ya Kiuchumi na Kijamii Kule Waliko  na Nyumbani”.

Mkutano huu ambao utahudhuriwa na Watanzania kutoka Majimbo yote ya Marekani, Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Kimarekani, unalenga kuwakutanisha wadau hao na wajumbe kutoka Serikalini, Taasisi za Umma na Sekta Binafsi ili kubadilishana mawazo na uzoefu na kuangalia namna bora ya kutumia fursa na rasilimali zilizopo katika kukuza uchumi na kupata maendeleo endelevu ya Jumuiya hiyo ya Diaspora na Taifa kwa ujumla.

Wakati wa Mkutano huu mada mbalimbali za ueleimishaji zitatolewa  kwa lengo la kueleza kwa kina fursa mbalimbali za uwekezaji, biashara na utalii zilizopo nchini. Mada hizo ni pamoja na Uhamiaji na Uraia, Mchakato wa Katiba mpya, Vitambulisho vya Uraia kwa Dispora, Mifuko ya Hifadhi za Jamii na Pensheni, masuala ya Ardhi na Nyumba, umuhimu wa Bandari ya Dar es Salaam kwa Diaspora, Usajili wa Makampuni na upatikanaji wa Leseni za Biashara kwa Diaspora, masuala ya Kodi, Masoko ya Mitaji na Hisa, masuala ya Nishati ya Mafuta na Gesi, Bima, Uwekezaji katika Kilimo na mada kuhusu Uchumi na Fedha zinazotumwa kutoka nje na Diaspora (Remittances).
Baraza la DICOTA lilianzishwa rasmi mwaka 2008 na kikundi cha watu 30 wakiwa na lengo la kushirikiana na Serikali na Sekta Binafsi katika kuleta maendeleo endelevu kwa kutumia ujuzi, elimu, maarifa na mitaji waliyoipata wakiwa ughaibuni. Baraza hilo linaongozwa na Dkt. Ndaga Mwakabuta na Katibu wake ni Bi. Lyungai Mbilinyi.

Mkutano wa kwanza wa DICOTA ulifanyika mwaka 2009 mjini Houston, Texas ukifuatiwa na ule wa mwaka 2010 uliofanyika mjini Minneapolis, Minnesota. Mkutano wa Tatu ulifanyika mwaka 2011 mjini Dulles, Virginia ukifuatiwa na mkutano wa mwaka 2012 uliofanyika Chicago, Illinois.

Mbali na Balozi Sefue, Viongozi Waandamizi wengine kutoka Serikalini wanaohudhuria mkutano huu ni pamoja na Mhe. Liberata Mulamula, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Bw. Alphayo Kidata, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bibi Rosemary Jairo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Bi. Susan Mzee, Mshauri wa masula ya Diaspora kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

-mwisho-

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.