Tuesday, November 15, 2016

Waziri Mahiga akutana na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Maendeleo wa Finland


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Maendeleo wa Finland, Mhe. Kai Mykkanen alipomtembelea kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam. Wawili hao wamezungumzia masuala mbalimbali kuhusu masuala ya biashara, uwekezaji na maendeleo ya huduma za kijamii nchini. Mhe. Kai katika mazungumzo hayo ameahidi kupitia Wizara yake ataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuongeza kasi ya ukuaji wa shughuli za maendeleo sambamba na kuendelea kushawishi sekta binafsi za Finland kuja kuwekeza nchini.

Mhe. Waziri, Balozi Dkt. Augustine Mahiga akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Maendeleo wa Finland  Mhe. Kai Mykkanen

Mazungumzo yakiendelea

Mhe. Waziri, Balozi Dkt. Augustine Mahiga akimsikiliza  Waziri wa Biashara za Kimataifa na Maendeleo wa Finland  Mhe. Kai Mykkanen walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam

Monday, November 14, 2016

Waziri Mahiga apokea hati ya utambulisho kutoka kwa Konseli Mkuu wa Ubalozi mdogo wa Oman Zanzibar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Konseli Mkuu wa Ubalozi mdogo wa Oman, Zanzibar Mhe. Ahmed Hamood Al Habs alipowasili Wizarani Jijini Dar es Salaam kabla ya kukabidhi hati ya utambulisho 

Mhe. Wiziri Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Konseli Mkuu wa Ubalozi mdogo wa Oman, Zanzibar Mhe. Ahmed Hamood Al Habs
Mhe. Waziri Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na  Konseli Mkuu wa Ubalozi wa mdogo wa Oman Zanzibar Mhe. Ahmed Hamood Al Habs mara baada ya kukabidhi hati ya utambulisho

Mazungumzo yakiendelea 

Wakiwa katika picha ya pamoja

Friday, November 11, 2016

Waziri Mahiga akutana na Balozi wa Zambia nchini


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi. Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Balozi wa Zambia nchini, Mhe. Judith Kapijimpanga alimpomtembelea leo Wizarani Jijini Dar es Salaam. Katika mazungumzo yao wamejadili masuala mbalimbali ya kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili. Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni kuhusu kuboresha na kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji inayoziunganisha Tanzania na Zambia, na masuala ya mazingira hasa kwa upande wa Ziwa  Tanganyika. 
Mhe. Balozi Dkt. Mahiga akifafanua jambo kwa Balozi wa Zambia nchini Mhe.Kapijimpanga walipokutana kwa mazungumzo Wizarani
Mkutano ukiendelea
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Samuel Shelukindo (wa pili kulia) akifuatilia mazungumzo. Wa kwanza kulia  ni Afisa wa Wizara.
Wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo

Thursday, November 10, 2016

Kaimu Katibu Mkuu Mambo ya Nje akutana na Mhariri Mtendaji wa TSN

Kaimu Katibu Mkuu wa  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi akiongoza kikao alipokutuna na ujumbe kutoka Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) Wizarani jijini Dar es Salaam

Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) Dkt. Jim J. Yonazi (kulia) akifuatilia mazungumzo wengine ni Mkuu wa kitengo cha Utafiti wa Kampuni hiyo Bi.Ichikael Maro na Afisa Biashara wa Wizara, Bw. Amadeus Mzee
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Samuel Shelukindo (kushoto), na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasilano Serikalini,  Bi. Robi Bwiru wakifuatilia mazungumzo. Wengine Maafisa kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

UMOJA WA MATAIFA WAISHUKURU SERIKALI YA TANZANIA

Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena, umeishukuru Serikali ya Tanzania kwa kusaidia kwa hali na mali ujenzi na hatimaye kuelekea ukamilishwaji wa Majengo mapya ambayo yatatumika kwa shughuli za iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ( ICTR) ambayo ilihitimisha majukumu yake mwaka jana.

Shukrani hizo zimetolewa siku ya jumatano na Bw.Theodor Meron, ambaye ni Rais wa Mahakama za Kimataifa za Kesi za Masalia na Utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka zote muhimu za zilizokuwa Mahakama za Kimataifa zilizoshughulikia mauaji ya halaiki yaliyotokea Rwanda na Yugoslavia ya zamani ( IRMCT).

Bw. Theodor Meron alikuwa akiwasilisha Ripoti yake ya Nne kuhusu IRMCT mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa . Ripoti ambayo imeanisha maendeleo ya kipindi cha mpito kutoka ICTR na ICTY kwenda IRMCT kazi ambayo amesema inakwenda vizuri ingawa kumekuwapo na changamoto kadhaa.

“Wakati ninapowasilisha ripoti hii, nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa mchango mkubwa na ushirikiano ambao tumeupata kutoka serikali ya Tanzania, takribani wiki tatu zijazo majengo hayo yatazinduliwa rasmi baada ya kuwa yamekamilika”. Akasema Bw. Meroe

Baadhi ya changamoto hizo kwa upande wa iliyokuwa ICTR ni pamoja na kutokamatwa hadi sasa kwa watuhumiwa watatu ambao inaelezwa wapo mafichoni. Ni pili ni mahali pa kuwapeleka watu ambao ama wamekwisha maliza kutumikia vifungo vyao na kuachiwa huru. Watu hao wamekosa nchi ya kuwapokea na hadi sasa bado wanaendelea kuishi nchini Tanzania.

Na kwa sababu hiyo, Rais wa IRMCT ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa ushirikiano wa kuwachukua watu hao ambao hawana mahali pa kwenda na kwa wale walioko mafichoni nchi ambazo wamejificha watoe ushirikiano kwa kuwafichua na kuwakamata ili hatimaye sheria iweze kuchukua mkondo wake

Kwa upande wake, Tanzania kupitia Mwakilishi wake katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, amesema Tanzania inakaribia kuhitimishwa kwa ujenzi wa makazi mapya ya iliyokuwa ICTR katika eneo la Lakilaki ndani ya wakati na kwa bajeti iliyopangwa.

“Kwa namna ya pekee tunampongeza Msajili wa Mahakama, Bw. John Hopkins kwa uongozi wake na ushirikiano wake ambao umewezesha kukamilisha hatua hii muhimu sana”. Alisisitiza Balozi.

Aidha kukamilika kwa majengo hayo na ambayo yapo katika ardhi ya Tanzania ni heshima na fahari kubwa na ya kipekee kwa Tanzania na wananchi wake kutokana na jukumu kubwa iliyobeba ya kuwa mwenyeji wa Mahakama ya Kimataifa ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda kwa niaba ya Jumuiya ya Kimataifa. 

Balozi Manongi pia amepongeza uratibu uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa kupitia Ofisi ya Mshauri wa Sheria, Ofisi ya Msajili na the Hegue ya kuhakikisha kwamba, pamekuwapo na utaratibu mzuri wa kurithishana kutoka ICTR kwenda IRMCT. Na kwamba kazi hiyo haikuwa nyepesi.

Akizungumzia kuhusu kazi za IRMCT, Balozi amesema, Tanzania ingependa kuona Taasisi za Kitaifa zinawezeshwa ili ziweze kushughulikia kwa ukamilifu, haki na usawa na kwa kuzingatia sheria za kimataifa kesi zinazopelekwa kwenye Taasisi hizo za kitaifa.Aidha akasema uzoefu ambao umepatikana kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na ICTR pamoja na ile ya ICTY ni vema ukatumika kama mfano katika Mahakama nyingine za Kimataifa.

Kwa upande wa mashahidi, Tanzania imesisita umuhimu wa mashahidi kulindwa na kuhakikishiwa usalama wao dhidi ya vitisho mara baada ya kutoa ushahidi.Kuhusu watu walioachiwa huru baada ya kukamilisha vifungo vyao na bado wapo nchini Tanzania. Tanzania imeungana na wazungumzaji wengine katika mkutano huo wa kutaka pawepo na majadiliano ya kina ya kuangalia namna gani ya kuwasaidia watu hao.

Vilevile Tanzania imetoa wito kwa nchi zile ambazo zinahisiwa kwamba zinawahifadhi watuhumiwa watatu ambao wapo mafichoni na wanatakiwa kufikishwa katika vyombo vya sheria kutoa ushirikiano ili hatimaye haki itendeke.Watuhumiwa ambao wametajwa kuwa walihusika kwa namna moja ama nyingine katika mauaji ya Kimbari nchini Rwanda na wapo mafichoni hadi sasa ni Augustin Bizimana, Felicien Kabuga na Proitas Mpiranya. 

Kwa mujibu wa Ripoti iliyowasilishwa mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, watuhumiwa hao watakapopatikana kesi zao zitafanyika katika Mahakama hiyo mpya nchini Tanzania.Uamuzi kwa kuwa na matawi ya IRMCT huko Arusha na the Hague, Uholanzi unatokana na maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia azimio nambari 1966 la mwaka 2010.

Kupitia Azimio hilo Baraza la Usalama liliamua kwamba, baada ya kumalizika rasmi kwa ICTR ( 2015) na ICTY ( 2017) Tanzania ambayo ndiyo ilikuwa mwenyeji wa ICTR itapewa jukumuu la kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka zote muhimu za iliyokuwa ICTR ikiwa ni pamoja na kumalizia kesi zitakazokuwa zimebaki. Huku the Hague ikiwa na dhamana hiyo hiyo kwa kazi zilizokuwa za iliyokuwa ICTY.

Mahakama za Kimataifa za Rwanda na Yugoslavia ambazo zimefanya kazi kubwa ya kuwafikisha mbele ya sheria watuhumiwa karibu wote waliohusika na matukio ya kutisha ya ukiukwaji wa haki za binadamu ziliazishwa mwaka 1990 na Umoja wa Mataifa.
Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati wa uwasilishwaji wa Ripoti ya utendaji kazi wa IRMCT ambapo alimshukuru kwa namna ya pekee Msajili wa IRMCT Bw. John Hopkins kwa uongozi wake na ushirikiano ambao ameonyesha katika ujenzi wa majengo mapya huko Lakilaki lakini pia katika kusimamia kipindi cha mpito na makabidhiano kutoka ICTR kwenda IRMCT.
Rais wa IRMCT, Bw. Theodor Meron akiwasilisha mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hapo siku ya jumatano, Ripoti ya utendaji kazi wa Matawi ya Mahakama za Kimataifa za Kesi za Masalia zinachokua nafasi ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ( ICTR) na Mauaji ya halaiki yaliyotokea katika iliyokuwa Yugoslavia ya zamani ( ICTY. Bw. Meron alitumia pia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wa hali na mali katika ujenzi wa majengo yanayochokua nafasi ya ICTR majengo hayo yamejengwa katika eneo la Lakilaki Mkoani Arusha

Wednesday, November 9, 2016

Waziri Mahiga akutana na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China Nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing alipomtembelea Wizarani Jijini Dar es Salaam. Mazungumzo yao yalijikita katika kujadidili masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano zaidi baina ya Tanzania na China na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo Nchini.
Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa China nchini Mhe. Dkt.Youqing


Mazungumzo yakiendelea

Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga akimsikiliza  Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Dkt. Youqing

Tuesday, November 8, 2016

Mwambata wa jeshi wa Jamhuri ya watu wa China nchini atembelea Wizara ya Mambo ya Nje



Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbelwa Kairuki akiwa pamoja na mwambata wa Jeshi wa Jamhuri ya watu wa China hapa nchini, Meja Jenerali He Xinchong alipomtembelea wizarani leo Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao waliongelea kuhusiana na Ziara ya Jenerali FAN Changlong Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni Kuu ya Jeshi la Jamhuri ya watu wa China, inayotarajiwa kufanyika  nchini kuanzia tarehe 19 hadi 21 Novemba, 2016.





Friday, November 4, 2016

Waziri wa Mambo ya Nje akutana na Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji Bw. Jeffrey Labovitz alipotembelea Wizarani Jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji ametembelea nchini kwa mara ya kwanza toka shirika hilo lijiunge na Umoja wa Mataifa.  Mazungumzo hayo yalijikita katika kujadili hali ya wakimbizi nchini, biashara haramu ya binadamu, hali ya wahamiaji haramu, na ushiriki wa watanzania wanaoishi ughaibuni katika kuchangia maendeleo ya nchi.
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga akimsiliza Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji Bw. Labovitz



Mkutano ukiendelea

Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji Bw. Labovitz wakipeana mikono mara baada ya mazungumzo
Mkurugenzi wa Diaspora (Watanzania waishio ughaibuni) Balozi Anisa Mbega (kushoto) akiwa pamoja na maafisa wa Wizara wakifuatilia mazungumzo

Wakiwa katika picha ya pamoja

Israel yazindua Kituo cha Kutoa VIZA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Prof. Jumanne Maghembe (Mb) ambaye alikuwa Mgeni Rasmi kwenye sherehe za kufungua Kituo cha Kutoa viza za kwenda nchini Israel akiwasilisha hotuba katika ufunguzi huo. Prof. Maghembe alipongeza uamuzi wa Israel kufungua kituo hicho hapa nchini kwa kuwa kitarahisisha ziara za kwenda Israel kwa Watanzania. Aidha, alirejea kauli ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu dhamira ya Serikali ya kufungua Ubalozi nchini Israel. Prof. Maghembe alieleza kuwa idadi ya watalii kutoka Israel kuja Tanzania inaendelea kuongezeka na jana alikutana na wakala wa usafirishaji kutoka nchi hiyo ambao wana nia ya kuanza safari za ndege za kila wiki kutoka Israel hadi mkoani Katavi (charter flights) kutembelea  maoeneo ya utalii.  Ndege aina kama hiyo inafanya safari za kuja Tanzania katika mikoa ya kaskazini mara mbili kwa mwaka. Prof. Maghembe alisisitiza umuhimu wa Tanzania kushirikiana na Israel katika sekta ya teknolojia hususan mbinu za kitaalamu za kukabiliana na ujangili wa wanayamapori nchini.Kituo cha viza kitakuwa na ofisi za muda kwenye Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Israel nchini Tanzania mwenye makazi yake Nairobi, Kenya, Mhe. Yahel Vilan akitoa neno la ukaribisho wakati wa sherehe za ufunguzi. Alisema anashukuru Mungu ametimiza ombi alilotoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokutana naye Ikuku, Dar es Salaam. Mhe. Rais aliomba Serikali ya Israel ifungue Kituo cha Viza hapa nchini jambo ambalo limetia leo hii. Aliongeza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi maarufu nchini Israel, hivyo anatarajia ahadi ya kufungua Ubalozi wa Tanzania nchini humo litatekelezwa hivi karibuni.
Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima (kushoto) akifuatilia hotuba za sherehe za ufunguzi wa kituo cha viza cha Israel

Balozi wa Israel akihutubia washiriki wa sherehe za ufunguzi wa kituo cha viza.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Prof. Jumanne Maghembe na Balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake Nairobi, Kenya, Mhe. Yahel Vilan wakikata utepe kuashiria kituo cha kutoa viza cha Israel kimefunguliwa rasmi.
Ofisi ya Kituo cha Kutoa Viza cha Israel ambacho kwa sasa kipo katika Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro.

Picha ya pamoja.

Balozi wa Israel atembelea Wizara ya Mambo ya Nje

Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima akizungumza na Balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake Nairobi, Kenya, Mhe. Yahel Vilan ambaye alitembelea Wizarani leo.
Mazungumzo yao yalijikita katika masuala ya ushirikiano wa kidiplomasia katika maeneo mbalimbali yakiwemo miradi ya maendendeleo hususan katika sekta za afya,elimu, biashara, kilimo na Ulinzi. 
Mhe. Vilan akizungumza ambapo alieleza kuwa Israel itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kuwa inatekeleza azma ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.



Wakiwa katika picha ya pamoja.

Mazungumzo yakiendelea.

TAHADHARI KWA WATANZANIA WAISHIO AU WANAOENDA NCHINI ETHIOPIA


MTANZANIA ANG′ARA UMOJA WA MATAIFA



Jana, tarehe 03 Novemba, 2016, Nchi Wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zimemchagua kwa mara ya pili mtanzania Prof. Chris Maina Peter, Mhadhiri wa sheria katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuwa Mjumbe wa Kamisheni ya Sheria za Kimataifa ya Umoja wa Mataifa (the International Law Commission (ILC) yenye jumla ya Wajumbe 34.



Kwa mara ya kwanza Prof. Peter alichaguliwa kwa mara ya kwanza Novemba 2011, kuwa Mjumbe kwenye Kamati hiyo kwa kipindi cha miaka mitano (5) kuanzia 2012-2016, hivyo ushindi huo utamfanya kuwa Mjumbe kwenye Kamati hiyo kwa kipindi kingine cha miaka 5 kuanzia 2017-2021. Kwa upande wa Afrika, uchaguzi huo ulijumuisha wagombea 16 kuwania nafasi nane za Bara hilo, ambapo wagombea kutoka nchi za Algeria, Misri, Kenya, Moroko, Afrika Kusini na Tanzania waliibuka kidedea kwenye uchaguzi huo.



Kamisheni ya Sheria za Kimataifa ya Umoja wa Mataifa (Iternationa Law Commission (ILC) ilianzishwa mwaka 1948 kwa madhumuni ya kufanya tafiti, kuendeleza na kutunga sheria za Kimataifa (promotion/research, development and codification of international law). Sambamba na majukumu hayo, ILC inao wajibu wa kuushauri Umoja wa Mataifa kuhusu masulaa yote yanayohusu sheria za kimataifa.



Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kumpongeza Prof. Chris Maina Peter kwa ushindi huo ambao si kwamba umemjengea heshima kubwa yeye peke yake bali Tanzania kwa ujumla. Wizara itaendelea kutoa msaada na ushauri kwa Prof. Peter na Watanzania wengine wenye nafasi kama hizo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuongeza na kuimarisha nguvu na ushawishi wa Tanzania katika Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia kwa ujumla. Aidha, Wizara inapenda kuwakumbusha Watanzania wote wenye sifa za kitaaluma kuchangamkia nafasi mbalimbali za ajira zinazotolewa na Umoja wa Mataifa na Jumuiya nyingine za Kikanda pamoja na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za kiutendaji zinazojitokeza.





Thursday, November 3, 2016

WAZIRI MAHIGA AKUTANA NA BALOZI WA UMOJA WA FALME ZA KIARABU NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Falme za kiarabu nchini Mhe. Abdulla Ibrahim Ghanim Al Suweid katika mazungumzo yao balozi Al Suwied alimweleza Mhe. Waziri juu ya maandalizi ya Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) baina ya Tanzania na UAE ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 19 na 20, Dicemba, 2016 huko Abu Dhabi, UAE.
Wa kwanza kulia ni Katibu wa Waziri Bw. Gerald Mbwafu pamoja na Afisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Hangson Mgaka, nao wakifuatilia kwa makini mazungumzo kati Waziri Mahiga na Balozi Al Suweid (Hawapo pichani).
Mazungumzo yakiendelea




********************************************


Tarehe 04 Novemba, 2016, Mhe. Dkt. Augustine P Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alikutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Abdulla Ibrahim Ghanim Al Suweid, Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini. Balozi huyo alikuja kuzungumzia maandalizi ya Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) baina ya Tanzania na UAE ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 19 na 20, Disemba, 2016 huko Abu Dhabi, UAE. 

Sambamba na Mkutano wa JPC, Mheshimiwa Waziri na Balozi walizungumzia pia kuhusu ombi la UAE la kufanyika Kongamano la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na UAE ambalo UAE imependekeza lifanyike wakati wa mkutano wa JPC huko Abu Dhabi, UAE.


Katika mkutano huo wa JPC maeneo ya ushirkiano ambayo yatazungumziwa na kukubaliwa ni pamoja na sekta ya Uchumi, Miundombinu (Bandari, Viwanja vya Ndege pamoja na Reli), Biashara, Uwekezaji, Viwanda, Kilimo, Afya, Utalii pamoja na Nishati ya Mafuta na Gesi. 

Aidha, viongozi hawa walizungumzia pia mikataba mbalimbali ambayo itasainiwa wakati wa mkutano huo wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano. Mheshimiwa Balozi alisisitiza kuwa Tanzania itumie fursa hii adhimu kwa kujiandaa kikamilifu katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi na UAE. 

Kwa upande Mheshimiwa Waziri Mahiga alishukuru kupokea taarifa hiyo na kuahidi kufuatilia kwa karibu ili kuona Mkutano huo wa JPC unafanyika na kufanikiwa kwa manufaa za nchi zote mbili.