Tuesday, August 21, 2018

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Wanawake amewasili Nchini leo.

Mhe. Bi Phumzile Mlambo-Ngcuka akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga alipowasili Ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika hilo.
Mhe. Balozi. Dkt Augustine Mahiga akiwa katika mazungumzo na Mhe Bi. Phumzile Mlango.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wanawake, Mhe. Bi Phumzile Mlambo-Ngcuka akiwa ameongozana na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Katika Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Balozi Celestine Mushy mara baada ya kumpokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya zaira ya kikazi Nchini kuanzia tarehe 21 hadi 24 Agosti, 2018


Mhe. Bi Phumzile Mlambo-Ngcuka  akimweleza jambo Balozi Mushy wakati wa mazungumzo yao mara baada ya kuwasili nchini


Tanzania ya tia fora kwenye Tamasha la Michezo la Afrika Mashariki jijini Bujumbura


Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Tanzania (waliovalia jezi nyeupe) ikichuana na timu ya wanawake ya mpira wa miguu ya Burundi katika uwanja wa mpira wa Gitega, Burundi. Katika pambano hili timu ya Taifa ya Tanzania iliibuka na ushindi mnono wa magoli 8-1 dhidi ya timu ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Burundi.

Kufuatia ushindi huu timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Wanawake  ya Tanzania inatarajia kukutana na Timu ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Kenya katika mchezo utakaofanyika siku ya Alhamis terehe 23 Agosti 2018 kwenye uwanja wa mpira wa Gitega, Burundi.

Aidha, timu ya mpira wa pete ya Taifa ya Tanzania pia iliibuka na ushindi mnono wa magoli 79-14 dhidi ya timu ya mpira wa pete ya Burundi. Kufuatia shindi huo timu ya Taifa ya mpira wa pete inatarajia kukutana na timu ya mpira wa pete ya Uganda hapo kesho tarehe 22 Agosti, 2018 katika viwanja vya Chuo cha Ualimu cha ENS jijini Bujumbura

Vilevile timu ya mchezo wa Karate ya Taifa nayo imeanza kushiriki mchezo huo katika hatua mbalimbali, ambapo hadi sasa mwenyeji wa tamasha hilo Burundi ndiye anayeongoza kushida kwenye vipengele vingi vya mchezo huo.

Tanzania katika Tamasha hili inashiriki katika michezo minne tofauti ambayo ni Riadha (mashindano bado hayajaanza), mpira wa miguu (kwa timu ya wanawake pekee), karate na mpira wa pete.

Tamasha la kwanza la Michezo la Afrika Mashariki lilianza  kufanyika tarehe 15 Agosti na litafikia tamati Agosti 30, 2018 nchini Burundi.

Moja wa msambuliaji wa timu ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Tanzania akiwachambua mabeki wa timu ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Burundi. Katika mchezo huo Tanzania iliibuka na ushindi wa magoli 8 - 1

Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Tanzania ikicheza dhidi ya timu ya mpira wa miguu ya wanawake ya Burundi katika uwanja wa mpira wa Gitega, Burundi.
Timu ya  mpira wa miguu ya Wanawake ya Tanzania ikishangilia ushindi pamoja mashabiki waliojitokeza kushuhudia shindano hilo

Ufunguzi wa Mkutano wa JPC kati ya Tanzania na Uganda jijini Kampala

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, Balozi Patrick Mugoya akisoma hotuba ya ufunguzi ya Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda unaofanyika jijini Kampala kuanzia tarehe 21 hadi 23 Agosti 2018. Balozi Mugoya katika hotuba yake alisisitiza umuhimu wa Tanzania na Uganda kuboresha miundombinu na kuondoa vikwazo vya kibiashara ili kupunguza gharama za kufanya biashara kati ya Tanzania na Uganda

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvator Mbilinyi ambaye pia ni kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya maafisa waandamizi akisoma hotuba katika ufunguzi wa mkutano wa JPC. Bw. Mbilinyi alisema kuwa Mkutano huo pamoja na mambo mengine utathimni utekelezaji wa masuala yaliyokubalika wakati wa mkutano wa kwanza wa JPC uliofanyika Arusha mwezi Aprili 2017 na kuweka mikakati ya utekelezaji kwa masuala ambayo hayajakamilika.
Balozi Mugoya na Bw. Mbilinyi wakiwa katika meza kuu kabla hawajasoma hotuba za ufunguzi.
Kutoka kushoto ni Bw. Mbilinyi, Bw. Innocent Luoga, Kamishna wa Nishati kutoka Wizara ya Nishati na Bi. Tuma Abdallah Kaimu Mhariri Mtendaji wa kampuni ya magazeti ya Serikali (TSN) wakiwa katika meza kuu.

Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia hotuba za ufunguzi wa Mkutano wa JPC. Kutoka kushoto ni Bi. Mwadawa Ali kutoka kampuni ya magazeti ya Serikali (TSN), Bw. Paul Makelele kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Bw. Karim Msemo wa Wizara ya Mifugo.





Sehemu ya ujumbe wa Uganda ukifuatilia ufunguzi wa mkutano wa JPC. 


Mhandisi Robert Marealle kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akiongea jambo katika mkutano wa JPC.


Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Erick Ngilangwa na Bi. Elizabeth Rwitunga ambao ni sehemu ya sekretarieti ya mkutano huo wakinukuu masuala muhimu yanayozungumzwa.

Ujumbe wa Tanzania

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, Balozi Patrick Mugoya na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvator Mbilinyi wakibadilishana mawazo baada ya ufunguzi wa mkutano wa JPC kukamilika.

Picha ya Pamoja

Monday, August 20, 2018

Matukio na Picha Mbalimbali za Kongamano la tano la Diaspora.



Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein akiwasili katika viwanja vya Tibirinzi na kupokelewa na Viongozi mbalimbali.

Mhe. Rais wa Serikali Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, akihotubia wakati wa Kongamano.


Pichani ni, Waziri wa Ofisi ya Rais Zanzibar, Mhe Issa Haji Ussi Gavu (kulia) akiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Serikali  ya Tanzania, Mhe. Balozi Ramadhan Mwinyi (Kati), pamoja na Katibu mkuu  Ofisi ya Raisi Zanzibar, Mhe Salum Maulid (kushoto) 
Picha ya pamoja ya Viongozi na baadhi ya Wanadiaspora.
Baadhi ya Wanadiaspora wakichangia na kuuliza maswali wakati wa Kongamano








Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la UN WOMEN kuzuru nchini



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wanawake (UN Women), Mhe. Bi. Phumzile Mlambo-Ngcuka anategemea kufanya ziara ya kikazi hapa nchini kuanzia tarehe 21 hadi 24 Agosti, 2018. Ziara hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Shirika hilo na Tanzania.

Akiwa nchini, Bi. Mlambo-Ngcuka atahudhuria Mkutano wa Usawa wa Kijinsia,Malengo ya Maendeleo Endelevu na Vyombo vya Habari (Gender Equality, Sustainable Development Goals and Media Summit), utakaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 22 hadi 24 Agosti, 2018. 

Pamoja na kuhudhuria mkutano huo, Mkurugenzi huyo atatembelea baadhi ya miradi inayofadhiliwa na UN Women katika mkoa wa Dar es Salaam. Aidha, Bi.  Mlambo-Ngcuka ataonana na viongozi wa kitaifa na viongozi wengine wa Serikali.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma.
20 Agosti, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania na Uganda zinatarajiwa kusaini  Mkataba wa Makubaliano (MoU) kuhusu uendelezaji wa Bomba la kusafirisha gesi asilia litakaloanzia hapa nchini na kuishia Uganda na makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya elimu na mafunzo (Education and Training).
Uwekaji saini wa MoU hizo utafanyika katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) Kati ya Tanzania na Uganda utakaofanyika Kampala kuanzia tarehe 21 hadi 23 Agosti 2018.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo utaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb).
Mkutano huo wa JPC unafanyika pamoja na mambo mengine ni utekelezaji wa azma ya Viongozi wa nchi hizo, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara hususan, katika ujenzi wa miundombinu itakayoboresha biashara kati ya Tanzania na Uganda.
 Maeneo mbalimbali ya ushirikiano yatajadiliwa katika mkutano huo yakiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, usafiri wa majini, reli, anga, nishati ya Umeme na vituo  vya kutoa huduma kwa pamoja mipakani ambayo yana mchango mkubwa katika ukuaji wa  uchumi na biashara ya nchi hizo.
Maeneo mengine yatakayojadiliwa ni pamoja na ushirikiano katika Kilimo, utalii, biashara za mipakani na afya. Aidha, Mkutano huo utatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za mazingira, maji na michezo.
Mkutano wa kwanza wa JPC ulifanyika Arusha mwezi Aprili 2017 ambapo pande mbili zilikubaliana kushirikiana katika maeneo  mbalimbali ambayo mkutano wa Kampala utapata fursa ya kutathmini utekelezaji wake na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
 20 Agosti 2018


Sunday, August 19, 2018

KONGAMANO LA TANO DIASPORA LAFANYIKA MJINI CHAKE CHAKE, KISIWANI PEMBA.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

        TAARIFA KUHUSU KONGAMANO LA TANO LA DIASPORA

 Watanzania waishio ughaibuni wamekutana Chake Chake, kisiwani Pemba tarehe 18 na 19 Agosti, 2018 katika Kongamano la Tano la Diaspora kufuatia  utaratibu uliowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar  kuwakutanisha kila mwaka Watanzania waishio ughaibuni.

Kongamano hilo ambalo liliandaliwa na Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi chini ya Idara ya Ushirikano wa Kimataifa na uratibu wa masuala ya Diaspora pamoja  na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki liliwakutanisha Wanadiaspora zaidi ya 300 katika viwanja vya Tibirinzi, Pemba. Wadau mbalimbali wa hapa nchini kutoka Serikalini na Sekta binafsi walihudhuria Kongamano hilo. 

Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  alikuwa mgeni rasmi akiambatana na viongozi wengine waliohudhuria kongamano hilo akiwemo;  Balozi Seif Ali Idd, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Haji Issa Ussi Gavu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mawaziri, Makatibu na Naibu Makatibu Wakuu, Mabalozi na Watendaji wa Serikali zote za Muungano.

Katika kongamano hilo Wanadiaspora hao walipata fursa ya kufuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa ikiwa ni pamoja na Diaspora na Maendeleo; Uraia;  Sheria za Uhamiaji na kufahamishwa fursa zilizopo nchini kwa ajili ya uwekezaji kwa manufaa Wanadiaspora na Taifa kwa ujumla. Aidha, Watanzania hao waishio ughaibuni walipata  fursa ya kuuliza maswali pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu masuala mbalimbali yenye lengo la kuendeleza umoja huo na maendeleo ya nchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwahakikishia Watanzania hao kuwa Serikali zao zinatambua umuhimu wa Watanzania waishio ughaibuni na hivyo itaendelea kuwashirikisha  katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi. Vilevile, Mheshimiwa Rais Shein aliwahimiza Wanadiaspora hao kuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu na aliwasihi wazidi kuitangaza na kuwekeza nchini kwa wingi.


Nae mwakilishi wa Watanzania waishio ughaibuni Bw. Adolf Makaya, Katibu wa Baraza la Dunia la Diaspora (TGDC), kwa niaba ya wanadiaspora hao, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuwathamini na kutambua umuhimu wao katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi.

Sambamba na hayo, Wanadiaspora  walipata fursa ya kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo kisiwani Pemba ikiwa ni pamoja na kutembelea hoteli ya kitalii ya Manta Resort iliyopo Makangale kisiwani Pemba. Hoteli hiyo imekuwa gumzo na kivutio kikubwa cha utalii kutokana na kuwa na chumba kilicho chini ya bahari.

Kwa upande wake, Balozi Seif Ali Idd, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alifurahishwa na mahudhurio mazuri ya Wamadiaspora na kuona kuwa ni fursa kubwa kwao kuona maendeleo ya nchi yao na pia kujenga maelewano mazuri na Serikali.

Kwa ujumla, kongamano hilo limefanyika kwa mafanikio makubwa ambapo viongozi wa Serikali pamoja na wanadiaspora hao waliweza kupata fursa ya kujadiliana namna mbalimbali za kuwashirikisha Wanadiaspora hao katika maendeleo yao na ya Taifa kwa ujumla.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
19 Agosti 2018

Saturday, August 18, 2018

Mkuutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC umemalizika mjini Windhoek Namibia

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa hafla ya kufunga Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mjini Windhoek, Namibia tarehe 18 Agosti 2018.
Katika Mkutano huo Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan alisaini itifaki ya kazi na ajira, itifaki ya Kulinda Hakimiliki ya Wagunduzi wa aina Mpya za Mbegu za Mimea ya mwaka 2017.
Pia amesaini Tamko la nchi wanachama wa SADC la kutokomeza malaria katika ukanda wa SADC ifikapo mwaka 2030 na maboresho ya Katiba inayosimamia masuala ya Kamati ndogo ya Wakuu wa Polisi katika Organ.
Mhe. Samia Suluhu Hassan aliwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambapo aliwashukuru wanachama wote kwa kuendelea kuiamini Tanzania katika nafasi za uongozi ndani ya Jumuiya hiyo pamoja na kuahidi kuendelea kushirikiana katika shughuli za maendeleo, siasa, ulinzi, na usalama.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akifuatilia tukio la utiwaji saini wa itifaki katika mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliomalizika tarehe 18 Agosti 2018 Windhoek, Namibia.
Mwenyekiti wa SADC na Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Hage Geingob akihutubia katika hafla ya kufunga mkutano wa 38 wa  Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika mjini Windhoek, Namibia.

Katibu Mtendaji wa SADC. Dkt. Stergomena L. Tax akihutubia katika hafla ya kufunga mkutano wa  38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali ambapo aliwapongeza viongozi wote walioteuliwa kushika nafasi mbalimbali na kuahidi ushirikiano katika utekelezaji wa agenda za SADC.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (kati) na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda wa Wizara ya Mambo  ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Innocent Shiyo (kulia) wakifuatilia mkutano.

Ujumbe kutoka Serikali ya Tanzania ukifuatilia utiwaji saini wa itifaki mbalimbali za ushirikiano.



Tanzania yateuliwa rasmi kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC

Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaofanyika mjini Windhoek, Namibia, kuanzia tarehe 17 hadi 18 Agosti 2018, umemteua Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha Agosti 2018 mpaka Agosti 2019.

Kufuatia uteuzi huo, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atapewa rasmi jukumu la Uenyekiti wa SADC katika Mkutano mkuu ujao wa 39 utakaofanyika Tanzania mwezi Agosti 2019.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC unaofanyika mjini Windhoek, Namibia kuanzia tarehe 17 hadi 18 Agosti 2018.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akifuatilia ufunguzi wa mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali mjini Windhoek, Namibia. Kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Afika Kusini, Mhe Lindiwe Sisuli.
Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof Adolf Mkenda akifuatilia hafla ya ufunguzi wa mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali mjini Windhoek, Namibia.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Dkt. Stergomena L. Tax akitoa hotua ya ufunguzi wa mkutano pamoja na taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa Jumuiya ambapo alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi waliomaliza muda na nchi wanachama kwa ushirikiano walioutoa katika utekelezaji wa malengo na mipango mbalimbali ya kanda.
Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini na Mwenyekiti wa SADC aliyemaliza muda, Mhe. Cyril Ramaphosa akikabidhi nafasi ya uenyekiti kwa mwenyekiti mpya na Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Hage Geingob.

Mwenyekiti wa SADC na Rais wa Namibia, Mhe. Hage Geingob akihutubia mara baada ya kukabidhiwa nafasi ya uenyekiti wa SADC mjini Windhoek, Namibia ambapo aliishukuru Serikali ya Afrika kusini kwa uongozi mahiri kwa kipindi chote cha uongozi wake na aliahidi kushirikiana na wanachama wote katika kuiletea kanda maendeleo na kupunguza umasikini.
Wanafunzi walioshinda shindano la insha wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena Tax na Mwenyekiti wa SADC, Mhe. Cyril Ramaphosa njini Windhoek ,Namibia.

Sehemu nyingine ya Wanafunzi walioshinda shindano la insha wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena L. Tax na Mwenyekiti wa SADC, Mhe. Cyril Ramaphosa njini Windhoek ,Namibia.

Waandishi wa habari walioshinda shindano la mwandishi bora wa SADC katika radio, gazeti na televisheni wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena Tax na Mwenyekiti wa SADC, Mhe. Cyril Ramaphosa njini Windhoek ,Namibia.
Kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango (SMZ), Bw. Ali Juma Khamis  pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikaiano wa Afrika Mashariki , Balozi Innocent Shiyo wakifuatilia mkutano.
Kutoka Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu wakifuatilia mkutano.
Wa pili kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Edwin Mhede pamoja na Afisa Mambo ya Nje Mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Agness kayola (kulia) wakifuatilia mkutano.

Kutoka kustoto ni Balozi wa Tanzania nchini Namibia mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini, Mhe. Sylisvester Ambokile na Naibu Mwanasheria Mkuu, Bw. Evaristo Longopa wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa mkutano.


Ujumbe kutoka Serikali ya Tanzania ukufuatilia mkutano.

Sehemu nyingine ya ujumbe huo ukifuatilia mkutano.


Waasisi wa SADC wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Tiafa wa Namibia  na wimbo wa SADC ukipigwa, kushoto ni Rais mstaafu wa kwanza  wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Sam Nujoma na kulia kwake ni Rais wa mstaafu wa kwanza wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Joaquim Chissano.

Wake za Waheshimiwa marais walifuatilia hafla ufunguzi wa Mkutano

Picha ya pamoja