Tanzania na Uganda zinatarajiwa
kusaini Mkataba wa Makubaliano (MoU)
kuhusu uendelezaji wa Bomba la kusafirisha gesi asilia litakaloanzia hapa
nchini na kuishia Uganda na makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya elimu
na mafunzo (Education and Training).
Uwekaji saini wa MoU hizo
utafanyika katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano
(JPC) Kati ya Tanzania na Uganda utakaofanyika Kampala kuanzia tarehe 21 hadi
23 Agosti 2018.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano
huo utaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb).
Mkutano huo wa JPC unafanyika
pamoja na mambo mengine ni utekelezaji wa azma ya Viongozi wa nchi hizo, Mhe.
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ya kuimarisha
ushirikiano wa kibiashara hususan, katika ujenzi wa miundombinu itakayoboresha
biashara kati ya Tanzania na Uganda.
Maeneo mbalimbali ya ushirikiano yatajadiliwa
katika mkutano huo yakiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, usafiri wa
majini, reli, anga, nishati ya Umeme na vituo
vya kutoa huduma kwa pamoja mipakani ambayo yana mchango mkubwa katika
ukuaji wa uchumi na biashara ya nchi
hizo.
Maeneo mengine yatakayojadiliwa
ni pamoja na ushirikiano katika Kilimo, utalii, biashara za mipakani na afya.
Aidha, Mkutano huo utatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za
mazingira, maji na michezo.
Mkutano wa kwanza wa JPC
ulifanyika Arusha mwezi Aprili 2017 ambapo pande mbili zilikubaliana
kushirikiana katika maeneo mbalimbali
ambayo mkutano wa Kampala utapata fursa ya kutathmini utekelezaji wake na
kuibua maeneo mapya ya ushirikiano.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
20 Agosti 2018
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.