TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania na Uganda zimepata mafanikio
makubwa kupitia Mikutano ya Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC)
iliyofanyika Arusha Aprili 2017 na sasa wa Kampala unaohitimishwa leo.
Kauli hiyo ilitolewa kwa pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mhe .Dkt.
Augustine Mahiga (Mb) na mwenzake wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa walipokuwa
wanasoma hotuba za ufunguzi wa mkutano huo.
Mafanikio yaliyoelezwa ni pamoja na kusainiwa kwa Mikataba ya Makubaliano tisa
ikiwemo Mikataba ya kushirikiana katika uendelezaji wa bomba la kusafirisha
gesi asilia kutoka Dar Es Salaam hadi Uganda na ushirikiano katika masuala ya
elimu na mafunzo iliyosainiwa leo katika mkutano wa Kampala.
Mkutano huo ulijulishwa kuwa utekelezaji wa mikataba hiyo unaridhisha na inalenga
kurahisisha ukuaji wa uchumi wa nchi hizo ili kutimiza azma ya viongozi wake,
Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Mhe. Yoweri Museveni wa Uganda ya
kukuza biashara kati ya nchi hizo.
Mikataba iliyosainiwa inahusu uendelezaji wa miradi ya miundombinu
mbalimbali ikiwa ni pamoja na nishati ya Umeme, barabara hususan za mipakani,
bandari, reli na usafiri wa anga.
Kufuatia mikataba hiyo miradi
mbalimbali ipo katika hatua tofauti za utekelezaji ikiwemo mradi wa kuzalisha
umeme wa Kikagati/ Murongo uliopangwa kukamilika mwaka 2020. Aidha, Shirika la
Ndege la Tanzania litaanza safari za moja kwa moja kutoka Dar Es Salaam hadi
Entebbe mwishoni mwa mwezi huu kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa masuala ya anga
katika mkutano wa Arusha mwezi Aprili 2018
Miradi mingine ni ya ukarabati wa
bandari za Bell na Bukasa na ukarabati wa meli za Kagawa na Pamba kwa upande wa
Uganda ambayo italeta muunganiko mzuri katika usafirishaji hasa baada ya Reli
ya Kisasa ya kiwango cha kimataifa inayojengwa na Tanzania itakapokamilika.
Waheshimiwa Mawaziri walisisitiza umuhimu wa Serikali za Tanzania na Uganda
kuwekeza ipasavyo katika ushoroba wa kati ili kuleta muunganiko kwa ajili ya
kukuza biashara. Aidha. Walisisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo visivyo vya
kibiashara na kushughulikia changamoto za mipakani kwa haraka kadri
zinavyojitokeza
Kutokana na umuhimu wa utekelezaji wa miradi inayoafikiwa katika mikutano hiyo,
pande zote mbili ziliwakilishwa na viongozi wa ngazi ya juu wakiwemo Mawaziri
na Makatibu Wakuu.
Kwa upande wa Tanzania, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Mhe. William Lukuvi. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Mhandisi Isack Kamwele, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles
Mwijage na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu walishiriki mkutano huo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki,
Kampala
23 Agosti 2018
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.