Tanzania na Uganda za azimia kukuza
biashara kati yao
Tanzania na Uganda zimeazimia
kuondoa vikwazo vya kibiashara ili kukuza kiwango cha biashara kati yao ambacho
kwa takwimu zilizopo sasa zinaonesha kipo chini mno.
Hayo yalibainishwa katika mkutano
wa Jukwaa la biashara kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika leo kando ya
Mkutano wa pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) unaofanyika
kwa silku tatu jijini Kampala tokea tarehe 21 Agosti 2018.
Mgeni Rasmi katika mkutano huo
ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Ushirikia ya
Uganda, Balozi Julius Onen alieleza kuwa Tanzania na Uganda zina nafasi kubwa
ya kukuza biashara endapo njia za usafiri zitaboreshwa, vikwazo visivyo vya
kibiashara vitaondolewa pamoja na kuwa na mikakati ya pamoja ya kuweka viwango
vya ubora vinavyotambulika katika nchi zote na kanda nzima kwa ujumla.
Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na
wawakilishi mbalimbali wa Tanzania akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema kuwa Mamlaka ya
Bandari imeboresha kwa kiasi kikubwa huduma zake ikiwemo kuanza upya kwa njia
ya Dar Es Salaam- Mwanza hadi bandari ya Bell nchini Uganda. Alisema
kufunguliwa kwa njia hiyo kumepunguza idadi ya siku za kusafirisha mizigo
kutoka Dar Es Salaam hadi Uganda ambapo kwa sasa mizigo inasafirshwa kwa siku
nne na kwa kiwango kikubwa na gharama
nafuu.
Jambo hilo liliungwa mkono na
wafanyabiashara wa Uganda walioshiriki mkutano huo ambapo waliipongeza TPA
kutokana na hatua inazozichukua kuboresha huduma katika Bandari ya Dar Es
Salaam na walikiri kuwa kufunguliwa kwa njia ya Dar Es Salaam-Mwanza hadi
Bandari ya Bell kumepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za kufanya biashara
pamoja na muda wa kusafirisha bidhaa zao.
Balozi Onen aliendelea kueleza
kuwa licha ya changamoto zilizopo za kufanya biashara kati ya Uganda na
Tanzania lakini vihatarishi vya kufanya biashara na Tanzania ni vichache
ukilinganisha na nchi nyingine. Hivyo,
aliwsihi wafanyabiashara wa Uganda na Serikali kwa ujumla kuimarisha ushirikiano
wa kibiashara na nchi hiyo.
Alibainisha kuwa Tanzania na
Uganda zinaweza kufaidika zaidi kibiashara kutokana na nchi zote kuwa kwenye
eneo la Maziwa Makuu ambalo lina soko kubwa kutokana na idadi kubwa ya watu
katika eneo hilo. Hivyo alizihimiza Serikali zaTanzania na Uganda kufanya
uwekezaji mkubwa katika ushoroba wa kati (central corridor) ili kukuza
biashara.
Mkutano wa JPC unatarajiwa
kufungwa rasmi Alhamisi kwa kikao cha ngazi ya Mawaziri ambapo Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb),
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi (Mb),
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi. Isack Kamwele (Mb) na
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu (Mb) watashiriki mkutano huo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki,
Kampala
22 Agosti 2018
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.