TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU MKUTANO WA JUKWAA LA USHIRIKIANO
KATI YA CHINA NA AFRIKA (FOCAC)
Mkutano
wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na China
(FOCAC) utafanyika Beijing kuanzia tarehe 01 hadi 04 Septemba, 2018.
Ujumbe
wa Tanzania kwenye mkutano huo utaongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa. Viongozi wengine watakaoshiriki
Mkutano huo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Balozi Dkt. Augustine Mahiga; Mhe. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Fedha na
Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mhe. Rashid Ali Juma, Waziri wa
Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na
Viongozi wengine Waandamizi.
Mkutano
huo utafunguliwa na Rais wa China, Mhe. Xi Jinping ambaye pia ni Mwenyekiti wa jukwaa
hilo, kwa kushirikiana na Mwenyekiti Mwenza, Rais wa Afrika Kusini, Mhe.
Matamela Cyril Ramaphosa, utahudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika
ambaye pia ni Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame, Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Mhe. Antonio Guterres na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika ambaye pia
ni Rais wa Chad, Mhe. Idriss Deby Itino. Mkutano huo pia utashuhudia uchaguzi
wa Mwenyekiti Mwenza mpya kutoka Afrika.
Kaulimbiu
ya Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika kwa mwaka 2018 ni
“China na Afrika: Kuelekea Jumuiya Imara kwa mustakabali wa wote kupitia ushirikiano
kwa manufaa ya wote” (China and Africa: Toward an Even Stronger Community with
a Shared Future through Win-Win Co-operation).
Mkutano
wa Wakuu wa Nchi na Serikali utatanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu
kitakachofanyika tarehe 01 Septemba, 2018. Kikao hicho pamoja na mambo mengine
kitapitia agenda za mkutano huo na kuziwasilisha kwenye kikao cha Mawaziri
kitakachofanyika tarehe 02 Septemba, 2018.
Mkutano
wa Jukwaa la Ushirikiano kati Afrika na China pamoja na mambo mengine utajadili
namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na China na kufanya mapitio ya
mikakati ya pamoja ya maendeleo iliyopo kati ya Afrika na China. Jukwaa hilo
ambalo lilianzishwa mwaka 2000 huwaleta pamoja viongozi wa Afrika na China
kujadili masuala ya ushirikiano na maendeleo na kutathmini utekelezaji wa
makubaliano mbalimbali yanayofikiwa kati yao.
Aidha,
masuala ya ushirikiano katika uendelezaji Miundombinu kama Barabara, Reli, Bandari
na upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa Bara la Afrika yatajadiliwa kwa kina.
Agenda nyingine itahusu kilimo cha kisasa ambapo China itatoa uzoefu wake
katika kutumia sayansi na ubunifu wa kiteknolojia katika kufikia uzalishaji
wenye tija na kuongeza thamani kwa mazao ili kuwa na soko la uhakika.
FOCAC
2018 pia itajadili masuala ya biashara na uwekezaji ambapo kwa kuona umuhimu
huo, Mhe. Xi Jinping, Rais wa China atafungua rasmi Mkutano wa Jukwaa la
Biashara kati ya China na Afrika utakaofanyika tarehe 03 Septemba, 2018.
Mkutano
wa kwanza wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa hili ulifanyika Beijing mwaka 2006 na Mkutano
wa Pili ulifanyika nchini nchini Afrika Kusini mwaka 2015.
Wakati
wa Mkutano wa pili, China ilitangaza mpango kabambe wa kuhamasisha mapinduzi ya
viwanda na kilimo cha kisasa kwa Afrika wenye gharama ya Dola za Marekani bilioni
60 katika utekelezaji wake. Kufuatia ushirikiano kupitia Jukwaa hilo biashara
kati ya China na Afrika imeongezeka pamoja na ongezeko la ushirikiano wa
kiutamaduni na biashara baina ya watu wa China na Afrika.
Pembezoni
mwa Mkutano huo, Tanzania na China zimeandaa Kongamano la Biashara ambalo
litafunguliwa rasmi na Mhe. Waziri Mkuu tarehe 02 Septemba, 2018. Kongamano
hilo ambalo litajadili kwa kina masuala ya uwekezaji na biashara kati ya
Tanzania na China litashirikisha takribani makampuni 80 kutoka nchi hizi mbili.
Imetolewa na:
Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma.
30 Agosti 2018
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.