Serikali ya Tanzania imeonesha
nia ya wazi ya kuongeza maeneo ya ushirikiano katika sekta ya elimu ya juu na
Serikali ya Namibia ambapo ushirikiano huo utawezesha walimu na wanafunzi kuwa
na progamu za kubadilishana kwa lengo la kupeana uzoefu na kujengeana uwezo.
Hayo yamesemwa wakati wa ziara
ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Prof. Adolf F. Mkenda katika chuo kikuu cha Namibia cha Sayansi na Teknolojia Mjini Windhoek, Namibia tarehe 09 Agosti 2018.
Katika ziara hiyo Prof. Mkenda
aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Namibia mwenye makazi yake mjini
Pretoria nchini Afrika Kusini, Mhe. Balozi Sylivester Ambokile, Balozi wa
Namibia nchini Tanzania, Mhe. Theresia Samaria na Mkurugenzi wa Sera na Mipango
katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. James
Lugaganya.
Lengo la ziara hiyo ni kujadili
namna ya kuongeza ushirikiano katika sekta ya elimu ya juu kwenye masuala ya utafiti
na ugunduzi katika taaluma za teknolojia zinazotolewa na vyuo vitakavyoingia
makubaliano ya ushirikiano.
“Nimekuja tushirikishane mikakati mbalimbali tunayoweza kujiwekea ili kuvifanya vyuo vyetu viwe bora ndani ya kanda na Afrika kwa ujumla pia tujadili mbinu mpya za kielimu ambazo Tanzania na Namibia zinaweza zikashirikiana,”alisema Prof. Mkenda
Pia akaeleza nchi nyingi za
Afrika zinapata changamoto ya uwezo mdogo na uhaba wa rasilimali fedha katika
kuhakikisha upatikanaji wa malazi kwa wanafunzi, upatikanaji wa elimu kwa
vitendo na kwamba ni vema Tanzania na Namibia zikatumia fursa za ushirikiano wa
elimu zinazosainiwa katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Namibia cha Sayansi na Teknolojia,
Dkt. Tjama Tjivikua alieleza kuwa hadi sasa chuo kimefanikiwa kuanzisha
ushirikiano na taasisi, makampuni na viwanda mbalimbali nchini humo na hata nje
ya nchi ili kuwawezesha wahitimu katika chuo hicho kupata nafasi ya elimu kwa
vitendo.
“Jitihada hizi zimeshaanza
kuleta matunda kwa kuwa kwa sasa wahitimu wa chuo hiki wamefanikiwa kupata
ajira katika taasisi hizo na wengine walifanikiwa kupata ajira kabla ya kuhitimu
muda wa mafunzo” alisema Dkt. Tjivikua
Vilevile chuo kinashirikiana
na wadau mbalimbali ambapo alieleza Tanzania ni mmoja wa wadau kupitia chuo cha
Sayansi ya Kilimo Sokoine(SUA) na chuo kikuu cha Ardhi, wadau wengine ni pamoja
na Afrika Kusini, Cameroon, Kenya,
Botwana, Uswiss, na mashirika mengine ya kimataifa.
Balozi wa Tanzania nchini
Namibia, Mhe. Sylivester Ambokile naye alisema kwa kuwa jumuiya ya wanamibia
imezungukwa na jamii inayozungumza Kiswahili hivyo ni vema ushirikiano uliopo
ukazidi kuimarishwa kwa kuingiza lugha ya Kiswahili katika idara za lugha za
kigeni kwenye vyuo vikuu nchini Namibia.
“Katika hafla ya utambulisho
wangu kwa Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Hage Geingob niliwasilisha wazo la
Kiswahili kuingizwa katika Idara za Lugha ya kigeni na lilipokelewa vizuri,
hivyo kwa sasa ofisi za ubalozi zinafanya jitihada za kukumbushia katika sekta
husika ili utekelezaji wake ukamilike mapema”. alisema Mhe. Balozi Ambokile
Nchini Namibia elimu ya juu
imeanza mwaka 1979/1980 kutokana na kuchelewa huko kuliifanya Namibia kuhitaji
Walimu wa taaluma mbalimbali kutoka mataifa mengine. Tanzania ni miongoni mwa
nchi yenye walimu wengi katika vyuo vikuu ya Namibia. Pamoja na kuwepo kwa
ushirikiano huo Chuo kikuu cha Namibia cha Sayansi na Teknolojia tangu
kuanzishwa kwake mwaka 1992 kimekuwa kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo
cha Sokoine (SUA) katika kupata wataalamu wazuri wa masuala ya mifugo ambao
wamekuwa wakirejea baada ya masomo na kulitumikia taifa kwa tija.
====================================================
Katibu Mkuu, Prof. Mkenda akitembelea maeneo ya chuo kikuu cha Namibia cha Sayansi na Teknolojia ili kuweza kujionea uendeshaji wa vipindi vya masomo na mpangilio wa majengo kwa ajili ya madarasa na malazi ya wanafunzi. |
Katibu Mkuu, Prof. Mkenda na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo na uongozi wa chuo, wa kwanza kulia ni Balozi wa Namibia nchini Tanzania, Mhe. Theresia Samaria, kulia kwa Prof. Mkenda ni Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Ambokile na pembeni yake ni Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Bw. James Lugaganya. |
Mazungumzo yakiendelea. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.