Sunday, August 19, 2018

KONGAMANO LA TANO DIASPORA LAFANYIKA MJINI CHAKE CHAKE, KISIWANI PEMBA.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

        TAARIFA KUHUSU KONGAMANO LA TANO LA DIASPORA

 Watanzania waishio ughaibuni wamekutana Chake Chake, kisiwani Pemba tarehe 18 na 19 Agosti, 2018 katika Kongamano la Tano la Diaspora kufuatia  utaratibu uliowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar  kuwakutanisha kila mwaka Watanzania waishio ughaibuni.

Kongamano hilo ambalo liliandaliwa na Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi chini ya Idara ya Ushirikano wa Kimataifa na uratibu wa masuala ya Diaspora pamoja  na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki liliwakutanisha Wanadiaspora zaidi ya 300 katika viwanja vya Tibirinzi, Pemba. Wadau mbalimbali wa hapa nchini kutoka Serikalini na Sekta binafsi walihudhuria Kongamano hilo. 

Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  alikuwa mgeni rasmi akiambatana na viongozi wengine waliohudhuria kongamano hilo akiwemo;  Balozi Seif Ali Idd, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Haji Issa Ussi Gavu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mawaziri, Makatibu na Naibu Makatibu Wakuu, Mabalozi na Watendaji wa Serikali zote za Muungano.

Katika kongamano hilo Wanadiaspora hao walipata fursa ya kufuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa ikiwa ni pamoja na Diaspora na Maendeleo; Uraia;  Sheria za Uhamiaji na kufahamishwa fursa zilizopo nchini kwa ajili ya uwekezaji kwa manufaa Wanadiaspora na Taifa kwa ujumla. Aidha, Watanzania hao waishio ughaibuni walipata  fursa ya kuuliza maswali pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu masuala mbalimbali yenye lengo la kuendeleza umoja huo na maendeleo ya nchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwahakikishia Watanzania hao kuwa Serikali zao zinatambua umuhimu wa Watanzania waishio ughaibuni na hivyo itaendelea kuwashirikisha  katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi. Vilevile, Mheshimiwa Rais Shein aliwahimiza Wanadiaspora hao kuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu na aliwasihi wazidi kuitangaza na kuwekeza nchini kwa wingi.


Nae mwakilishi wa Watanzania waishio ughaibuni Bw. Adolf Makaya, Katibu wa Baraza la Dunia la Diaspora (TGDC), kwa niaba ya wanadiaspora hao, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuwathamini na kutambua umuhimu wao katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi.

Sambamba na hayo, Wanadiaspora  walipata fursa ya kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo kisiwani Pemba ikiwa ni pamoja na kutembelea hoteli ya kitalii ya Manta Resort iliyopo Makangale kisiwani Pemba. Hoteli hiyo imekuwa gumzo na kivutio kikubwa cha utalii kutokana na kuwa na chumba kilicho chini ya bahari.

Kwa upande wake, Balozi Seif Ali Idd, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alifurahishwa na mahudhurio mazuri ya Wamadiaspora na kuona kuwa ni fursa kubwa kwao kuona maendeleo ya nchi yao na pia kujenga maelewano mazuri na Serikali.

Kwa ujumla, kongamano hilo limefanyika kwa mafanikio makubwa ambapo viongozi wa Serikali pamoja na wanadiaspora hao waliweza kupata fursa ya kujadiliana namna mbalimbali za kuwashirikisha Wanadiaspora hao katika maendeleo yao na ya Taifa kwa ujumla.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
19 Agosti 2018

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.