Bw. Addo Komba Afisa kutoka Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo, akikabidhiwa kombe kufuatia ushindi timu ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Tanzania kwenye Tamasha la Michezo la Afrika Mashariki lililofanyika Bujumbura, Burundi.
Tamasha la Kwanza la Michezo la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililokuwa likifanyika jijini Bujumbura limefikia tamati leo tarehe 29 Septemba, 2018. Hafla ya kufunga tamasha hilo ilihudhuriwa na Viongozi waandamizi wa Serikali kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchini Burundi.
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Bw. Liberatus Mfumukeko alisema maadhimisho ya tamasha hilo yameleta tija kubwa katika kuleta na kuimarisha umoja na shirikiano, kuibua na kuendeleza vipaji mbalimbali vya wananchi wa Afrika Mashariki.
Mhe. Sindimwo Gaston Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi, kwa upande wake amesema ni fahari kubwa kwa Burundi kuandaa tamasha hilo lililofanyika kwa kipindi cha wiki mbili. Aliongeza kusema washiriki wa wamichezo hiyo watakuwa mabalozi wa kuelezea sifa nzuri za amani na utulivu ulipo nchini Burundi tofauti na inavyosemwa na baadhi ya watu.
Katika tamasha hilo Tanzania imeshinda kombe moja la mpira wa miguu wa wanawake ,medali ya fedha katika riadha, mpira wa pete na karatee.
Tamasha hili lilifanyika kuanzia tarehe 16 hadi 29 Agosti 2018, katika Jiji la Bujumbura na Gitega nchini Burundi. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.