Monday, November 16, 2020

PROFESA KABUDI AKIAPISHWA KUWA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI

 

Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akiapa mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi na Mhe. Dkt. Philip Mpango wakiapa, Ikulu Chamwino jijini Dodoma. Mhe. Dkt. Philip Mpango ameapa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango

Saturday, November 14, 2020

BALOZI IBUGE AKUTANA NA BALOZI WA CHINA NCHINI

 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke ofisini kwake jijini Dodoma.

Katika kikao hicho Katibu Mkuu, Balozi Ibuge na Balozi Wang Ke pamoja na mambo mengine wameongelea juu ya mapendekezo ya mabadiliko ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu nafasi za uwakilishi wa kudumu kwa Bara la Afrika.

katika Kikao hicho Balozi Ibuge amesisitiza msimamo wa Tanzania kuunga mkono nia ya Bara la Afrika kuwa na nafasi mbili za uwakilishi wa kudumu katika Baraza hilo. Nchi za Afrika zinataka uwakilishi huo uwe na nguvu ikiwa ni pamoja na kupata nafasi moja ya kura ya Veto kama walivyokubaliana katika mkutano wa Ezulwini  na Azimio la Sirte la mwaka 1999. 

Balozi Ibuge pia amezungumzia kuhusu utekelezaji wa mambo maalum ambayo yamo katika Hotuba ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli  aliyoitoa wakati wa kuzindua Bunge la 12, tarehe 13 Novemba 2020 jijini Dodoma, ambapo amemuomba Balozi Wang Ke kufikisha mambo yaliyomo katika hotuba hiyo kwa wawekezaji wa China ili kuwekeza nchini.

Balozi Ibuge amesema maono ya Mhe. Rais aliyoyasema katika hotuba yake ni utekelezaji wa moja ya kauli iliyowahi kutolewa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa "wakati wengine wanatembea Watanzania tunatakiwa tukimbie." ili kufikia maendeleo kwa haraka. 

Kwa Upande wake Balozi Wang Ke amemuhakikishia Balozi Ibuge, kwamba China iko pamoja na Bara la Afrika na kwamba wanaunga mkono  mapendekezo ya Bara la Afrika ya kuwa na nafasi mbili za kudumu katika Baraza hilo.

Balozi Wang Ke ameelezea kufurahishwa na maono ya Mhe. Rais yaliyobainishwa katika Hotuba hiyo na kuahidi kuendelea kuisaidia Tanzania ili kufanikisha maono hayo kwa vitendo na kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo. 

Viongozi hao pia wamejadiliana na kukubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kindugu baina ya Tanzania na China kwa faida ya pande zote mbili.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimkaribisha Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke alipokutana naye ofisini kwake jijini Dodoma.



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke walipokutana ofisini kwake jijini Dodoma.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo hayo walipokutana ofisini kwake jijini Dodoma.


Balozi Wang Ke akizungumza katika kikao hicho 






Friday, November 13, 2020

WABUNGE WA AFRIKA MASHARIKI WAHIMIZWA KUTANGULIZA MASLAHI YA TANZANIA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekutana na Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki na kuwahimiza kutanguliza  maslahi ya Tanzania katika kutekeleza majukumu yao.

Mhe. Ibuge amesema hayo jijini Dodoma alipokutana na Wabunge hao na kusisitiza kuwa maslahi ya Tanzania ni lazima yawe kipaumbele chao katika kutekeleza majukumu yao  ili kufanikisha ushiriki wa Tanzania kikamilifu katika mtangamano wa  Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 “Endeleeni kushikilia msimamo wa kutanguliza maslahi ya Tanzania siku zote, muendelee kufanya kazi hiyo nzuri  kwenye masuala mengine yote yanayogusa maslahi ya nchi yetu,” amesema Balozi Ibuge na kuongeza kuwa nafasi yao kama wabunge wa Afrika Mashariki inatokana na uwepo wa jimbo lao ambalo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mtangamano huo.

Balozi Ibuge pia amewataka Wabunge hao kuwasiliana mara kwa mara na Serikali ili kupata maoni, ushauri na msimamo wa Serikali katika kujadili na kupitisha masuala mbalimbali ndani ya bunge hilo.

Balozi Ibuge amewataka wabunge hao kujiepusha na migogoro ndani ya Bunge na Jumuiya kwani kufanya hivyo kutaiwezesha Tanzania kujiweka sawa katika nyanja za siasa na diplomasia na kuwapongeza kwa utendaji kazi wao na hasa jinsi walivyoshughulikia suala la Muswada binafsi wa Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Wabunge hao Mhe. Adam Kimbisa aliishukuru Wizara kwa kukutana nao kuwapa muongozo wa namna ya kushughulikia mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya Bunge na Jumuiya kwa ujumla.

Mhe. Kimbisa alimuahakikishia Katibu Mkuu kuwa Wabunge hao  wataendelea kuhakikisha maslahi ya Tanzania yanazingatiwa katika hatua zote za mtangamano kupitia ushiriki wao katika Bunge la Afrika Mashariki.

 


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) ofisini kwake Jijini Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge katika Picha ya pamoja na Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) walipomtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma




SALAMU ZA PONGEZI




 

Tuesday, November 10, 2020

COMORO YAIPONGEZA TANZANIA KWA UCHAGUZI HURU, AMANI NA HAKI

Rais wa Visiwa vya Comoro Mheshimiwa Azali Assouman ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufanya uchaguzi huru, amani na haki.

Rais wa Visiwa vya Comoro ameipongeza Tanzania leo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa tayari kuondoka nchini na kurejea Comoro baada ya kushuhudia hafla ya uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli uliofanyika Novemba 5 Jijini Dodoma.

Rais Assouman anasema Tanzania ni nchi ya Amani na utulivu wa kisiasa kwani wakati wote wa tukio la kuapishwa kwa Dkt Magufuli aliona mambo ambayo yanapaswa kuigwa na mataifa mengine hususan kwenye nyakati za uchaguzi.

"Kwa kweli tangu nimefika hapa Tanzania nimeona mambo mazuri na ambayo tunapaswa kuyaiga sisi viongozi wa mataifa mengine," Amesema Rais Assouman

Mbali na kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo ya uchaguzi, pia Rais Assouman ameliahidi ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika Nyanja za mbalimbali ikiwemo diplomasia ya uchumi, biashara, uwekezaji na utalii.

“Najisikia niko nyumbani kwa sababu uhusiano wetu umeimarishwa zaidi, mahusiano yetu yamekuwa katika masuala ya kijamii, utamaduni, biashara na mambo mengine mengi” Amebainisha Rais Assouman.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Sylvester Mabumba amesema kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Comoro katika kuhakikisha kuwa sera ya uchumi wa nchi zote mbili unakua zaidi.

"Sisi tuatendelea kushirikiana vyema na Comoro kibiashara ili kukuza sera ya 2025 tunaifikia ipasavyo kwa kuhakikisha kuwa uchumi wetu unafikia kiwango cha juu sana, naamini kuwa tunapokuwa na masoko ya uhakika Viswa vya Comoro uchumi wetu utakuwa zaidi," Amesema Balozi Mabumba.

Kwa Upande wake Balozi wa Visiwa Vya Comoro nchini Tanzania mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed amesema kuwa kuna fursa nyingi za kiuchumi ambazo Comoro na Tanzania zinaweza kushirikiana.

Rais Assouman aliwasili nchini Novemba 4 kwa ajili ya kuhudhuria hafla ya uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli uliofanyika Novemba 5 Jijini Dodoma ambapo baada ya shughuli hiyo alipata fursa ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ambapo na kujiona vivutio mbalimbali vya utalii nchini.

Serikali ya Tanzania na Visiwa Comoro zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo, elimu, afya, biashara na uwekezaji.


Rais wa Visiwa  vya Comoro, Mhe. Azali Assouman akiongea na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA),kabla ya kuondoka nchini na kurejea nchini Comoro. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe.Sylivester Mabunda  akifuatiwa na Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed.   


Rais wa Visiwa  vya Comoro, Mhe. Azali Assouman akiondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA), baada ya kushuhudia hafla ya Uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli iliyofanyika Novemba  5, 2020 Jijini Dodoma na Baadaye alitembelea Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro


Rais wa Visiwa  vya Comoro, Mhe. Azali Assouman, akiangalia kikundi cha ngoma   kabla ya kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA), baada ya kushuhudia hafla ya Uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli iliyofanyika Novemba 5, 2020, Jijini Dodoma na Baadaye alitembelea Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro

Kikundi cha Ngoma kikiburudisha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere kabla ya kuondoka kwa Rais wa Visiwa  vya Comoro, Mhe. Azali Assouman



Rais wa Visiwa  vya Comoro, Mhe. Azali Assouman, akiagana na Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe.Sylivester Mabunda katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA), Jijini Dar es Salaam


Rais wa Visiwa  vya Comoro, Mhe. Azali Assouman, akiaga tayari kwa  kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere(JNIA), kwa kutumia Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania)





Thursday, November 5, 2020

MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI AKILA KIAPO CHA URAIS

Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akila kiapo cha kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye sherehe za uapisho zilizofanyika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akila kiapo cha kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye sherehe za uapisho zilizofanyika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akihutubia hadhira iliyohudhuria sherehe ya uapisho katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, muda mfupi baada ya kula kiapo. 

Friday, October 23, 2020

NCHI ZA AFRIKA ZAHIMIZWA KUSHIKAMANA ILI KUONDOKANA NA UTEGEMEZI

Nchi za Afrika zimehimizwa kushikamana katika masuala ya maendeleo, biashara na uwekezaji ili kuondokana na utegemezi jambo litakaloliwezesha Bara hilo kufanya mambo yake kwa uhuru bila kuingiliwa na mataifa mengine ya nje kwa kisingizio cha demokrasia na haki za binadamu.

Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na Kiongozi wa Mabalozi wa nchi za Afrika hapa Tanzania Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed wakati Mabalozi hao walipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ikiwa ni utaratibu wa kukutana na Mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo na Tanzania.

Kiongozi huyo wa Mabalozi hapa nchini ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro amesema njia pekee ya Afrika kutoingiliwa katika mambo yake ya ndani ni kuhakikisha kuwa bara hilo linaweka mikakati madhubuti itakayowezesha bara hilo kujitegemea.

"Njia pekee ya Afrika kutoingiliwa katika mambo yake ya ndani ni kuhakikisha kuwa sisi kama waafrika tunaweka mikakati madhubuti itakayowezesha bara letu kujitegemea kwa umoja, mshikamano wetu wenyewe," Amesema Dkt. Mohamed

Nae Balozi wa Kenya hapa Nchini Mhe. Dan Kazungu amesema kikao hicho cha mabalozi wa Afrika na Prof. Kabudi hususani katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, umewawezesha mabalozi hao kufahamu namna Tanzania ilivyojiandaa kutekeleza demokrasia na kuwataka waafrika kujivunia nchi zao na kuwa wazalendo.

"MKutano wa leo umetuwezesha sisi mabalozi wa Afrika tunaowakilisha nchi zetu hapa Tanzania kufahamu namna Tanzania ilivyojiandaa kutekeleza demokrasia na kuwataka waafrika kujivunia nchi zao na kuwa wazalendo," Amesema Balozi Kazungu.   

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ameitumia fursa hiyo kuwaeleza Mabalozi hao namna Tanzania inavyoheshimu na kukuza diplomasia na mahusiano baina ya nchi za Afrika,kulinda demokrasia na haki za binadamu lakini pia kutumia fedha zake katika kuleta maendeleo ya watu na vitu jambo lililoiwezesha Tanzania kuingia katika nchi za uchumi wa kati kabla ya muda uliotarajiwa.  

"Waheshimiwa Mabaalozi napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania inaheshimu na imedhamiria kukuza diplomasia na mahusiano baina ya nchi za Afrika, kulinda demokrasia na haki za binadamu pamoja na kuhakikisha kuwa inatumia fedha zake za ndani katika kuleta maendeleo ya watu na vitu jambo lililoiwezesha Tanzania kuingia katika nchi za uchumi wa kati kabla ya muda uliotarajiwa," Amesema Prof. Kabudi.  

Mkutano huo uliohudhuriwa Mabalozi 15 na wawakilishi wa Balozi 8 walitumia fursa hiyo kumuombea Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baba wa Taifa hayati Julius Kambarage Nyerere kama Baba wa demokrasia Barani Afrika pamoja na kuuombea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28.

Mabalozi waliohudhuria katika mkutano huo ni Balozi wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed, Balozi wa Msumbiji, Mhe. Patricio Clemente, Balozi wa Namibia, Mhe. Theresia Samaria, Balozi wa Somalia, Mhe. Mohammed Abdi, Balozi wa Morocco, Mhe. Abdelilah Benryane, Balozi wa Zambia, Mhe. Benson Chali.

Wengine ni Balozi wa Burundi, Mhe. Gervais Abayeho, Balozi wa Kenya, Mhe. Dan Kazungu, Balozi wa Ethiopia, Mhe. Yonas Yosef Sanbe, Balozi wa Misri, Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abdulwafa, Balozi wa Angola, Mhe. Sandro De Oliveira, Balozi wa Malawi, Mhe. Chembe Mnthali, Balozi wa Saharawi, Mhe. Mahayub Buyema, Balozi wa Rwanda, Mhe. Meja Jenerali, Charles Karamba pamoja na Balozi wa Algeria, Mhe. Ahmed Djelal.

Wawakilishi waliowakilisha Balozi nane ni Bw. Jaafar Nasir Abdalla kutoka Ubalozi wa Sudan, Mr. Sizwe Ernest Mayoli kutoka Ubalozi wa Afrika Kusini, Balozi William Wani Ruben kutoka Ubalozi wa Sudani Kusini, Bibi. Bintu Bwala Ekikor kutoka Ubalozi wa Nigeria, Bw. Kamal Krista kutoka ubalozi wa Libya, Bw. Adjanga Bissa Benjamin kutoka ubalozi wa DRC, Bibi. Musekura Esezakutoka ubalozi wa Uganda pamoja na Bw. Chrispen Chibuwe kutoka Ubalozi wa Zimbabwe.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiongea na Mabalozi mbalimbali wa nchi za Afrika hapa nchini Tanzania leo jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akiwaonesha Mabalozi (hawapo pichani)  ilani ya Chama Cha Mapinduzi wakati mkutano ukiendelea



Mkutano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi na Mabalozi ukiendelea  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi mara baada ya kumaliza mkutano



Wednesday, October 21, 2020

TROIKA YA SADC YARIDHISHWA NA MAZINGIRA YA UCHAGUZI MKUU

Asasi ya Ushirikiano wa Siasa,Ulinzi na Usalama (TROIKA) ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeridhishwa na mazingira ya hali ya siasa nchini Tanzania yanaruhusu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Octoba 28,2020 na kwamba wataendelea kufuatilia mazingira ya uchaguzi huo.

Akizungumza katika Mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao Jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amesema TROIKA imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu tangu awali mchakato wa uchaguzi hapa nchini na kwamba imeridhishwa na mazingira ya amani yaliyopo hali inayoruhusu uchaguzi huo kufanyika.  

"Leo katika mkutano wangu na TROKA ulifanyika kwa njia ya mtandao mwenyekiti wa TROIKA ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Botswana Dkt. Lemogang Kwape ameoneshwa mazingira ya hali ya siasa nchini Tanzania yanaruhusu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Octoba 28, 2020 na kwamba wataendelea kufuatilia mazingira ya uchaguzi huo," Amesema Prof. Kabudi

Prof. Kabudi ameongeza kuwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipate uhuru kwamba uchaguzi huu unagharamiwa kwa fedha ya walipa kodi maamuzi ambayo yamefanyika kwa kutambua kuwa demokrasia ndio jambo kubwa katika uhai,utashi na kielelezo cha Taifa ambalo ni huru kama ilivyo Tanzania.

Kuhusu waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi mkuu wa Octoba 28, Prof Kabudi amesema TROIKA imefanya tathimini ya awali ya hali ya usalama na kisiasa na kwamba Tanzania inategemea kuwapokea waangalizi kutoka Umoja wa Afrika na wale wa kutoka katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amepokea nakala za hati za utambulisho za Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson.

Katika mazungumzo yao Prof. Kabudi amesema WFP imekuwa ni miongoni mwa mashirika ya Kimataifa ambayo yanaushirikiano mzuri na Tanzania ambapo kwa mwaka 2018 WFP imenunua tani 160,000 za nafaka na 2019 wamenunua tani 36,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 21 fedha ambazo zimesaidia wakulima wadogowadogo katika kuboresha kilimo.  

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson amesema wamejadiliana namna ya kuendeleza ushirikiano baina ya pande hizo mbili hususani kusaidia wakulima wadogowadogo nchini kuboresha kilimo,kuboresha mazingira ya lishe na kwamba shirika hilo lina mpango wa kuongeza msaada wanaoutoa kwa Tanzania. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akieleza jambo wakati mkutano wa TROIKA ukiendelea. Mkutano huo ulifanyika kwa njia ya mtandao leo Jijini Dar es Salaam.  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akipokea nakala ya hati za utambulisho za Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson leo jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiongea na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson leo jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi leo jijini Dar es Salaam



Monday, October 19, 2020

CHINA: TUHESHIMIANE, KUACHA KUINGILIA MASUALA YA NDANI YA NCHI NYINGINE

China imetoa wito kwa mataifa mengine duniani kuheshimiana na kuacha kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kwa kisingizio chochote kile na kueleza kuridhishwa kwake na namna mchakato wa Uchaguzi mkuu unavyoendelea hapa nchini.

Kauli hiyo imetolea na Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke Jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na kuongeza kuwa ni lazima Mataifa yote yaendeleze mahusiano mema miongoni mwao na kutoingilia masuala ya ndani ya Mataifa mengine.  

"Ni vyema Mataifa yote yakaendeleza mahusiano mema miongoni mwao na kuhakikisha kuwa hayaingilii masuala ya ndani kati ya Taifa moja na jingine," Amesema Balozi Wang Ke.  

Aidha Balozi Wang Ke ameongeza kuwa China itaendelea kuheshimu masuala ya ndani ya Mataifa yote Tanzania ikiwemo na kueleza kuridhika kwake na mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu zinavyoendelea nchini na kuwatakia Watanzania kila la heri katika uchaguzi huo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi,Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema  ushirikiano iliopo baina ya Tanzania na China kisiasa, kiuchumi na kijamii ni madhubuti na imara na kwamba Tanzania itaendelea pia kuheshimu mashirikiano na mataifa mengine.  

Aidha Katibu Mkuu Balozi Brigedia Jenerali Ibuge ameishukuru China kwa Ushirikiano wake wa kimkakati kwa Tanzania na kwamba uhusiano huo utaendelea kudumishwa kwa maslahi ya pande zote mbili.

"Serikali ya Tanzania kwa kweli inaishukuru China kwa Ushirikiano wake wa kimkakati na tunakuahidi kwamba uhusiano wetu utaendelea kudumishwa kwa maslahi mapana ya pande zote mbili," amesema Balozi Ibuge.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea na Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke wakati walipokutana kwa mazungumzo leo Jijini Dar es Salaam

Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke akimuelezea jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge



Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke akimkabidhi kitabu kinachoelezea maendeleo ya China Katibu  Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge





Friday, October 16, 2020

BALOZI IBUGE AKUTANA, KUMUAGA BALOZI WA NIGERIA

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, amekutana na kumuaga Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada ambaye amemaliza muda wake wa utumishi hapa nchini.  

Mazungumzo hayo yamefanyika leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, Balozi Ibuge amemtakia maisha mema na kumsihi kuwa balozi mwema kwa Tanzania nchini Nigeria na kwingineko duniani.

Balozi Ibuge amesema kuwa Nigeria imekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na Tanzania hasa katika kuunga mkono jitihada za kuimarisha sekta mbalimbali nchini ikiwemo sekta za usafirishaji, utalii, biashara na uwekezaji na usafirishaji

“Leo nimekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Gada ambae amemaliza muda wake wa utumishi hapa nchini na anarudi Nigeria, na kwa hakika mazungumzo marefu na yamelenga urafiki baina ya nchi zetu mbili na watu wetu pamoja na ushirikiano uliopo wa kibiashara, kibenki lakini pia tumezungumzia namna ambavyo Nigeria inapiga hatua kama Tanzania inavyopiga hatua, na mfano mzuri ni kuwa Nigeria ilipojenga mji wake mkuu mpya (Abuja) walikuja Tanzania kuja kujifunza na kupata ramani ya Dodoma ambayo wamemaliza kuijenga na sisi sasa tunaendelea kuijenga Dodoma tangu tulipotangaza rasmi kuhamia Dodoma mwaka 1973" Amesema Balozi, Brigedia Jenerali Ibuge  

Balozi Brigedia Jenerali Ibuge amemhakikishia Balozi Gada, kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Nigeria utaendelea kuimarika ikiwa ni ishara ya kuwaenzi waasisi wa mataifa ya Tanzania Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Rais wa kwanza wa Nigeria Nnamdi Azikiwe ambapo viongozi hawa walikuwa ni sehemu ya juhudi za kukomboa bara la Afrika na hata kusimi mwa Afrika. 

Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesisitiza kuwa Tanzania na Nigeria zitaendelea kushirikiana katika sekta ya uwekezaji na biashara kwa maslahi mapana ya mataifa yote mawili ambapo pia ametoa wito kwa wafanyabiashara kutoka nchini Nigeria kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta za benki na utalii. 

Kwa upande wake, Balozi Sherlock ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano iliyompatia wakati wote alipokuwa akitekeleza majukumu yake nchini na kuahidi kuwa ushirikiano uliopo utaendelezwa hasa ikizingatiwa kuwa Nigeria na Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri na imara tangu miaka ya 1962.

”Nimekuja kumuaga Katibu Mkuu kama ishara ya ushirikiano wetu kati ya Nigeria na Tanzania kwa kweli nashukuru sana kwa ushirikiano nilioupata wakati wa utumishi wangu hapa nchini, nikiwa hapa nimeona uchumi wa Tanzania ukikua kila wakati jambo ambalo ni zuri hapa kwetu Afrika, pia namshukuru Katibu Mkuu, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kwa kuuendeleza ushirikiano wetu kwa kweli naiona Tanzania kama nyumbani kwangu pia,"Amesema Balozi Gada.  

Nigeria itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania za kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuhakikisha kuwa inasonga mbele kimaendeleo,” amesema Balozi Gada.

Tanzania na Nigeria zimekuwa na uhusiano wa kidiplomasia tangu Serikali ya Nigeria ilipofungua ubalozi wake nchini Tanzania mwaka 1962.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimkaribisha Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada alipokenda kumuaga leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada akiongea na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati alipokwenda kumuaga leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimuelezea jambo Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada wakati alipokwenda kumuaga   


Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada akimkabidhi zawadi Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada  

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge pamoja na Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa kutoka Wizarani na Ubalozi wa Nigeria hapa nchini 








Tuesday, October 13, 2020

Tanzania Kutumia Maonesho Makubwa ya Qatar Kutangaza Utalii


Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Fatma Rajab alikutana na Shirika la Qatar Travel Mart (QTM) linalojishughulisha kutangaza utalii wa ndani na nje ya Qatar pamoja na kuandaa Maonesho ya Utalii. Shirika hilo linajiandaa kufanya Maonesho Makubwa ya Utalii  yatakayofanyika tarehe 17-19 November 2021. Mataifa mengi ya kigeni ya Asia, Ulaya na Marekani yanatarajiwa kushiriki Maonesho hayo pamoja na ofisi za Kibalozi ziliopo Qatar.

 Maonesho hayo yatatoa fursa kwa nchi kutangaza Biashara, uwekezaji na Sanaa. Mhe. Balozi amewaahidi kuwa Tanzania itashiriki kikamilifu kwenye Maonesho hayo. Aidha kabla ya Maonesho hayo Ubalozi utaandaa Mkutano wa Mtandao Webinar Conference mwezi Desemba 2020 baina ya Shirika hilo la QTM na TTB na ZTC ili kuelezea vivutio vya Utalii vya Tanzania na kukaribisha watalii kutoka Qatar

 

Friday, October 9, 2020

TANZANIA,CHINA ZAKUBALIANA KUIMARISHA MAHUSIANO YA KIMKAKATI

 Tanzania na China zimekubaliana kuendeleza mahusiano ya kimkakati baina yao ili kuwezesha uwepo wa ulingo sawa miongoni mwa mataifa katika kusimamia maslahi na maendeleo ya nchi husika katika jumuiya za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John kabudi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke na kusisitiza umuhimu wa Mataifa kuheshimiana na kutokubali kuingilia uhuru wa mambo ya ndani ya nchi kwa kisingizio cha haki za binadamu,demokrasia ama jambo lolote jingine.  

Ameongeza kuwa mazungumzo hayo ya kimkakati yalilenga pia kutambua kuwa mwaka huu ni mwaka wa 55 tangu Tanzania na China zisaini mkataba wa urafiki ambao uliweka msingi wa mahusiano makubwa na ya dhati  katika nyanja za ulinzi na usalama,afya,kilimo, elimu na miundo mbinu ambapo mpaka sasa China ni Taifa linaloongoza hapa nchini kwa uwekezaji wa moja kwa moja kwa kuwekeza zaidi ya miradi 700 yenye thamani ya dola za Kimarekani (USD) bilioni 7.1 na kutengeneza zaidi ya ajira 87,000 kwa watanzania.

Kwa upande wake Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke amesema China wakati wote ni Rafiki mwaminifu na wa kudumu wa nyakati zote kwa Tanzania na kwamba kutimiza miaka 55 ya urafiki wa nchi hizo ni kielelezo tosha na siku zote wataendelea kuuheshimu na kuuenzi urafiki huo.

Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Riitta Swan pamoja na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Pamela O'Donnell, ambapo pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi na mabalozi waliadili masuala mbalimbali ikiwemo kuimarisha mahusiano, Uwekezaji na Biashara, Afya, Elimu pamoja na Utalii.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akiongea na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke wakati walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam 

Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati wa mazungumzo yao leo jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimkaribisha Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Riitta Swan kabla ya kuanza kwa mazungumzo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimuonesha Balozi wa Canada nchini, Mhe. Pamela O'Donnell sheria ya uchaguzi kabla ya kumkabidhi sheria hiyo pamoja na nyaraka nyingine zinazohusu masuala ya uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 28 Oktoba 2020