Saturday, August 31, 2013

M23 yachakazwa




M23 yachakazwa

Na Habari Leo

KIKUNDI cha waasi cha M23 kinachopambana na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kimeripotiwa kupigwa vibaya na kutikisa nguvu za kikundi hicho kutokana na baadhi ya wapiganaji wake kuripotiwa kupoteza maisha.

Mapigano baina ya M23 na Jeshi la Serikali ya DRC linalosaidiwa na Kikosi Maalumu cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO), yameibuka upya ndani ya wiki hii.

Habari za kiintelijensia ambazo gazeti hili limezipata zinasema kuwa, kutokana na shambulio hilo, Serikali ya Rwanda imelazimika kuingilia kati kusaidia waasi hao kwa kupeleka bataliani mbili zenye jumla ya askari 1,700 huko DRC, ili waweze kukabiliana na nguvu ya majeshi ya DRC, Monusco na Brigedi ya Majeshi ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa yenye mamlaka ya kujibu mapigo (FIB).

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, Rwanda imepeleka bataliani hizo mbili zenye askari 850 kila moja saa 24 zilizopita na kwamba wamevuka mpaka kuingia DRC katika eneo la Kibumba, lakini wanashindwa kusonga mbele.

Habari zaidi zinasema sababu ya Rwanda kupeleka askari wake hao ni kusaidia M23 ambao walipigwa sana Agosti 23 na 27, mwaka huu katika eneo la vilima vya Kibati na haijulikani kama kweli waasi hao wako katika eneo hilo au wamekwishakimbia kutokana na kipigo walikichopata.

“M23 walitandikwa sana Agosti 23 na 27 katika eneo la vilima vya Kibati, na wala haijulikani kama wapo hai au vipi, ndio maana sasa hivi Rwanda imepeleka batalioni zao kuwapa nguvu, lakini wanashindwa kusonga mbele maana hawajielewi kwa sababu ya kipigo walichopata,” kilisema chanzo kimoja cha habari.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, eneo la Kibati ndilo eneo kubwa la M23 ambalo wamekuwa wakitumia kuhifadhi silaha zao za kivita, lakini wakati wa mapambano majeshi ya DRC, MUNUSCO na FIB yalisambaratisha kabisa ngome hiyo ya waasi.

FIB inaundwa na askari wengi wa Afrika Kusini na Tanzania. Habari zaidi zinasema kwa sasa majeshi ya DRC, Monusco na FIB yanawasubiri kwa hamu askari hao wa Rwanda kuingia uwanja wa vita ili kukabiliana nao kama walivyokabiliana na waasi wa M23.

“Taarifa tulizonazo hivi sasa Rwanda inajiuliza iwapo isonge mbele kupambana au irudi nyuma, ikifikiria pia kipigo walichopata M23,” kilisema chanzo kimoja cha habari.

Inaelezwa kwamba, kutokana na kipigo walichopata M23 siku chache zilizopita kimepelekea Rwanda kujikuta ikikiri na kusema ukweli juzi kuwa inakisaidia kikundi hicho cha waasi.

Vyanzo hivyo vya habari viliendelea kusema kuwa, mwaka jana mwezi Mei, Baraza la Usalama la UN katika ufuatiliaji wake lilibaini majeshi ya Rwanda kushiriki vurugu zinazoendelea ndani ya DRC, hali iliyosababisha Nchi za Maziwa Makuu kuingilia kati ili kuleta suluhu bila kuishirikisha Rwanda ambayo ilionekana kuwa na maslahi ndani ya mgogoro huo.

Katika hatua nyingine, taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa zilisema, Waziri Bernard Membe alikutana na Mabalozi wa Mataifa matano ambayo ni wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kujadili masuala mbalimbali ya Kikanda na hasa mgogoro wa DRC.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Waziri Membe alipokutana na mabalozi hao alishukuru Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kutoa tamko la kulaani vikali tukio la kuuawa kwa mlinzi wa Amani wa Tanzania na kutuma salamu za pole kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na familia ya marehemu.

Waziri Membe pia aliomba baraza hilo kuitaka Rwanda kuacha kuingiza majeshi yake DRC kwa nia ya kusaidia waasi wa M23 na kuongeza kuwa linapokuja suala la FIB wito wao ni “akishambuliwa mmoja, wameshambuliwa wote.”

Mabalozi aliokutana nao Waziri Membe ni kutoka Urusi, Uingereza, Ufaransa, Marekani na China, nchi ambazo zinajulikana kama wajumbe wa kudumu wa Baraza hilo la Usalama.

Wakati huo huo, Waziri Membe alisema Rais Yoweri Museveni ameitisha kikao cha dharura cha Nchi za Maziwa Makuu, mjini Kampala ili kujadili mgogoro huo wa DRC kitakachofanyika Septemba 4 na Septemba 5, mwaka huu. Alisema Septemba 4 utakuwa mkutano wa Mawaziri na Septemba 5 utakuwa mkutano wa Marais wa nchi hizo.

Katika hatua nyingine, jeshi la Afrika Kusini limetamba kuwa lipo tayari kuongeza nguvu kwa wapiganaji wa Monusco kwa kuwa wanaamini wana jeshi imara lenye uwezo wa kuchakaza `wakorofi’.

Kauli hiyo imetolewa na Luteni Jenerali wa Jeshi la Afrika Kusini, Derrick Ngwebi alipozungumza na wapiganaji katika kambi ya Thaba Tshwane, jijini Pretoria. “Tuko imara na tayari kwa lolote huko DRC. Hatuna chembe ya shaka,” alisema na kuongeza kuwa, Umoja wa Mataifa umewaomba Afrika Kusini kuongeza zana za kivita huko Mashariki kwa DRC.

“Kikosi cha mizinga kinatoka Tanzania na kimeshatua DRC. Kwa upande wa helikopta za kivita Umoja wa Mataifa ulituomba tujiandae, nasi tumefanya hivyo na nawahakikishieni, kazi itafanyika,” alisema Ngwebi na kuongeza kuwa, imeshatanguliza askari na helikopta tatu za kivita wakati ikijipanga kupeleka helikopta zaidi na za kisasa za kivita.

Wiki iliyopita, Rais Jacob Zuma aliliambia Bunge la Afrika Kusini kuwa nchi yake imeshapeleka askari 1,345 huko Mashariki na DRC.


Kwa hisani ya:  www.habarileo.co.tz




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.