Friday, August 30, 2013

Mhe. Membe azungumza na Mabalozi kutoka nchi tano Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali nchini DRC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini ambao pia nchi zao ni Wanachama wa Kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (Permanent 5) kuhusu  hali inayoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Mhe. Membe pia aliwapa taarifa za kuitishwa kwa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) utakaofanyika mjini Kampala, Uganda tarehe 5 Septemba, 2013 kuhusu DRC. Nchi tano wanachama wa Baraza la Kudumu la Usalama la Umoja wa Mataifa ni China, Marekani, Ufaransa, Uingereza na Urusi. Mkutano na Mabalozi hao umefanyika Wizarani tarehe 30 Agosti, 2013.
Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Lu Youqing (kushoto) akitafakari jambo wakati wa mazungumzo yao na Mhe. Membe (hayupo pichani). Wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Celestine Mushy (kulia) na Afisa kutoka Ubalozi wa China.

Balozi wa Uingereza hapa nchini, Mhe. Diana Melrose (wa tatu kushoto) akiwa na Wajumbe kutoka Urusi, Ufaransa na Marekani wakati wa Mkutano wao na Mhe. Membe (hayupo pichani) kuhusu hali nchini DRC.

Mhe. Membe akitoa shukrani kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia Mabalozi hao kwa kulaani mauaji ya Mwanajeshi wa Tanzania yaliyotokea huko Mashariki mwa DRC tarehe 28 Agosti, 2013 kwa kushambuliwa na kundi la Waasi la M23  wakati Kikosi cha Kulinda Amani cha  Umoja wa Mataifa (MONUSCO)kwa kushirikiana na Majeshi ya Serikali ya DRC na Force Intervention Brigade (FIB) wakilinda amani. Anayesikiliza kwa makini ni Mhe. Alfonso Lenhardt, Balozi wa Marekani hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.