TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA RAIS
WA JAMHURI YA WATU WA CHINA, MHE. XI JINPING NCHINI, TAREHE 24 – 25 MACHI 2013
ILIYOTOLEWA NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, MHE. BERNARD
K. MEMBE (MB), TAREHE 22 MACHI 2013
1.0 UTANGULIZI
1.1 Ndugu waandishi, nimewaita leo ili
kuwaeleza kuhusu ziara ya kihistoria hapa nchini ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa
China, Mhe. Xi Jinping ambayo itafanyika hivi karibuni. Najua mtakuwa
mmekwishasikia kuwa Rais huyu atafika nchini hivi karibuni.
Sasa
niwatangazie rasmi kuwa taarifa hii ni sahihi na ziara hiyo itafanyika tarehe
24 – 25 Machi, 2013. Ziara hii ni ya kwanza kwa Rais Xi barani Afrika mara tu
baada ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo ya Urais mnamo tarehe 14 Machi, 2013.
1.2 Mahusiano
ya Tanzania na China yametoka
mbali, tangu enzi ya waanzilishi wa mataifa haya mawili, yaani Mwalimu Julius
Nyerere wa Tanzania na Mao Zedong wa
China. Ifahamike kuwa, kutokana na mahusiano haya ndipo mmoja ya miradi mikubwa
kabisa iliyofanywa na China barani Afrika ulitokea. Mradi huu ni reli ya
Tanzania na Zambia (TAZARA). Pamoja na kuwa mradi wa kimaendeleo, reli hii ya
TAZARA ilitusaidia katika ukombozi wa bara la Afrika – kama moja ya njia za
usafiri, hivyo kuifanya China kuwa rafiki wa kweli. Mradi mwingine mkubwa ni
ujenzi wa jengo la Umoja wa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia. Haya, kati ya
mengineyo, yanafanya ugeni huu kuwa wa kihistoria na heshima kubwa kwetu.
1.3 Rais
Xi anakuja kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya
Mrisho Kikwete na akiwa nchini atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Mheshimiwa
Rais Kikwete, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.
Dkt Ali Mohamed Shein. Mheshimiwa Xi ataambatana na mke wake, pamoja na Maafisa
Waandamizi wa Serikali ya China wasiopungua 25.
2.0 RATIBA YA MGENI KWA KIFUPI
2.1 Rais Xi Jinping atawasili nchini siku ya
jumapili tarehe 24 Machi, 2013 saa 10:25 jioni katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ndege maalumu aina ya Boeing 747 ambapo
atalakiwa na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
2.2 Baadaye Rais Xi pamoja na ujumbe wake
watafanya mazungumzo rasmi na Rais Jakaya Kikwete pamoja na Viongozi Waandamizi
wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mazungumzo hayo yataanza saa
12:15 jioni na yatafanyikia Ikulu.
2.3 Baada ya mazungumzo rasmi, Rais Xi pamoja
na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete watashuhudia utiaji saini wa Makubaliano
na Mikataba mbalimbali (kumi na tisa) ya ushirikiano baina ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania/na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande mmoja na Serikali ya Jamhuri ya
Watu wa China kwa upande mwingine. Kwa kifupi mikataba hiyo inahusu kukuza
uwekezaji na biashara baina ya nchini za Tanzania na China, kukuza ushirikiano
wa kiutamaduni baina ya nchi hizi mbili na watu wake, nk.
2.4
Baada ya tukio hilo, Rais Xi pamoja na
ujumbe wake watahudhuria dhifa ya kitaifa itakayoandaliwa kwa heshima yake na Rais Jakaya Kikwete.
Dhifa hiyo itafanyika Ikulu kuanzia saa 1:40 usiku. Hilo ndilo litakuwa tukio
la mwisho kwa siku ya kwanza.
2.5 Siku itakayofuata ya tarehe 25 Machi, 2013
saa 3:10 asubuhi Rais Xi atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Ali Mohamed Shein pamoja na ujumbe wa
Viongozi Waandamizi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
2.6 Tukio litakalofuata litakuwa ni uzinduzi na
makabidhiano rasmi ya kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere kilichojengwa kwa msaada wa Serikali ya China kwa lengo la
kumuenzi Mwalimu Nyerere. Baada ya makabidhiano ndipo Rais Xi atatoa hotuba
maalumu kwa Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla. Hotuba hiyo itajikita katika
kuelezea Sera ya Serikali mpya ya China kwa bara la Afrika. Watu kutoka kada mbalimbali
kama vile Wahadhiri wa Vyuo Vikuu, Wanafunzi, Wabunge, Viongozi na Maafisa
Waandamizi wa Serikali, Wafanyabiashara, n.k. wamealikwa kuhudhuria ukumbini
hapo.
2.7 Mchana wa tarehe 25 Machi, 2013 Rais Xi
Jinping ataelekea katika Makaburi ya Wataalamu wa Kichina ya Majohe yaliyopo
katika kijiji cha Majohe – Ukonga ambapo atatoa heshima zake kwa Wachina
waliofariki wakati wakijenga Reli ya TAZARA.
2.8 Baada ya hapo Rais Xi ataelekea Uwanja wa
Ndege wa Julius K. Nyerere ambapo ataondoka saa 10:40 jioni kuelekea nchini
Afrika Kusini kuhudhuria Mkutano wa tano wa Wakuu wa Nchi za BRICS.
3.0 FAIDA
ILIYOPATA TANZANIA KUTOKANA NA UHUSIANO NA CHINA
3.1 Jambo kubwa Tanzania inalojivunia tangu
kuanzisha uhusiano na China ni kukua kwa urafiki wa karibu sana na China; urafiki wa kuaminiana na kusaidiana katika
nyanja mbalimbali za kitaifa, kikanda na kimataifa. Uhusiano huo wa karibu
unazidi kukua kila kukicha.
3.2 Kwa upande wa ushirikiano wa kiuchumi
Tanzania inajivunia miradi mbalimbali ya kimaendeleo iliyotekelezwa kwa
ushirikiano na China. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na:
i. Mradi
wa Reli ya TAZARA – kama nilivyoeleza hapo awali Mradi huu umekuwa mhimili na
kiungo muhimu sana katika ukuzaji wa uchumi wa Tanzania na nchi jirani za
Zambia, DRC, Zimbabwe n.k, hususan
katika sekta ya usafirishaji wa rasilimali ghafi, bidhaa za kibiashara
na abiria
ii. Kiwanda
cha nguo cha URAFIKI – (licha ya changamoto kadhaa zinazokikabili) kiwanda hiki
kimetoa ajira kwa Watanzania wengi, pamoja na soko kwa pamba inayolimwa hapa nchini.
iii. Miradi
mikubwa ya maji ya Shinyanga, Dar es Salaam na Pwani.
iv. Viwanja
vya kisasa vya michezo – Uwanja wa Taifa (Dar es Salaam) na Karume Stadium
(Zanzibar).
v. Kituo
cha maonesho na majaribio ya zana za kilimo cha Mvomero, Morogoro.
vi. Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius K. Nyerere. Manufaa ya Kituo hiki
cha Mikutano ni kama yale yanayopatikana katika Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Arusha (AICC).
vii. Mradi
wa ujenzi wa mkongo wa Taifa kwa Tanzania bara na Zanzibar – mradi huu ni
muhimu sana katika maendeleo ya sekta ya Teknohama (Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano). Manufaa yake yatapatikana si tu hapa Tanzania lakini pia kwa nchi
za jirani kama vile Rwanda, Burundi, n.k, kwani huduma hii itatolewa kibiashara.
viii. Mradi
wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam – Mradi huu utakapokamilika
hapo mwakani utatupatia uhakika wa umeme, pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa
gharama zake. Pia utapelekea kupungua kwa gharama za maisha kwa ujumla na kukua
kwa kipato cha mtu mmoja mmoja kiuchumi.
ix. Manufaa
mengine mengi yanatarajiwa kupatikana mara baada ya ziara.
4.0 MATARAJIO YA TANZANIA KUTOKANA NA ZIARA HII
4.1 Katika ziara hii ya kihistoria Tanzania
inatarajia kufaidika kwa namna mbalimbali kama ifuatavyo:
i. Kufungua
milango ya uwekezaji katika sekta mbalimbali. Ziara hii inafuatiliwa na
kumulikwa na nchi karibu zote duniani; pamoja na makampuni makubwa kila kona ya
dunia. Ziara ya Rais wa huyu wa China inatuma ujumbe kwa wawekezaji kote
duniani kuhusu mazingira mazuri na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini
Tanzania.
ii. Wakati
wa ziara hii mikataba na makubaliano zaidi ya 19 yatatiwa saini kati ya
Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa upande mmoja, na Serikali ya China kwa upande mwingine (tafadhali rejea kiambatisho Na.1 kwa
orodha ya Makubaliano na Mikataba iyakayotiwa saini.)
Kama
ilivyoelezwa hapo awali, Mikataba na makubaliano haya yanagusa sekta za kilimo
kibiashara, uwekezaji, uendelezaji wa miundombinu, miradi ya maji na umeme,
fursa za kimasomo kwa vijana wa Kitanzania nchini China, nk.
5.0 HITIMISHO
5.1 Uhusiano
kati ya Tanzania na China ni wa muda mrefu tangu miaka ya 1950 wakati bado
Tanzania (Tanganyika kwa wakati huo) ikiwa katika harakati za kupigania Uhuru.
Mwaka kesho (2014) nchi zetu mbili zitasherehekea miaka 50 ya uhusiano wa
kidiplomasia. Uhusiano huu unatoa picha ya ukaribu uliopo kati ya Serikali za
nchi za Tanzania na China pamoja na watu wake.
5.2 Hivyo basi, napenda kuchukua fursa hii
kuwaomba Watanzania wote kwa ujumla tujitokeze kwa wingi kumlaki Rais Xi
Jinping atakapokuwa anawasili kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K.
Nyerere mpaka Hoteli ya Serena atakapofikia kwa kupitia Barabara ya Pugu/Julius
K. Nyerere.