Friday, March 22, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


220px-Coat of arms of Tanzania.svg f1f71
 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA RAIS WA JAMHURI YA WATU WA CHINA, MHE. XI JINPING NCHINI, TAREHE 24 – 25 MACHI 2013 ILIYOTOLEWA NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, MHE. BERNARD K. MEMBE (MB), TAREHE 22 MACHI 2013
1.0     UTANGULIZI
1.1     Ndugu waandishi, nimewaita leo ili kuwaeleza kuhusu ziara ya kihistoria hapa nchini ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping ambayo itafanyika hivi karibuni. Najua mtakuwa mmekwishasikia kuwa Rais huyu atafika nchini hivi karibuni.
Sasa niwatangazie rasmi kuwa taarifa hii ni sahihi na ziara hiyo itafanyika tarehe 24 – 25 Machi, 2013. Ziara hii ni ya kwanza kwa Rais Xi barani Afrika mara tu baada ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo ya Urais mnamo tarehe 14 Machi, 2013.
1.2     Mahusiano  ya  Tanzania na China yametoka mbali, tangu enzi ya waanzilishi wa mataifa haya mawili, yaani Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Mao Zedong  wa China. Ifahamike kuwa, kutokana na mahusiano haya ndipo mmoja ya miradi mikubwa kabisa iliyofanywa na China barani Afrika ulitokea. Mradi huu ni reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA). Pamoja na kuwa mradi wa kimaendeleo, reli hii ya TAZARA ilitusaidia katika ukombozi wa bara la Afrika – kama moja ya njia za usafiri, hivyo kuifanya China kuwa rafiki wa kweli. Mradi mwingine mkubwa ni ujenzi wa jengo la Umoja wa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia. Haya, kati ya mengineyo, yanafanya ugeni huu kuwa wa kihistoria na heshima kubwa kwetu.
 1.3    Rais Xi anakuja kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na akiwa nchini atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Kikwete, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein. Mheshimiwa Xi ataambatana na mke wake, pamoja na Maafisa Waandamizi wa Serikali ya China wasiopungua 25.
2.0     RATIBA YA MGENI KWA KIFUPI
2.1     Rais Xi Jinping atawasili nchini siku ya jumapili tarehe 24 Machi, 2013 saa 10:25 jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ndege maalumu aina ya Boeing 747 ambapo atalakiwa na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
2.2     Baadaye Rais Xi pamoja na ujumbe wake watafanya mazungumzo rasmi na Rais Jakaya Kikwete pamoja na Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mazungumzo hayo yataanza saa 12:15 jioni na yatafanyikia Ikulu.
2.3     Baada ya mazungumzo rasmi, Rais Xi pamoja na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete watashuhudia utiaji saini wa Makubaliano na Mikataba mbalimbali (kumi na tisa) ya ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania/na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa upande mmoja na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa upande mwingine. Kwa kifupi mikataba hiyo inahusu kukuza uwekezaji na biashara baina ya nchini za Tanzania na China, kukuza ushirikiano wa kiutamaduni baina ya nchi hizi mbili na watu wake, nk.
2.4     Baada ya tukio hilo, Rais Xi pamoja na ujumbe wake watahudhuria dhifa ya kitaifa itakayoandaliwa  kwa heshima yake na Rais Jakaya Kikwete. Dhifa hiyo itafanyika Ikulu kuanzia saa 1:40 usiku. Hilo ndilo litakuwa tukio la mwisho kwa siku ya kwanza.
2.5     Siku itakayofuata ya tarehe 25 Machi, 2013 saa 3:10 asubuhi Rais Xi atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Ali Mohamed Shein pamoja na ujumbe wa Viongozi Waandamizi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
2.6     Tukio litakalofuata litakuwa ni uzinduzi na makabidhiano rasmi ya kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kilichojengwa kwa msaada wa Serikali ya China kwa lengo la kumuenzi Mwalimu Nyerere. Baada ya makabidhiano ndipo Rais Xi atatoa hotuba maalumu kwa Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla. Hotuba hiyo itajikita katika kuelezea Sera ya Serikali mpya ya China kwa bara la Afrika. Watu kutoka kada mbalimbali kama vile Wahadhiri wa Vyuo Vikuu, Wanafunzi, Wabunge, Viongozi na Maafisa Waandamizi wa Serikali, Wafanyabiashara, n.k. wamealikwa kuhudhuria ukumbini hapo.
2.7     Mchana wa tarehe 25 Machi, 2013 Rais Xi Jinping ataelekea katika Makaburi ya Wataalamu wa Kichina ya Majohe yaliyopo katika kijiji cha Majohe – Ukonga ambapo atatoa heshima zake kwa Wachina waliofariki wakati wakijenga Reli ya TAZARA.
2.8     Baada ya hapo Rais Xi ataelekea Uwanja wa Ndege wa Julius K. Nyerere ambapo ataondoka saa 10:40 jioni kuelekea nchini Afrika Kusini kuhudhuria Mkutano wa tano wa Wakuu wa Nchi za BRICS.
 
3.0     FAIDA ILIYOPATA TANZANIA KUTOKANA NA UHUSIANO NA CHINA
3.1     Jambo kubwa Tanzania inalojivunia tangu kuanzisha uhusiano na China ni kukua kwa urafiki wa karibu sana na China;  urafiki wa kuaminiana na kusaidiana katika nyanja mbalimbali za kitaifa, kikanda na kimataifa. Uhusiano huo wa karibu unazidi kukua kila kukicha.
3.2     Kwa upande wa ushirikiano wa kiuchumi Tanzania inajivunia miradi mbalimbali ya kimaendeleo iliyotekelezwa kwa ushirikiano na China. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na:

            i.    Mradi wa Reli ya TAZARA – kama nilivyoeleza hapo awali Mradi huu umekuwa mhimili na kiungo muhimu sana katika ukuzaji wa uchumi wa Tanzania na nchi jirani za Zambia, DRC, Zimbabwe n.k, hususan  katika sekta ya usafirishaji wa rasilimali ghafi, bidhaa za kibiashara na abiria
 
           ii.    Kiwanda cha nguo cha URAFIKI – (licha ya changamoto kadhaa zinazokikabili) kiwanda hiki kimetoa ajira kwa Watanzania wengi, pamoja na soko kwa pamba inayolimwa hapa nchini.
 
         iii.    Miradi mikubwa ya maji ya Shinyanga, Dar es Salaam na Pwani.
 
          iv.    Viwanja vya kisasa vya michezo – Uwanja wa Taifa (Dar es Salaam) na Karume Stadium (Zanzibar).
 
           v.    Kituo cha maonesho na majaribio ya zana za kilimo cha Mvomero, Morogoro.
 
          vi.    Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius K. Nyerere. Manufaa ya Kituo hiki cha Mikutano ni kama yale yanayopatikana katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
 
        vii.    Mradi wa ujenzi wa mkongo wa Taifa kwa Tanzania bara na Zanzibar – mradi huu ni muhimu sana katika maendeleo ya sekta ya Teknohama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano). Manufaa yake yatapatikana si tu hapa Tanzania lakini pia kwa nchi za jirani kama vile Rwanda, Burundi, n.k, kwani huduma hii itatolewa kibiashara.
 
      viii.    Mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam – Mradi huu utakapokamilika hapo mwakani utatupatia uhakika wa umeme, pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama zake. Pia utapelekea kupungua kwa gharama za maisha kwa ujumla na kukua kwa kipato cha mtu mmoja mmoja kiuchumi.
 
          ix.    Manufaa mengine mengi yanatarajiwa kupatikana mara baada ya ziara.

 
4.0     MATARAJIO YA TANZANIA KUTOKANA NA ZIARA HII
4.1     Katika ziara hii ya kihistoria Tanzania inatarajia kufaidika kwa namna mbalimbali kama ifuatavyo:
 

            i.    Kufungua milango ya uwekezaji katika sekta mbalimbali. Ziara hii inafuatiliwa na kumulikwa na nchi karibu zote duniani; pamoja na makampuni makubwa kila kona ya dunia. Ziara ya Rais wa huyu wa China inatuma ujumbe kwa wawekezaji kote duniani kuhusu mazingira mazuri na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.

 
           ii.     Wakati wa ziara hii mikataba na makubaliano zaidi ya 19 yatatiwa saini kati ya Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande mmoja, na Serikali ya China kwa upande mwingine (tafadhali rejea kiambatisho Na.1 kwa orodha ya Makubaliano na Mikataba iyakayotiwa saini.)
 
Kama ilivyoelezwa hapo awali, Mikataba na makubaliano haya yanagusa sekta za kilimo kibiashara, uwekezaji, uendelezaji wa miundombinu, miradi ya maji na umeme, fursa za kimasomo kwa vijana wa Kitanzania nchini China, nk.
 
5.0     HITIMISHO
5.1     Uhusiano kati ya Tanzania na China ni wa muda mrefu tangu miaka ya 1950 wakati bado Tanzania (Tanganyika kwa wakati huo) ikiwa katika harakati za kupigania Uhuru. Mwaka kesho (2014) nchi zetu mbili zitasherehekea miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia. Uhusiano huu unatoa picha ya ukaribu uliopo kati ya Serikali za nchi za Tanzania na China pamoja na watu wake.
5.2     Hivyo basi, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba Watanzania wote kwa ujumla tujitokeze kwa wingi kumlaki Rais Xi Jinping atakapokuwa anawasili kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K. Nyerere mpaka Hoteli ya Serena atakapofikia kwa kupitia Barabara ya Pugu/Julius K. Nyerere.


 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.