TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia
salamu za pongezi Mheshimiwa Xi Jinping kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya
Watu wa China.
Rais Jinping
alichaguliwa Jumanne wiki hii kuwa Rais wa China kuchukua nafasi ya Mheshimiwa
Hu Jintao ambaye amemaliza muda wa uongozi wa miaka 10.
Katika salamu
zake za pongezi, Rais Kikwete amemwambia Rais Jinping: “Naomba uniruhusu nitumie nafasi
hii kukupongeza kwa dhati kutokana na ushindi wako mkubwa na uliostahiki wa
kuwa Rais wa taifa lako kubwa.”
“Kama
unavyojua China na Tanzania zimekuwa na mahusiano maridadi kwa zaidi ya miaka
50 kwa sasa. Tunawashukuru waanzilishi ya mataifa yetu: Mwenyekiti Mao Tse Tung
na Waziri Mkuu Chou En Lai kwa upande wa China na Rais Julius Kambarage Nyerere
kwa upande wa Tanzania. Urafiki huu umedumu na kuhimili muda wote, umekuwa wa
kudumu kwa hakika wakati wote umedumishwa, umelelewa na kuendelezwa na vizazi
vilivyofuatia vya viongozi wa nchi zote mbili, “ amesema Rais
Kikwete na kuongeza:
“Mataifa yetu
mawili rafiki yanashirikiana kwenye masuala mengi yanayohusu mataifa yetu yenyewe
mawili, masuala ya kikanda na yale ya kimataifa, na wakati wote tumeungana
mkono katika uwanja wa kimataifa. Napenda kukuhakishia utayari wangu binafsi na
ule wa Serikali yangu kufanya kazi nawe katika kuendeleza uhusiano huu na kuufikisha
kwenye hatua kubwa zaidi.”
Amesisitiza
Rais Kikwete: “Sisi katika Tanzania tunajiandaa kwa ari kubwa na matarajio makubwa
kukupokea Mheshimiwa baadaye mwezi huu kwenye ziara yako ya kwanza ya
Kiserikali katika Tanzania. Hakuna shaka kuwa siyo tu kwamba ziara yako itakuwa
ya kihistoria bali pia itasaidia kuimarisha mahusiano ya nguvu na ya karibu
sana ya urafiki na uhusiano ambayo umedumu kwa furaha baina ya mataifa yetu
mawili na watu wake, pamoja na Afrika kwa jumla.”
Amemalizia
Rais Kikwete katika salamu zake za pongezi: “Nakutakia Mheshimiwa kila la
heri na kila aina ya mafanikio wakati unajiandaa kuanza kazi na wajibu wako wa
heri wa kuongoza taifa lako kubwa na wananchi rafiki wa China ili kuwaelekeza
kwenye hatua kubwa zaidi ya maendeleo.”
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar
es Salaam.
15
Machi, 2013
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.