Wednesday, July 20, 2016

Waziri Mahiga asaini Mkataba wa Uenyeji wa Benki ya Afrika Mashariki

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Dkt. Augustine Mahiga pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Bi. Vivienne Yeda wakisaini Mkataba wa Uenyeji (Host Agreement) wa Ofisi za  Benki hiyo nchini. Hafla hiyo ilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki tarehe 20 Julai, 2016.
Waziri Mahiga na Bi. Yeda wakibadilishana Mkataba mara baada ya kuusaini.
Dkt. Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na Bi. Yeda, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Baraka Luvanda  (kulia) na Mkuu wa Biashara wa EADB hapa nchini Bi. Juliana Sweke (kushoto).


Picha na Reginald Philip 

Waziri Mahiga asaini Mkataba wa uenyeji wa Benki ya EADB

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) amesaini Mkataba wa uenyeji (Host Agreement) wa Ofisi za Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) na Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Bi. Vivienne Yeda. Mkataba huo umesainiwa leo katika Ofisi za Wizara  kwa lengo la kurasimisha kisheria Ofisi za Benki hiyo zilizopo nchini.

Aidha, uwekaji saini wa mkataba huo ni utekelezaji wa agizo la Mkutano wa Wakuu wa Nchi  Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki  uliofanyika tarehe 2 Machi, 2016  Mjini Arusha -Tanzania. Mkutano huo pamoja na mambo mengine uliazimia kuanzishwa kwa Ofisi za Benki hiyo katika Makao Makuu ya kila nchi Mwanachama ili kuwezesha utekelezaji madhubuti wa shughuli za Benki hiyo. 

Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki ni Taasisi ya Fedha iliyoanzishwa mwaka 1967 chini ya iliyokuwa  Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa lengo la kutoa misaada ya kifedha na misaada mingine  ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

EADB ilianzishwa wakati iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa na wanachama watatu ambao ni Tanzania, Kenya na Uganda.  Rwanda ilijiunga na Benki hiyo  mwaka 2007 na kufanya nchi wananchama waliojiunga kufikia wanne.

Kwa upande wa Tanzania, EADB imeisaidia kutoa mikopo mbalimbali katika miradi ya maendeleo kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB). Pia, katika kulipa kipaumbele suala la Afya, Benki hiyo  imeweka mpango wa kusaidia afya ya uzazi kwa akinamama hususan,  katika maeneo ya vijijini.

Miradi mingine inayofadhiliwa na EADB hapa nchini ni pamoja na miradi ya Umeme hasa kwa maeneo ya vijijini, na miradi ya maji na usafi wa mazingira.

Akiongea katika hafla hiyo,  Mhe. Waziri Mahiga aliahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha uendeshaji wa Benki hiyo unafanikiwa. “Karibuni sana na pale inapotokea  mmekwama katika jambo lolote linalohitaji usaidizi wa Serikali au ushauri tupo tayari kutoa ushirikiano” alisema Waziri Mahiga.

Waziri Mahiga azungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mkutano wa AU

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mapema leo mchana kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika uliomalizika hivi karibuni nchini Rwanda. Katika mkutano huo Mhe. Waziri alielezea mambo mbalimbali yaliyojadiliwa katika Mkutano huo ikiwemo suala zima la Haki za Wanawake katika kufanya maamuzi, kupata nafasi za Uongozi na kushirikishwa kwenye utatuzi wa migogoro mbalimbali Barani Afrika. Kaulimbiu ya mkutano huo ilihusu "Haki za binadamu hususan za Wanawake".  Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizarani, Bi. Mindi Kasiga.
Dkt. Mahiga akionyesha kwa waandishi wa habari Hati yake ya Kusafiria (passport) aliyopatiwa wakati wa mkutano wa AU. Hati hiyo imeanzishwa na Umoja wa Afrika kwa lengo la kuimarisha umoja na kurahisisha mawasiliano. Kulia  ni Bi. Kasiga.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri Mahiga kwenye mkutano uliowakutanisha naye.


Picha na Reginald Philip

Tuesday, July 19, 2016

Taasisi ya Aga Khan kuendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya maendeleo

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi (kulia) akizungumza na Mkurugenzi wa masuala ya Kidiplomasia katika Taasisi ya Aga Khan, Balozi Arif Lalani alipotembelea Wizarani kwa ajili ya kujitambulisha na kueleza nia ya Taasisi hiyo ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika miradi ya maendeleo hususan katika sekta ya elimu na afya.
Sehemu ya wageni walioambatana na Balozi Lalani (hayupo pichani). Kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Taasisi ya Aga Khan nchini, Bw. Amin Kurji nao wakisikiliza mazungumzo kati ya Balozi Muombwa na Balozi Lalani (hawapo pichani).
Balozi Lalani naye akizungumza na Balozi Mwinyi  alipotembelea Wizarani.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Bi. Ramla Khamis (kushoto), pamoja na Afisa Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Hellen Mgeta wakifuatilia mazungumzo.
Mazungumzo yakiendelea
Balozi Mwinyi akiagana na  Balozi Lalani na Bw. Kurji  mara baada ya kumaliza mazungumzo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ashiriki maadhimisho miaka 59 ya Aga Khan kuongoza Ismailia

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Dkt. Susan Kolimba (Mb.), akizungumza katika maadhimisho ya Miaka 59  ya Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Shia Ismailia, Mtukufu Aga Khan tangu aliposhika nafasi hiyo.Katika hotuba yake Dkt. Kolimba alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mtukufu Aga khan kwa mafanikio katika kipindi cha uongozi wake na kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo iliyochini ya Taasisi yake. Kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Ismailia hapa nchini, Bw. Amin Kurji.  
Mkurugenzi wa masuala ya kidiplomasia katika Taasisi ya Aga Khan,  Balozi Arif Lalani pamoja na wageni waalikwa waliohudhuria hafla hiyo wakimsikiliza Mhe. Kolimba (hayupo pichani) alipokuwa akiendelea kuzungumza kwenye maadhimisho hayo.
Katibu wa Naibu Waziri, Bw. Adam Isara(Kulia) akifuatilia hotuba ya Mhe. Kolimba pamoja na Afisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Hellen Mgeta. 
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Bi. Ramla Khamis (wa pili kutoka kushoto), akiwa pamoja na Maafisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati wa hafla hiyo.  
Sehemu ya wageni waalikwa waliohudhuria hafla hiyo nao wakimsikiliza Dkt. Kolimba, wa pili kutoka kulia ni Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Masaharu Yoshinda.
Wageni waalikwa . 
Mhe. Dkt. Kolimba na Bw. Kurji wakiwatakia afya njema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mtukufu Aga Khan wakati wa hafla hiyo. 
Dkt. Kolimba akitambulishwa kwa wageni waalikwa na Bw. Kurji
Dkt. Susan Kolimba akipokea maelezo kutoka kwa mtaalam aliyebuni mchoro waa Chuo Kikuu cha  Aga Khan kitakachojengwa Jijini Arusha.


Picha na Reginald Philip

Monday, July 18, 2016

Tanzania yapewa tuzo za ustawi wa jamii na ushirikishaji wa wanawake katika mkutano wa AU

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia Mhe. Naimi Aziz (kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Balozi Samwel Shelukindo mara baada ya kukabidhiwa tuzo za Tanzania. 
Balozi Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akipokeza tuzo za Tanzania kutoka kwa afisa wa Umoja wa Afrika wakati wa Mkutano wa Umoja wa Afrika.


Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Serikali ya Tanzania imepewa tuzo 2 za masuala ya Ustawi wa Jamii pamoja na ushirikishwaji wa wanawake katika ngazi ya maamuzi ya Serikali na Taasisi mbalimbali katika Mkutano wa 27 wa Umoja wa Nchi za Afrika (AU) uliofanyika hivi karibuni Kigali nchini Rwanda.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi, Augustine Mahiga, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo yaliyojadiliwa katika mkutano wa 27 wa Umoja wa nchi za Afrika uliofanyika hivi karibuni Kigali nchini Rwanda.
“Tanzania imetambuliwa na AU kama nchi ambayo kwa miaka 15 sasa imekua na mikakati mbalimbali ya kitaifa ya kuzingatia haki za wanawake na kutimiza malengo ya Milenia,” alisema Balozi Mahiga
Aliongeza kuwa Tanzania ni kati ya nchi tano bora katika bara la Afrika ambazo zimepewa tuzo hizo.
Katika hatua nyingine, Balozi Mahiga amasema kuwa katika mkutano huo wa 27 viongozi wa Afrika walizungumzia mambo mbalimbali ikiwemo hati ya kusafiria Afrika (passport), ambayo itawezesha watu wa bara hilo kusafiri katika nchi zote za Afrika.
Balozi Mahiga aliongeza kuwa, lengo la kuanza kutumia hati hiyo ya kusafiria kwa nchi za Afrika ni kutoa vikwazo vilivyokuwepo wakati wa kutembelea na kusafiri ndani ya nchi hizo.
Aidha, Balozi Maiga amesema kwamba, kutolewa kwa hati ya kusafiria ya Afrika ni ishara ya Umoja na mshikamano, hati hizo zimeanza kutolewa kwa marais na viongozi wa Serikali wa nchi ambazo zilihudhuria mkutano huo. Hati hizo zitatumika kwa kuzingatia sheria za kila nchi.
Hali kadhalika, mkutano huo ulijadili migogoro ya nchi za Burundi na Sudani Kusini ambapo viongozi hao walikubaliana kupeleka Jeshi la Umoja wa Afrika nchini Sudani Kusini ili kutenganisha majeshi ya pande mbili zinazoendelea kupigana nchini humo.
Aidha, mgogoro wa Burundi bado unaendelea kupatiwa ufumbuzi kutokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye aliteuliwa na mapema mwaka huu na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkutano wa 27 wa Umoja wa nchi za Afrika wenye wanachama 54 ulifanyika Kigali nchini Rwanda tarehe 18 mwezi huu, ukiwa ni mkutano wa pili kwa mwaka huu ulikua na kauli mbiu inayosema mwaka wa haki za binadamu.

Sunday, July 17, 2016

NEPAD yahimiza Viwanda Barani Afrika

Kikao cha NEPAD kikiendelea
Dkt. Ibrahim Mayaki, Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Maendeleo Afrika 


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

NEPAD yahimiza uanzishwaji wa Viwanda ili kukwamua uchumi wa Bara la Afrika
KIGALI, Rwanda

Afrika inahitaji juhudi za pamoja ili kukuza sekta ya viwanda ambayo itasaidia kwa kiasi kubwa kunyanyua uchumi wa bara la Afrika na hatimaye kupunguza umaskini na kuleta maisha bora.

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa NEPAD, chombo cha utendaji cha Umoja wa Afrika, Dkt. Ibrahim Mayaki wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Umoja wa Afrika zilizopo kwenye mpango huo wa maendeleo barani Afrika.

Kwenye upande wa ajira na viwanda kwa mfano, Dkt. Miyaki alisema kuwa bara la Afrika kwa sasa ndilo lenye vijana wengi kuzidi mabara mengine duniani hivyo kuna nguvu kazi kubwa ambayo isipotafutiwa mpango mahsusi wa ajira kutazidisha umasikini barani humo. Viwanda vya Afrika vikiongezeka, ajira kwa vijana zitapatikana, uzalishaji utaongezeka na biashara ndani ya Afrika itashamiri.

“Changamoto kubwa barani Afrika ni biashara, ambapo nchi haziuziani bidhaa zake, miundombinu hafifu na umasikini uliokihiri” alisema na kuongeza kuwa wakati muafaka umefika kwa Afrika kuweka mikakati endelevu ya pamoja baina ya nchi za Kiafrika ili kuhakikisha changamoto hizi zinatafutiwa ufumbuzi.

Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa Mpango wa Maendeleo Afrika (NEPAD) uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Umoja wa Afrika Jijini Kigali Rwanda, wajumbe walielezwa kuwa biashara ina nafasi kubwa ya kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda barani Afrika iwapo misingi imara ya kuendeleza biashara na viwanda itazingatiwa.

Akizungumzia hali halisi nchini Tanzania, Mhe. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye alimwakilisha Mhe. Rais Magufuli kwenye mkutano huo, alisema “NEPAD pia wametambua kwamba biashara ya ndani barani Afrika inaendelea kuwa na jukumu kubwa katika ukuaji wa uchumi na viwanda vya nchi zetu za Kiafrika”.

Hivi karibuni Waziri Mahia alitangaza Bungeni kuwa Wizara yake sasa inaweka mikakati madhubuti kwa ajili ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje yenye muelekeo wa uchumi wa viwanda (Economic Diplomacy of Industrialization) ambao utazingatia dhamira ya Serikali ya Tanzania kunyanyua sekta ya viwanda.

“Nimewaelekeza wasaidizi wangu wamualike maalamu wa Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa ili aje kutuelezea umuhimu wa agenda hii ya biashara na uchumi wa viwanda nchini kwetu” alisema Waziri Mahiga.

Alimalizia kuwa “ili utekelezaji wa mkakati wa Diplomasia ya Uchumi wa Viwanda ufanikiwe, ni muhimu Serikali nzima na nchi kwa ujumla kuwa thabiti kwenye kutekeleza sera za viwanda na za uchumi na kuzingatia misingi ya kufanya biashara iliyoelezwa hapa na wataalamu”.

Akielezea umuhimu wa Afrika kukuza viwanda kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa Dkt. Carlos Lopez alisema kuwa japokuwa Afrika imechelewa kufanya mapiduzi ya viwanda ikilinganishwa na yale ya Ulaya miaka 200 iliyopita, bado Afrika ina nafasi kubwa ya kunyanyua uchumi wake kupitia viwanda na biashara ya ndani baina ya nchi zake.

Kilele cha Mkutano wa 27 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unatarajiwa kufunguliwa tarehe 17-18 Julai ambapo Wakuu hao wanatarajiwa  kupitisha ajenda kadhaa ikiwemo uchaguzi wa Kamishna na Kauli Mbiu ya mwaka huu ambayo ni Haki za Binadamu, Haki za Wanawake.   

Mwisho.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki


 17 Julai 2016.

Friday, July 15, 2016

Kikao cha 39 cha Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika pichani

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) mwenye miwani mbele, akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Idaya Afrika Balozi Samweli Shelukindo katika Mkutano wa 29 wa Umoja wa Afrika, Mkutano huo umewakutanisha Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi 54 Mkutano huo umefanyika nchini Rwanda. 
Waziri Mahiga akifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea, nyuma kulia ni Balozi Shelukindo na  Balozi Naimi Azizi nao wakiwa katika kikao hicho.

Sehemu ya Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika 

Kikao cha 39 cha Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika



Waziri Mahiga ahudhuria Kikao cha 29 cha Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika

KIGALI, Rwanda

Kikao cha 29 cha Baraza la Mawaziri wa Nchi 54 zinazounda Umoja wa Afrika kimekamilika Jijini Rwanda leo huku mawaziri hao wa mambo ya nje wakisisitiza amani na usalama na utekelezaji wa haraka wa maamuzi yenye lengo la kuleta maendeleo ya kiuchumi na kunyanyua maisha ya wananchi barani Afrika.

Akifugua kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Mhe. Dkt. Nkosozana Dlamini Zuma amesema kuna umuhimu wa kuhakikisha Afrika iko salama na ina amani baina yake na wananchi wake,  ili kufikia malengo ya kijikwamua kiuchumi barani Afrika. Aliwaasa Mawaziri hao kusimamia kikamilifu na kuharakisha utekelezaji wa maazimio mbalimbali yanayowekwa na chombo hicho muhimu kwa Afrika ili kuharakisha maendeleo ya Afrika.

Alielezea umuhimu wa kuharakisha utatuzi wa migogoro sugu barani Afrika ambayo sio tu inahatarisha usalama wa raia wa maeneo hayo, lakini pia husababisha raia hao kupoteza makazi yao ya kudumu na kukimbilia nchi nyingine, tatizo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya bara la Afrika.

Alikemea mgogoro unaoendelea Sudani Kusini na kukumbusha Mawaziri hao ahadi ya Umoja wa Afrika iliyowekwa na nchi wanachama wakati wakiadhimisha miaka 50 ya umoja huo ya kunyamazisha bunduki ifikapo mwaka 2020.

“Waheshimiwa Mawaziri, unawajibu wa kuweka dhamira ya dhati ili ku timiza ahadi hiyo kwa Waafrika na kwa vizazi vijavyo barani mwetu“ alisema. gt5“

Dkt. Zuma akiwa na mwenyeji wa Kikao hicho cha mawaziri, Mhe. Louise Mushekiwabo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda kwa pamoja walihimiza suala la ulinzi na usalama barani Afrika lina umuhimu wa kipekee na ndio maana kauli mbiu ya Mkutano Mkuu wa 27 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika nchini Rwanda imejijkia kwenye haki za binadamu hususan haki za wanawake.

“Tutumie kauli mbiu hii kama chachu ya kukataa kabisa migogoro barani kwetu, na pale inapoanza tuwahi kuitafutia ufumbuzi kabla haijaeuka kuwa vita“ alisema Kamishna Zuma kwa kumalizia.

Akitoa maoni yake kuhusu msisitizo wa amani na usalama kwenye kikao hicho cha siku mbili, Mhe. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki  alielezea kuwa Serikali ya Tanzania inafuatilia kwa karibu amri ya kusitisha mapigano iliyotolewa na viongozi wakuu wawili wa Sudani ya Kusini, yaani Rais Salva Kiir na makamu wake. Alisema ni hatua muhimu ya kuhakikisha usalama wa raia na kuleta amani ya kudumu nchini humo.

Kikao cha Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika kilitanguliwa na Kikao cha Mabalozi wanaowakilisha nchi zao kwenye makao makuu ya UA nchini Ethiopia. Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali unatarajiwa kuanza tarehe 17-18 Julai, ambapo Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais atamwakilisha Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Maufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki

 15 Julai 2016.

Tuesday, July 12, 2016

Balozi wa Tanzania nchini Kuwait akutana na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa nchi hiyo

Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhe. Dkt. Mahdhi Juma Maalim akiwa katika picha ya pamoja na Bw. Abdulwahab Al-Bader, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait-Kuwait Fund for Arab Economic Development (KFAED). Mhe. Dkt. Maalim alikutana na kufanya mazungumzo na Bw. Al-Bader ambapo walijadili masuala muhimu katika kuharakisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maedneleo ambayo inasubiri ufadhili wa mfuko huo. Aidha, Balozi Maalim alisifu mchango mkubwa wa KFAED katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania na kumwahidi  Mkurugenzi huyo kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika juhudi za kuimarisha zaidi mahusiano kati ya Tanzania na Kuwait hususan KFAED.
Balozi Dkt. Maalim akiwa na Mkurugenzi Mkuu, Bw. Al-Bader pamoja na baadhi ya Maafisa wa KFAED.

Waziri Mahiga apokea msaada wa madawati 105 kutoka Jumuiya ya Mabohora nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza zoezi la makabidhiano ya madawati kutoka Jumuiya ya Mabohora iliyopo hapa nchini, jumuiya hiyo imechangia jumla ya madawati 105 yenye thamani ya shilingi milioni kumi. Hii ni katika kuiunga  mkono Serikali kwenye zoezi la kuchangia madawati nchi nzima lililo tangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Madawati hayo yametengenezwa hapa nchini na Kampuni ya Jambo. Tukio hilo lilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere uliopo jijini Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabohora, Mhe. Shehe Zainuddin Adamjee naye akizungumza na waandishi wa habari kwenye makabidhiano ya madawati.
Sehemu ya Waandishi wa Habari wakisikiliza kwa makini Waziri Mahiga (hayupo pichani)
Sehemu ya wawakilishi wa Jumuiya hiyo wakimsikiliza kwa makini Mhe. Waziri Mahiga
Waziri Mahiga akiwaonyesha waandishi wa habari moja ya dawati kati ya yaliyotolewa na Jumuiya ya Mabohora. Wizara itakabidhi madawati hayo kwa Mamlaka husika  kwa ajili ya kusambazwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akiwa na Viongozi Wakuu wa Jumuiya ya Mabohora nchini, Mhe. Shekh Tayabali Hamzabhai ( (kushoto) na Shekh Zainuddin Adamjee, Makamu Mwenyekiti (kulia) wakati wa hafla fupi ya kukabidhi madawati.