Sunday, July 17, 2016

NEPAD yahimiza Viwanda Barani Afrika

Kikao cha NEPAD kikiendelea
Dkt. Ibrahim Mayaki, Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Maendeleo Afrika 


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

NEPAD yahimiza uanzishwaji wa Viwanda ili kukwamua uchumi wa Bara la Afrika
KIGALI, Rwanda

Afrika inahitaji juhudi za pamoja ili kukuza sekta ya viwanda ambayo itasaidia kwa kiasi kubwa kunyanyua uchumi wa bara la Afrika na hatimaye kupunguza umaskini na kuleta maisha bora.

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa NEPAD, chombo cha utendaji cha Umoja wa Afrika, Dkt. Ibrahim Mayaki wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Umoja wa Afrika zilizopo kwenye mpango huo wa maendeleo barani Afrika.

Kwenye upande wa ajira na viwanda kwa mfano, Dkt. Miyaki alisema kuwa bara la Afrika kwa sasa ndilo lenye vijana wengi kuzidi mabara mengine duniani hivyo kuna nguvu kazi kubwa ambayo isipotafutiwa mpango mahsusi wa ajira kutazidisha umasikini barani humo. Viwanda vya Afrika vikiongezeka, ajira kwa vijana zitapatikana, uzalishaji utaongezeka na biashara ndani ya Afrika itashamiri.

“Changamoto kubwa barani Afrika ni biashara, ambapo nchi haziuziani bidhaa zake, miundombinu hafifu na umasikini uliokihiri” alisema na kuongeza kuwa wakati muafaka umefika kwa Afrika kuweka mikakati endelevu ya pamoja baina ya nchi za Kiafrika ili kuhakikisha changamoto hizi zinatafutiwa ufumbuzi.

Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa Mpango wa Maendeleo Afrika (NEPAD) uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Umoja wa Afrika Jijini Kigali Rwanda, wajumbe walielezwa kuwa biashara ina nafasi kubwa ya kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda barani Afrika iwapo misingi imara ya kuendeleza biashara na viwanda itazingatiwa.

Akizungumzia hali halisi nchini Tanzania, Mhe. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye alimwakilisha Mhe. Rais Magufuli kwenye mkutano huo, alisema “NEPAD pia wametambua kwamba biashara ya ndani barani Afrika inaendelea kuwa na jukumu kubwa katika ukuaji wa uchumi na viwanda vya nchi zetu za Kiafrika”.

Hivi karibuni Waziri Mahia alitangaza Bungeni kuwa Wizara yake sasa inaweka mikakati madhubuti kwa ajili ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje yenye muelekeo wa uchumi wa viwanda (Economic Diplomacy of Industrialization) ambao utazingatia dhamira ya Serikali ya Tanzania kunyanyua sekta ya viwanda.

“Nimewaelekeza wasaidizi wangu wamualike maalamu wa Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa ili aje kutuelezea umuhimu wa agenda hii ya biashara na uchumi wa viwanda nchini kwetu” alisema Waziri Mahiga.

Alimalizia kuwa “ili utekelezaji wa mkakati wa Diplomasia ya Uchumi wa Viwanda ufanikiwe, ni muhimu Serikali nzima na nchi kwa ujumla kuwa thabiti kwenye kutekeleza sera za viwanda na za uchumi na kuzingatia misingi ya kufanya biashara iliyoelezwa hapa na wataalamu”.

Akielezea umuhimu wa Afrika kukuza viwanda kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa Dkt. Carlos Lopez alisema kuwa japokuwa Afrika imechelewa kufanya mapiduzi ya viwanda ikilinganishwa na yale ya Ulaya miaka 200 iliyopita, bado Afrika ina nafasi kubwa ya kunyanyua uchumi wake kupitia viwanda na biashara ya ndani baina ya nchi zake.

Kilele cha Mkutano wa 27 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unatarajiwa kufunguliwa tarehe 17-18 Julai ambapo Wakuu hao wanatarajiwa  kupitisha ajenda kadhaa ikiwemo uchaguzi wa Kamishna na Kauli Mbiu ya mwaka huu ambayo ni Haki za Binadamu, Haki za Wanawake.   

Mwisho.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki


 17 Julai 2016.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.