Tuesday, July 5, 2016

Prof. Mbarawa afungua Semina kuhusu Maendeleo ya Viwanda

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb.) akihutubia kwenye ufunguzi wa Semina ya Kimataifa kati ya China na Afrika kuhusu ushirikiano wa kuendeleza viwanda inayofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Julai 5, 2016.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt Susan Kolimba (Mb.) akitoa hotuba kwenye ufunguzi wa semina ya Kimataifa kati ya China na Afrika kuhusu ushirikiano wa kuendeleza viwanda inayofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Lu Youqing  naye akihutubia kwenye ufunguzi wa Semina hiyo
Baadhi ya Wadau walioshiriki katika Semina ya Kimataifa kati ya China na Afrika kuhusu ushirikiano wa kuendeleza viwanda  iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam wakifuatilia jambo. Mstari wa mbele kutoka kulia ni Prof. Ibrahim Lipumba, Prof. Moshi na Dkt. Reginald Mengi
Baadhi ya Wakuu wa Idara/Vitengo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia semina hiyo. Kutoka kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu, Bw. Paul Kabale; Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, Bw. Lucas Suka; Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Balozi Baraka Luvanda; na Mkurugenzi Idara ya Diaspora, Balozi Anisa Mbega.
Sehemu nyingine ya Wakuu wa Idara/Vitengo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Wa pili kutoka kulia ni mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki, na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu, Bw. Nigel Msangi nao wakisikiliza kwa makini hotuba zilizokuwa zikiendelea kutolewa kwenye Semina hiyo
Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Usimamizi wa Raslimali watu, Bw. Hamid Mbegu; Mkurugenzi wa Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Kijamii, Bw. Eliab Chodota na Mkuu wa Kitengo cha Teknologia ya Mawasiliano, Bibi. Achentalika Maunda wakifuatilia jambo wakati wa Semina.
Katibu wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (tai nyekundu), Bw. Adam Isara naye akisikiliza hotuba za ufunguzi katika semina hiyo
Sehemu ya Washiriki wa Semina ya Kimataifa kati ya China na Afrika kuhusu ushirikiano wa kuendeleza viwanda iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam wakifuatilia Jambo.
Sehemu ya Waandishi wa Habari walio hudhuria ufunguzi wa Semina ya Kimataifa kati ya China na Afrika kuhusu ushirikiano wa kuendeleza viwanda wakitekeleza majukumu yao
Mhe. Kolimba na akijadiliana jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima wakati wa Ufunguzi wa Semina ya Kimataifa kati ya China na Afrika kuhusu ushirikiano wa kuendeleza viwanda
Naibu Waziri, Mhe. Suzan Kolimba akizungumza na Chombo cha Habari cha Kimataifa cha CCTV na kuelezea Faida na Madhumuni ya Semina hiyo
Picha ya pamoja mara baada ya kumaliza Ufunguzi wa Semina






TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Semina kuhusu Maendeleo ya Viwanda

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) amesema kuwa bila ya ujenzi wa miundombinu ya uhakika, Tanzania haitaweza kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025.

Alitoa kauli hiyo leo, wakati wa semina ya maendeleo ya viwanda iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ubalozi wa China na kufanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mhe. Waziri alisema kuwa ili miundombinu imara iweze kujengwa nchini, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi trilioni 11.8 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo na kati ya hizo asilimia 46 ni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. “Asilimia 46 ya bajeti ya maendeleo ni kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa miradi ya miundombinu mbalimbali kama barabara, reli ya kiwango cha kimataifa, ununuzi wa ndege na meli”.  

Prof. Mbarawa aliyashukuru makampuni ya China kwa kuwekeza nchini katika miradi mbalimbali mikubwa lakini bado alitoa wito kwa makampuni mengine kutoka nchi hiyo kuja  kuwekeza kwa wingi hapa nchini.

Aliyashauri makampuni kutoka nchini China yaje kuingia ubia na makampuni ya hapa nyumbani katika uendelezaji wa miradi mbalimbali kama ya reli barabara na nishati. Aliendelea kueleza kuwa ili kuendeleza sekta ya viwanda nchini, tunahitaji msaada wa mtaji, utaalamu na elimu ya ufundi kutoka kwa marafiki zetu kama nchi ya China.

Aidha, Prof. Mbarawa alisisitiza umuhimu wa kuboresha kiwango cha uzalishaji katika sekta ya kilimo ambayo ndio imeajiri Watanzania wengi hapa nchini. “Sekta ya kilimo imekuwa ikikua kwa asilimia 4 hadi 5 hapa nchini lakini ukuaji huo haujajikita hasa katika kiwango cha uzalishaji (productivity)”. Prof. Mabarawa alisema ili watu wetu waweze kufaidika na kilimo lazima kiwango cha uzalishaji kiboreshwe na  Serikali ya awamu ya tano imejipanga kulifanyia kazi suala hilo.

Mhe. Waziri alihitimisha hotuba yake kwa kuahidi kuwa Serikali itazingatia utunzaji wa mazingira itakapokuwa inatekeleza ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo iliyomo kwenye Mwaka wa Fedha 2016/2017 na miaka mingine itakayofuata.

Akizungumza awali, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba (Mb) aliishukuru Serikali ya Watu wa China kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo. Alirejea dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kushirikiana na China hususan katika Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika (FOCAC). Alisema Tanzania kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi 4 ambazo China itahamishia viwanda vyake ni ushahidi wa wazi kuwa nchi hizi mbili zina uhusiano mzuri wa kihistoria.

Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Dkt. Lu Youqing alisisitiza umuhimu wa kukuza sekta ya viwanda hapa nchini. Alisema sekta ya viwanda ikikua, itapelekea kufikiwa kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, itaongeza ajira, mapato ya Serikali na hivyo kuifanya nchi kujitegemea kifedha. Alimalizia kwa kuihakikishia Tanzania kuwa nchi yake itatimiza yale yote iliyoyaahidi kwenye Mkutano wa FOCAC uliofanyika Afrika Kusini mwaka 2015.
 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.