Mkutano wa
siku mbili wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
(SADC) umefunguliwa rasmi katika Hoteli ya Safari mjini Windhoek, Namibia
tarehe 13 Agosti 2018.
Ujumbe wa
Tanzania katika mkutano huu unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga ambaye ameambatana na
viongozi waandamizi wa Serikali ya Tanzania ambao ni pamoja na Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda;
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (anayesimamia masuala ya
Ujenzi) Mhandisi Joseph Myamhanga, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt.
Evaristo Longopa; Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu
Kazungu na Naibu Katibu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Edwin
Paul Mhede.
Mkutano huu
ni sehemu ya mikutano ya awali ya maandalizi ya mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi
na Serikali wa SADC utakaofanyika tarehe 17 na 18 Agosti 2018 mjini
Windhoek, Namibia. Mikutano mingine ya awali ni mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC
uliofanyika tarehe 9 na 11 Agosti 2018 na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali
wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa , Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on
Politics, Defence and Security) utakaofanyika tarehe 16 Agosti 2018 ambao
utapitia na kujadili hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Kanda kwa kipindi
cha Agosti 2017 hadi Agosti 2018.
Mkutano wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na
Usalama utahusisha nchi tatu za SADC Organ TROIKA na wajumbe
wake ambao ni Angola (Mwenyekiti wa sasa wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa
Siasa, Ulinzi na Usalama), Zambia (Makamu
Mwenyekiti wa Organ) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mwenyekiti wa Organ
aliyemaliza muda wa uenyekiti wa Asasi).
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utapokea, kujadili na kutolea
maamuzi ya mapendekezo mbalimbali yanayotokana na mikutano ya kisekta na kamati
za jumuiya kwa kipindi cha mwaka 2017/18. Pamoja
na mambo mengine mkutano huu;
Utafanya uteuzi wa Mwenyekiti wa SADC na inatarajiwa kuwa Jamhuri
ya Namibia ambayo ni Makamu Mwenyekiti wa sasa itateuliwa kuwa
Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha 2018/2019. Nafasi ya Makamu mwenyekiti
itajazwa pia na nchi itakayoteuliwa ambayo itajulikana tarehe 17Agosti 2018.
Uteuzi wa Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama
ya SADC. Inatarajiwa kuwa Jamhuri ya Zambia, ambayo ni Makamu Mwenyekiti wa
sasa itateuliwa kuwa Mwenyekiti kwa kipindi cha 2018/2019. Hivi sasa
Tanzania ni Mwenyekiti anayemaliza muda wake kwenye Asasi
ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on
Politics, Defence and Security).
Mambo
mengine yanayotarajiwa kujitokeza na kujadiliwa katika mkutano huu ni pamoja na; masuala ya fedha;
Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Viwanda wa SADC
(Report on the operationazaition) na Maendeleo ya Viwanda;
Kutia saini itifaki
mbalimbali ikiwa ni pamoja na itifaki ya Kulinda
Hakimiliki ya Wagunduzi wa aina Mpya za Mbegu za Mimea ya mwaka 2017. Pia Mkutano huu utatoka na tamko la nchi wanachama wa SADC la kutokomeza
malaria katika ukanda wa SADC ifikapo mwaka 2030.
==========================================================
Mwenyekiti mpya wa Mawaziri wa SADC, Mhe. Nandi-Ndaitwa akihutubia mara baada ya kupokea nafasi hiyo. Katika hotuba yake alisistiza umuhimu wa kuwawezesha vijina kwa kuwa ndio nguzo kuu katika kuinua uchumi wa taifa lolote duniani sambamba na uwekezaji katika viwanda. Pamoja na hayo akaeleza malengo makuu ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni kuondoa umasikini na kuinua uchumi ndani ya kanda. |
Wa kwanza kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Namibia mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini, Mhe. Sylivester Ambokile na wajumbe wengine wa Serikali ya Tanzania wakifuatilia ufunguzi wa mkutano. |
Sehemu nyingine ya wajumbe kutoka Serikali ya Tanzania wakifuatilia mkutano. |
Balozi wa Namibia nchini Tanzania pamoja na wajumbe wengine wa mkutano huo wakifuatilia hafla ya ufunguzi. |