TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA KUHUSU KONGAMANO LA TANO LA
DIASPORA
Watanzania waishio ughaibuni wamekutana Chake Chake, kisiwani Pemba
tarehe 18 na 19 Agosti, 2018 katika Kongamano la Tano la Diaspora
kufuatia utaratibu uliowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwakutanisha
kila mwaka Watanzania waishio ughaibuni.
Kongamano hilo ambalo liliandaliwa na Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi chini ya Idara ya Ushirikano wa Kimataifa na uratibu wa masuala ya
Diaspora pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki liliwakutanisha Wanadiaspora zaidi ya 300 katika viwanja vya
Tibirinzi, Pemba. Wadau mbalimbali wa hapa nchini kutoka Serikalini na
Sekta binafsi walihudhuria Kongamano hilo.
Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi alikuwa mgeni rasmi akiambatana na viongozi wengine
waliohudhuria kongamano hilo akiwemo; Balozi Seif Ali Idd, Makamo wa Pili
wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Mhe. Haji Issa Ussi Gavu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Mawaziri, Makatibu na Naibu Makatibu Wakuu, Mabalozi na Watendaji
wa Serikali zote za Muungano.
Katika kongamano hilo Wanadiaspora hao walipata fursa ya kufuatilia mada mbalimbali
zilizowasilishwa ikiwa ni pamoja na Diaspora na Maendeleo; Uraia; Sheria
za Uhamiaji na kufahamishwa fursa zilizopo nchini kwa ajili ya uwekezaji kwa
manufaa Wanadiaspora na Taifa kwa ujumla. Aidha, Watanzania hao waishio
ughaibuni walipata fursa ya kuuliza maswali pamoja na kutoa ushauri kwa
Serikali kuhusu masuala mbalimbali yenye lengo la kuendeleza umoja huo na
maendeleo ya nchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwahakikishia
Watanzania hao kuwa Serikali zao zinatambua umuhimu wa Watanzania waishio
ughaibuni na hivyo itaendelea kuwashirikisha katika masuala mbalimbali ya
maendeleo ya nchi. Vilevile, Mheshimiwa Rais Shein aliwahimiza Wanadiaspora hao
kuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu na aliwasihi wazidi kuitangaza na kuwekeza
nchini kwa wingi.
Nae mwakilishi wa Watanzania waishio ughaibuni Bw. Adolf Makaya,
Katibu wa Baraza la Dunia la Diaspora (TGDC), kwa niaba ya wanadiaspora hao,
aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuwathamini na kutambua umuhimu wao katika
kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi.
Sambamba na hayo, Wanadiaspora walipata fursa ya kujionea vivutio
mbalimbali vilivyopo kisiwani Pemba ikiwa ni pamoja na kutembelea hoteli ya
kitalii ya Manta Resort iliyopo Makangale kisiwani Pemba. Hoteli hiyo imekuwa
gumzo na kivutio kikubwa cha utalii kutokana na kuwa na chumba kilicho chini ya
bahari.
Kwa upande wake, Balozi Seif Ali Idd, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
alifurahishwa na mahudhurio mazuri ya Wamadiaspora na kuona kuwa ni fursa kubwa
kwao kuona maendeleo ya nchi yao na pia kujenga maelewano mazuri na Serikali.
Kwa ujumla, kongamano hilo limefanyika kwa mafanikio makubwa ambapo viongozi wa
Serikali pamoja na wanadiaspora hao waliweza kupata fursa ya kujadiliana namna
mbalimbali za kuwashirikisha Wanadiaspora hao katika maendeleo yao na ya Taifa
kwa ujumla.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
19 Agosti 2018