Wednesday, November 7, 2018

Tangazo kwa Umma


TANGAZO KWA UMMA

TAARIFA KUHUSU UTHIBITISHAJI WA NYARAKA

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kuukumbusha Umma kwamba wale wote wanaohitaji kupata huduma ya kuthibitisha vyeti na nyaraka mbalimbali wanatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:

(1)  Huduma hizo zinatolewa katika Ofisi za Wizara Mjini DODOMA jengo la LAPF, Barabara ya Makole Ghorofa la 6.

(2) Malipo ya nyaraka zitakazothibitishwa yatalipwa kwa njia ya benki, akaunti namba 0150275408200 Foreign Collection Account, CRDB Bank kwa kiasi cha Shilingi Elfu Kumi na Tano tu kwa kila nyaraka (@TSHS 15,000/=). Hati ya malipo ya benki iwasilishwe Wizarani ili kuthibitisha malipo hayo.

(3) Mteja mwenye nyaraka yeyote inayohusu masuala ya talaka, ndoa, hali ya ndoa, tangazo la kuzaliwa, cheti cha kuzaliwa, Cheti cha Kifo, cheti cha ndoa anatakiwa kuanzia ofisi za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Registration, Insolvency, Trusteeship Agency- RITA) Dar es Salaam.

(4) Vyeti vyote vinavyoletwa Wizarani kwa ajili ya kuthibitishwa, havina budi kupelekwa kwanza katika Taasisi za Tanzania zilizotoa vyeti/nyaraka hizo ili vihakikiwe na kuthibitishwa. Aidha, kwa vyeti au nyaraka zilizotolewa na mamlaka za nchi za nje zinatakiwa kupelekwa kwenye Balozi wa nchi amabayo vyeti hivyo vilitolewa kwa ajili ya uhakiki.

(5) Mteja anayeleta nyaraka za ajira (Mkataba wa ajira) anatakiwa kuanzia ofisi za Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (Tanzania Employment Services Agency –TAESA)

(6)Mteja anayeleta nyaraka iliyo katika lugha tofauti na kingereza anatakiwa kufanya Tafisri ya nyaraka hiyo na kuiambatisha na nyaraka halisi iliyofanyiwa tafsiri. Aidha, tafsiri ya nyaraka ifanywe na BAKITA, BAKWATA na taasisi zilizosajiliwa na kutambulika na Serikali.

(7) Kwa yeyote mwenye Power of Attorney na Deed Poll ahakikishe imesajiliwa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kabla ya kuiwasilisha Wizarani.

(8)Nakala ya nyaraka yeyote inayotakiwa kufanyiwa uhakiki imbatane na nakala halisi ya nyaraka hiyo.

(9)Mteja anatakiwa kuandika barua kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiomba nyaraka hizo zithibitishwe na kueleza matumizi tarajiwa ya nyaraka hizo nje ya nchi. Aidha, Barua ya Katibu Mkuu iambatishwe na nakala (copies) za nyaraka zilizothibitishwa na taasisi husika ambazo zinahitaji kuthibitishwa na Wizara.


WATEJA WOTE WANAOMBWA KUZINGATIA RAI KWAMBA HUDUMA HIZI ZITAKUWA ZINATOLEWA SIKU YA JUMANNE NA ALHAMISI TU, KUANZIA SAA 3.00 ASUBUHI HADI SAA 6:00 MCHANA.

Imetolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Tanzania na New Zealand kuimarisha sekta ya ufugaji

Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Hamisi Ulega (kulia) amekutana na kufanya mazungumzl na Balozi wa New Zealand nchini, Mhe. Mike Burrell alipomtembelea ofisini kwake jana. Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walijadili namna Tanzania na New Zealand zitakavyoweza kushirikiana zaidi katika kuboresha sekta ya mifugo na uvuvi nchini.
Mhe. Mike Burrell akisisitiza jambo katika mazungumzo hayo. Mwingine katika picha ni Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Bertha Makilagi
Mhe.Abdallah Hamisi Ulega akiagana na Mgeni wake, Mhe. Mike Burrell

Naibu Balozi wa Israel nchini Mhe. David Eyal atembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiongea jambo na Naibu Balozi wa Israel nchini mwenye  makazi yake jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Eyal David alipotembelea Taasisi hiyo jana  (5/11/2018) kwa ajili ya  kuona kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child Heart - SACH) la nchini Israel kwa kushirikiana na JKCI. Jumla ya watoto 85 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi, upasuaji wa moyo wa kufungua na bila kufungua kifua. 

 Mhe. David akiongozana na mkuu wa kitengo cha ufundi na matengeneza cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mhandisi Abella Rwiguza akielekea  kuangalia ukarabati wa  jengo jipya la watoto la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati  alipotembelea Taasisi hiyo jana  (5/11/2018)  kwa ajili ya  kuona kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child Heart - SACH) la nchini Israel kwa kushirikiana na JKCI.

Mhe. David akiangalia kipimo kinachoonyesha jinsi moyo  unavyofanya kazi (ECHO Cardiogram) alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jana  kwa ajili ya  kuangalia  kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto(Save a Child Heart - SACH) la nchini Israel kwa kushirikiana na JKCI.

Mhe. David akiongea na wazazi wa watoto wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipotembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya  kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child Heart - SACH) la nchini Israel kwa kushirikiana na JKCI. Jumla ya watoto 85 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi, upasuaji wa moyo wa kufungua na bila kufungua kifua.

Mhe. David akisalimiana na Mkuu wa kitengo cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU) ambaye ni daktari bingwa wa wagonjwa mahututi Vivienne Mlawi alipotembelea  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jana    kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya  kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child Heart - SACH) la nchini Israel kwa kushirikiana na JKCI. Jumla ya watoto 85 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi, upasuaji wa moyo wa kufungua na bila kufungua kifua.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi na Naibu Balozi wa Israel nchini mwenye  makazi yake jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Eyal David pamoja na wafanyakazi wengine na JKCI na Israel wakimuombea Daktari bingwa wa usingizi kwa watoto na wagonjwa mahututi Marehemu Onesmo Mhewa aliyefariki mwanzoni mwa  mwezi wa tano mwaka huu. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Balozi wa Israel nchini mwenye  makazi yake jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Eyal David pamoja na wafanyakazi wengine wa JKCI na Israel mara baada ya kumalizika kwa ziara yake ya kutembelea  Taasisi hiyo  jana kwa ajili ya kuangalia  kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa na Shirika la Okoa moyo wa mtoto Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child Heart - SACH) la nchini Israel kwa kushirikiana na JKC. 

Mkuu wa kitengo cha ufundi na matengeneza cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mhandisi Abella Rwiguza akimweleza  Naibu Balozi wa Israel nchini mwenye  makazi yake jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Eyal David jinsi ukarabati wa jengo la watoto unavyoendelea. Mhe. David alitembelea Taasisi hiyo jana  kwa ajili ya  kuangalia kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child Heart - SACH) la nchini Israel kwa kushirikiana na JKCI. 

Tuesday, November 6, 2018

TAARIFA YA UFUNGUZI WA KONGAMANO LA BIASHARA NA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA MISRI,




TAARIFA YA UFUNGUZI WA KONGAMANO LA BIASHARA NA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA MISRI, 
Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Misri limefunguliwa leo katika hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam. Kongamano hilo limeandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Misri hapa nchini chini ya uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wafanyabiashara na wawekezaji wapatao 35 kutoka Misri wameshiriki kwenye Kongamano hilo kwa lengo la kutafuta  fursa katika sekta za kilimo, mifugo, viwanda, madini na ujenzi.

Mgeni rasmi katika Kongamano hilo alikuwa ni Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Mahiga aliwakaribisha wafanyabiashara hao kuja kuwekeza nchini Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo kilimo, madini na utalii. Aidha, Waziri Mahiga alisifia mahusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Misri na juhudi za Serikali ya Tanzania kuendelea kuboresha mazingira ya biashara hapa nchini ili kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji.

Kongamano hilo linafanyika leo na kesho na linaenda sambamba na mikutano ya ana kwa ana (B2B) kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Misri kwa lengo la kuangalia fursa mbalimbali zitakazowezesha kuanzishwa kwa ushirikiano katika Nyanja za biashara na uwekezaji. Aidha kesho kuna mikutano kati ya taasisi za serikali na wafanyabiashara hao (B2G). Taasisi zinazotarajiwa kutoa mada ni TIC, Tanzania Food and Drug Authority (TFDA) na Tanzania Bureau of Standard (TBS).

Ujumbe huo wa wafanyabiashara utaelekea Zanzibar tarehe 08 Novemba 2018 kwa ajili ya kushiriki kwenye Kongamano katika hoteli ya Hyatt Park, Zanzibar tarehe 09 Novemba, 2018

Sunday, November 4, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inapenda kuwajulisha wananchi na jumuiya ya kimataifa kupitia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi kuhusu masuala ya ushoga yaliyoongelewa na Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam hivi karibuni.

Katika mkutano wake na vyombo vya habari, Mhe. Mkuu wa Mkoa alitangaza kampeni ya kukabiliana na vitendo vya ushoga katika jiji la Dar es Salaam.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ingependa kufafanua kwamba, hayo ni mawazo yake na sio msimamo wa Serikali.

Aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ingependa kutumia nafasi hii kukumbusha na kusisitiza kwamba, itaendelea kuheshimu mikataba yote ya kimataifa inayohusu haki za binadamu ambayo imesaini na kuridhia.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea na itaendelea kuheshimu na kulinda haki hizo kama zilivyo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Imetolewa na:

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dodoma.

 04 Novemba, 2018

Friday, November 2, 2018

Dkt. Ndumbaro ashiriki Mkutano wa nchi za mwambao wa Bahari ya Hindi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akiwa kwenye Mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya nchi za mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) unaofanyika Durban, Afrika Kusini  kuanzia tarehe 2 Novemba,  2018. Mhe. Dkt. Ndumbaro anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo ambao pamoja na mambo mengine nchi hizo zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika kutekeleza miradi ya maendeleo iliyo chini ya maeneo tisa vipaumbele kwa IORA ambayo ni usalama na ulinzi wa bahari; biashara na uwekezaji; usafiri wa bahari; uvuvi; menejimenti ya udhibiti wa majanga; taaluma, sayansi na teknolojia; utalii na utamaduni; uchumi bahari; na uwezeshaji wanawake. Mwingine katika picha ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan M. Mwinyi
Mkutano ukiendelea
Picha ya pamoja ya Mawaziri
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan M. Mwinyi (kushoto) akijadiliana jambo na mmoja wa wajumbe wakati wa Mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya nchi za mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA). Balozi Mwinyi aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye kikao cha 20 cha Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi kilichofanyika tarehe 31 Oktoba na tarehe 01 Novemba, 2018.

===================================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya nchi za mwambao wa Bahari ya Hindi unaofanyika Durban, Afrika Kusini leo tarehe 2 Novemba,  2018
Mkutano huu umetanguliwa na Kikao cha 20 cha Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 01 Novemba, 2018 ambapo ujumbe huo uliongozwa na Balozi Ramadhan M. Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Jumuiya ya nchi za mwambao wa Bahari ya Hindi (Indian Ocean Rim Association – IORA) ilianzishwa mwaka 1997 awali, ikijulikana kama Indian Ocean Rim Association for Regional Cooperation IORA-AC kabla ya kubadilishwa kuwa IORA mwaka 2013. Jumuiya hii inaundwa na nchi wanachama 21 ambazo ni Afrika Kusini, Australia, Bangladesh, Comoro, India, Indonesia, Jamhuri ya Kiislam ya Iran, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kenya, Malaysia, Madagascar, Mauritius, Msumbiji, Shelisheli, Singapore, Somalia, Sri Lanka, Sultani ya Oman, Thailand, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Yemen. Tanzania ni moja kati ya nchi waanzilishi wa Jumuiya hii.
Katika muundo wake, IORA pia ina washirika wa mazungumzo (Dialogue Partners) saba (7) ambao ni Jamhuri ya Watu wa China, Japan, Marekani, Misri, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ambao hushiriki katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Jumuiya.
Katika uongozi, Afrika Kusini ndie Mwenyekiti wa sasa wa IORA akisaidiana na Umoja wa Falme za Kiarabu kama Makamu Mwenyekiti. Hivyo, Mheshimiwa Lindiwe Sisulu (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Kusini aliongoza mkutano huu.
Lengo kuu la IORA ni kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi. Ikumbukwe kwamba Bahari ya Hindi ni eneo muhimu sana kiuchumi, kirasilimali, kiusalama pamoja na maendeleo kwa ujumla.
Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ya mwaka 2001 inaelekeza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ishirikiane na nchi jirani, za mbali na zenye malengo mema katika sura za kikanda, kimataifa na pande mbili kwa manufaa yetu. Huu ndio msingi wa Tanzania kuendelea kushiriki katika IORA kwani inatusaidia kujenga mahusiano yanayolenga kukuza uchumi; tunapata fursa ya kutangaza na kuvutia uwekezaji katika uchumi bahari (blue economy); na tunashiriki katika kuandaa na kutekeleza mikakati ya kikanda ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi. Vilevile, kupitia IORA tunashiriki katika mfumo wa kupeana taarifa za kibiashara (IORA Trade Repository); kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukuza biashara ndogo na za kati (SMEs); pamoja na kushirikiana kwenye kulinda usalama katika Bahari ya Hindi.
Pamoja na mambo mengine, Mkutano huu wa 18 wa Mawaziri umeridhia  maombi ya nchi za Maldives na Myanmar kujiunga uanachama wa IORA.  Vilevile, Mawaziri wamekubali maombi ya nchi za Uturuki na Jamhuri ya Korea (Korea Kusini) kuwa Washirika wa Mazungumzo
Aidha, nchi mbalimbali wanachama ikiwemo Tanzania wameahidi kuendelea kushirikiana katika kutekeleza miradi ya maendeleo iliyo chini ya maeneo tisa vipaumbele kwa IORA ambayo ni usalama na ulinzi wa bahari; biashara na uwekezaji; usafiri wa bahari; uvuvi; menejimenti ya udhibiti wa majanga; taaluma, sayansi na teknolojia; utalii na utamaduni; uchumi bahari; na uwezeshaji wanawake.
Jumuiya hii ni fursa nyingine muhimu sana kwa Tanzania kwa kuwa ina malengo mazuri yenye maslahi kwa nchi na Ukanda kwa ujumla. 
 Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika MasharikiDodoma.
02 Novemba, 2018

Thursday, November 1, 2018

Dkt. Ndumbaro aapa kuwa Mbunge wa EALA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro(Mb) ameapishwa rasmi kuwa Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika tukio hilo Dkt. Ndumbaro alisindikizwa na Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe na Mhe Pamela Maasay kutoka Tanzania. Aidha, mara baada ya kuapishwa alishiriki kikao cha Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (East Africa Legislative Assembly - EALA), ambalo lilijadili na kupitisha muswada wa Sheria ya kuanzisha Taasisi ya Takwimu ya Afrika Mashariki, tukio hilo limefanyika kwenye Bunge la Afrika Mashariki jijini Arusha.



Dkt. Ndumbaro akiwa tayari kwa vikao vya Bunge la Afrika Mashariki mara baada ya kuapishwa.





Tuesday, October 30, 2018

Balozi Mteule wa Umoja wa Falme za Kiarabu awasilisha Nakala za Hati za Utambulisho

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), amepokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania Mhe. Khalifa Abdulrahman Mohammed Al Marzooqi, tukio hilo limefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam tarehe 29 Octoba, 2018.
Balozi Mteule Mhe. Khalifa Abdulrahman Mohammed Al Marzooqi akimweleza jambo Dkt. Mahiga mara baada ya kuwasilisha nakala za hati zake za utambulisho.


Waziri Mwijage awa Mgeni rasmi maadhimisho ya Taifa la Uturuki.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage(Mb.), akihutubia kwenye hafla ya maadhimisho ya Taifa la Uturuki, katika hotuba yake Mhe. Mwijage aliishukuru Uturuki kwa kuendelea kuwa mshirika mkubwa wa jitihada za Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuwaletea Watanzania maendeleo. Maadhimisho hayo yalifanyika katika makazi ya Balozi wa Uturuki jijini Dar Es Salaam Tarehe 29 Octoba, 2018.
Viongozi kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania wakisikiliza kwa makini hotuba iliyokuwa ikitolewa na Mhe. Mwijage
Mhe. Mwijage akiendelea kuhutubia.
Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Mhe. Ali Davutoglu naye akihutubia wakati wa maadhimisho ya Taifa la Uturuki, Mhe. Davutoglu, alisema Uturuki itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano za kubadalisha maisha ya watu masiikini.
Mhe. Mwijage (wa kwanza kushoto), na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Jestas Nyamanga (wa pili kutoka kushoto) wakimsikiliza Balozi Davutoglu wakati akihutubia.
Mhe. Mwijage akigonganisha glasi na Balozi Davutoglu kwa kuwatakia afya njema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Joseph Magufuli na Rais Recep Tayyıp Erdoğan wa Uturuki. 
Mhe. Mwijage akisalimiana na Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania Mhe. Monica Patricio walipokutana kwenye maadhimisho ya Taifa la Uturuki
Bw. Jestas Nyamanga akizungumza na Balozi wa Uturuki Mhe. Davutoglu 








Monday, October 29, 2018

Tanzania na China zaadhimisha miaka 50 ya ushirikiano katika sekta ya afya

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), akihutubia kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya Ushirikiano kati ya Tanzania na China katika sekta ya afya ambapo Dkt. Mahiga ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta ya Afya, ambapo imeendelea kuleta Madaktari wakujitolea katika Hospitali mbalimbali zilizopo nchini zikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Aidha, Tanzania na China zimekuwa na mahusiano katika sekta ya Afya, tangu mwaka 1968 ambapo madaktari kutoka jimbo la Shandong wamekuwa wakija Tanzania kutoa Huduma za Afya katika mikoa mbalimbali nchini.

Madhimisho hayo yalihudhuriwa na Dkt. Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu Mstaafu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalim,
maadhimisho hayo yamefanyika katika Ubalozi wa Jamhuri ya watu wa China nchini.
Dkt. Salim Ahmed Salim (kulia) akisikiliza kwa makini hotuba iliyokuwa ikitolewa na Dkt. Mahiga
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Prof. Mohammed Janab (kushoto) akisikiliza kwa makini hotuba ya Mhe. Waziri

Balozi wa Jamhuri ya watu wa China, Mhe. Wang Ke, akihutubia kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya ushirikiano kati  ya Tanzania na Jamhuri ya watu wa China katika sekta ya afya ambapo ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kuendelea na kuimarisha sekta ya afya. Mhe. Balozi Wang Ke kwa kutambua umuhimu wa sekta hiyo na kutokana na mahusiano mazuri waliyonayo imeendelea kuleta nchini madaktari bingwa watakao kuwa wanatoa matibabu bure kwenye mikoa mbalimbali nchini. 
Juu na chini ni sehemu ya wageni waliohudhuria maadhimisho hayo wakifuatilia kwa makini hotuba mbalimbali zilizokuwa zikitolewa 
Dkt. Mahiga akiendelea kuhutubia.

Wakikata keki ya maadhimisho ya miaka 50 ya Ushirikiano kati ya Tanzania na China kwenye sekta ya Afya. 
Picha ya pamoja na Madaktari Bingwa kutoka Jamhuri ya Watu wa China.









Dkt. Ndumbaro akutana na Balozi Kenya

aa
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (kulia) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Kenya nchini Mhe. Dan Kazungu. Mazungumzo yao yalihusu kuimarisha ushirikiano kati ya nchi mbili ikiwemo kutatua changamoto za kibiashara
Mhe. Naibu Waziri akiendelea na mazungumzo na Balozi wa kenya nchini

Mhe. Naibu Waziri akiagana na Balozi wa Kenya baada ya kumaliza mazungumzo yao.