Thursday, March 28, 2019

TANGAZO LA MAFUNZO YA KILIMO NCHINI ISRAEL


28 Machi 2019

TAARIFA KWA UMMA

TANGAZO LA MAFUNZO YA KILIMO NCHINI ISRAEL

UTANGULIZI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inatangaza ufadhili wa mafunzo katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini Israel. Mafunzo hayo ni ya miezi 11 kuanzia mwezi Septemba, 2019 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Serikali ya Israel kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mafunzo hayo yatahusisha pia vitendo (field attachment) kwenye mashamba makubwa ya mazao mbali mbali yakiwemo ya matunda, mbogamboga, ufugaji, uvuvi na mazao mengine ya biashara kwa ujira maalum.

SIFA NA VIGEZO VYA MWOMBAJI

  1. Awe ni raia wa Tanzania mwenye umri wa kati ya miaka 20-35 pamoja na cheti cha kuzaliwa na Kitambulisho cha Uraia.  
  2.  Awe amehitimu mafunzo ya Kilimo katika ngazi ya shahada ya Chuo Kikuu,Stashahada au Astashahada ya Vyuo vya kilimo vinavyotambulika nchini.
  3.  Awe na afya njema.  
  4.  Awe na ujuzi wa kuandika na kuongea lugha ya Kiingereza.   
  5. Awe na uwezo wa kufanya kazi na watu wa tamaduni mbalimbali.  
  6.  Awe tayari kurejea nchini baada ya mafunzo yake.         

UTARATIBU WA KUFANYA MAOMBI

Maombi yote yatumwe kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki yakiwa yameambatishwa na nakala za nyaraka zifuatazo:


     i.     Cheti cha kuzaliwa na uraia.  

   ii.      Vyeti vya kitaaluma.

 iii.        Hati ya Kusafiria au uthibitisho wa maombi ya pasipoti.

  iv.      Cheti cha kuthibitisha afya kutoka hospitali inayotambulika.

    v.    Barua ya kuonesha sababu za kushiriki mafunzo hayo  (Motivation letter) kwa lugha           ya Kiingereza.

  vi.        Wasifu (Curriculum Vitae).

 vii.        Picha mbili ndogo (Passport size).

viii.        Majina na anwani za wadhamini watatu wanaoishi nchini akiwemo mwalimu wa                 Chuo ulichohitimu.

Maombi yote yatumwe kupitia anwani ifuatayo: -

Katibu Mkuu,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Jengo la LAPF
Ghorofa ya 6,
Barabara ya Makole,
S.L.P   2933,
DODOMA.

Au kwa baruapepe; mafunzo.israel@nje.go.tz 

Mwisho wa kupokea maombi ni tarehe 12 Aprili, 2019

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.

Fursa za ajira.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

NAFASI ZA AJIRA KATIKA SEKRETARIETI YA JUMUIYA YA MADOLA, LONDON, UINGEREZA.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inawahimiza Watanzania wenye sifa kuomba nafasi za ajira katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, London, Uingereza.

Ajira hizo ni kama ifuatavyo:-

1.           Mshauri wa masuala ya Miundombinu na Usanifu wa Majengo        (Advisor Infrustructure and Architecture);
2.           Mkurugenzi wa masuala ya Uchumi, Vijana na Maendeleo      Endelevu (Senior Director, Economic, Youth and Sustainable         Development) na
3.           Mshauri  na Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Ushindani (Advisor and Head,   Trade and Competitiveness section).

Watanzania wenye sifa wanahamasishwa kuomba nafasi hizo hasa ikizingatiwa kuwa, nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola ambazo hazina watumishi wengi katika ngazi ya maafisa waandamzi watapewa  kipaumbele ili kuimarisha uwiano wa kikanda katika nafasi hizo za ajira.
Kwa kuzingatia sera ya Jumuiya ya Madola ya usawa wa kijinsia, Sekretarieti ya taasisi  inawahimiza wanawake wengi zaidi wenye vigezo kuomba nafasi hizo.
Taarifa zote muhimu kuhusu fursa hizo za ajira zinapatikana kwa kupitia tovuti http://thecommonwealth.org.jobs.
Mwisho wa kutuma maombi kwa nafasi hizo ni tarehe 10 Aprili, 2019; tarehe 16 Aprili, 2019 na tarehe 17 Aprili, 2019, mtawalia.

 Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma
28 Machi, 2019.



Balozi Seif Ali Iddi akutana na Rais wa Bunge la Cuba.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Rais wa Bunge la Cuba, Mhe. Esteban Lazo Harnandez, mjini Havana, Cuba.
Mhe. Harnandez kulia akipokea zawadi ya mlango wa mji Mkongwe kutoka kwa Balozi Seif kama ishara ya kufunguliwa milango ya kuitembelea Zanzibar.

 Mhe. Harnandez akimtembeza Mhe. Balozi Iddi katika sehemu mbalimbali za jengo la Bunge ya Cuba lenye historia ya muda mrefu ambazo zimewekwa kama kumbukumbu ya taifa hilo.
Mhe. Balozi  Iddi wa pili kutoka kulia na ujumbe wake akifanya mazungumzo na uongozi wa Wizara ya Afya mjini Havana, Cuba.

=====================================


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amelitembelea Bunge la Cuba na kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa bunge la nchi hiyo, Mhe. Esteban Lazo Harnandez.  
Katika mazungumzo baina ya viongozi hao wawili, Mhe. Harnandez ameahidi kuwa, Cuba itaendelea kudumisha ushirikiano wake wa kidiplomasia na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuendeleza wananchi wake licha ya taifa hilo la Caribean kupita katika mabadiliko ya kisiasa, uchumi na utamaduni. 
Mhe. Harnandez alieleza kuwa, kutokana na mabadiliko yaliyopo sasa katika mfumo wa dunia  katika masuala ya uchumi, siasa na utamaduni Jamhuri ya Cuba imelazimika kufanya mabadiliko ya katiba yake ili yalingane na mfumo huo wa dunia inayoizunguka.
Alifafanua kuwa, tayari Bunge la Cuba limeshafanya marekebisho katika katiba yake kutoa nafasi kwa wananchi wake kuwa na uwezo na uhuru wa kumiliki nyumba, ardhi pamoja na uwepo wa waziri mkuu atakayekuwa na mamlaka ya kusimamia utendaji wa serikali.
Mhe. Harnandez alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, kwamba katika vikao vya bunge hilo vinavyotarajiwa kuanza wiki ijayo baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa wabunge, serikali ya nchi hiyo itakuwa imepiga hatua kubwa zaidi ya maendeleo kutokana na mabadiliko hayo.
Rais huyo wa Bunge la Cuba alisisitiza kwamba taasisi za kifedha zitalazimika kuzingatia ukusanyaji bora zaidi wa mapato katika maeneo yote ya uchumi ili kuimarisha ushiriki wa wananchi waliowengi katika mfumo huo.
Mhe. Harnandez alihitimisha kwa kumuhakikishia Balozi Seif kwamba,  uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili utaendelea kuimarishwa na kukuzwa katika muda wote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Iddi alimpongeza Mhe. Harnandez kwa kuchaguliwa tena kuliongoza bunge hilo na kueleza kuwa, hatua hiyo inaonesha wazi ishara halisi ya kukubalika vyema na wananchi wa nchi hiyo kupitia viongozi wake.
Halikadhalika, Mhe. Balozi Iddi alieleza kuwa, kwa ujumla Zanzibar itaendelea kufuatilia mabadiliko ya Cuba na kuangalia endapo inaweza kuiga mabadiliko hayo ili kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi walio wengi.
Mhe. Balozi Iddi na ujumbe wake ulihitimisha ziara yake  nchini humo kwa kufanya mazungumzo na uongozi wa Wizara ya Afya ya Cuba uliokuwa ukiongozwa na Naibu Waziri, Mhe. Bibi Marcia Cobas,  katika makao makuu ya wizara hiyo yaliyopo Havana, Cuba.
Katika mazungumzo hayo ya ushirikiano wa kindugu, Balozi Iddi alisema matunda ya darasa la madaktari wazalendo waliosimamiwa na wataalamu pamoja na wahadhiri wa nchi ya Cuba yameanza kutoa matumaini.Alifafanua kuwa, kitendo cha Serikali ya Cuba kukubali kupunguza gharama kubwa ya kuwaendeleza madaktari hao wazalendo wapatao 15 katika shahada ya juu ya udaktari wa uzamili nchini humo kinaendelea kuleta faraja kubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na watu wake.
Alisema wakati Zanzibar ikiendelea kutekeleza sera ya afya ya kuwa na miuondombinu ya huduma za afya katika umbali usiozidi kilomita tano kundi hilo na madaktari linaloendelea kuongezeka kila mwaka litakuwa mkombozi wa utekelezaji wa sera hiyo muhimu.
Naye Kaibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Bibi Asha Ali Abdullah, aliueleza uongozi huo wa Wizara ya Afya Cuba kwamba, hivi sasa Zanzibar  inapita katika kipindi cha kujiimarisha kwenye mapambano yake dhidi ya maradhi yasiyoambukiza.
Bibi Abdullah alisema maradhi yasiyoambukiza kama Kisukari pamoja na Shindikizo la Damu hivi sasa yamekuwa yakiathiri wananchi walio wengi na kuleta vifo vingi. Hata hivyo, jitihada zinachukuliwa ili kupunguza kasi  ya athari za maradhi hayo na kuimaliza kabisa kadhia hiyo kabisa.
Alibainisha kuwa, maradhi ya Malaria hivi  sasa yamepungua kutokana na kampeni kubwa iliyofanywa na serikali kwa kushirikiana na taasisi na mataifa wahisani katika kuangamiza vilui lui vya maradhi hayo.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya Zanzibar alimuhakikishia Naibu Waziri wa Afya wa Cuba kwamba ushauri wote walioupata katika ziara yao kwenye taasisi za Afya nchini Cuba likiwemo suala la upatikanaji wa dawa litazingatiwa na iwapo linaweza kuleta afueni ya gharama kwa Zanzibar litachukuliwa hatua mara moja.

Mhe. Dkt. Ussi atembelea Shamba Asilia nchini Cuba

Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Ufugaji na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Dkt. Makame Ali Ussi,  ametembelea shamba la mimea asilia ( organic farm ) nchini Cuba, ambapo alipata maelezo juu ya uzalishaji wa mazao mbalimbali bila kutumia kemikali ambapo  mradi huo umeweza kuajiri wafanyakazi takribani 200 wakiwemo wazee na vijana. Wa pili kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Shamba hilo, wa pili kutoka kulia ni mkalimani Bi. Beatriz Soto na wa kwanza kushoto ni Afisa kilimo, Bw. Jose Antonio. 
 Mhe. Dkt. Ussi akiendelea kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa shamba hilo, Bw.Miguel Angel Lopez, wa kwanza kulia ni Afisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Mohamed Kamal Mohamed, akisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa. 
 Mhe. Dkt. Ussi akiendelea kupata maelezo juu ya kilimo cha miwa.
Juu na chini  Mhe. Dkt.  Ussi akipata maelezo namna ya utengenezaji wa mbolea isiyokuwa na kemikali yeyote.







Bw. Lopezi akimwonyesha Mhe.Dkt. Ussi teknolojia ya kifaa cha kupandia mazao.
 Mhe. Dkt. Ussi akizungumza na mmoja wa wakulima kwenye shamba hilo, aliyeonekana kufurahishwa na ujio wa Watanzania.
Sehemu ya mazao yanayopatikana kwenye shamba hilo.


Mhe. Balozi Seif ahudhuria maonesho ya kilimo Cuba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi,  na Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Ufugaji na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Dkt. Makame Ali Ussi, wakikaribishwa na Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba Mhe. Jose Miguel Rodriquez De Armas, kwenye Maonesho ya Kimataifa ya 22 ya Kilimo yaliyofanyika jijini Havana, Cuba.  Mhe. Balozi Seif Ali Iddi alialikwa kama mgeni rasmi kwenye maonyesho hayo yaliyofanyika mnamo tarehe18 Machi, 2019. Maonesho hayo yalihudhuriwa na wananchi zaidi ya  3000. 

Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, akitizama kikundi cha wakulima waliokuwa wameandaliwa kutoa burudani kwenye maonyesho hayo.
Burudani zikiendelea kutolewa na vikundi mbalimbali vya wakulima.

Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba Mhe. Jose Miguel Rodriquez De Armas, akihutubia kwenye ufunguzi wa maonyesho hayo.
Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, akitembelea na kujionea mazao mbalimbali yanayolimwa nchini Cuba kwenye mabanda ya makampuni mbalimbali ya wafanyabiashara na yawakulima.



Balozi Seif Ali Iddi afanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo wa Cuba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, amekutana na kufanya mkutano na Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba, Mhe. Guastavo Rodriguez Roller. Mkutano huo ulijikita katika kuwajengea uwezo wakulima kwenye mazao ya kimkakati, ikiwemo kilimo cha pamba, miwa na maembe.


Mkutano ukiendelea kati ya ujumbe kutoka Tanzania ukiongozwa na Mhe. Balozi Seif Ali Iddi na ujumbe wa Cuba ukioongozwa na Mhe. Guastavo Rodriguez Roller.
Mhe. Balozi  Iddi, akimkabidhi Waziri wa Kilimo wa Cuba, Mhe. Guastavo Rodriguez Roller, zawadi ya mlango wa mji Mkongwe ikiashiria ukaribisho wa ushirikiano mpya wa sekta ya kilimo kati ya Tanzania na Cuba.

==================================


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ameipongeza Serikali ya Cuba kupitia Wizara ya  Kilimo na Mifugo kwa mtazamo wake wa  kuanzisha ushirikiano mpana zaidi baina ya  Zanzibar na Tanzania katika sekta hiyo muhimu.

Akizungumza na Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Cuba, Mhe. Guastavo Rodriguez Roller, katika makao makuu ya wizara hiyo mjini Havana, Balozi Seif  alieleza kuwa, Zanzibar na Cuba zimekuwa na ushirikiano ya karibu katika sekta za afya na elimu kwa kipindi kirefu sasa suala ambalo limeleta mafanikio makubwa.

Balozi Seif alibainisha kuwa, kwa kuwa maonyesho ni moja ya njia ya kubadilishana mawazo kitaaluma alimuomba Waziri wa Kilimo wa Cuba kutenga muda wa kushiriki katika Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Tanzania yanayofanyika  mwezi  Agosti wa kila mwaka nchini.

Kwa upande wake,  Mhe. Roller alibainisha kwamba, Cuba imebarikiwa kuwa na hekta milioni 10,000,000 ambazo zinatoa ajira kwa wakulima zaidi ya  5,000.Alifafanua kuwa, asilimia 70% ya ardhi hiyo ina maliasili, asilimia 3.5 inatumika kufuga na zaidi ya asilimia 60 inatumika katika uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na kilimo pekee.

Wednesday, March 27, 2019

Waziri Mkuu atembelea Mji wa Serikali uliopo Mtumba, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza alipotembelea Jengo  la  Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki linalojengwa kwenye Mji wa Serikali uliopo Mtumba jijini Dodoma. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri Mkuu alizipongeza baadhi ya Wizara kwa kukamilisha majengo ya Ofisi zao na kuzitaka Wizara  zote kuhakikisha zinakamilisha hatua za mwisho za ujenzi huo ikiwa ni pamoja na kusawazisha maeneo na kuweka miundombinu muhimu kama maji na umeme kabla ya tarehe 15 Aprili 2015. Aidha, aliziagiza Taasisi kama TANESCO, TARULA na DUWASA kukamilisha kuweka huduma hizo muhimu  za umeme, maji na barabara kwenye mji huo. Tayari Wizara 20 zimekamilisha majengo ya ofisi zao kwa zaidi ya asilimia 98. Wengine katika picha ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Anisa Mbega (kulia) na  Katibu wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kutaribu mpango wa Serikali kuhamia Dodoma,  Bw. Meshack Bandawe (katikati). Ziara hiyo imefanyika tarehe 27 Machi 2019
Baadhi ya mafundi wanaoendea na ujenzi wa jengo la ofisi za Wizara Mtumba wakiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Deus Kaganda wakati wa ziara ya Waziri Mkuu kwenye Mji wa Serikali uliopo Mtumba
Mhe. Waziri Mkuu akikagua moja ya chumba cha ofisi katika jengo la Wizara lililopo Mtumba 
Mhe. Waziri Mkuu akitoa maelekezo kwa Kaimu Katibu Mkuu, Balozi Mbega alipotembelea jengo la Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lililopo Mtumba jijini Dodoma. Pamoja na mambo mengine ameitaka Wizara kuharakisha usawazishaji wa eneo la nje (landscaping) la jengo hilo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Mhe. Petrobas Katambi. Kushoto ni Meneja wa Mradi wa ujenzi wa ofisi za Wizara,  Mhandisi Elikyus Msigwa.
Katibu wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kutaribu mpango wa Serikali kuhamia Dodoma,  Bw.  Bandawe (mwenye kipaza sauti) akitoa taarifa fupi kwa Mhe. Waziri Mkuu kuhusu ujenzi wa ofisi mbalimbali za Wizara
Mhe. Waziri Mkuu akitoa maelekezo kuhusu kukamilisha ujenzi wa ofisi za Wizara kwenye mji wa Serikali uliopo Mtumba. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Mhe. Jenista Mhagama 
Sehemu ya Watumishi wa Umma walioshiriki ziara ya Waziri Mkuu kwenye Mji wa Serikali
Watumishi wakimsikiliza Mhe. Waziri Mkuu (hayupo pichani)
Mhe. Kassim Majaliwa akimpongeza Katibu wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kutaribu mpango wa Serikali kuhamia Dodoma,  Bw. Meshack Bandawe kwa kuratibu mpango huo kikamilifu.









Fursa za mafunzo nchini Thailand


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

FURSA ZA UFADHILI WA MASOMO KWA WATANZANIA

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea fursa za ufadhili wa masomo ya muda mrefu katika fani mbalimbali kutoka Serikali ya Thailand.

Kozi hizo zitakazotolewa kwenye Vyuo mbalimbali nchini humo, zitajikita katika fani za Filosofia ya Uchumi Timilifu; Mabadaliko ya Tabianchi, Usalama wa Chakula; Afya ya Jamii na Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Wizara inawahimiza Watanzania wenye sifa kuomba nafasi hizo za mafunzo zilizotangazwa na Serikali ya Thailand kwa mwaka 2019.

Mwisho wa kuomba nafasi hizo ni tarehe 31 Machi 2019. Kwa maelezo zaidi kuhusu kozi hizo na namna ya kuomba, tafadhali tembelea tovuti  ifuatayo: http://www.tica.thaigov.net


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje Na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
27 Machi 2019

Nchi za SADC zimeahidi kushikamana na Saharawi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Pretoria Afrika Kusini tarehe 25 na 26 Machi 2019. Mkutano huo ni maalum kwa ajili ya kuonesha mshikamano na nchi ya Saharawi, ambapo washiriki walielezea dhamira yao ya kusimama pamoja na Saharawi.

Dkt. Damas Ndumbaro akisalimiana na Rais wa Saharawi, Mhe. Brahim Ghali katika ukumbi wa mikutano jijini Pretoria.

Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC na wawakilishi wa Wakuu Nchi na Marafiki wa Sharawi walioshiriki mkutano huo wakiwa katika picha ya pamoja.

Tuesday, March 26, 2019

Balozi wa Tanzania nchini Sudan akutana na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika

Balozi wa Tanzania nchini Sudan, Mhe. Silima Kombo Haji,  amekutana na kufanya  mazungumzo rasmi na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika (International University of Africa - IUA), Profesa Kamal Muhammed Ubeid, mjini Khartoum, Sudan. Katika mazungumzo baina yao, Prof. Ubeid alimhakikishia Balozi Silima kuwa, chuo hicho kitaendeleza ushirikiano  na Tanzania kwa kuendelea kutoa ufadhili wa elimu ya juu kwa wanafunzi wengi zaidi wa Kitanzania kadri hali itakavyoruhusu.
Takribani wanafunzi wa Kitanzania wapatao 517 wanaosoma katika vyuo mbalimbali nchini Sudan ambapo 490 kati yao wanasoma katika chuo hicho kilichopo Khartoum katika fani mbalimbali zikiwemo uhandisi wa mafuta na gesi, uchumi, udaktari na dawa na maabara, sheria, lugha na fani nyinginezo. 


Balozi Silima mara baada ya mazungumzo na Profesa Ubeid.

Mtanzania ateuliwa kuongoza Taasisi ya Kimataifa nchini China

Balozi Ali Mchumo

=============================================================
Balozi Mstaafu, Mhe. Ali Mchumo (Pichani) kutoka Tanzania ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya International Network for Bamboo and Rattan (INBAR) yenye makao yake makuu mjini Beijing, China. Taarifa ya uteuzi wake imetangazwa tarehe 25 Machi 2019 katika tovuti ya taasisi ya INBAR. Taasisi ya INBAR ilianzishwa mwaka 1997 kwa madhumuni ya kukuza matumizi ya mianzi (Bamboo) kama njia endelevu ya utunzaji wa mazingira . Taasisi hiyo inaundwa na nchi wanachama 45 na ina ofisi zake za kanda nchini  Ethiopia, Ghana na Equador. Tanzania ni mojawapo ya nchi mwanachama mwanzilishi wa taasisi hiyo na imenufaika na uwepo wa taasisi hiyo kupitia miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na INBAR pamoja na mafunzo kwa wataalam wa zao la mianzi. 


Mawaziri wa Afrika wakutana Morocco

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco, Mhe. Nasser Bourita,  baada ya kuwasili kwenye ukumbi wa mkutano.

Dkt. Mnyepe amemwakilisha Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Kabudi (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenye mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika kuhusu maamuzi ya Umoja wa Afrika (AU) kuunga mkono jitihada za usuluhishi wa mgogoro wa eneo la Sahara Magharibi kati ya Morocco na Saharawi uliofanyika jijini Marrakech, Morocco tarehe 25 Machi, 2019.
Katibu Mkuu, Dkt. Mnyepe akifuatilia mazungumzo na michango ya wajumbe kutoka nchi mbalimbali wakati wa mkutano huo.
Katibu Mkuu, Dkt. Mnyepe wa tatu kutoka kushoto, mstari wa nyuma, akiwa katika picha ya pamoja ya Mawaziri na Wawakilishi wa Mawaziri walioshiriki mkutano huo.


Monday, March 25, 2019

Nafasi za ajira katika Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

NAFASI ZA AJIRA KATIKA JUMUIYA YA NCHI ZA UKANDA WA MAZIWA MAKUU (ICGLR)

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawahimiza Watanzania wenye sifa kuomba nafasi za ajira katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) yenye makao makuu Bujumbura, Burundi; Kituo cha Kikanda cha Kupambana na Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia (Regional Training Facility on SGBV) kilichopo Kampala, Uganda na Kituo cha Demokrasia na Utawala Bora cha Levy Mwanawasa (Levy Mwanawsa Regional Centre for Democracy and Good Governance) kilichopo Lusaka, Zambia. Ajira hizo ni kama ifuatavyo:-

SEKRETARIETI YA MAZIWA MAKUU

  1. Mkurugenzi wa Utawala na Fedha (Director, Administration and Finance);
  2. Mkurugenzi wa Nyaraka na Mikutano (Director, Documentation and Conferences);
  3. Mkurugenzi wa Mawasiliano (Director, Communications);
  4. Mshauri wa Masuala ya Sheria (Legal Adviser).

KITUO CHA DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA CHA LEVY MWANAWASA

  1. Mkurugenzi wa Kanda (Regional Director);
  2. Mkuu wa Utafiti (Head, Research);
  3. Mkuu wa Jukwaa na Uchunguzi (Head, Fora and Observatories).

KITUO CHA KIKANDA CHA KUPAMBANA NA UKATILI NA UNYANYASAJI WA KIJINSIA
  1. Mratibu wa Mafunzo (Training Coordinator) na
  2. Mratibu wa masuala ya TEHAMA, Utafiti na Elimu (IT, Research and Knowledge Coordinator).
Waombaji wa nafasi hizo wanapaswa kuwasilisha barua za maombi katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kabla ya tarehe 4 Aprili 2019 ili yaweze kuwasilishwa kwenye Sekretarieti ya ICGLR kwa wakati.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma
25 Machi 2019