Monday, November 16, 2020
PROFESA KABUDI AKIAPISHWA KUWA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
Saturday, November 14, 2020
BALOZI IBUGE AKUTANA NA BALOZI WA CHINA NCHINI
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke ofisini kwake jijini Dodoma.
Katika kikao hicho Katibu Mkuu, Balozi Ibuge na Balozi Wang Ke pamoja na mambo mengine wameongelea juu ya mapendekezo ya mabadiliko ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu nafasi za uwakilishi wa kudumu kwa Bara la Afrika.
katika Kikao hicho Balozi Ibuge amesisitiza msimamo wa Tanzania kuunga mkono nia ya Bara la Afrika kuwa na nafasi mbili za uwakilishi wa kudumu katika Baraza hilo. Nchi za Afrika zinataka uwakilishi huo uwe na nguvu ikiwa ni pamoja na kupata nafasi moja ya kura ya Veto kama walivyokubaliana katika mkutano wa Ezulwini na Azimio la Sirte la mwaka 1999.
Balozi Ibuge pia amezungumzia kuhusu utekelezaji wa mambo maalum ambayo yamo katika Hotuba ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati wa kuzindua Bunge la 12, tarehe 13 Novemba 2020 jijini Dodoma, ambapo amemuomba Balozi Wang Ke kufikisha mambo yaliyomo katika hotuba hiyo kwa wawekezaji wa China ili kuwekeza nchini.
Balozi Ibuge amesema maono ya Mhe. Rais aliyoyasema katika hotuba yake ni utekelezaji wa moja ya kauli iliyowahi kutolewa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa "wakati wengine wanatembea Watanzania tunatakiwa tukimbie." ili kufikia maendeleo kwa haraka.
Kwa Upande wake Balozi Wang Ke amemuhakikishia Balozi Ibuge, kwamba China iko pamoja na Bara la Afrika na kwamba wanaunga mkono mapendekezo ya Bara la Afrika ya kuwa na nafasi mbili za kudumu katika Baraza hilo.
Balozi Wang Ke ameelezea kufurahishwa na maono ya Mhe. Rais yaliyobainishwa katika Hotuba hiyo na kuahidi kuendelea kuisaidia Tanzania ili kufanikisha maono hayo kwa vitendo na kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo.
Viongozi hao pia wamejadiliana na kukubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kindugu baina ya Tanzania na China kwa faida ya pande zote mbili.
Friday, November 13, 2020
WABUNGE WA AFRIKA MASHARIKI WAHIMIZWA KUTANGULIZA MASLAHI YA TANZANIA
Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge
amekutana na Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki na kuwahimiza
kutanguliza maslahi ya Tanzania katika
kutekeleza majukumu yao.
Mhe. Ibuge
amesema hayo jijini Dodoma alipokutana na Wabunge hao na kusisitiza kuwa maslahi ya Tanzania ni lazima yawe kipaumbele chao katika kutekeleza majukumu yao ili
kufanikisha ushiriki wa Tanzania kikamilifu katika mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Endeleeni kushikilia msimamo wa kutanguliza maslahi ya Tanzania siku zote, muendelee kufanya kazi hiyo nzuri kwenye masuala mengine yote yanayogusa maslahi ya nchi yetu,” amesema Balozi Ibuge na kuongeza kuwa nafasi yao kama wabunge wa Afrika Mashariki inatokana na uwepo wa jimbo lao ambalo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mtangamano huo.
Balozi Ibuge
pia amewataka Wabunge hao kuwasiliana mara kwa mara na Serikali ili kupata maoni,
ushauri na msimamo wa Serikali katika kujadili na kupitisha masuala mbalimbali
ndani ya bunge hilo.
Balozi Ibuge
amewataka wabunge hao kujiepusha na migogoro ndani ya Bunge na Jumuiya kwani
kufanya hivyo kutaiwezesha Tanzania kujiweka sawa katika nyanja za siasa na
diplomasia na kuwapongeza kwa utendaji kazi wao na hasa jinsi
walivyoshughulikia suala la Muswada binafsi wa Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi
wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza
katika kikao hicho Mwenyekiti wa Wabunge hao Mhe. Adam Kimbisa aliishukuru Wizara
kwa kukutana nao kuwapa muongozo wa namna ya kushughulikia mambo mbalimbali
yanayoendelea ndani ya Bunge na Jumuiya kwa ujumla.
Mhe. Kimbisa
alimuahakikishia Katibu Mkuu kuwa Wabunge hao
wataendelea kuhakikisha maslahi ya Tanzania yanazingatiwa katika hatua
zote za mtangamano kupitia ushiriki wao katika Bunge la Afrika Mashariki.
Tuesday, November 10, 2020
COMORO YAIPONGEZA TANZANIA KWA UCHAGUZI HURU, AMANI NA HAKI
Rais
wa Visiwa vya Comoro Mheshimiwa Azali Assouman ameipongeza Serikali ya Tanzania
kwa kufanya uchaguzi huru, amani na haki.
Rais
wa Visiwa vya Comoro ameipongeza Tanzania leo jijini Dar es Salaam wakati
alipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa tayari kuondoka nchini na
kurejea Comoro baada ya kushuhudia hafla ya uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli uliofanyika Novemba 5 Jijini
Dodoma.
Rais
Assouman anasema Tanzania ni nchi ya Amani na utulivu wa kisiasa kwani wakati
wote wa tukio la kuapishwa kwa Dkt Magufuli aliona mambo ambayo yanapaswa
kuigwa na mataifa mengine hususan kwenye nyakati za uchaguzi.
"Kwa
kweli tangu nimefika hapa Tanzania nimeona mambo mazuri na ambayo tunapaswa
kuyaiga sisi viongozi wa mataifa mengine," Amesema Rais Assouman
Mbali
na kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo ya uchaguzi, pia Rais Assouman ameliahidi
ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika Nyanja za mbalimbali ikiwemo
diplomasia ya uchumi, biashara, uwekezaji na utalii.
“Najisikia
niko nyumbani kwa sababu uhusiano wetu umeimarishwa zaidi, mahusiano yetu yamekuwa
katika masuala ya kijamii, utamaduni, biashara na mambo mengine mengi”
Amebainisha Rais Assouman.
Kwa
upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Sylvester Mabumba amesema
kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Comoro katika kuhakikisha
kuwa sera ya uchumi wa nchi zote mbili unakua zaidi.
"Sisi
tuatendelea kushirikiana vyema na Comoro kibiashara ili kukuza sera ya 2025 tunaifikia
ipasavyo kwa kuhakikisha kuwa uchumi wetu unafikia kiwango cha juu sana,
naamini kuwa tunapokuwa na masoko ya uhakika Viswa vya Comoro uchumi wetu
utakuwa zaidi," Amesema Balozi Mabumba.
Kwa
Upande wake Balozi wa Visiwa Vya Comoro nchini Tanzania mhe. Dkt. Ahmada El
Badaoui Mohamed amesema kuwa kuna fursa nyingi za kiuchumi ambazo Comoro na
Tanzania zinaweza kushirikiana.
Rais
Assouman aliwasili nchini Novemba 4 kwa ajili ya kuhudhuria hafla ya uapisho wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli uliofanyika
Novemba 5 Jijini Dodoma ambapo baada ya shughuli hiyo alipata fursa ya kutembelea
hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ambapo na kujiona vivutio mbalimbali vya utalii
nchini.
Serikali
ya Tanzania na Visiwa Comoro zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali
ikiwemo, elimu, afya, biashara na uwekezaji.
Kikundi cha Ngoma kikiburudisha katika Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa Julius Nyerere kabla ya kuondoka kwa Rais wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Azali Assouman |
Rais wa Visiwa
vya Comoro, Mhe. Azali Assouman, akiagana na Balozi wa Tanzania nchini
Comoro, Mhe.Sylivester Mabunda katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius
Nyerere (JNIA), Jijini Dar es Salaam |
Rais wa Visiwa
vya Comoro, Mhe. Azali Assouman, akiaga tayari kwa kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa Julius Nyerere(JNIA), kwa kutumia Ndege ya Shirika la Ndege la
Tanzania (Air Tanzania) |
Monday, November 9, 2020
Thursday, November 5, 2020
MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI AKILA KIAPO CHA URAIS
Tuesday, October 27, 2020
Friday, October 23, 2020
NCHI ZA AFRIKA ZAHIMIZWA KUSHIKAMANA ILI KUONDOKANA NA UTEGEMEZI
Nchi za Afrika zimehimizwa kushikamana katika masuala ya maendeleo, biashara na uwekezaji ili kuondokana na utegemezi jambo litakaloliwezesha Bara hilo kufanya mambo yake kwa uhuru bila kuingiliwa na mataifa mengine ya nje kwa kisingizio cha demokrasia na haki za binadamu.
Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na Kiongozi wa Mabalozi wa nchi za Afrika hapa Tanzania Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed wakati Mabalozi hao walipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ikiwa ni utaratibu wa kukutana na Mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo na Tanzania.
Kiongozi huyo wa Mabalozi hapa nchini ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro amesema njia pekee ya Afrika kutoingiliwa katika mambo yake ya ndani ni kuhakikisha kuwa bara hilo linaweka mikakati madhubuti itakayowezesha bara hilo kujitegemea.
"Njia pekee ya Afrika kutoingiliwa katika mambo yake ya ndani ni kuhakikisha kuwa sisi kama waafrika tunaweka mikakati madhubuti itakayowezesha bara letu kujitegemea kwa umoja, mshikamano wetu wenyewe," Amesema Dkt. Mohamed
Nae Balozi wa Kenya hapa Nchini Mhe. Dan Kazungu amesema kikao hicho cha mabalozi wa Afrika na Prof. Kabudi hususani katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, umewawezesha mabalozi hao kufahamu namna Tanzania ilivyojiandaa kutekeleza demokrasia na kuwataka waafrika kujivunia nchi zao na kuwa wazalendo.
"MKutano wa leo umetuwezesha sisi mabalozi wa Afrika tunaowakilisha nchi zetu hapa Tanzania kufahamu namna Tanzania ilivyojiandaa kutekeleza demokrasia na kuwataka waafrika kujivunia nchi zao na kuwa wazalendo," Amesema Balozi Kazungu.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ameitumia fursa hiyo kuwaeleza Mabalozi hao namna Tanzania inavyoheshimu na kukuza diplomasia na mahusiano baina ya nchi za Afrika,kulinda demokrasia na haki za binadamu lakini pia kutumia fedha zake katika kuleta maendeleo ya watu na vitu jambo lililoiwezesha Tanzania kuingia katika nchi za uchumi wa kati kabla ya muda uliotarajiwa.
"Waheshimiwa
Mabaalozi napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania inaheshimu na imedhamiria kukuza
diplomasia na mahusiano baina ya nchi za Afrika, kulinda demokrasia na haki za
binadamu pamoja na kuhakikisha kuwa inatumia fedha zake za ndani katika kuleta
maendeleo ya watu na vitu jambo lililoiwezesha Tanzania kuingia katika nchi za
uchumi wa kati kabla ya muda uliotarajiwa," Amesema Prof. Kabudi.
Mkutano huo uliohudhuriwa Mabalozi 15 na wawakilishi wa Balozi 8 walitumia fursa hiyo kumuombea Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baba wa Taifa hayati Julius Kambarage Nyerere kama Baba wa demokrasia Barani Afrika pamoja na kuuombea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28.
Mabalozi
waliohudhuria katika mkutano huo ni Balozi wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Ahamada
El Badaoui Mohamed, Balozi wa Msumbiji, Mhe. Patricio Clemente, Balozi wa
Namibia, Mhe. Theresia Samaria, Balozi wa Somalia, Mhe. Mohammed Abdi, Balozi
wa Morocco, Mhe. Abdelilah Benryane, Balozi wa Zambia, Mhe. Benson Chali.
Wengine ni Balozi wa Burundi, Mhe. Gervais Abayeho, Balozi wa Kenya, Mhe. Dan Kazungu, Balozi wa Ethiopia, Mhe. Yonas Yosef Sanbe, Balozi wa Misri, Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abdulwafa, Balozi wa Angola, Mhe. Sandro De Oliveira, Balozi wa Malawi, Mhe. Chembe Mnthali, Balozi wa Saharawi, Mhe. Mahayub Buyema, Balozi wa Rwanda, Mhe. Meja Jenerali, Charles Karamba pamoja na Balozi wa Algeria, Mhe. Ahmed Djelal.
Wawakilishi waliowakilisha Balozi nane ni Bw. Jaafar Nasir Abdalla kutoka Ubalozi wa Sudan, Mr. Sizwe Ernest Mayoli kutoka Ubalozi wa Afrika Kusini, Balozi William Wani Ruben kutoka Ubalozi wa Sudani Kusini, Bibi. Bintu Bwala Ekikor kutoka Ubalozi wa Nigeria, Bw. Kamal Krista kutoka ubalozi wa Libya, Bw. Adjanga Bissa Benjamin kutoka ubalozi wa DRC, Bibi. Musekura Esezakutoka ubalozi wa Uganda pamoja na Bw. Chrispen Chibuwe kutoka Ubalozi wa Zimbabwe.
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiongea na Mabalozi
mbalimbali wa nchi za Afrika hapa nchini Tanzania leo jijini Dar es Salaam
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi
akiwaonesha Mabalozi (hawapo pichani)
ilani ya Chama Cha Mapinduzi wakati mkutano ukiendelea
Mkutano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi na Mabalozi ukiendelea
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi
akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi mara baada ya kumaliza mkutano |
Wednesday, October 21, 2020
TROIKA YA SADC YARIDHISHWA NA MAZINGIRA YA UCHAGUZI MKUU
Asasi
ya Ushirikiano wa Siasa,Ulinzi na Usalama (TROIKA) ya Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) imeridhishwa na mazingira ya hali ya siasa nchini
Tanzania yanaruhusu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Octoba 28,2020 na kwamba
wataendelea kufuatilia mazingira ya uchaguzi huo.
Akizungumza katika Mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao Jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amesema TROIKA imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu tangu awali mchakato wa uchaguzi hapa nchini na kwamba imeridhishwa na mazingira ya amani yaliyopo hali inayoruhusu uchaguzi huo kufanyika.
"Leo katika mkutano wangu na TROKA ulifanyika kwa njia ya mtandao mwenyekiti wa TROIKA ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Botswana Dkt. Lemogang Kwape ameoneshwa mazingira ya hali ya siasa nchini Tanzania yanaruhusu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Octoba 28, 2020 na kwamba wataendelea kufuatilia mazingira ya uchaguzi huo," Amesema Prof. Kabudi
Prof. Kabudi ameongeza kuwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipate uhuru kwamba uchaguzi huu unagharamiwa kwa fedha ya walipa kodi maamuzi ambayo yamefanyika kwa kutambua kuwa demokrasia ndio jambo kubwa katika uhai,utashi na kielelezo cha Taifa ambalo ni huru kama ilivyo Tanzania.
Kuhusu waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi mkuu wa Octoba 28, Prof Kabudi amesema TROIKA imefanya tathimini ya awali ya hali ya usalama na kisiasa na kwamba Tanzania inategemea kuwapokea waangalizi kutoka Umoja wa Afrika na wale wa kutoka katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amepokea nakala za hati za utambulisho za Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson.
Katika mazungumzo yao Prof. Kabudi amesema WFP imekuwa ni miongoni mwa mashirika ya Kimataifa ambayo yanaushirikiano mzuri na Tanzania ambapo kwa mwaka 2018 WFP imenunua tani 160,000 za nafaka na 2019 wamenunua tani 36,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 21 fedha ambazo zimesaidia wakulima wadogowadogo katika kuboresha kilimo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson amesema wamejadiliana namna ya kuendeleza ushirikiano baina ya pande hizo mbili hususani kusaidia wakulima wadogowadogo nchini kuboresha kilimo,kuboresha mazingira ya lishe na kwamba shirika hilo lina mpango wa kuongeza msaada wanaoutoa kwa Tanzania.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi
akieleza jambo wakati mkutano wa TROIKA ukiendelea. Mkutano huo ulifanyika kwa
njia ya mtandao leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John
Kabudi akipokea nakala ya hati za utambulisho za Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la
Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson leo
jijini Dar es Salaam
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John
Kabudi akiongea na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa
Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson leo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi
Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah
Gordon-Gibson akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi leo jijini Dar es Salaam
Monday, October 19, 2020
CHINA: TUHESHIMIANE, KUACHA KUINGILIA MASUALA YA NDANI YA NCHI NYINGINE
China
imetoa wito kwa mataifa mengine duniani kuheshimiana na kuacha kuingilia masuala
ya ndani ya nchi nyingine kwa kisingizio chochote kile na kueleza kuridhishwa
kwake na namna mchakato wa Uchaguzi mkuu unavyoendelea hapa nchini.
Kauli hiyo imetolea na Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke Jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na kuongeza kuwa ni lazima Mataifa yote yaendeleze mahusiano mema miongoni mwao na kutoingilia masuala ya ndani ya Mataifa mengine.
"Ni vyema Mataifa yote yakaendeleza mahusiano mema miongoni mwao na kuhakikisha kuwa hayaingilii masuala ya ndani kati ya Taifa moja na jingine," Amesema Balozi Wang Ke.
Aidha Balozi Wang Ke ameongeza kuwa China itaendelea kuheshimu masuala ya ndani ya Mataifa yote Tanzania ikiwemo na kueleza kuridhika kwake na mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu zinavyoendelea nchini na kuwatakia Watanzania kila la heri katika uchaguzi huo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi,Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema ushirikiano iliopo baina ya Tanzania na China kisiasa, kiuchumi na kijamii ni madhubuti na imara na kwamba Tanzania itaendelea pia kuheshimu mashirikiano na mataifa mengine.
Aidha Katibu Mkuu Balozi Brigedia Jenerali Ibuge ameishukuru China kwa Ushirikiano wake wa kimkakati kwa Tanzania na kwamba uhusiano huo utaendelea kudumishwa kwa maslahi ya pande zote mbili.
"Serikali ya Tanzania kwa kweli inaishukuru China kwa Ushirikiano wake wa kimkakati na tunakuahidi kwamba uhusiano wetu utaendelea kudumishwa kwa maslahi mapana ya pande zote mbili," amesema Balozi Ibuge.
Balozi
wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke akimuelezea jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert
Ibuge |
Friday, October 16, 2020
BALOZI IBUGE AKUTANA, KUMUAGA BALOZI WA NIGERIA
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, amekutana na kumuaga Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada ambaye amemaliza muda wake wa utumishi hapa nchini.
Mazungumzo
hayo yamefanyika leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo
pamoja na mambo mengine, Balozi Ibuge amemtakia maisha mema na kumsihi kuwa balozi
mwema kwa Tanzania nchini Nigeria na kwingineko duniani.
Balozi
Ibuge amesema kuwa Nigeria imekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na
Tanzania hasa katika kuunga mkono jitihada za kuimarisha sekta mbalimbali
nchini ikiwemo sekta za usafirishaji, utalii, biashara na uwekezaji na
usafirishaji
“Leo
nimekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Gada ambae amemaliza muda wake wa
utumishi hapa nchini na anarudi Nigeria, na kwa hakika mazungumzo marefu na yamelenga
urafiki baina ya nchi zetu mbili na watu wetu pamoja na ushirikiano uliopo wa
kibiashara, kibenki lakini pia tumezungumzia namna ambavyo Nigeria inapiga
hatua kama Tanzania inavyopiga hatua, na mfano mzuri ni kuwa Nigeria ilipojenga
mji wake mkuu mpya (Abuja) walikuja Tanzania kuja kujifunza na kupata ramani ya
Dodoma ambayo wamemaliza kuijenga na sisi sasa tunaendelea kuijenga Dodoma tangu
tulipotangaza rasmi kuhamia Dodoma mwaka 1973" Amesema Balozi, Brigedia Jenerali Ibuge
Balozi
Brigedia Jenerali Ibuge amemhakikishia Balozi Gada, kuwa uhusiano wa
kidiplomasia kati ya Tanzania na Nigeria utaendelea kuimarika ikiwa ni ishara
ya kuwaenzi waasisi wa mataifa ya Tanzania Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere pamoja na Rais wa kwanza wa Nigeria Nnamdi Azikiwe ambapo viongozi
hawa walikuwa ni sehemu ya juhudi za kukomboa bara la Afrika na hata kusimi mwa
Afrika.
Balozi
Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesisitiza kuwa Tanzania na Nigeria
zitaendelea kushirikiana katika sekta ya uwekezaji na biashara kwa maslahi
mapana ya mataifa yote mawili ambapo pia ametoa wito kwa wafanyabiashara kutoka
nchini Nigeria kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta za benki na utalii.
Kwa
upande wake, Balozi Sherlock ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa ushirikiano iliyompatia wakati wote alipokuwa akitekeleza majukumu
yake nchini na kuahidi kuwa ushirikiano uliopo utaendelezwa hasa ikizingatiwa
kuwa Nigeria na Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri na imara tangu miaka ya 1962.
”Nimekuja kumuaga Katibu Mkuu kama ishara ya ushirikiano wetu kati ya Nigeria na Tanzania kwa kweli nashukuru sana kwa ushirikiano nilioupata wakati wa utumishi wangu hapa nchini, nikiwa hapa nimeona uchumi wa Tanzania ukikua kila wakati jambo ambalo ni zuri hapa kwetu Afrika, pia namshukuru Katibu Mkuu, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kwa kuuendeleza ushirikiano wetu kwa kweli naiona Tanzania kama nyumbani kwangu pia,"Amesema Balozi Gada.
Nigeria
itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania za kukabiliana na
changamoto mbalimbali na kuhakikisha kuwa inasonga mbele kimaendeleo,” amesema
Balozi Gada.
Tanzania
na Nigeria zimekuwa na uhusiano wa kidiplomasia tangu Serikali ya Nigeria ilipofungua
ubalozi wake nchini Tanzania mwaka 1962.
Katibu
Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia
Jenerali Wilbert Ibuge akimuelezea jambo Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi
Isa Gada wakati alipokwenda kumuaga |
Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada akimkabidhi zawadi Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge
|
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge pamoja na Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa kutoka Wizarani na Ubalozi wa Nigeria hapa nchini |
Thursday, October 15, 2020
Tuesday, October 13, 2020
Tanzania Kutumia Maonesho Makubwa ya Qatar Kutangaza Utalii
Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Fatma Rajab alikutana na Shirika la Qatar Travel Mart (QTM) linalojishughulisha kutangaza utalii wa ndani na nje ya Qatar pamoja na kuandaa Maonesho ya Utalii. Shirika hilo linajiandaa kufanya Maonesho Makubwa ya Utalii yatakayofanyika tarehe 17-19 November 2021. Mataifa mengi ya kigeni ya Asia, Ulaya na Marekani yanatarajiwa kushiriki Maonesho hayo pamoja na ofisi za Kibalozi ziliopo Qatar. |
Maonesho hayo yatatoa fursa kwa nchi kutangaza Biashara, uwekezaji na Sanaa. Mhe. Balozi amewaahidi kuwa Tanzania itashiriki kikamilifu kwenye Maonesho hayo. Aidha kabla ya Maonesho hayo Ubalozi utaandaa Mkutano wa Mtandao Webinar Conference mwezi Desemba 2020 baina ya Shirika hilo la QTM na TTB na ZTC ili kuelezea vivutio vya Utalii vya Tanzania na kukaribisha watalii kutoka Qatar |
Friday, October 9, 2020
TANZANIA,CHINA ZAKUBALIANA KUIMARISHA MAHUSIANO YA KIMKAKATI
Tanzania na China zimekubaliana kuendeleza mahusiano ya kimkakati baina yao ili kuwezesha uwepo wa ulingo sawa miongoni mwa mataifa katika kusimamia maslahi na maendeleo ya nchi husika katika jumuiya za kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John kabudi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke na kusisitiza umuhimu wa Mataifa kuheshimiana na kutokubali kuingilia uhuru wa mambo ya ndani ya nchi kwa kisingizio cha haki za binadamu,demokrasia ama jambo lolote jingine.
Ameongeza kuwa mazungumzo hayo ya kimkakati yalilenga pia kutambua kuwa mwaka huu ni mwaka wa 55 tangu Tanzania na China zisaini mkataba wa urafiki ambao uliweka msingi wa mahusiano makubwa na ya dhati katika nyanja za ulinzi na usalama,afya,kilimo, elimu na miundo mbinu ambapo mpaka sasa China ni Taifa linaloongoza hapa nchini kwa uwekezaji wa moja kwa moja kwa kuwekeza zaidi ya miradi 700 yenye thamani ya dola za Kimarekani (USD) bilioni 7.1 na kutengeneza zaidi ya ajira 87,000 kwa watanzania.
Kwa upande wake Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke amesema China wakati wote ni Rafiki mwaminifu na wa kudumu wa nyakati zote kwa Tanzania na kwamba kutimiza miaka 55 ya urafiki wa nchi hizo ni kielelezo tosha na siku zote wataendelea kuuheshimu na kuuenzi urafiki huo.
Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Riitta Swan pamoja na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Pamela O'Donnell, ambapo pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi na mabalozi waliadili masuala mbalimbali ikiwemo kuimarisha mahusiano, Uwekezaji na Biashara, Afya, Elimu pamoja na Utalii.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi akiongea na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke wakati walipokutana kwa
mazungumzo leo jijini Dar es Salaam Balozi
wa China nchini, Mhe. Wang Ke akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati wa
mazungumzo yao leo jijini Dar es Salaam Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi
akimkaribisha Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Riitta Swan kabla ya kuanza
kwa mazungumzo Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi akimuonesha Balozi wa Canada nchini, Mhe. Pamela O'Donnell sheria ya
uchaguzi kabla ya kumkabidhi sheria hiyo pamoja na nyaraka nyingine zinazohusu
masuala ya uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 28 Oktoba 2020